Historia ya uhifadhi wa wanyamapori, misitu na maliasili kwa ujumla una historia ndefu sana ambayo imekuwepo kabla ya ukoloni kuingia kwenye nchi zetu za Afrika. Maisha ya watu yaliongozwa na miiko na tamaduni ambazo kwa kiasi kikubwa zilikuwa ni rafiki kwa mazingira na uhifadhi kwa ujumla. Jamii zilikuwa uelewa mzuri kuhusu maliasili ambazo ziliwazunguka na walielewa sana maeneo ya kutumia rasilimali zao na maeneo ambayo siyo ya kutumia rasilimali zao.

Kwa kutumia ujuzi, mila na tamaduni ambazo zilihusiana na uhifadhi wa maliasili na misitu waliweza kuishi vizuri na mazingira yao yaliyowazunguka. Hii ndio maana Afrika ina historia ndefu sana ya uhifadhi wa misitu na wanyamapori. Kuna aina ya misitu iliyotunzwa na haikuruhusiwa shughuli za uvunaji kuendelea katika misitu hiyo. Hivyo waliheshimu uwepo wa misitu hiyo na kuwa ni njia moja ya kufanya maliasili hizo kuendelea kuwepo hadi leo.

Kwenye sayansi ya uhifadhi na usimamizi wa maliasili zetu tunatakiwa kuwa wanye busara kujua namna ya kutumia uelewa wa jamii kuhusu maliasili zinazowazunguka kuhifadhi maliasili muhimu kama vile misitu na wanyamapori. Jamii hizi ambazo zipo kwenye maeneo ya karibu na hifadhi za misitu na wanyamapori zinajua mambo mengi sana ambayo katika ulimwengu wa sayansi yanaweza yasielezeke lakini yana mchango muhimu sana kwenye uhifadhi wa wanyamapori na misitu.

Jamii hizi zinaweza kuwa na uzoefu wa miaka mingi hata zaidi ya miaka 200, hivyo hurithi mila na tamaduni kuhusiana na mazingira yanayowazunguka na mahusianao yao na maliasili hizi. Tunatakiwa kuelewa uhusiano huo wa jamii na maliasili hizi muhimu ili kuona namna ambavyo vyote kwa pamoja vinaweza kuwa na manufaa endelevu kwa pande zote za jamii na misitu.

Mafanikio ya uhifadhi endelevu ni kutambua mapema kabisa ujuzi, uelewa na mitazamo ya jamii kuhusu uwepo wa maliasili kwenye maeneo yao. Hatua hii ndio itakayofanya kutumia mbinu na mipango ambayo kwa kujadiliana kwa pamoja itaonekana yenye manufaa na yenye kuendeleza uhifadhi kwa manufaa ya sasa na ya baadaye.

Kwa kutoa nafasi ya jamii kushiriki na kuwa sehemu muhimu ya kufanya maamuzi kwenye uhifadhi wa maliasini na rasilimali ambazo wanazifahamu itasaidia sana kujenga taswira na mfumo ambao utaifanya jamii kujiona wao ndio wamiliki na wanawajibika kutunza na kuhifadhi maliasili zao. Badala ya kuwaachia watalaamu waliaosoma na waliotoka sehemu tofauti na sehemu hizo zenye maliasili kuwa ndio wafanya maamuzi kwenye maliasili za sehemu husika ambayo hawaijui vizuri, hakutakuwa na matokeo bora ya kudumu na hii itapelekea jamii kuona kama imetengwa na haina nafasi ya kushiriki na kufaidika kutokana nauwepo wa rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao.

Kwa kutambua hilo, serikali wadau wa mazingira na uhifadhi wanatakiwa kuangalia tena sera ya ushriki wa jamii kwenye uhifadhi wa maliasili zao kwa kujumuisha ujuzi, uelewa na ufahamu wao ambao ni muhmu kwa ajili ya kuhifadhi misitu na wanyamapori kwa pamoja. Kwa kufanya hivyo inatakiwa iendane sambamba na jamii kupata faida moja kwa moja kwani wao ndio wahusika kataka maamuzi na wanagharimia kuhifadhi rasilimali hizo.

Hivo basi, miradi yote ya serikali na ya  watu binafsi inatakiwa kujua kwa kina mila na desturi za jamii ili kushirikiana nao kwenye uhifadhi wa wanyamapori na misitu. Kwa kuelewa hilo kazi ya uhifadhi inakuwa rahisi kwani utajua hatua za kuchukua na kipi cha kufanya na kipi cha kuacha. Aidha kuna baadhi ya miradi na sehemu mbali mbali ambapo wamefanikiwa kwa kutumia kanuni hii ya kuishirikisha jamii kikamilifu katika uhifadhi kwa kuwapa nafasi kubwa ya kufanya maamuzi na kutoa maoni yao ya namna bora ya kuhifadhi na kutumia maliasili zao bila kuharibu asili yake na uwepo wake.

Hakuna njia ya amani ya kuhifadhi maliasili kama kutoa nafasi kubwa jamii kuwa sehemu ya maamuzi, kupanga mipango endelevu ya uhifadhi na kuhakikisha jamii inanufaika kwa ushiriki wao katika uhifadhi wa maliasili hizo. Pia jambo hili liende sambamba kwa pande zote mbili kuweka mipango yao mezani na kujadili kila mpango kina, ili iweze kueleweka kwa jamii na watoa maamuzi ya namna bora ya kuhifadhi rasilimali hiyo kwa pamoja. Hata kama zitakuwa na mbinu na mipango ya kisasa na ya kisayansi, elimu inatakiwa ili jamii ilewe kwa undani kila kinachoendelea kwenye maliasili zao, naamini jamii itakuwa na furaha kushiriki na kufanya kazi kwa pamoja na watalaamu kwa sababu ya uelewa huo.

Ujuzi, uelewa, mila na tamaduni za jamii zinaweza kuwa tunu na silaha nzuri kwenye uhifadhi wa maliasili, tuangalie namna bora ya kuunganisha na kuzitumia kuborsha sekta ya maliasili.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania