Ndugu msomaji wa makala hizi za wanyamapori uhali gani? Karibu katika mfululizo wa makala zetu kuhusu NYOKA aina ya SWILA. Leo tunaendelea na mfululizo wa makala zetu kuhusu nyoka jamii ya swila kama kawaida. Katika makala ya leo nakuletea aina nyingine ya swila ambaye anaitwa SWILA SHINGO NYEUSI (BLACK-NECKED SPITTING COBRA) ambae kwa jina la kisayansi hujulikana kama NAJA NIGRICOLLIS. Swila hawa wapo wa aina mbili na wote tutakwenda kuona namna ya kuwatofautisha.
Jina la swila ahwa limetokana na rangi nyeusi katika shingo ambayo ni rahisi kuwatofautisha na swila wengine lakini pia ni miongoni mwa swila ambao hurusha sumu kama njia ya kujihami pale wanapo hisi wanaweza kudhuriwa na maadui au binaadamu. Na sasa moja kwa moja tujikite katika kuwafahamu zaidi swila hawa ambao nao ni miongoni mwa swila hatari pia. Swila wa Misri (Egyptian Cobra): Nyoka Mwenye Sumu Inayoua Haraka Zaidi
JINSI YA KUWATAMBUA SWILA SHINGO NYEUSI
Hapa Afrika Mashariki nyoka hawa wapo aina mbili kutokana na mpangilio wa rangi katika miili yao. Aina ya kwanza wana rangi ya kahawia au zaituni ambayo imepauka kwa chini huku shingoni wakiwa na miraba yenye rangi ya kahawia. Aina ya pili wana rangi nyeusi, kijivu au kahawia iliyo kolea zaid mithili ya kufanana na wekundu na mraba mmoja au zaidi wenye rangi ya pinki maeneo ya shingoni.
Katika jamii hii ya swila kuna wengine huwa na rangi nyeusi kichwani na shingoni huku sehemu ya mwili ikiwa na rangi ya kijivu. Rangi nyeusi shingoni ndio kielelezo kikubwa katika kuwatambua swila hawa.
Wana vichwa vipana, miili yenye umbo la bomba huku magamba yao yakiwa nyororo zaidi. Wana mikia mirefu ambayo huchukuwa asilimia 15-20 ya urefu wote wa miili yao. Mfahamu Swila Msitu (Forest Cobra): Nyoka Mwenye Sumu Hatari Sana
Kwa wale wenye rangi nyeusi au kijivu huwa wana safu za magamba zipatazo 17-25 sehemu ya kiwiliwili na mara nyingi hawa huwa na urefu usiozidi mita 2 (wastani wa mita 1-1.5). Watoto huwa na rangi ya kijivu huku kichwa na shingo vikiwa na rangi nyeusi. Rangi hii ya kijivu kwa watoto huendelea kuwepo mpaka wanapofikisha urefu wa mita moja na zaidi.
Kwa baadhi ya maeneo hapa Tanzania swila hawa huwa na rangi nyeusi ambayo imeunganika moja kwa moja toka kichwani hadi shingoni bila kuwa na muingiliano wa rangi nyingine hapo katikatio ya kichwa na shingo.
Kwa wale wenye rangi ya kahawia au zaituni pia huwa na safu za magamba kati ya 17-25 sehemu ya kiwiliwili japo wao huwa na urefu mpaka mita 2.7 (wastani wa mita 1.3-2). Hawa huwa ni wakubwa zaidi na wana vichwa vipana na vikubwa zaidi kulijo wale wenye rangi nyeusi.
Kuna baadhi ya swila hawa huwa ni vigumu sana kuwatofautisha na swila wa Misri hasa kutokana na maumbile yao na mpangilio wa rangi katika miili yao. Njia pekee ya kuwatofauytisha kwa haraka swila shingo nyeusi na swila wa Misri ni uwepo wa magamba chini ya macho kwa swila wa MIsri ambayo kwa swila shingo nyeusi hakuna magamba hayo.
Japo kuna spishi mbali mbali za swila shingo nyeusi, lakini wastani wa ukubwa wa jamii hii ya swila huwa na wastani wa urefu kati ya mita 1.5-2.5 ambapo ni sawa na wastani wa futi 5-8.
Swila shingo nyeusi (Picha na angolafieldgroup.com)
TABIA ZA SWILA SHINGO NYEUSI
Hawa ni miongoni mwa swila ambao wanarusha sumu kama walivyo swila wa Msumbiji. Wanapo hisi kudhuriwa hujihami kwa kurusha sumu hawa sehemu ya machoni mwa adui ili kumdhuru asiweze kuwashambulia. Wana uwezo wa kurusha sumu hiyo kwa umbali wa mita tatu au zaidi. Mfahamu Nyoka Hatari Zaidi Duniani, Ana Uwezo Mkubwa Sana Wa Kuua Anapouma
Swila hawa huwa wanainua miili yao na kutaka kujua nini kinaendelea kabla ya kujongea mbele haraka. Hii ni sifa inayo watofautisha swila shingo nyeusi na jamii nyingine za swila kama swila wa Misri na swila Msitu ambao wao wanapo tishiwa tu basi hujongea mbele haraka kwa lengo la kushambulia.
Wanapo tishiwa hutanua mashingo yao kama swila wengine. Mashingo yao yanapo tanuka huwa na alama ya kipekee kabisa ambayo huwezi kuiona kwa swila wengine ambayo ni umbo lililo nyooka na lenye alama nyeusi sehemu ya nchani.
Wanapendelea sana kuishi maeneo ya ardhini japo wana uwezo wa kupanda miti na hata pale wanapoamua kumkimbia adui yao huwa wanapanda hata kwenye miamba.
Kwa wakubwa hupendelea kufanya mawindo yao majira ya usiku japo kuna wakati huwa wana wind ahata mchana hasa kwenye maeneo ambayo sio makazi ya watu. Wadogo hupendelea kufanya mawindo majira ya mchana ili kuepuka changamoto kwa swila wakubwa na maadui wengine.
Muda ambao hawafanyi mawindo hupendelea kupumzika kwenye mashimo yaliyo achwa na mchwa, kwenye matundu ya miti na magogo ya zamani zaidi.
Swila shingo nyeusi (Picha na Anima Pictures Archive)
MAENEO WAPATIKANAYO SWILA SHINGO NYEUSI
Swila hawa wanapatikana zaidi maeneo ya ukanda wa pwani, maeneo ya savana yenye ukavu na unyevu nyevu lakini pia maeneo ambayo yana hali ya nusu jangwa. Maeneo haya huwa na muinuko wa chini ya mita 1700 kutoka usawa wa bahari.
Nchi ambazo wanapatikana swila hawa ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, magharibi mwa Afrika mpaka Senegali na Kusini Magharibi mwa Namibia.Mambo Usiyoyajua Kuhusu Tofauti Zilizopo Kati Ya Nyoka Aina Ya Cobra(Fira/Swila) Na Black Mamba(Koboko)
Hapa nchini Tanzania swila shingo nyeusi wanapatikana kwa wingi zaidi maeneo ya Pwani, Kanda ya Kati na Kaskazini. Tafiti zinaonesha kuwa maeneo ya Kusini na Magharibi mwa Tanzania nyoka hawa sio wengi ni nadra sana kuwaona na pengine hawapo katika baadhi ya maeneo kabisa. Japo kuthubitisha hili tafiti nyingi zaidi zinahitajika.
CHAKULA
Swila hawa wanakula vyakula aina mbali mbali kama vyura, ndege, vifaranga wa kuku na mayai pia, jamii nyingine za nyoka na mijusi. Tafiti zinaonesha kuwa kuna wakati wameonekana wakiwinda hata kenge wakubwa na kuwameza. Mara chache sana swila hawa huonekana wakiwinda panya.
KUZALIANA
Mara baada ya kupandana jike hutaga wastani wa mayai kati ya 8-20 yenye ukubwa wa sentimita 2.5-4 ambayo huchukua siku 60-70 mpaka watoto kutoka kwenye mayai. Muda sahihi wa mayai kutoa watoto hutegemea zaidi jotoridi na mgandamizo wa hali ya hewa katika mazingira husika. Jike akisha taga mayai huwa hana usimamizi nayo, huwa anahakikisha anataga mayai sehemu salama kisha huyaacha na watoto hutoka kwenye mayai.
Watoto wanapotoka kwenye mayai huwa na urefu wa kati ya sentimita 20-30(inchi 8-12).MBali na kuwa ni wadogo ila huwa tayari wana sumu na uwezo wa kujilinda wenyewe bila kuwa na usimamizi wa mama na huanza kujitegemea mara tu watokapo kwenye mayai.
SUMU
Swila shingo nyeusi ni miongoni mwa nyoka hatari, pia ambao sumu yao ina madhara makubwa sana kwa binaadamu. Sumu ya swila hawa inaathiri zaidi misuli japo tafiti zinaonesha sumu huathiri pia mfumo wa neva. Dalili za athari ya sumu toka kwa nyoka hawa zinafanana kabisa na zile za sumu toka kwa swila wa Msumbiji ambae makala yake nimesha kuletea hapo nyuma kabla ya makala hii. Mfahamu kwa undani Swila wa Msumbiji na Swila wa Msumbiji: Nyoka Mwenye Sumu Kali Ambaye Watu Wengi Hawamjui
Miongoni mwa dalili za sumu ya swila hawa ni pamoja na kumuangalia mtu sumu kwenye macho endapo atakuwa alirushiwa sumu na swila hawa.
Endapo utataka kujua mengi na kwa undani kuhusu sumu hii basi nikuombe upitie makala ya SWILA WA MSUMBIJI utajifunza mengi kuhusu sumu ya nyoka huyu kwani dalili na athari zake zinafanana.
MWISHO
Nakusihi mpenzi msomaji wa makala hizi kuendelea kufuatilia mfululizo wa makala hizi ili uzidi kujifunza mambo mengi sana kuhusu nyoka jamii ya swila. Katika makala ijayo nitakuwekea mezani spishi nyingine ya swila mpaka pale tutakapo wamaliza swila mwapatikanao Afrika mashariki hususani hapa nchuni Tanzania.
Makala hii imehaririwa na Hillary Mrosso. Kwa maswali, ushauri au maoni kuhusu makala hii usisite kuwasiliana nami,
Sadick Omary Hamisi
Simu; 0714116963
Email; swideeq.so@gmail.com
Instagram; wildlife_articles_tanzania
Facebook; Sadicq Omary Kashushu/Envirocare and wildlife conservation
Tovuti; www.wildlifetanzania.co.tz