Kwa muda wote ambao binadamu wamedumu katika uso wa dunia, tembo pia walikuwepo, lakini sasa tumeingia katika mshtuko mkubwa sana, tunaweza tukawa katika hatua za mwisho kabisa za kuwatowesha milele. Katika maeneo ya savanna ya bara la Afrika ambako ndio viumbe hawa wameishi kwa milenia yote, idadi yao imepungua kwa kiasi kikubwa sana karibu mara tatu ya tembo wote kuanzia mwaka 2007- 2014. Katika misitu ya Afrika ya kati, wamepungua kwa asilimia 66, kati ya mwaka 2008 – 2016. Kila siku tembo wengine 55 huuwawa. Na nyuma ya janga hili kuna kitu kimoja tu ndio hupelekea haya yote; uhitaji wa meno ya tembo.

Mwishowe, serikali zimeamka na kuanza kuchukua hatua, kuzuia wanaoua tembo kwa ajili ya masoko ya meno ya tembo duniani kote, na kutambua kuwa uwindaji halali wa tembo ndio huchochea uhitaji wa mweno ya tembo, na pia uwindaji halali wa tembo ndio unaofunika uwindaji haramu au ujangili wa tembo kutofahamika. China wamechukua hatua kuzuia meno ya tembo na pia kufunga biashara yake ya meno ya tembo. Pia Hon Kong wamepitisha sheria ya kufanya hiyo. Marekani nao wamechukua hatua ya kufunga karibia kila biashara za meno ya tembo kwenye maeneo yao, Umoja wa Ulaya nao wamefuta utaratibu huo wa kufunga biashara hizo haramu ambazo zinachochea mauaji ya tembo.

Licha ya kuwa ni wahisani wa kubwa wa uhifadhi wa tembo katika bara la Afrika, bado Umoja wa Ulaya una bishara nzuri sana ya meno ya tembo iliyoshamiri katika masoko ya ndani. Ndani ya umoja wa Ulaya ni halali kufanya biashara bila zuio lolote, ya vitu vilivyotengenezwa na meno za tembo ambavyoo yamepatikana kabla ya mwaka 1947. Kwa mara ya kwanza biashara hii imegundulika kuwa inafunika biashara zote haramu zinazoendelea katika umoja huu wa Ulaya. Kumekuwa na uvumi wa taarifa kuwa nchi za Ulaya zinauza na kununua mapambo ya kale ambayo yametengenezwa na meno ya tembo, lakini biashara haramu inajumuisha mapambo hayo yaliyotengenezwa na meno ya tembo ambao wameuwawa katika miaka ya hivi kabirbuni.

Katika kujifunza na kutafiti bidhaa mbali mbali zilizotengenezwa na meno ya tembo, tume ya umoja wa Ulaya ilibaini yafuatayo;

Robo tatu (74.3%) ya meno ya tembo yaliyofanyiwa utafiti yamegundulika kuwa ni mapambo kale yaliyotengezwa na meno ya tembo ambayo yalipatikana kwa njia haramu.

Moja ya tano (19%) kati ya vipande vya meno ya tembo vilivyotafitiwa ilionekana kuwa vimetoka kwa tembo ambao waliishi miaka ya 1990 na 2000 waliuwawa baada ya dunia kupitisha sheria ya kuzuia ujangili.

Hili ndio tatizo la umoja wa Ulaya, kwamba kila nchi ambayo ilichunguzwa na kutafitiwa iligudulika wanajihusisha na biashara hii haramu kwa mwavuli wa kufanya biasharaa halali.

Majaribio ya hivi karibuni ya meno ya tembo yalifanyika baada ya mwaka 2010.

Hii ni wazi kuwa umoja wa Ulaya ulikuwa haujasimamia ipasavyo sheria za meno ya tembo, na biashara haramu za meno ya tembo kufanyika kwa uwazi katika maduka na kwa njia ya mtandao karibu kila sehemu ya nchi hizo. Tume ya Ulaya inapitia tena mazuio ya Umoja wa Ulaya kuhusu biashara ya meno ya tembo kama yanaendana na kile wanachokitaka.

Katiaka ripoti hii kila kitu kimeelezwa kuhusiana na mwafaka huo na hatua za kuchukua. Kuhakikisha tembo wanahifadhiwa na kulindwa, tume inatakiwa kuhakikisha kuwa mianya yote ya biashara haramu inafungwa na pia bidhaa zote za kale zilizotengenezwa na maeno ya tembo zinafungiwa kabisa, pia kuzuia kabisa uagizaji wa meno ya tembo kutoka Ulaya na kufunga kabisa masoko ya ndani ya meno ghafi ya tembo. Kwa kufanya hivyo ndio njia pekee kutunza hadhi Ulaya kama kiongozi katika mapambano haya dhidi ya ujangili wa tembo Afrika.

Radiocarbon testing study

Kwa siku za hivi karibuni umoja wa Ulaya ulisema kuwa hakuna ushahidi wowote kuwa vifaa na bidhaa za mapambo ya kale yaliyotengenezwa na maeno ya tembo kuwa yanachochea biashara haramu ya meno ya tembo na hata ujangili. Ili kupatikane ushaidi kwamba nchi za umoja wa Ulaya zinazojihusisha na biashara ya visanamu na mapambo ya vitu vya kale ambavyo vimetengenezwa na meno ya tembo, kuwa biashara hiyo ni mwavuli wa biashara haramu ya meno ya tembo, na pia hakuana uhakika kuwa meno ya tembo yaliyotengeneza mapambo hayo kuwa ni ya zamani au ya kabla ya miaka 1947.

Ili ukweli ujulikane, hatua za makusudi zilichukuliwa ambapo ilipendekezwa kuwa utafiti wa kisayansi ufanyike ili kubaini ukweli wa mambo, na hapo ndipo vipande 109 vya meno ya tembo kutoka katika nchi mbali mbali za umoja wa Ulaya vilinunuliwa, na shirika la kitafiti la Elephant Action League walitoa msaada mkubwa kufanikisha upatikanaji wa vipande hivyo kwa ajili ya utafiti.

Bidhaa zote zilizonunuliwa kwa ajili ya utafiti zilichaguliwa kwa vigezo vya kuangali vyeti vya biashara hiyo, miaka, bei na sehemu zilipotoka bidhaa hizo kuhakikisha kila bidhaa muhimu zinazohitajika kwa utafiti zinakuwepo. Haijalishi bidhaa hizo zimetangazwa kutengenezewa na maeno ya tembo yaliyopatikana kabla ya 1947 au la. Baada ya hapo zilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi katika maabara ya radiocarbon iliyopo katika chuo kikuuu cha Oxford nchini uingereza kwa ajili ya kufanyiwa utafiti.

Matokeo ya utafiti huo ulionyesha bila shaka yoyote kuwa bidhaa zote za mapambo zilitengenezwa na meno ya tembo ambayo yaliuzwa katika nchi za Ulaya yalipatikana kwa njia haramu na sio kweli kuwa meno hayo ya tembo yalipatikana kabla ya mwaka 1947 kama wanavyosema wanaojihusisha na biashara hiyo.

Na pia utafiti ulibaini kuwa bidhaa za meno ya tembo zilizokuwa zinauzwa kwenye masoko na kwenye maduka mbali mbali katika nchi za umoja wa Ulaya, ni tembo ambao wameuwawa miaka ya hivi karibuni na hakuna cheti chochote cha uhalali wa kufanya biashara hiyo kwa wafanyabiashara hii ya meno ya tembo, wenyewe walikuwa wanasema tu kwa mdomo kuwa bidhaa zao au meno hayo ya tembo yemepatikana kabla ya mwaka 1947.

Hivyo kwa utafiti huu ulionyesha kwenye baadhi ya nchi zilizochunguzwa kuwa bidhaa zote zilizokuwa zinauzwa zilikuwa ni bidhaa haramu, nchi hizo ni Bulgaria, Uhispania, Italia, Ufaransa na Uholanzi, tafiti zimebainisha kuwa bidhaa zilizotengenezwa na meno ya tembo zilikuwa sio halali kabisa, kwasababu zilionyesha tembo walioishi baada ya mwaka 1947.

Masoko ya meno ya tembo yaliyopo ulaya ambayo hujawahi kuyasikia kabisa

Umoja wa Ulaya una sheria kwamba bidhaa ambazo zimetengenezwa na meno ya tembo au meno ya tembo yaliyochakatwa ambayo yalipatikana kabla ya mwaka 1947 yanaweza kufanyiwa biashara ndani ya umoja wa Ulaya bila mazuio ya aina yoyote. Na pia kuna sheria kuwa, meno ya tembo ambayo yamezalishwa kati ya mwaka 1947 hadi 1990 yanaweza kufanyiwa biashara katika umoja wa Ulaya kwa kibali maalumu au cheti kilichotolewa na serikali. Na meno ya tembo ambayo yamepatikana baada ya mwaka 1990, yalifungiwa kabisa na hakuana ruhusa ya kuuza wala kununua meno hayo.

Kwa mantiki hii ni kwamba bidhaa zilizotengenezwa na meno ya tembo zinaweza kuuzwa popote katika Umoja wa Ulaya ili mradi tu muuzaji aseme hizi bidhaa zake zimetengenezwa na meno ya tembo ambayo yalipatikana kabla ya mwaka 1947. Hakuna udhibitisho mwingine wa kisheria unaoeleza kwamba bidhaa hizo zimetengnezwa na meno ya tembo yenye umri wa miaka mingapi, yani hakuna kipimo cha kubaini bidhaa za meno ya tembo zinazouzwa zina umri gani, ingawa mwaka 2017 Ufaransa ilipendekeza kuwa bidhaa zote zenye uzani wa gramu 200 zilizotengenezwa na meno ya tembo ziuzwe kwa cheti maalumu.

Taarifa za Tume ya Ulaya zinaonyesha kuwa kiasi cha tani kadhaa za meno ya tembo yakiwa ghafi na yakiwa yemechakatwa huuzwa ndani ya umoja huo kihalali kabisa kila mwaka. Mamlaka za usimamizi wa sheria na polisi wanasema wanashindwa kukamata watu wanaohusika na biashara hii kwa sababu hakuna namna ya kubaini bidhaa hiyo ina umri gani, yani imetengenezwa na meno ya tembo kabla ya 1947 au baada ya mwaka huo, hakuna kifaa cha kupimia umri wa meno ya tembo.

Njia ya uhakika ya kubaini miaka ya meno ya tembo ni kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya Radiocarbon, ambayo ni njia rahisi ya kujua biashara haramu ya meno ya tembo ambayo yamepatikana kipindi cha hivi karibuni. Meno hayo yanayouzwa kwa uwazi kabisa kwa watu binafsi na kwenye mitandao na hata kwa wanaojihusisha na biashara hii ya bidhaa za mapambo.

Nchi nyingi za Ulaya zina shehena kubwa sana ya meno ya tembo ghafi ambayo yapo tangu kipindi cha ukoloni. Kwa sheria za sasa wanaruhusiwa kuziuza au kununua kwenye masoko ya ndani tu, lakini mwaka 2017 tume ya nchi za Ulaya ilishauri kusitishwa kwa usafirishaji wa meno ghafi ya tembo, na kwa taarifa za mwaka 2018 zinasema wanachama wa umoja huo wameridhia makubaliano hayo ya kusitisha biashara za uagizaji meno ya tembo.

Ulaya inabakia kuwa msafirishaji halali wa meno ya tembo yaliyochakatwa kwa nchi za Asia ambako masoko ya meno ya tembo yanachochea janga la ujangili katika bara la Afrika. Uchambuzi wa ripoti hii utaangalia biashara za meno ya tembo ndani ya umoja wa Ulaya ukiachilia mbali biashara ya usafirishaji kwenye nchi zingine.

Jinsi ambavyo sheria za meno ya tembo huko Ulaya zilivyotengeneza mwanya kwa ujangili kushamiri

Biashara ya meno ya tembo kwa Umoja wa Ulaya ilizuiwa kabisa baada ya tembo kupewa ulinzi wa hali ya juu sana na baada ya makubaliano ya mkataba wa CITES, makubaliano ambayo serikali zilikubaliana kudhibiti biashara za bidhaa za wanyamapori (Julai mosi 1975 kwa tembo wa Asia na Januari 18, 1990 kwa tembo wa Afrika). Kwa sheria za umoja wa Ulaya ni kwamba meno yote ya tembo ambayo yamepatikana baada ya mwaka 1947 na kabla ya mwaka 1990 hayataruhusiwa kuingia katika biashara bila cheti cha kibali kutoka kwa serikali za nchi husika, bali bidhaa za meno ya tembo ambazo zimetokana na tembo walioishi kabla ya mwaka 1947 yanaweza kuuza au kuingia katika biashara bila kuwepo kwa cheti au kibali chochote na hii ndio mwanya wa kushamiri kwa biashara haramu na kukua kwa ujangili ulipoanzia.

Hakuna kipande chochote cha meno ya tembo kilichonunuliwa kwa ajili ya utafiti huu wa (kutumia Radiocarbon) kiliuzwa kwa cheti maalumu au kibali, na utafiti wa hivi karibuni umebaini kuwa meno ya tembo yaliyopo katika mzunguko yametokana na tembo waliouwawa miaka michache ya hivi karibuni.

Kasi ya kusitisha biashara ya meno ya tembo

Biashara ya kimataifa ya meno ya tembo ilishasitishwa na CITES tangu mwaka 1989, lakini bado kuna nchi ambazo ziliendelea na biashara hiyo ndani ya nchi zao wenyewe. Lakini kuna ushahidi wa kila namna unaoonyesha jinsi ambavyo biashara ya meno ya tembo kwenye masoko ya ndani ya nchi inavyosababisha na kuchochea janga la ujangili wa tembo wa Afrika, tunantakiwa kufanya kila linalowezekana kusitisha biashara ya masoko ya ndani ya meno ya tembo kwenye nchi zinazofanya biashara hizo.

Shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia uhifadhi na maumbo asilia (ICUN), lilipitisha maazimio mwaka 2016, ya kutaka kufungwa kwa masoko yote ya ndani yanayojihusisha na meno ya tembo, jambo ambalo limeungwa mkono na shirika la umoja uwa mataifa la udhibiti wa biashara ya wanyama na mimea mwitu iliyopo hatarini kutoweka (CITES), CITES wametoa wito kwa nchi zote ambazo zinajiuhusisha na biashara ya meno ya tembo kwenye nchi zao, kuyafunga masoko hayo kwani ndio kichocheo kikuu cha ujangili wa tembo katka bara la  Afrika.

Sasa nchi nyingi duniani zipo katika harakati za kufanyia kazi mapendekezo hayo ya kufunga na kusitisha biashara ya meno ya tembo kwenye nchi zao, au kwenye masoko ya ndani.

Hong Kong ambayo ndio inaongoza duniani kwa kuwa na masoko makubwa ya meno ya tembo, mwezi januari mwaka 2018 wametamka kufuta na kusitisha kabisa biashara ya meno ya tembo kwa miaka mitatu ijayo.

China ilisitisha biashara ya meno ya tembo na bidhaa za meno ya tembo Desemba mwaka 2017, ikimaanisha biashara zote za meno ya tembo sasa ni haramu au ni kinyume na sheria kabisa, isipokuwa kwa kile walichokiita “mapambo halisi” au “genine antique”, tayari hadi hapa juhudi za nchi ya China zimeonekana, na taarifa zinasema baada ya kufikia uamuzi huo biashara ya meno ya tembo iliporomoka kwa 65% mwishoni mwa mwaka 2017.

Marekani nayo imechukua hatua za kusitisha biashara za meno ya tembo chini ya sheria ya spishi zilizopo katika hatari ya kutoweka, kwa kuipa sheria nguvu ili kuzuia kuuza, kununua na kusafirisha meno ya tembo sehemu yoyote ile.

Ulaya nao katika harakati za kusitisha kabisa biashara ya meno ya tembo kwenye masoko ya ndani ya nchi wanachama wa umoja huo, wamedhamiria kusitisha kabisa biashara hiyo ya meno ya tembo, hakuna kununua, kuuza au kusafirisha kwenda kwenye nchi nyingine ikiwa ni pamoja na nchi za umoja huo. Ikiwa imetoa msamaha kwa masharti makali sana kwenye vifaa vya miziki ambavyo vina meno ya tembo, lakini pia kwa kuuzia makubusho meno ya tembo.

Nchi mbalimbali duniani sio tu zinasitisha masoko ya meno ya tembo kwenye nchi zao, bali wanazitaka nchi za umoja wa Ulaya kufanya hivyo pia. Nchi mbali mbali duniani kote wameridhia na kutia saini kusitisha baishara za meno ya tembo, katika ripoti hii zaidi ya watu milioni moja wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau wa uhifadhi wa wanyamapori kuzitaka nchi zinazoendesha biashara hizi kusitisha mara moja.

Hitimisho na mapendekezo

Kutokana na utafiti uliofnyika kila kitu sasa kipo wazi, na Ulaya haina budi kuachana na msimamo wake kuwa haijihusishi na biashara haramu ya meno ya tembo, kutokana na mwanya uliokuwepo uendeshaji wa biashara za bidhaa ya vitu na mapambo yaliyotengenezwa na meno ya tembo kufanyika bila kibali chochote kulitengeneza nafasi na mianya mikubwa ya biashara haramu kushamiri, hivyo kuchochea ujangili wa tembo katika bara la Afrika. Hivyo basi sasa ni wakati wa kuchukua hatua za kusitisha kabisa biashara za aina hiyo kwa nchi za Ulaya.

Tume ya Ulaya imetangaza kuweka mazuio mengine kwa biashara ya meno ya tembo miezi michache ijayo. Watafiti wa mambo wanasema mazuio hayo yatakuwa na tija endapo yatazibiti biashara ya bidhaa au mapambo ambayo yametengenezwa na meno ya tembo ambayo ndio hutoa mwanya kwa biashara nyingine haramu kuendelea bila kujulikana Ulaya nzima.

Kusitisha kwa biashara ya meno ya tembo inaoendelea sasa katika umoja wa Ulaya itasaidia sana katika kuweka mfano au kielelezo kizuri kwa nchi nyingine za Ulaya kuchukua hatua katika kusitisha na kupambana na ujangili.

Pamoja na kwamba ulaya imedhamiria kusitisha biashara ya meno ya tembo kwenye masoko yake ya ndani, imetoa msamaha kwenye vitu hivi ambavyo vingi villitengenezwa na meno ya tembo;

Vitu au bidhaa zilizotengenezwa na meno ya tembo chini ya asilimia 10 (kwa ujazo) na ambazo zimetengenezwa kabla ya mwaka 1947.

Vifaa vya muziki ambavyo vilitengenezwa kabla ya mwaka 1975 na viwe vina kiasi cha chini ya asilimia 20 ya meno ya tembo.

Bidhaa au vile vitu muhimu sana ambavyo vina angalau miaka 100, vitu hivyo vitakaguliwa na kuchunguzwa na wataalamu kabla ya msamaha huo kutolewa.

Msamaha maalumu utatolewa kuwa vitu vidogo sana ambavyo vinajumuisha michoro ya aina mbali mbali ambayo imechorwa na kiasi kidogo sana cha meno ya tembo na pia kama inahusisha biashara kati ya makumbusho ambazo zimeruhusiwa kisheria.

Kila linalowezekana linatakiwa kufanyika ili kusitisha na kuzuia kabisa biashara ya meno ya tembo sehemu yoyote ile duniani, kwa sababu endapo kutakuwa na kibali cha kuuza, kununua au kusafirisha meno ya tembo sehemu yoyote ile duniani, basi tujue tutakua tumeamsha tena mambo magumu amabayo yatatusumbua na kutugharimu kuyadhibiti tena.

Vita dhidi ya ujangili vinatugharimu vitu vingi sana, ukiachilia mbali fedha na rasilimali nyingine, kupambana na ujangili inatugharimu maisha yetu, siku zote maisha ya watu ambao wanasimamia rasilimali hizi yapo hatarini. Hii ni kutokana na tamaa ya utajiri, rushwa, umasikini, sheria dhaifu za uhifadhi na usimamizi; na yote inachochewa na kitu kimoja kikubwa, mahiaji makubwa ya meno ya tembo kwenye nchi nyingi za Asia, Ulaya na Marekani.

Naamini kabisa hatua amabzo nchi mbali mbali zinachukua ili kunusuru tembo wetu ni muhimu sana, na tunataka dunia yote ifahamu jambo hili moja hakuna kizazi chochote cha sasa au baadaye kitakachofurahia unyama huu dhidi ya wanyamapori hasa tembo. Tuwaache wanyamapori waendelee kuwepo kwa faida ya wengi.

Ripoti hii niliyoichambua ina mambo mengi ambayo yapo kwa mifano na picha, napongeza juhudi zote hizi katika kutumia teknolojia kupambana na ujangili, hii ni hatua moja kubwa sana ambayo itasaidia kuchukua hatua nyingine kubwa zaidi katika uhifadhi wa wanyamapori na maliasili kwa ujmla. Tutumie kila tulicho nacho kwa manufaa zaidi na kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi si kwa binadamu pekee bali hata wanyamapori na viumbe hai wengine.

ASANTE SANA!

Mchambuzi wa ripoti hii ni;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania