Wanyamapori na mazingira yao asili ni uti wa mgongo wa sekta ya utalii nchini Kenya, na pamoja na ukweli huo bado nchi ya Kenya inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa rasilimali hizo kwa sababu mali mbali kama vile ujangili, biashara haramu ya wanyama na mimea mwitu. Wahifadhi na watalamu wa masuala haya ya wanyamapori wanakiri kuwa licha ya kuwa nchi ya Kenya imefunga kabisa biashara ya pembe za faru na meno ya tembo, bado uhalifu wa wanyamapori umekuwa ndio tishio kubwa linalopelekea kupungua na kupotea kwa wanyamapori tangu miaka ya 1970 hadi sasa.

Spishi nyingi za wanyamapori zinazohusishwa sana kwenye biashara hii haramu ni meno ya tembo husafirishwa yakiwa ghafi au yakiwa yameshatengenezwa husafirishwa hadi Asia, ngozi za wanyama pori wanaokula nyama jamii ya paka (cat family) kama vile simba, duma, chui husafirishwa kama viungo au wakiwa hai kwenda nchi za Ulaya, Mashariki ya kati, na Marekani. Reptilia kama vile mijusi, nyoka, vinyonga na kobe husafirishwa sana wakiwa hai, sumu zao au sehemu za viungo vyao kwenda nchi za Ulaya, Marekani na Mashariki ya Kati. Kakakuona nao ni wanyama wanaosafirishwa sana wakiwa hai au magamba yao kwenda nchi za Mashariki na Kusini mwa Asia. Magogo au miti ya (Sandalwood) husafirishwa kama magogo na kufikia nchi za Mashariki ya Asia. Mimea ya Alovera nayo piani miongoni mwa spishi zinazosafirishwa kwa njia haramu kwenda Ulaya na Asia.

Mwelekeo wa ujangili

Nchi ya Kenya ilifuta vibali vyote halali ya uwindaji binafsi mwaka 1973, lakini udhaifu bado ulibakia kwenye sheria ambayo iliwaruhusu viongozi wabadhirifu wa serikali kuuza kwa mnada meno ya tembo yaliyokuwa kwenye chumba huko Mombasa, jambo ambalo lilitoa mwanya kwa biashara haramu ya meno ya tembo kushika hatamu. Kenya ilitangaza kufunga kabisa biashara ya meno ya tembo kutokana na mahitaji ya biashara hiyo kuwa makubwa katika nchi za Asia na Japani. Miaka ya 1970 na 1988 baadhi ya viongozi wa ngazi za juu serikalini walishutumiwa kwa kuuza meno ya tembo.

Nchi ya Kenya iliunda tena uongozi wake uliokuwa unasimamia masuala ya uhifadhi wa wanyamapori mnamo mwaka 1989 na kusababisha kuundwa kwa shirika la kiserikali la huduma za wanyamapori lililojulikana kama Kenya Wildlife Servce (KWS) ambapo pamoja na mambo mengine liliwajibika katika kusimamia na kuangalia kwa karibu wanyamapori, shirika hili kwa mara ya kwanza liliongozwa na mkurugenzi ambaye alikuwa ni mtafiti wa mambo ya kale na pia alikuwa ni muhifadhi wa wanyamapori Richard Leakey.

Chini ya uongozi wa Leakey waliamua kuunda kikosi cha migambo ambao watakuwa na jukumu la ulinzi wa wanyamapori, haikuishia hapo baada tu ya kuunda kikosi hicho cha mgambo kilianza kampeni ya kupinga ujangili iliyopelekea nchi ya Kenya kuchoma shehena yake yote ya meno ya tembo iliyokuwa stoo, yenye thamani ya dola za kimarekani million 3. Kwa kufanya hiyo nchi ya Kenya ilipeleka ujumbe kwa dunia kuwa hawako tayari kuvumilia vitendo vya kijangili thidi ya wanyamapori. Kampeni hiyo ilikuwa na matunda mazuri kwa sababu iliamsha uelewa kwa ngazi zote serikalini na kwa jamii ili kupambana na ujangili.

Kwa kadri dunia inavyoendelea kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kwenye mambo mbali mbali hasa kwenye karne ya 21, njia nyingi za kufanya ujangili ziliingia na kuanza kuzamisha juhudi zote zilizopatikana katika kipindi cha nyuma, kutokana na hali ya watu kuwa masikini, kiwango cha juu cha rushwa na udhaifu uliokuwepo kwenye sheria za wanyamapori halikadhalika mahitaji ya meno ya tembo katika masoko ya nchi za Vietnam na China yalikuwa makubwa sana hivyo mambo hayo yalifungua milango kwa majangili kushamiri sana katika nchi ya Kenya.

Kwa ujumla wake hivi ndio vitu vinavyopelekea ujangili wa meno ya tembo na pembe za faru katika nchi ya Kenya.

  1. Rushwa kwa baadhi ya viongozi wa serikali na wale wa sekta binafsi hasa maeneo ya usafirishaji;
  2. Kuongezeka kwa bei ya meno ya tembo na pembe za faru kwenye masoko haramu inayochochewa na mahitaji kutoka nchi za Mashariki ya Asia.
  • Kupitisha silaha isivyo halali katika maeneo ya mipaka ya nchi ya Kenya na pia kukosekana kwa amani eneo la Kaskazini mwa Kenya;
  1. Urahisi wa usafirishaji wa nyara za wanyamapori na pia urahisi wa majangili kutembea kokote wanakotaka katika mipaka ya Kenya ambayo haina usimamizi makini;
  2. Kupanuka kwa makazi ya watu kwenye maeneo muhimu ya faru na tembo; na
  3. Udhaifu ulipo kwenye sheria za wanyamapori, hasa mtuhumiwa anapokamatwa na nyara.

Kama ripoti hii inavyoonyesha kuwa rushwa kwa viongozi wa serikali na wale wa sekta binafsi ndio kichocheo kikuu cha ujangili na kushamiri kwa biashara haramu ya pembe za faru na meno ya tembo. Jambo hili pia limeonyeshwa kwenye ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu madawa ya kulevya na uhalifu. Kazi kubwa inahitajika sana ili kupambana na hali hii inayomaliza wanyamapori hawa wenye thamani kubwa kwenye maisha na ikolojia nzima ya viumbe hai.

Asante sana kwa kusoma makala hii, naamini umepata picha kubwa ya hali ya mambo yalivyo kwa jirani zetu Kenya. Kumbuka kuwa haya ni machache niliyochambua katika  ripoti hii maarufu iliyotolewa na shirika la TRAFFIC yenye kichwa WILDLIFE PROTECTION AND TRAFFICKING ASSESSMENT IN KENYA iliyoandikwa na Sam Weru.

Karibu tuendelee kujifunza kila siku hapa hapa.

Mchambuzi wa ripoti hii ni;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania