Habari msomaji wa wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tutajifunza kwa pamoja mambo mbali mbali yaliyopo kwenye sheria ya uhifadhi wa wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009. Tutajifunza hatua kwa hatua kipengele kwa kipengele hadi tumalize sheria hii yote. Ili tupate uelewa kwa njia rahisi na kila mtanzania ajue wajibu wake na majukumu yake kwa mujibu wa sheria hii. Kwenye kipengele cha leo tutajifunza kuhusu umiliki wa wanyamapori kisheria kifungu cha 4 sehemu ya kwanza ya sheria hii. Tunahitaji sana kufahamu nini ambacho sharia inasema na inafanya kuhusu wanyamapori. Karibu tujue zaidi.
4.-(1) Kifungu hiki kinaeleza kwamba wanyamapori wote waliopo Tanzania wataendelea kuwa mali ya Uma na watabakia kuwa chini ya uangalizi wa Rais kwa niaba ya watu wa watanzania. Kwa hiyo hifadhi zote za wanyamapori, mbuga zote, mapori yote wanyama waliopo humo watakuwa ni mali ya Uma wa watanzania, na mali hii imewekwa chini ya Rais kama mwangalizi wa mali hii kwa niaba ya watanzania wote.
(2) Endapo mtu yeyeote amechukua mnyamapori kisheria, umiliki wa mnyama huyo utakuwa kwa mujibu wa sharia hii ya wanyamapori kuwa ni haki ya mtu huyo. Hapa ni kwamba endapo mtu amaekamata myamapori kisheria au amewinda au kwa namna yoyote ile akawa na mnyamapori huyo kisheria, mtu huyo atakuwa ndie mmiliki halali wa mnyamapori huyo.
(3) Endapo spishi za wanyamapori watakuwa wamekamatwa kisheria kwa kibali au kwa lesseni au haki ya kutumia wanyamapori iliyotolewa, au iliyotolewa kwa mujibu wa sheria hii, umiliki wa mnyama huyo, utakuwa kwa mujibu wa matakwa ya sharia hii, na kwa vigezo na masharti ya lesseni, itakuwa ni mali ya mwenye lesseni, au mali ya muhusika. Hapa ni kwamba wale watakao kuwa na vibali au lesseni ya kukamata wanyamapori watakapo kamata wanyama kwa mujibu wa sheria na masharti ya vibali na lesseni zao, nyara hizo au wanyamapori hao watakuwa wake au watakuwa wa mtu mwenye lesseni hiyo.
(4) Kabla ya kutumika kwa sheria hii, mnyamapori yoyote ambaye ambaye anamilikiwa kisheria na mtu yeyote,mnyama huyo atakuwa, kulingana na matakwa ya sharia hii ataendelea kuwa chini ya mtu husika aliyekuwa naye. Hapa kwenye kipengele hichi anasema kwamba kama ikitokea kabla ya matumizi ya sharia hii ya wanyamapori, mtu alikuwa na wanyamapori wake kihalali au kisheria, ataendelea kuwa nao hivyo hivyo kwa mujibu wa sharia hii ya wanyamapori.
(5) Isipokuwa kulingana na lesseni yoyote au haki ya kutumia wanyamapori, Hakuna kitu katika sehemu hii kitakacho fikiriwa kumhamishia mtu yeyote umiliki wa aina yoyote wa mnyama anayehifadhiwa akipatikana akiwa amekufa au anakufa. Hapa sheria inasema isipokuwa kulingana na sheria hutakiwa kumpa mtu mwingine umiliki wa mnyama yeyote aliyekufa au anayekufa.
(6) Pale ambapo mtu yeyote atachukua mnyama kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kinyume na sheria na kinyume na sheria hii, umiliki wa mnyamapori huyo hautakwenda kwa mtu huyo. Kwa namna nyingine sheria inasema mtu yeyote ambaye amepata mnyamapori kwenye maeneo yaliyohifadhiwa au kutengwa kwa ajili ya wanyamapori kinyume na sheria atakuwa amehalifu sheria hii ya wanyamapori, hivyo mtu huyo hatapewa umiliki wa mnyamapori huyo.
(7) Waziri anaweza, kwa kanuni, kuamuru kusajili na kusimamia kiolezo (specimens) za wanyama wanaotumika kwa sababu za kitamaduni na za kimila na jamii. Kwa wanyamapori wanaotumika kwenye maeneo mabali mbali na jamii zetu, waziri mwenye dhamana anaweza kutoa amri ya wanyama hao kusajiliwa na kusimamiwa kwa karibu zaidi.
Hivyo Rafiki, hayo ni baadhi ya mambo muhimu kuyajua ili tuweze kwenda sambamba kwenye suala la uhifadhi wa wanyamapori na mazingira. Sheria imeweka wazi utaratibu wote wa namna ya kumiliki wanyamapori kisheria na kwa mujibu wa sheria za wanyamapori.
Naamini umepata kitu cha kukusaidia, hivyo basi tukutane sehemu ya pili ya sheria hii ambayo tujifunza kuhusu (objectives) shabaha, nia na lengo la sheria hii ya wanyamapori. Hivyo mshirikishe na mwenzako maarifa haya muhimu.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569