Hali na mwenendo wa ujangili na biashara haramu ya wanyama na mimea pori imekuwa tishio sana kwa sasa hapa duniani. Wanyamapori ambao wanawindwa sana na kufanyiwa biashara haramu wamekuwa ni wanyamapori muhimu sana katika mfumo wa ikolojia ya maisha ya viumbe hai. Katika kipindi hiki cha maendeleo ya sayansi na teknolojia kimekuwa kipindi kibaya sana kwa wanyama kama faru na tembo, kutokana na masoko ya meno na pembe za faru kuhitajika sana na kuwa na matumizi makubwa kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Asia.

Katka uchambuzi wa ripoti hii inayonyesha ushiriki wa nchi ya Kenya katika ujangili na usafirishaji wa bidhaa haramu za wanyamapori na vitu vingine ni wa hali ya juu sana, imetajwa kwenye ripoti hii kuwa katika bara la Afrika nchi ya Kenya ndio kitovu na sehemu muhimu ya kusafirishia bidhaa haramu za wanyamapori na bidhaa nyingine za mimea. Ili kujua zaidi kuhusu ujangili wa wanyamapori hawa na biashara zao nakukaribusha kwenye makala hii muhimu inayogusia wanyama hawa wailil, faru na tembo. Jina la riporti hii tunayoichambua ni “WILDLIFE PROTECTION AND TRAFFICKING ASSESSMENT IN KENYA” iliyotoka Mei 2016 na kuandikwa na Sam Weru.

Tembo

Mapango wa 2011 – 2020 wa uhifadhi na usimamizi wa tembo nchini Kenya unasema kuwa idadi ya tembo imeporomoka sana kwa kipindi cha miaka 100 iliyopita sababu kubwa ikiwa ni biashara ya meno ya tembo. Idadi ya tembo imepungua sana kutoka makadirio ya tembo 167,000 mwaka 1973 hadi 20,000 mwaka 1990. Ingawa kunaweza kukawa na ugumu wa kulinganisha ubora wa taarifa miongo iliyopita na taarifa zinazopatikana sasa. Lakini taarifa za hivi karibuni mwaka 2014 zinaonyesha kuwa idadi ya tembo katika nchi ya Kenya inakadiriwa kufikia 32,000 zikionyesha zilikuwa zinapungua kwa miaka mitatu iliyopita.

Aidha, kutokana na tathimini iliyofanywa na ripoti hii inaonyesha kuwa licha ya kwamba tembo ni wanyama ambao wametafitiwa sana nchini Kenya, lakini kumekuwa na ukosefu wa taarifa za kitafiti za zaidi ya miaka 8 maka 20 za tembo ambao wanaishi kwenye misitu. Taarifa zilizopo kwenye machapisho mengi ni taarifa za utafiti wa tembo wa savanna pekee. Hivyo kuna idadi kubwa ya taarifa ambazo zinahitajika ili kukadiria vizuri idadi ya tembo katika nchi ya Kenya.

Hata hivyo ujangili, kubadilika kwa maeneo ya malisho ya tembo imekuwa ni moja kati ya sababu kuu za kuporomoka kwa idadi ya tembo nchini Kenya. Kwa miaka zaidi ya 25 taasisi inayoshughulika na huduma za wanyamapori Kenya (Kenya Wildlife Services, KWS) na watafiti wengine wa tembo wameandika kuwa kubadilika kwa maeneo ya tembo nchini Kenya ni kwasababu ya uuaji, kuharibika kwa makazi yao kutokana na ukame, na kupotea kwa maeneo mtawanyiko na njia za tembo ni kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya watu na mifugo.

Pia kuna sababu nyingine ziliyopelekea kupungua kwa idadi ya tembo, kama ilivyoainishwa kwene ripoti hii ni shughuli nyingi za kimaendeleo na kujipatia kipato kama vile upanuzi wa mashamba, ujenzi wa makazi ya binadamu, upanuzi wa miundombinu ya barabara, uchimbaji wa madini, ukataji wa misitu na miti ya asili, kuongezeka kwa idadi ya mifugo, kuharibika na kukauka kwa maeneo ya ardhioevu nk.

Faru

Miaka ya 1960, idadi ya faru katika bara la Afrika ilikadiriwa kuwa ni zaidi ya 100,000 lakini idadi hiyo haikuendlea kuongezeka kama ilivyotarajiwa bali ilipungua kwa kasi sana na kufikia idadi ndogo sana ya 2410 mwaka 1995. Sababu kubwa iliyopelekea kupungua kwa faru kiasi hiki ni biashara ya uwindaji wa wanyamapori hawa kushindwa kusimamiwa ipasavyo na kutoa mwanya kwa majangili kuanza uharibifu kwa wanyamapori hawa muhimu. Baada ya utekelezaji wa maagizo ya CITES idadi ya faru weusi imeongezeka kidogo sana na kufikia faru 5081 mwaka 2013. Leo asilimia 96 ya faru weusi wanapatikana katika nchi nne pekee hapa barani Afrika, nchi hizo ni Afrika ya Kusini, Namibia, Kenya na Zimbabwe. Hii inaifanya Kenya kuwa nchi ya kipekee duniani kuwahifadhi wanyama hawa ambao wapo katika hatari kubwa ya kutoweka.

Historia ya faru nchini Kenya inamulika hali ya mambo ilivyo katika sehemu nyingine barani Afrika. Mwaka 1970 Kenya ilikuwa na idadi kubwa ya faru inayofikia 20,000 lakini idadi hiyo iliendelea kupungua zaidi kutokana na ujangili uliokithiri miaka ya 1970 na 1980. Kutokana na hali hiyo mamlaka ya serikali ya Kenya kwa mara ya kwanza ilanzisha bustani ya kuwahifadhi wanyama hawa iliyoitwa Rhino Santuary, katika hifadhi ya taifa ya ziwa Nakuru mwaka 1987, bustani hiyo iliyoanzishwa ilikuwa chini ya uangalizi mkali sana wa serikali ya Kenya, juhudi hizo za serikali ya Kenya zilizaa matunda baada ya spishi ya faru weusi wa Mashariki kuongezeka kutoka 381 mwaka 1987 na kufikia faru 648 mwaka 2014 sawa na ongezeko la asilimia 70 kwa miaka 27.

Halikadhalika ongezeko la faru weupe walioingizwa nchini Kenya kutoka Afrika Kusini ambapo idadi yao imeongezeka kutoka faru 74 mwaka 1992 na kufikia faru 399 mwaka 2014. Kwa hali hiyo nchi ya Kenya kwa sasa inashika nafasi ya tatu duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya faru weusi na weupe ambao idadi yao ilifikia 1047 mwaka 2014. Faru nchini Kenya wanalindwa na kuhifadhiwa kwenye bustani (sanctuaries) 16 za serikali na za binafsi moja ipo katika ukanda wa ulinzi wa hali ya juu (Intensive Protection Zone) katika hifadhi ya taifa ya Tsavo na sehemu nyingine zinazohifadhi wanyama hawa ni maeneo ya mtawanyiko na maeneo ya asasi za kijamii au maeneo ya hifadhi ya jamii.

Mpango mkakati wa faru nchini Kenya wa mwaka 2012 – 2016 umekusudia ongezeko la asilimia 5 ya faru kwa mwaka, lakini hali halisi inaonyesha kukithiri kwa vitendo vya kijangili vinakwamisha kufikia malengo hayo. Kwa sasa kiwango cha ujangili wa faru nchini Kenya kimekuwa na kufikia asilimia 6 kwa mwaka. Kiwango hicho ni kikubwa sana na kimezidi kabisa kiwango cha faru wanachozaliwa, hiyo ndio changamoto kubwa sana inayoikabili nchi ya Kenya kwa sasa kwenye masula haya ya uhifadhi wa spishi za wanyama hawa.

Faru weupe wa Kaskazini (Northen white rhino) ni spishi ya faru ambayo inaaminika kutoweka kabisa katika mwitu, kutoweka kwa spishi ya faru huyu aliyekuwa amesalia katika hifadhi ya taifa ya Garamba katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo mwaka 2006. Kwa kuwa spishi nne za faru hawa zilihamishiwa nchini Kenya kwa ajili ya kuzaliana ili baadaye wawarudishe kwenye maeneo yao ya mwanzo, kwa bahati mbaya mpango wa kufanya hivyo haukufanikiwa kwasababu faru wote walikufa bila hata kuzaliana, chanzo cha kifo ni kutokana na sababu za kiasili.

Makazi na maeneo ya faru weusi na weupe yamepungua sana kwa kadri siku zinavyokwenda. Ripoti inaonyesha kulikuwepo wa faru kwenye maeneo ya nchi ya Kaskazini mwa Chadi na katika nchi ya Sudani. Hali halisi sivyo ilivyo sasa, meneo ya faru yamekuwa madogo sana na yapokatika nchi chache za Kusini na Mashariki mwa bara la Afrika. Watumiaji wa mwisho wa meno ya tembo na pembe za faru Kusini mwa Asia na Mashariki ya Kati imebadilika kabisa kwa sasa. Kwenye miaka ya 1970 na 1990 nchi za Yemeni, Japani, Korea Kusini, Taiwani na China walikuwa ndio watumiaji wakuu na ndio waliokuwa na mahitaji makubwa ya pembe za faru.

Matumizi makubwa ya pembe za faru Kusini mwa Asia ilikuwa ni kwa ajili ya dawa za asili (dawa za kienyeji) wakati kwa nchi ya Yemeni walihitaji sana pembe za faru kwasababu ya kutengeneza hala za kuwekea au kubebea visu na majambia. Lakini katika miaka ya 2000 kumekuwa na mlipuko mkubwa zaidi wa uhitaji wa pembe za faru katika nchi ya Vietnam ambao wamekuwa wakitumia pembe za faru kama sehemu ya kuonyesha utajiri au heshima fulani kwenye jamii pamoja na matumizi ya dawa za asili.

Kabla sijamalizia kipengele hiki kuhusu faru nchini Kenya, nataka tuone mpango mkakati wa nchi ya Kenya katika kuhakikisha faru wanahifadhiwa kwa vizazi vjiavyo. Mpaka kufikia mwaka 2014 nchi ya Kenya ilikuwa na idadi ya faru 1047, na kwa mwaka huo faru waliouwawa kwa ujangili ilifikia faru 35.

Kuna malengo na mkakati wa uhifadhi na usimamizi wa faru weusi nchini Kenya wa mwaka 2012 – 2016 mkakati huo ulieleza dhamira na malengo makubwa waliyonayo kuhusu uhifadhi wa faru weusi kwa kusema kuhifadhi angalau faru weusi wapatao 750 kabla ya kufikia mwishoni mwa mwaka 2016, na kufikia kiwango cha ongezeko la asilimia 5 cha ukuaji, na kiasi chini ya asilimia 1 ya mauaji yanayosababishwa na binadamu na magojwa. Mpango huo ulilenga kuwa na maono ya kufikia faru 2000 kwenye hifadhi zao. Na ili kufikia malengo na maono hayo, mikakati ifuatayo iliazimiwa;

  1. kupunguza uuaji haramu wa faru ili uwe chini ya asilimia 1 kwa mwaka na pia kupunguza kabisa biashara ya pembe za faru na nyara nyingine za faru
  2. kuendelea kusimamia na kutoa taarifa za kitaalamu zitakazosaidia katika uhifadhi, idadi yao na katika kuweka programu za kiutekelezaji.
  3. kufikia na kuendeleza kiwango cha ukuaji wa asilimia 6 wa faru weusi katika bustani zilizoanzishwa kwa ajili ya uhifadhi wa faru na kiasi cha chini kiwe kukua kwa asilimia 5 ili kufikia malengo ya kuwa na faru weusi 750 kabla ya mwaka 2016.
  4. kuandaa maeneo salama kwa ajili ya kupanua maeneo ya uhifadhi wa ongezeko la faru.
  5. Kukuza ufahamu na uelewa kwa umma kuhusu faru ilikwa pamoja kupata ushirikiano kimataifa katika kuwahifadhi wanyama hawa.
  6. Kutengeneza mfumo na ushirikiano ili kujenga uwezo wa utekelezaji wa mikakati hiyo.

Kuna sababu nyingi sana zilizopelekea nikachambua ripoti hii inayohusu tathimini ya ujangili wanyama na mimea pori katika nchi ya Kenya. Ikumbukwe kuwa Kenya ni moja ya nchi za Afrika mashariki ambayo imepakana na Tanzania kwa upande wa kaskazini mashariki, na pia ni nchi ambayo tunashirikiana mambo mengi ikiwepo mfumo wa ikolojia ya wanyamapori hasa wanyamapori wanaohama kama vile tembo, nyumbu nk. Hivyo tunahitaji kujua kinachoendelea kwa kuhusu wanyamapori na biashara haramu. Kama nilivyochambua kwenye ripoti hii matatizo waliyonayo Kenya kwenye uhifadhi na usimamizi wa maliasili hayana tofauti na matatizo tuliyonayo sisi katika uhifadhi na usimamizi wa maliasili. Hivyo kuichambua ripoti hii ni muhimu ili tujifunze mambo yanavyokwenda na tuchukue hatua stahiki.

Haya niliyoyachambua hapa siyo yote, tutaendelea na uchambuzi wa ripoti hii muhimu maana ina mambo mengi mazuri ya kujifunza na kuyafanyia kazi, hivyo basi fuatilia uchambuzi mwingine ili kujua yanayoendelea, na pia nakushauri usome ripoti hiyo ni muhimu sana.

Asante sana!

Mchambuzi wa ripoti hii ni;

Hillary Mrosso

+2255 683 862 481

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania