Biashara ya wanyamapori na mimea mwitu ni muhimu hapa duniani kwa ajili ya kukidhi baadhi ya mahitaji muhimu ya binadamu, tunahitaji wanyamapori na mimea kwa sababu mbali mbali kama vile chakula, dawa, nguo na hata kwa matumizi ya ujenzi wa nyumba au sehemu za kuishi. Hivyo kwa namna yoyote ile uwepo wa wanyamapori ni muhimu sana kwa ajili ya kukidhi baadhi ya mahitaji hayo muhimu.
Kwasababu hiyo, tumekuwa tunatumia rasilimali hizi ambazo kwa kiasi kikubwa zipo kwenye maeneo yetu na nyingine zimehifadhiwa na kusimamiwa na sheria kali ili kuepuka matumizi ambayo sio endelevu. Msingi wa uhifadhi wa wanyamapori na mimea mwitu, au misitu ni kwa ajili ya kutumiwa kwa uendelevu ili kuhakikisha rasilimali hizi zinaendelea kuwepo kwa faida ya vizazi vingi vya sasa na badaye.
Shida inakuja pale tunapokosa usawa katika matumizi ya maliasili tulizo nazo; dunia inashuhudia mabadiliko makubwa sana ya matumizi yaliyozidi ya maliasili hizi muhimu, jambo ambalo linatupa hofu kuwa rasilimali hizi za wanayma na mimea kama zinaweza kuendelea kuwepo kwa miongo michache ijayo. Kulingana na tafiti nyingi pamoja na taarifa nyingi zilizopo kwenye vyanzo mbali mbali kama vile majarida, makala, vitabu na kwenye mitandao ya intaneti inaonyesha hali mbaya ya siku zijazo endapo tutaendelea kuwa na matumizi haya makubwa ya rasilimali hizi kwa siku za sasa.
Katika moja ya majarida maarufu sana yanayoelezea kwa kina biashara za wanyamapori na mimea, jarida hili limejikita kufuatilia, kutafuta na kubaini njia zote haramu za usafirishaji, uuzaji na usambazaji wa wanyamapori, mimea na hata sehemu au viungo vya wanyama au mimea. Jarida hili linajulikana kama TRAFFIC, Traffic wametoa majarida mengi sana yaliyosheheni taarifa muhimu sana ambazo zikifanyiwa kazi zitasaidia sana kupunguza biashara haramu za wanyamapori na mimea.
Hivyo basi kazi kubwa ya jarida hili maarufu ni kutafuta suluhisho kwa changamoto ambazo zipo kwenye usimamizi wa wanyamapori, hasa biashara ya wanyamapori. Ili taarifa hizo wanazozipata zisaidie serikali, wadau na watumiaji wa bidhaa au wanyamapori, pia kujua mienendo na hali ya mambo ilivyo kuhusiana na uzito wa mambo hasa kwenye biashara ya wanyamapori. Naamini kabisa endapo wahusika watapata taarifa halisi za namna mambo yanavyenda na hali ya baadaye ya maliasili za wanyamapori na mimea watafanya maamuzi chanya, ambayo yatasaidia sana uhifadhi wa wanyamapori na rasilimali hizi kwa ujumla.
Aidha, kwa nchi zote wanachama walioridhia makubaliano ya kimataifa ya kusitisha biashara za wanyamapori na mimea mwitu ambayo ipo hatarini kutoweka CITES, wanatakiwa wafahamu ukweli wa mambo ulivyo licha ya uwepo wa sharia kali za nchi wanachama na sheria za kimataifa za udhibiti wa biashara za wanyamapori na mimea hiyo.
Kama tutakavyojifunza kupitia uchambuzi wa jarida hili, tutaona hali ya mambo ilivyo katika nchi mbali mbali hapa duniani. Ukweli ni kwamba licha ya kwamba kuna baadhi ya spishi za wanyamapori na mimiea ambazo zimeainishwa na CITES kwamba hazitakiwi kuuzwa, lakini biashara ya wanyamapori na mimea mingine ambayo ilikuwa haipo katika hali mbaya ya kutoweka sasa inafikiriwa kuingizwa katika orodha ya wanyama na mimea ambayo ipo hatarini kutoweka, hii ni kutokana na biashara yake kuwa kubwa na mahitaji yake kwa watu kuwa makubwa.
Bila kupoteza wakati ngoja tuingie kwenye uchambuzi wa jarida hili, ili kwa pamoja tufahamu yanayoendelea katika nchi nyingine; lakini pia yanaweza kutokea katika nchi yetu endapo tutachelewa kuchukua hatua stahiki kudhibiti jambo hilo. Karibu Rafiki msomaji wa makala hizi za wanyamapori tujuzane kwa undani hali ya mambo ilivyo;
1.Biashara ya Hondo hondo (Helmented Hornbill, Rhinoplax vigil)
Moja ya spishi za Hondo hondo zinazopatikana kwa wingi katika nchi ya Indonesia sasa zimeingia katika orodha ya spishi ya ndege walio hatarini kutoweka, hii ni kwa mujibu wa makala iliyoandikwa na Serene C.L, mwandishi ana ainisha namna ambavyo idadi ya ndege hawa ilivyokuwa kubwa, lakini sana idadi yao imeshuka kutokana na uhitaji wake kwenye nchi mbali mbali za Asia.
Kutokana na ujangili uliokithiri wa ndege hawa, mwaka 2015 ndege hawa waliingia katika orodha ya ndege ambao wamo hatarini kutoweka. Taarifa za kina zinaonyesha zaidi ya matukio tofauti tofaut 59 ya ukamataji wa nyara za ndege hawa, ambapo zaidi ya nyara 2878 za sehemu mbali mbali za ndege hawa zilikamatwa, ikiwa ni pamoja na kichwa ambacho ndio nyara kuu inayohitajika na watumiaji wa ndege hawa.
Kama ilivyo kwa ujangili wa wanyamapori wengine kama vile tembo na faru, majangili wa ndege hawa wana mtandao mkubwa sana unaohusisha watu mbali mbali ambao husaidia katika uasafirishaji wa nayara hizo kutoka Indonesia hadi China ambako ndio watumiaji wakuu wa nyara hizo za horn bill au hondo hondo.
Ili kukabiliana na tatizo hilo, ilifanyika washa iliyojulikana kama Helmented Hornbill Conservation and Actio Planning ambayo ilifanyika Sarawk Malasia kuanzia tarehe 19 – 20 Mai 2017. Ambapo watalamu 36, watekelezaji, mamlaka za wafanya maamuzi ambao walikuwa serikali kutoka China, Indonesia, Thailand na Malasia, pia walikuwepo watafiti na mashirika mmbali mbali yasiyo ya kiserikali. Lengo kuu la kuita wakuu wote na watalamu mbali mbali ilikuwa ni moja, ni kwa namna gani kwa kushirikiana wote kwa pamoja wanaweza kusaidia ndege hawa wasitoweke hapa duniani. Pamoja na kuafikiana mipango na mikakati ya kuwanusuru ndege hawa, pia walipata kuungwa mkono na mashirika makubwa kama vile IUCN, WCS, nk.
Pia katika warsha hiyo walikubaliana kwa pamoja kuainisha mambo yote yanayotishia kutoweka kwa ndege hawa, baadhi ya mambo waliyokubaliana kufanya kwa pamoja ili kuokoa spishi za ndege hawa ni kujenga ufahamu kujua mtawanyiko, ikoloia na baiolojia ya ndege hawa, jambo la pili walikubaliana kuelewa madhara yanayoletwa na uharibifu wa makazi ya ndege hawa, ukame na uvamizi wa maeneo ya ndege hawa, jambo la tatu walikubaliana kuhusu biashara ya ndege hawa, utekelezaji wa sheria na sera za usimamizi wa nedge hawa na maeneo yake muhimu na jambo la nne na la mwisho walikubaliana kuharibu kabisa biashara na mtandao wote wa majangili na watumiaji wa nyara za ndege hawa.
Pia ili kuhakikisha waliyokubaliana yanaanza kufanyiwa kazi mara moja, kwa pamoja walikubaliana kuunda kikundi kitakachojihusisha kwa ukaribu na ndege hawa, mfano wa kikundi hicho waliamua kukiita helmented Hornbill working group, ambacho kitafanya shughuli zake zote chini ya mwavuli wa shirika la IUCN.
Kazi yao kubwa itakuwa kuhakikisha utekelezaji wa makubaliano ya wajumbe waliyoridhia yanafanyiwa kazi. Pamoja na mambo mengine kikundi hicho kilichoundwa kitakuwa na wajibu wa kushirikiana na taasisi mbali mbali za utafiti wa ndege hawa, kushauri serikali kuhusiana na hali na mwenendo wa spishi hizo za ndege. Kazi yote hiyo ni kuhakikisha kila walichokubaliana kwenye mkutano kuhusiana na uhifadhi wa ndege hawa kinafanyiwa kazi mapema.
Baada ya kusoma makala hii katika jarida la traffic bulletin, nimeona mambo mengi ambayo kwa pamoja kama wahifadhi tunaweza kuyafanyia kazi ili kuendeleza uhifadhi wenye tija. Wepesi wa kutekeleza yale muhimu waliyokubaliana kwenye vikao na mikutano ni jambo jingine muhimu la kujifunza siku zote. Wote tunaofanya kazi katika sekta hii ya maliasili tunahitaji taarifa za aina hii kwa ajili ya kujua na kujiandaa, kwasababu majangili wa spishi za ndege hawa wanaweza kuhamia kwenye hifadhi zetu na kuanza kutusumbua. Tujifunze na tuchukua hatua!
2.Cambodia ni kiini cha kuongezeka kwa biashara ya meno ya tembo na pembe za faru kutoka katika bara la Afrika. (Cambodia’s increasing role in the African ivory and rhinoceros horn trade).
Kati ya mambo yanayogonga vichwa vya habari kwenye magazeti na kurasa nyingi za mashirika mmbali mbali ya uhifadhi hapa duniani ni kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo na pembe za faru. Tafiti nyingi zimefanyika na mengi yameandikwa kuhusiana na mada hii ya ujangili na biashara ya meno ya tembo. Ukweli ni kwamba tatizo limekuwa kubwa sana kwa nchi moja na hata kwa dunia kulitatua kwa njia rahisi, sasa limekuwa ni janga kubwa kwa dunia.
Pamoja na hali hiyo kuendelea duniani, bado kuna nchi ambazo kwa mujibu wa tafiti na majarida yaliyoandikwa katika ripoti hii inaonyesha kushamiri na kuenea kwa biashara hii, nchi ya Cambodia ni nchi inayotajwa sana kuwa kinara katika kusaidia sana kukua na kuenea kwa biashara ya meno ya tembo na pembe za faru, ngoja tuangalia uchambuzi wa makala moja iliyoandikwa na Thomas Gray na wenzake kuhusiana na nchi ya Cambodia kujihusisha na biashara hii haramu.
Ili kupambana na usafirishaji, biashara ya meno ya tembo na pembe za faru kunahitajika juhudi za makusudi ili kukabiliana na changamoto hii, pia utekelezaji wa sheria zilizopo ni njia muhimu ya kupambana na hali hii inayoendelea kumaliza wanyamapori wetu kutoka katika bara la Asia na Afika.
Tangu mwaka 2011 kumekuwa na matukio mbali mbali ya ukamataji wa nyara za meno ya tembo, Loxodonta Africana zaidi ya 15 na pia matukio sita ya ukamataji wa pembe za faru katika nchi ya Cambodia, pia inaonyesha kuwa nyara 24 za tembo na faru zilizokamatwa zimeripotiwa kutoka katika nchi mbali mbali na kufika Cambodia kama kituo na sehemu ya usafirishaji haramu wa nyara hizo.
Kwa mantiki hii ni kwamba nchi ya Cambodia imekuwa ndio sehemu muhimu ya kupokea nyara kutoka katika nchi za Afrika na Asia na huzisafirisha kwenda nchi nyingne ambazo zina uhitaji wa baidhaa hzio, nchi kama China, na miji yake maarufu hupokea kiasi kikubwa cha shehena ya nyara za meno ya tembo na pembe za faru kwa ajili ya shughuli mbali mbali walizonazo. Hivyo bandari na viwanja vya ndege vya Cambodia hutumika kama sehemu muhimu ya kupokea na kusafirisha bidhaa na nyara za wanyamapori hasa tembo na faru.
Kasi cha tani 1.35 kilishikiliwa huko Ho chi Mnh moja ya jiji ma arufu nchini Vietnam, taarifa zinaonyesha kuwa shehena hiyo ya meno ya tembo ilitoka Afrika magharibi kupitia Cambodia na kufika Vietnam, pia mwaka huo huo 2017 Oktoba kiasi cha sehena ya pembe 8 na meno ya tembo yenye uzito usiojulikana ilikamatwa katika uwanja wa ndege wa Bankok, ikiwa inatoka Zambia lakini ilipitia Cambodia.
Taarifa za utafiti zinaonyesha kiasi cha tani 13 za meno ya tembo na pembe za faru zenye uzito wa kilogramu 124 ambacho kwa mujibu wa taarifa hizi ni kiasi kikubwa sana kuwahi kukamatwa kwa mwaka 2016. Hali hii ndio inayopelekea nchi ya Cambodia kuwa nchi ya pili duniani kutiliwa shaka katika kujihusisha na biashara ya pembe za faru na meno ya tembo. Hii ni kwa mujibu wa Mfumo wa Taarifa ya Biashara ya Tembo (Elephant Trade Information System, ETIS).
Kiasi kikubwa cha shehena inayokamatwa na mamlaka za usimamizi huko Cambodia zinatokea kwenye viwanja vikubwa viwili ya ndege kwenye miji miwili, mji mkuu wa kibiashara wa Phnon Penh na Siem Reap ambao ni mji maarufu na pia ni njia kubwa ambayo hutumiwa zaidi na watalii wanaokuja kutalii nchini Cambodia. Pia inaonyesha kiasi kikubwa zaidi cha shehena ya pembe za faru kukamatwa nchini Cambodia hivi karibuni Novemba 2016, zenye uzani wa kilogramu 35.
Taarifa za kina zinaeleza kuwa pembe na meno haya zinatoka katika nchi sita za Afrika. Nchi hizo ambazo zimetajwa kuwa ni sehemu ambazo nyara hizi zimetoka ni Angola, Kenya, Msumbiji, Namibia, Afrika ya Kusini na Uganda. Hadi shehena hiyo kufikia Cambodia zilipita kwenye viwanja vya ndege vya nchi mbali mbali na baadhi ya bandari na viwanja vya ndege vilivyotumika zaidi ni Addis Ababa, Bangkok, Doha, Dubai, Singapure, Seoul, hivyo ni viwanja vya ndege na vituo ambavyo hutumika katika usafirishaji haramu wa meno ye tembo na pembe za faru kabla ya kufika Cambodia.
Aidha katika bandari kuu ya Preah Sihanoukivile nchini Cambodia shehena zenye uzani wa kilogramu 600 ambazo ni meno ghafi ya tembo zilishikiliwa na taarifa zinasema kuwa zimetoka katika nchi ya Msumbiji zikiwa zimefichwa kwenye shehena ya mahindi, na pia kiasi cha uzani wa kilogramu 3000 za meno ya tembo zilishikiliwa zikiwa zinatoka nchini Kenya, zilipitia Malasia zikiwa zimesafirishwa pamoja na maharage hadi kufika katika bandari kuu ya Cambodia hii ni kwa mujibu wa taarifa za Agasti 2016 na Mai 2014.
Katika bandari hii ya Cambodia, matukio mengi sana ya usafirishaji wa nyara kutoka nchi za Kenya hupitia hapa. Kuna taarifa za mwaka 2016, zinazoeleza namna bandari ya Kenya na bandari ya Cambodia zinavyojihusisha na usafirishaji wa nyara za wanyamapori. Kwa mfano Disemba mwaka 2016 zaidi ya kilo 1300 za meno ya tembo, mfuvu 10 ya paka wakubwa, mifupa yenye uzani wa kilo 82 na magmba (scales) ya Kakakuona yenye uzani wa kilo 137, yalishikiliwa huko Phnon Phenh huko Cambodia yakiwa yemefichwa kwenye uwazi ulio katika magogo ya mbao yakitokea Msumbiji.
Hali hii inaonyesha ni kwa namna gani nchi ya Cambodia ilivyo kitovu cha biashara hii ya nyara za tembo na faru, inasemekana pia hata wavietnamu na Wachina huja kufanya shughuli zao Cambodia kwa ajili ya urahisi na ni sehemu ambayo hupokea shehena za nyara kutoka katika nchi mbali mbali duniani, Afrika ndio ikiwa kinara mkuu, kwasababu nyara nyingi za wanyamapori zilizopo kwenye mizunguko ya kibiashara huko Cambodia hutokea katika nchi za Afrika.
Mwandishi wa makala hii katika jarida la TRAFFIC Bulletin, anamalizia makala yake kwa kuwa na wasi wasi kuwa endapo hali ya mambo itabakia kama ilivyo sasa, nchi ya Cambodia itakuwa zaidi ya hapo na itatumika kama sehemu kuu inayohusika na usambazaji wa nyara za tembo na faru kwenda sehemu nyingine zenye mahitaji ya nyara hizo kwa njia rahisi. Mfumo wa usimamizi na ukaguzi katika maeneo nyeti ya usafirishaji kama vile viwanja vya ndege na bandari uko dhaifu sana na unatoa mwanya kwa biashara hii haramu kushamiri nchini humo.
Hali ya mambo inaweza kubadilika endapo Cambodia itahitaji msaada wa kupambana na ujangili huu uliokithiri kwenye nchi yao. Mashirika mengi ya uhifadhi yapo tayari kusaidia hali hii isiendelee kuwa mbaya, maana kadri siku zinavyoenda mtumizi ya nyara hizi yanazidi kuongezeka hali ambayo inapelekea kupungua kwa wanyamapori hawa katika maeneo yao. Tushirikiane katika kupambana na ujangili ili kuokoa wanyama hawa wenye thamani kubwa kwa kizazi chetu na vizazi vingi vijavyo.
- ALTERNATIVELY EFFECTIVE: A CONFERENCE ON SUBSTITUTES TO BEAR BILE IN TRADITIONAL CHINESE MEDICINE IN MALAYSIA
Matumizi ya sehemu za miili na viungo vya wanyamapori kwa ajili ya dawa za asili limekuwa ni jambo la muda mrefu kwenye nchi za Asia hasa China, wanyamapori mbali mbali wanahusishwa na matumizi ya dawa za asili kwa ajili ya kutibu magojwa mbali mbali kwenye mwili wa binadamu. Tulizoea kusikia meno ya tembo na pembe za faru kutumika kama dawa za asili kutibu magonjwa mbali mbali, na sasa mnyama mwingine ameingia kwenye orodha ya wanyamapori muhimu ambao wanauliwa kila kukicha kwa ajili ya matumizi ya dawa za asili.
Sun Bear, Helarctus malayanus, ni mnyama anayewindwa kikatili katika nchi ya Malasia kwa sababu ya umuhimu wake kutibu baadhi ya magonjwa yanayowasumbua watu. Katika makala iliyoandikwa na Latita Gomez, katika jarida la Traffic bulletin lililotoka mapema Oktoba mwaka 2017 inaelezea kwa kina jinsi ambavyo wanyamapori hawa wanakabiliwa na hali mbaya ya baadaye kutokana na ujangili uliokithiri dhidi ya wanyamapori hawa, sababu kuu ya wanyama hawa kuuwawa ni Imani waliyonayo kwamba “nyongo” (bile) yake ni moja ya dawa muhimu za asili kutibu maradhi. Viungo na sehemu za miili ya wanyama hawa inaripotiwa na jarida hili kuonekana zikitumika sehemu mbali mbali za Asia.
Katika uchunguzi uliofanywa na jarida la Traffic mwaka 2012 nchini Malasia unaonyesha kabisa 48% ya biashara ya nyongo ya sun bear inayoendelea kufanyika katika maduka ya kuuza dawa za asili nchini China, wanafanya biashara hiyo kwa uwazi na bila wasiwasi wowote kwa sababu ni kama vile imehalalishwa kuuzwa. Wachambuzi wa maswala haya wanaendelea kusema kuwa kiasi cha 60% ya viungo vya wanyama hawa hupatikana kutoka sehemu za chini kabisa ambazo ndio kwenye maeneo au makazi ya wanyama hawa, jambo ambalo linahatarisha idadi yao kwenye hifadhi zao. Pia inaonyesha kwa taarifa za mwaka 2010 hadi 2011, katika nchi 17 ambazo zilifanyiwa utafiti na Traffic, nchi ya Malasia ndio inaonekana kinara wa ujangili wa wanyamapori hawa.
Licha ya ukali wa sheria ya uhifadhi wa wanyamapori hawa, na pia katika nchi ya Malasia bado kuna idadi kubwa ya wanyama hawa wanauwawa, inakadiriwa kuwa kwa takwimu za mwaka 2015 hadi machi 2017 taarifa za jarida hili zinaonyesha sun bear 10 walikuwa wanauwawa. Kutokana na tamaa ya fedha na Imani dhidi ya matumizi ya dawa za asili imepelekea uwindaji kuzidi kushika kasi katika nchi ya Malasia, matumizi mbali mbali ya silaha kama vile mitego ya waya, bunduki na mikuki inatumika kuwawinda wanyamapori hawa kwa sababu hutumika kama dawa za asili.
Kutokana na hali hiyo inayowakabili wanyamapori hawa, nchi ya Malasia iliamua kuchukua hatua za dharura na kuitisha mkutano na wadau wote wanaohusika na masuala ya dawa za kifamasia na dawa za asili kutoka sehemu mbali mbali duniani ambako wanyamapori hawa huwindwa kwa matumizi ya dawa za asili, ili kwa pamoja waje na mkakati mzuri ambao utapunguza mauaji ya sun bear kwa ajili ya dawa za kienyeji au dawa za aili. Jambo ambalo walilifanya mapema na kuandaa kongamano waliloliita “Alternative Effective”, namna nyingine bora zaidi ya kubadili matumizi ya nyongo na viungo vya sun bear kutibu maradhi ambayo ndio sababu ya ujangili wa sun bear.
Hakika, naamini kwa machache kati ya mengi yaliyopo kwenye makala hii umepata mwanga wa namna hali ya mambo inavyokwenda kwenye masuala ya uhifadhi wa wanyamapori katika nchi za wenzetu. Hii ni ishara tosha kwetu kufahamu kama hatua za makusudi hazitachuuliwa basi tutapoteza wanyamapori wetu walio wa thamani kwa ajili ya tamaa za watu wachache.
Wanyamapori sasa wana matumizi mengi kwenye nchi za wenzetu, matumizi ambayo ni kinyume na asili kabisa, hivyo basi mambo yanayoendelea katika nchi za wenzetu yatufanye tufikiri na kujua jambo kama hilo linaweza kutokea kwa wanyamapori na maliasili zetu, inaweza isiwe tena tembo na faru, lakini inaweza ikaenda kwenye wanyamapori wengine ambao uwepo wao porini ni muhimu kwenye ikolojia na mfumo mzima wa maisha ya viumbe hai hapa duniani.
Nakushukuru sana Rafiki kwa kusoma makala hii hadi mwisho, naamini umepata mwanga kwenye masuala haya ya uhifadhi wa maliasili zetu. Karibu tuendelee kujifunza zaidi kwenye makala ijayo hapa hapa kwenye mtandao wako wa Wildlife Tanzania. Pia usiache kuwashirikisha wengingi haya uliyojifunza hapa.
Hillary Mrosso
+255 683 862 481
www.mtalaam.net/wildlifetanzania