Unaweza kuwa unajiuliza kwanini nakazana kuandika makala kuhusu matumizi ya wanyamapori na ujangili. Jibu ni kwamba, ni eneo ambalo nimelifuatilia na kusoma maandiko mengi kuhusu matumizi ya wanyamapori na ujangili. Baada ya kusoma na kuona tatizo la ujangili na matumizi haramu ya wanyamapori ni kubwa na la kutisha kuliko inavyofikiriwa na wengi. Na endapo kasi hii ya ujangili haitapunguzwa au kudhibitiwa, tunaweza tusione hawa wanyama miongo michache ijayo.
Picha na Stella Bitanyi; Ikionyesha wanyama jamii ya swala waliowindwa kwa ujangili katika eneo la ikolojia ya Serengeti
Machapisho mengi yaliyoandika kuhusu ujangili, matumizi ya wanyamapori na biashara haramu yameandikwa kitaalamu sana kiasi ambacho mtu wa kawaida hawazi kusoma akaelewa taarifa hizo hasa taarifa za kitakwimu na kisayansi. Pamoja na hayo, wengi wanaosoma hawaoni ukubwa wa tatizo hili kwasababu baadhi ya taarifa nyingi za ujangili zimeandikwa kwa lugha laini sana ambayo inafanya ionekane ni tatizo dogo.
Lengo la kuandika mambo haya kila mara ni kutaka uma kujua ukubwa wa tatizo la ujangili, athari za kimazingira, kiuchumi na kiafya zinazoletwa na ujangili na matumizi ya nyamapori au mazao ya wanyamapori. Kupitia makala hizi najaribu kuwashirikisha kwa lugha nyepesi na rahisi ili kila mtu aone kuwa ujangili, matumizi ya wanyamapori na mazao yake, pamoja na biashara haramu za wanyamapori zanatishia usalama wa wanyamapori na kuleta majanga mengine mabaya.
Kupitia makala hizi natamani tuungane kwa pamoja, sehemu yoyote uliyopo ujue kuwa wanyamapori na rasilimali zetu muhimu zinateketea kwa kasi kubwa, hivyo tushirikiane na wadau wengine wenye mapenzi mema katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake. Kwa kufanya hivyo tutawarithisha watoto wetu na vizazi vingi vijavyo maliasili hizi muhimu.
Kama nilivyoandika kwenye makala iliyopita, nimeainisha ukubwa na changamoto zinazoletwa na ujangili na matumizi ya nyamapori. Leo nimepitia jarida moja la utafiti uliofanyika karibu sehemu kubwa ya Tanzania, utafiti huo ulikuwa ukiangalia matumizi ya nyamapori kwenye maeneo mbali mbali ya Tanzania. Utafiti huo uliofanywa na Slivia Ceppi na Martin Nielsen (2014) uliangalia jamii mbali mbali zilizo karibu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori namna wanavyojihusisha na ujangili na matumizi ya wanyamapori. Soma zaidi hapa Nyamapori Bado ni Sehemu Muhimu ya Mlo wa Jamii Nyingi za Watu Zinazoishi Karibu na Maeneo ya Hifadhi za Wanyamapori
Katika utafiti huu umetoa mwanga kuwa maeneo mengi yenye rasilimali za wanyamapori zinakabiliwa na ujangili na matumizi haramu ya nyamapori kama kitoweo. Hivyo, uwepo wa watu karibu na maeneo ya hifadhi za wanyamapori umechangia kushamiri kwa vitendo vya kijangili kaitika maeneo hayo.
Utafiti huu umebaini kuwa sio wote wanaofanya ujangili wa wanyamapori wanafanya hivyo kwasababu ya umasikini au njaa, Ceppi na Nielsen wanatuambia kuwa, baadhi ya watu wanaofanya ujangili wanafanya hivyo kwa sababu wana mapenzi na nyamapori, wengine wanafanya ujangili kwasabau wanaamini nyamapori ni nzuri kiafya kuliko nyama nyingine, wengine wanafanya ujangili kama sehemu ya utamaduni wao, hivyo kuwinda wanyamapori kwa ajili ya kitoweo au biashara sio lazima iwe ni kutimiza mahitaji ya muhimu ya kila siku kama chakula na fedha.
Kupitia utafiti huu umeainisha kuwa, matumizi ya nyamapori ni makubwa sana, mfano, inakadiriwa kuwa zaidi ya wanyamapori 40,000 hadi 200,000 wanavunwa kila kwa njia haramu kwa ajili ya matumizi ya nyamapori na biashara katika eneo la Serengeti. Idadi hii ya wanyama ni kubwa sana, na kwa kiasi kikubwa makadirio haya ni makadirio ya chini kulingana na namna utafiti ulivyofanyika.
Sasa unaweza kufikiria mwenyewe, watu wengi wanaoishi karibu na maeneo ya wanyamapori wanavyochangia kutoweka kwa idadi kubwa ya wanyamapori kwa kiasi hicho. Inawezekana kabisa takwimu hizi za idadi ya wanyamapori kuvunwa kwa njia haramu zimeongezeka maradufu kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na watumiaji wa nyamapori katika sehemu hizi.
Ndugu msomaji wa makala hii, unaweza kuona hali ilivyo hatari kwa wanyamapori wetu, endapo hatutachukua hatua za haraka kupambana na ujangili kwenye maeneo haya, tutapoteza wanyama wetu wa thamani kubwa. Nimeandika makala hii ili tushirikiane pamoja katika kupiga vita ujangili maana hauna manufaa kwa taifa na kwa vizazi vijavyo.
Nimependa sana utafiti huu uliofanywa na Ceppi pamoja na Nielsen kwasabu umegusa maeneo mengi yenye utajiri wa wanyamapori na kubaini zaidi ya asilimia 46 ya kaya zote (300) zilizohojiwa zinatumia nyamapori kama kitoweo. Hii ina maana kuwa kuna matumizi makubwa sana ya nyamapori na ujangili sehemu zote hizi utafiti huu ulipofanyika.
Wakati nasoma utafiti huu nilishituka sana kuona kuwa zaidi ya 91% ya majangili waliokamatwa katika eneo la Serengeti walikiri kuwa wanawinda wanyamapori kipindi nyumbu wanapohama (Wildebeest Migration). Hizi ni takwimu za kutisha sana zinazoonyesha kikuthiri kwa ujangili kwenye maeneo yeneye wanyamapori. Hivyo, juhudi za usimamizi na ulizi wa wanyamapori zinatakiwa kuongezwa zaidi sehemu zenye takwimu kubwa za ujangili kama sehemu hizi za njia za wanyama wanapohama kutoka eneo moja kwenda jingine. Soma zaidi hapa Tishio Kubwa Kwa Wanyamapori Na Mazingira Tanzania
Bahati nzuri nchi ya Tanzania imebarikiwa kuwa na idadi kubwa ya maeneo ya wanyamapori na misitu, maeneo haya yasipowekewa ulinzi wa kutosha tutapoteza idadi kubwa ya wanyamapori na mazingira yake, mwishowe yageuzwe kuwa mashamba. Hivyo basi, kunatakiwa kuwa na uwekezaji mzuri na wenye manufaa kwenye maeneo haya ili yasionekane hayana mchango kwa jamii na uhifadhi.
Rasilimali hizi za wanyama na mimea ni muhimu sana ili kufanya mifumo mingi ya kiikolojia kufanya kazi vizuri. Rasilimali hizi zikitunzwa vizuri ni chanzo kikubwa sana cha mapato kwa nchi, na pia kupitia usimamizi mzuri wa rasilimali hizi, tutapata huduma bora za shule, afya, maji, barabara, na miundombinu mingine muhimu, pia ni eneo ambalo linatoa ajira nyingi kwa wasomi na watu wengine. Hivyo kama jamii tunatakiwa kujua hakuna faida ya pamoja itakayotuletea maendeleo kupitia ujangili wa wanyamapori. Ujangili ni ubinafsi, uporaji, na dhuluma kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Asante sana kwa kusoma makala hii hadi mwisho, usiache kuwashirikisha wengine makala hii, watumie link nao wajifunze, ili kwa pamoja tupate elimu hii muhimu.
Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com