Habari rafiki, karibu kwenye makala yetu ya leo ambayo ni moja ya makala muhimu sana kwa watanzania kuisoma. Tanzania imejaliwa kuwa na idadi kubwa sana ya vivutio vya aina mbali mbali kama vya nchi kavu na vya baharini, kuna maeneo hapa hapa Tanzania mtu akipiga picha na kukuletea akakuonyesha utakataa kuwa ni Tanzania, kuna fukwe nyingi sana zenye hadhi na mandhari nzuri kwa ajili ya wageni na watu wanaopenda kutembelea fukwe na bahari, kuna mito na maziwa makubwa yenye kuvutia sana kuizunguka nchi yetu, kuna milima na mabonde makubwa yenye mvuto na mwonekao mzuri uwapo juu, kuna maelfu ya hekta za misitu minene, misitu ya kati na misitu ya vichaka.Kuna hifadhi za Taifa zaidi ya 16 sasa, kuna Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu, kuna wanyamapori na ndege wa kila aina wenye kuvutia sana kuna miamba na mawe, mapango na hata maeneo ya kihistoria mengi sana karibu kila mkoa kwenye nchi hii ya Tanzania.

Kuna watu wengi wenye tamaduni nyingi za asili wana mifumo ya maisha tofauti kabisa na watu wa kawaida, hii yote ipo katika ardhi ya Tanzania, kuna watu wakarimu na wenye utamaduni ambao utakuacha mdomo wazi, yani ni mengi sana ambayo yapo hapa Tanzania lakini cha ajabu maelfu kwa mamilioni ya watanzania hawajui vitu vingi walivyo navo.

Unaweza kukutana na mzungu, au mgeni kutoka nchi za nje anakwambia unaijua au ulishawahi kutembelea hifadhi ya Taifa ya Uduzungwa? Jibu la watu wengi ni hapana, anakuuliza tena ulishatembelea maeneo ya kihistoria huko Bagamoyo? Unamwambia sijawahi, anakuuliza tena ulisha tembelea fukwe yoyote ya bahari unasema hapana, looo! We mtanzania mbona unatia aibu, wewe unachojua vizuri nia hapo kwenye kijiji chako ulichozaliwa tuu? Au kwenye hako kamji ulikokulia basi, hujawahi kuinua hata mguu wako kutembelea sehemu zenye historia au sehemu za vivutio mbali mbali ambazo unazipenda, jamani wanatushida hadi wageni ambao sio Watanzania! Tubadilike jamani, watu wa kwanza kujua na kutembelea vivutio vyetu tuwe sisi wenyewe ili tuwe mabalozi wazuri. Na hii ndio maana utalii wetu haukui kwa kasi na kwa viwango vya kuridhisha kwa sababu yetu wenyewe kutojua namna ya kuutangaza utalii wetu na vivutio vyetu. Na njia nzuri ya kutangaza utalii na vivutio tulivyo navyo katika nchi yetu ni kwa kutembelea vivutio hivyo na kuvielewa, tukiwa na utamaduni wa namna hii tutafika mbali sana kwenye sekta ya utalii Tanzania.

Baaadya ya kuandika maneno hayo sasa nataka kukusaidia kujua namna na njia nzuri ya kwenda kutembelea hifadhi na maeneo yenye vivutio vya utalii. Watu wengi wanafikiri kuwa wanaotembelea hifadhi au vivutio mbali mbali ni watu weneye pesa nyingi sana, jambo ambalo sio kweli hata kidogo. Wanaoweza kutembelea hifadhi mara kwa mara , sio kwa sababu wana fedha nyingi ila ni kwasababu wana mipango mizuri na fedha wanazopata. Hivyo ni suala la mipango  na malengo na sio suala la kuwa na pesa nyingi. Pesa kila mtu anapata kwenye maisha yake lakini kila mtu ana matumizi yake binafsi, hivyo kwenye matumizi yao huwa wananunua vitu vingi na kulipia mambo yote ya msingi kwenye maisha yao kama vile  ada za watoto, chakula, kodi za nyumba, matibabu na mengine mengi. Lakini hakuna hata pesa wanayoweka pembeni kwa ajili yao.

Kumbuka hili siku zote, kutembelea hifadhi na maeneo mengine yenye vivutio sio dhambi wala anasa, bali ni moja ya hitaji lako la msingi kuwa na mapumziko ya mwili wako na kufurahia maisha na fedha zako ulizozipata kwa kufanya kazi. Hivyo jitengee hela kidogo kidogo kwa ajili ya kutembelea hifadhi na maeneo ya vivutio, hii ndio iwe hela yako ya starehe, kuwa na starehe na familia yako, tembelea maeneo ambayo huajawahi kufika, furahia maisha yako kwa kujiwekea ka bajeti kadogo kadogo kwa ajili ya starehe. Hata kama itachukuwa muda mrefu kufikisha kiasi hicho ambacho unahitaji kwa ajili ya kutembelea maeneo ya vivutio, endelea kujiwekea hako kautaratibu wewe mwenyewe au kama unafamilia fanya hivyo pia.

Maeneo ya vivutio huwa na bei tofauti tofauti, hivyo unapaswa kujiwekaea malengo na kujua mwaka huu unataka kutembelea hifadhi gani au unataka kwenda kuona vivitio sehemu gani, elewa hilo mapema itakusaidia kujipanga na kujua utaweka akiba kiasi gani kila mwezi au kila wiki kwa kadri ya utaratibu utakaoona unakufaa kufikia ndoto zako. Kwa mfano unataka kutembelea hifadhi ya Taifa ya Katavi mwaka huu, tafuta kujua gharama zote za Hifadhi ya Katavi, elewa jinsi unavyoweza kufika, pia ni vema sana kujua kwa nini unataka kwenda kutembelea hifadhi hii, nini ambacho kimekuvutia kutembelea hifadhi hii ya Katavi, hivyo ukishajua gharama na jinsi ya kufika sasa jipange ujue unawezaje kufikia gharama hizo ili uweze kutembelea hifadhi ya Katavi.

Unaweza kuwa na mfuko ambao umeupa jina la Katavi, halafu mnakuwa mnachangia kiasi mnachokubaliana na familia yako. Pia ni vizuri kabla ya kupanga ni kivutio gani utembelee, kaa chini na familia yako, kama unayo kisha mpange mnataka kwenda kutalii au kutembelea maeneo gani kwa kipindi husika, hivyo panga na familia yako kisha, jua ni gharama kiasi gani kinatakiwa, kisha mnaweza kushirikiana kuchangia mfuko huo wa starehe kwa ajili ya kutembelea hifadhi na vivutio mbali mbali.

Hivyo kama unataka kutimiza ndito zako mapema, anza kuwa na utaratibu kama niliokueleza hapo juu, pia kumbuka fedha unazoweka ni lazima zitunzwe kwa nidhamu kubwa sana ili zitumike kufanya kitu halisi mlicho kipanga. Nawashukuru sana, watanzania wote kwa kusoma makala haya, mshirkishe na mwenzako maarifa haya, ili na yeye kama ana ndoto ya kutembelea hifadhi basi atasidika na kuchukua hatua.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683248681

hillarymrosso@rocketmail.com