Habari msomaji  wa makala za mtandao huu wa Wildlife Tanzania, kama ilivyo kawaida na lengo la blogu hii ni kutoa maarifa na kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi wa wanyamapori na misitu. Lakini pia kuwa sehemu ambayo watanzania na watu wengine watapata taarifa mbali mbali za vivutio ambavyo vinapatikana Tanzania na kuwahamasisha watanzania kuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi za wanyama na vivutio mbali mbali hapa Tanzania. Jambo hili ndilo linalonivutia zaidi, kuwafikia wengi kwa maarifa haya muhimu. Lakini ili kufanikisha hayo yote lazima tujue utajiri wa maliasili tulio nao unakabiliwa na changamoto nyingi sana ambazo zinahitaji juhudi na mchango wa kila mmoja wetu ili kuzitatua na kuhakikisha usalama wake ili tuzidi kupata manufaa endelevu na manufaa kwa vizazi vijavyo.

Leo katika makala hii nimekuletelea uchambuzi wa ripoti moja inayoonyesha mambo yanayoendelea kwenye maliasili zetu, namna wanyama na mimea yetu inavyopukutika na kuishia kwenye mikono ya watu wachache ambao wanaishi kwenye mataifa makubwa. Katika makala hii utaona jinsi ambavyo meno ya tembo, pembe za faru na bidhaa nyingine ambazo ni nyara za wanyamapori na viumbe hai wengine zinavyovovuka mipaka na kwenda kuwatajirisha matajiri ambao wanaitegemea biashara hii ambayo kwa kiasi kikubwa inaendeshwa kwa njia haramu kabisa. Na kusababisha maelfu ya tembo na faru kutoweka na kuuwawa katika bara la Afrika. Ripoti hii ambayo nimeichambua kwa lengo la kujifunza na kujua yanayoendelea katika dunia hii kuhusu wanyamapori ambao serikali zetu inawalinda kwa gharama kubwa na watu wanajitolea maisha yao kwa ajili ya kulinda na kusimamia maliasili hizi.

Hii ni ripoti ambayo imeandaliwa na shirika la kimataifa lisilo la kiserikali linalojulikana kama Elephant Action League, shirika hili limejikita katika uchunguzi na kufanya tafiti za kina kuhusiana na ujangili na biashara haramu ya meno ya tembo, pembe za faru na wanyamapori kwa ujumla. Ili kubaini wahusika, mitandao yao, njia zao na namna wanavyoendesha biashara hiyo haramu, kukusanya taarifa zote muhimu zin azoonyesha na kudhihirisha kazi zao, kisha kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria sambamba na kuvunja kabisa mitandao yao yote inayorahisisha biashara hii kushamiri.

Hivyo ni shirika lenye watu wenye uwezo mkubwa na watalaamu wabobezi kwenye nyanja za upelelezi na uchunguzi, jambo ambalo limepelekea ripoti hii kuwa na taarifa za kweli na za kina sana ambazo ni ngumu kuzifahamu na kuzipata kirahisi. Taarifa zilizomo ndani ya ripoti hii zimekusanywa kutoka katika kitovu kikuu cha biashara hii na watumizi wakubwa wa meno ya tembo na pembe za faru. Ripoti hii iliyofanyiwa uchunguzi na taarifa kukusanywa kwa muda wa miezi kumi na kukamilika kwa ripoti hii mwishoni mwa mwaka 2015 imepewa kichwa  Blending Ivory, China’s Old Loophole, New Hopes.

Mwishoni mwa mwaka 2014, Elephant Action League, lilidhamiria kufanya utafiti wa kina katika nchi ya China ilituma timu ya watu wenye uwezo ili kujua mienendo na njia zote za biahara hii haramu ya meno ya tembo, hivyo walidhamiria kufanya uchunguzi na upelelezi kwenye masoko, viwanda na hata kwenye maeneo yote yenye viwanda, vinu na stoo za kuhifadhia meno ya tembo. Vile vile kwa mujibu wa ripoti hii inaonyesha kabisa jinsi ambavyo wachunguzi walivyokuwa na muda wa kufanya maohijiano na kuwauliza maswali wateja na wanunuzi wakubwa kwa wadogo wa meno ya tembo huko China. Jambo ambalo lilikuwa lilionyesha bila shaka yoyote kuwa wanunuzi na wafanyabiashara hii nchini China wanafanya kwa uhuru wote na wanapata faida kubwa sana kutokana na biashara hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu zilizomo ndani ya ripoti inaonyesha zaida ya tembo 25,000 hadi 50,000 huuwawa kila mwaka kwa ujangili katika bara la Afrika. Kwa takwimu hizi ambazo zinaonyesha idadi kubwa ya tembo kuuwawa kwa njia ya ujangili inatishia sana uwezekano wa wanyama hawa kuendelea kuwepo hapa duniani kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa. Kwa vyoyote vile iwe idadi hiyo inapungua au inakaribia kufikia takwimu hizo kwa mwaka, ukweli ni kwamba idadi ya tembo wanaokufa kwa ujangili ni kubwa kuliko tembo wanaozaliwa. Hii ni baada ya Dr. Wasser ambaye ni mtalaamu wa masuala ya DNA kutoaka katika Chuo Kikuu cha Wshington kufanya utafiti ili kugundua meno ya tembo yanayongia China yanatoka wapi na ni ya mwaka gani, baada ya utafiti huo inaonyesha idadi kubwa sana ambayo ni zaidi ya tembo 50,000 wanatoka katika bara la Afrika kila mwaka.

Pia alikwenda mabali zaidi kutambua sehemu ambayo tembo hao walio uwawa kikatili na majingili wametoka wapi na alihitimisha kwa kuonyesha idadi kubwa ya tembo kiasi asilimia 85 ya meno ya tembo wa msituni (forest  elephants)  yaliyo kamatwa mwaka 2006 hadi 2014 yalitoka katika Afrika ya Kati katika hifadi ya Tridom ambayo inazunguka Kaskazini Mashariki mwa Gaboni na Kaskazini Magharibi inapakana na Jamhuri ya Kongo na Kusini Mashariki imepakana na  Kameruni, na karibu na hifadhi ya Akiba ya Jamhuri ya Kati. Aidha, katika ugunduzi huo wa kitalaamu uliofanywa na mtalaamu huyu ulibaini zaidi ya asilimia 85 ya tembo wa savana waliokamatwa mwaka 2006  hadi 2016 walitokea Afrka Mashariki katika pori la Akiba la Selous Kusini Mashariki mwa Tanzania na katika pori la Akiba la Niassa (Niassa Game Reserve) Kaskazini mwa Zimbwabwe.

Kwa utafiti huu usio na shaka wa unaonyesha kiini kikuu au sehemu kuu ambayo ni kitovu kwa ujangili wa tembo ni Afrika ya Kati na Afrika Mashariki, Tanzania ikiwa ndio kitovu kikuu cha ujangili kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki.

Ripoti hii inaonyesha jinsi ambavyo mtandao wa ujangili na njia za usafirishaji na watu wanaohusika ulivyo mgumu kueleweka (complex) kwa urahisi kutokana na jinsi ambavyo mtandao huo unahusisha hadi watu ambao huwezi kuwadhania kuwa wanaweza kujihusisha na biashara hiyo haramu ya meno na pembe za faru pia njia ambazo hutumia kusafirisha kutoka katika bara la Afrika na kuwafikia walengwa katika bara la Asia, ambao ni China, Vietnam, Philipines na Malasia. Kwasababu sehemu kubwa ya meno ya tembo hutokea Tanzania na nchi nyingine za Afrika mashariki, sehemu kuu ya kusafirishia shehena hiyo ya meno ya tembo imekuwa ni kwa njia ya bandari na viwanja vya ndege. Kwa mujibu wa ripoti hii na ripoti nyingi zinazohusiha biashara haramu, bandari kuu ambazo hutumika zaidi kwa ajili ya kusafirisha bidhaa hizi hadi nchi za Asia ni bandari ya Mombasa na bandari ya Dare es salaam kwa upande wa Afrika Mashariki na bandari ya Durban kwa upande wa Afrika ya Kusini.

Na kama tunavyojua sehemu hizi za usafirishaji kama viwanja vya ndege na bandari huwa na usimamizi mkubwa wa mamlaka za serikali na polisi. Lakini sehemu hizi zimekuwa na udhaifu mkubwa sana ikiwa ni pamoja na manya mikubwa ya rushwa, hongo na njia mbovu za ukakugzi wa makontena na mizigo mingine. Na kwa mujibu wa ripoti hii kiasi kikubwa cha fedha na gharama nyingine hulipwa kama rushwa na hongo ili wasimamizi waruhusu usafirishwaji wa bidhaa hizi kwa walengwa. Ili kufanikisha adhma yao usafirishaji wa meno ya tembo na vitu vingine haramu, hutumia mawakala na watu hatari wanaojihusisha na biashara haramu za madawa ya kulevya, usafirishaji wa watu na watu wanaojihusisha na kusimamia vikundi vya kigaidi.

Soko la meno ya tembo China, meno ya tembo yanapofika katika nchi ya china kupitia njia mbali mbali hulipiwa kibali na kusambazwa kwa wauzaji wakubwa na wadogo ambao hufanya biashara hiyo kwa vibali vilivyotolewa na serikali ya China. Kwa jinsi biashara hii inavyoendeshwa katika nchi ya China ni ngumu kutambua uwepo wa biashara halali ya meno ya tembo na biashara isiyo halali. Hii ni kutokana na kibali cha kufanya biashara hii kilichoiruhusu China kuendelea na masoko ya ndani ya meno ya tembo bila kuagiza bidhaa nyingine kutoka nchi nyingine.

Kwa mujibu wa tathimini ya ripoti hii inaonyesha idadi kubwa ya mauaji ya tembo katika kipindi hiki ni makubwa mno, ukiachilia mauaji ya kwanza ya tembo ambayop yaliripotiwa kuwa mauaji makubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya ujangili, ambapo ripoti inaonyesha zaidi ya tembo laki moja (100,000) walipoteza maisha kwa shuighuli za ujangili katika bara la Afrika. Mauaji hayo ambayo yanaripotiwa kutokea kwenye miaka ya 1970 na 1980, yalitoa kiashiri kikubwa sana kinachoonyesha kutoweka kwa wanyama hawa kama juhudi za makusudi hazitachukuliwa. Hadi ilipofika mwaka 1989 CITES wakaamua kuchukua maamuzi ya kufungia biashara ya meneo ya tembo na usafirishaji wa bidhaa hizo. Katika tamko lililotolewa na CITES katika kipindi hicho China tayari ilikuwa na hazina kubwa sana ya meno ya tembo kwenye stoo zake kubwa, inakadiriwa kuwa ni zaidi ya tani 670 za meno ya tembo, kutokana na hali hiyo China iliruhusiwa kuendelea kuuza meno hayo kwenye masoko yake ya ndani.

 Soma Makala Hiii Uifahamu Kwa  Kina  CITES

China ilitegemewa kumaliza kabisa hazina yake ya meno ya tembo ilipofika mwaka 2004. Kutokana na sheria za CITES haikuruhusiwa kuagiza nje kiasi chochote cha meno ya tembo. Lakini kwa uchunguzi uliofanywa na timu ya Elephant Action League inaonyesha bado kuna kiasi kikubwa zaidi cha meno ya tembo, jambo ambalo linaiweka China kwenye ushiriki wa biashara haramu ingawa ilizuiliwa. Kwa kuwa ni ngumu kutambua meno ya tembo yaliyo halali na yale yasiyo halali hii imekuwa ni njia ya kuinufaisha sana China hasa katika uagizaji na ununuzi wa meno ya tembo kutoka sehemu mbali mbali kwa ajili ya kuuza kwenye masoko yake ya ndani na nchi nyingine jirani kama Vietinamu.

Unaweza kujiuliza ni kitu gani kinafanya biashara ya meno ya tembo kushamiri na kuwa na uhitaji mkubwa kwa China? vipo vitu vingi vinavyochangia hali hii moja ni kwamba taifa la China ni taifa lenye idadi kubwa sana ya watu, na kwa miaka michache ya nyuma kabla ya kukamilika kwa ripoti hii taifa la China limekua na ukuaji mzuri na mkubwa wa uchumi kwa wananchi wenye uchumi wa kati, ambao kwa mujibu wa taarifa zilizomo ndani ya ripoti hii inaonyesha kundi hili la watu kufanikiwa zaidi na kwa kuwa ni wengi hivyo hata mahitaji ya meno ya tembo kwa ajili ya matumizi yao binafsi ilikuwa ni kubwa. Hii ndio ilipelekea kuhitajika kwa meno ya tembo huko China kwa gharama yoyote. Jambo jingine kubwa lililosababisha kushamiri kwa biashara hii ndani ya taifa la China ni maamuzi ya CITES kuamua na kuruhusu baadhi ya nchi kama Botwsana, Namibia, Afrika ya Kusini na Zimbabwe kuuza hazina yao ya meno ya tembo tani 102 ziliuzwa kwa nchi ya China na Japani.

Kushamiri kwa biashara hii ndani ya taifa la China ni kutokana na maamuzi na udhaifu tulio nao kwenye sekta mbali mbali kwenye nchi zetu. Mamlaka za usimamizi na ukaguzi, rushwa na tamaa ya fedha na utajiri ndio vinagarimu sana wanyamapori wetu. Mpaka sasa ni ngumu kujua kama bishara ya meno ya tembo inayoendelea huko China na sehemu nyingine inafanyika kihalali kwa kufuata makubaliano ya CITES. Kama nilivyochambua kwa uchache baadhi ya mambo yaliyopo kwenye ripoti hii, inaonyesha kabisa kama mambo yataendelea kuachwa kama yalivyo hali hii itazidi kuwa mbaya kwa wanyama wetu ambao wanauwawa kikatili bila makosa yoyote.

Nilitaka kuendelea kuandika uchambuzi huu lakini nimeona makala itakuwa ndefu sana, hivyo nitaendelea na uchambuzi huu kwenye makala nyingine inayoelezae mambo mengi ambayo sijayataja kwenye makala hii. Kwa ufahamu huu na kujua jinsi mambo yanavyoenda katika hifadhi zetu na namna mataifa na wafanyabiashara wa meno ya tembo wanavyomezea mate tembo wetu bila hata kufikiri kuna siku wanyama hawa wataisha kabisa, wameamua kujinufaisha wenyewe na kuacha watu wanaotoa sadaka maisha yao na wanaolipa gharama kubwa ya kuwahifadhi na kuishi na wanyama hawa bila faida yopyote. Ninaomba serikali zetu, umoja wa mataifa, mashirika na wadau wote wa sekta hii popote duniani, pamoja na  kila mtu kupinga na kuchukua hatua ili kuwabaini wanaojihusisha na biashara hii ya ujangili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Maisha Ya Wanyamapori Yapo Mikononi Mwetu Wenyewe.

Asante sana!

Hillary Mrosso

+255 683 862 481/ +255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania