Zaidi ya asilimia 21 (21%) ya viumbe aina ya reptilia wapo hatarini kutoweka duniani. Reptilia ni wanyama wenye damu baridi, ambao miili yao ina magamba, na pia hutaga mayai.

Mfano wa reptilia ni nyoka, mamba, mijusi, kenge, kobe na vinyonga. Viumbe hawa wanaishi kwenye mazingira ya aina mbali mbali mfano, nchi kavu, majini.

Aina mbali mbali za Reptilia. Picha kutoka: lookingfordiagnosis.com

Reptilia wanapatikana maeneo mengi misituni, jangwani, milimani, mabondeni, maeneo oevu, kwenye mapango juu ya miti, mashambani na  hata kwenye makazi ya watu.

Viumbe hawa wana umuhimu mkubwa kwenye mazingira yao, mfano nyoka wanasaidia kupunguza idadi viumbe waharibifu kama vile panya. Baadhi ya mijusi wanatumika katika uchavushaji wa mimea na wengine wanatumika kama chakula kwa viumbe wengine kama ndege walao nyama.

Mijusi wanasaidia kudhibiti ongezeko la wadudu kama mbu, buibui na kusaidia wasiongezeke kupita kiasi na kusababisha madhara kwa viumbe hai wengine kama binadamu.

Reptilia pia wanafaida kiuchumi watalii wengi wanatembelea maeneo yenye viumbe hawa, kuona na kujifunza kuhusu nyoka, vinyonga, mamba na mijusi.

Pamoja na faida hizo kadhaa, bado  Reptilia ni kundi la wanyama ambao wanakabiliwa na changamoto nyingi sana. Kwanza, ni moja ya makundi ya viumbe hai ambao hawana taarifa nyingi. Lakini pia ni aina ya viumbe waliokosa mvuto kwenye masuala ya utafiti sehemu nyingi duniani.

Mfano, Oliver Speight pamoja na wenzake walifanya utafiti wa kina, uliochapishwa Machi mwaka 2025. Katika utafiti huo walipitia makala na majarida kisayansi zaidi 700, ambayo yameandika kuhusu reptilia.

Watafiti hao waliibua mambo ya msingi kuhusu reptilia, walionyesha kuwa ni wanyama ambao wanabaguliwa na hawapewi kipaumbele kwenye tafiti na miradi ya uhifadhi.

Miradi mingi ya uhifadhi inalenga kuwafikia wanyama wakubwa na wenye majina makubwa kama vile tembo, faru na simba,  ni nadra sana kuona miradi mikubwa ya uhifadhi wa reptilia.

Hali hii imesababisha kukosekana kwa hamasa na taarifa nyingi za viumbe hawa. Mfano, hakuna taarifa za kutosha kuhusu reptilia katika sehemu za Kusini mahariki mwa Asia, Afrika Magharibi, Amerika ya Kusini na Kusini mwa jangwa la Sahara.

Tafiti nyingi na hata machapisho mengi yametafiti nchi kama Marekani na Australia. Mwandishi anahoji kuhusu maeno yenye uwezekano mkubwa wa kuwa na wanyama hawa hayajafikiwa kifedha na kitafiti.

Katika moja ya majibu ya utafiti huo ulionyesha kuwa nchi zenye mapato makubwa na zenye hali nzuri kiuchumi ndio zimefanya vizuri katika tafiti za viumbe hawa na pia uelewa wa jamii kuhusu uhifadhi wa viumbe hawa upo juu kulinganisha na maeneo mengine.

Hii ina maana kuwa, ukosefu wa tafiti za kutosha na miradi ya kutosha kuhusu uhifadhi wa reptilia inachangia sana wanyama hawa kuendelea kutoweka na kupungua kutokana na kukosa elimu na utambuzi wa uhifadhi wa wanyama hawa.

Watu wengi kwenye nchi ambazo zimewekeza kwenye uhifadhi wa reptilia wana uelewa mkubwa wa reptilia na pia wanahamasika sana katika uhifadhi wa viumbe hawa. Zaidi soma makala hiiSwila wa Msumbiji: Nyoka Mwenye Sumu Kali Ambaye Watu Wengi Hawamjui

Tovuti ya Wikipidia inaonyesha watu wengi wanafuatilia na kutafuta taarifa za baadhi ya reptilia kama nyoka. Matokeo yanaonyesha aina ya nyoka wanaofuatiliwa kutafutwa zaidi mtandaoni ni wale wenye sumu na walio hatari. Ingawa kuna idadi ndogo ya machapisho ya kisayansi kuhusu aina hiyo ya nyoka. Zaidi soma makala Mjue Swila Mwekundu: Nyoka Wenye Uwezo wa Kujihami kwa Sumu

Hii inamaanisha kuwa, idadi kubwa ya viumbe hawa haifahamiki na watu wengi. Hii inaweza kuwa na madhara katika uhifadhi wa viumbe hawa, kwasababu kama watu hawajui maana yake hawawezi kutoa kipaumbele kuwalinda wala kutunza mazingira yake.

Utafiti huo umegusia baadhi ya changamoto zinazowapata reptilia sehemu zote duniani, kama vile kubadilika kwa matumizi ya ardhi, mfano upanuzi wa maeneo kwa ajili ya kilimo, ujenzi wa barabara, uchimbaji wa madini na ujenzi wa makazi ya watu.

Biashara ya reptilia imekuwa ikishika kasi sana sehemu nyingi duniani, mfano, matokeo ya utafiti uliochapishwa mwezi Mei, 2024, na Maxim Conrad Isaac na wenzake unaonyesha kuanzia mwaka 2000-2019 zaidi ya vinyonga hai 1,128,776 kutoka kwenye aina 108 za vinyonga wameripotiwa kuuzwa na kusafirishwa duniani.

Katika kipindi hicho pia zaidi ya vinyonga 193,093 kutoka katika aina 32 za vinyonga walitoka Tanzania. Hali hii inaonyesha ni kwa kiasi gani viumbe hawa wameingia katika mahitaji makubwa ya kibiashara duniani, ambayo inatishia kuendelea kupungua kwa kasi. Hata hivyo, uwepo wa biashara haramu za viumbe hawa umetajwa sana sehemu nyingi duniani, ikiwemo Tanzania.

Aidha, kushamiri kwa mimea vamizi imekuwa ni janga kubwa kwenye maeneo mengi ya hifadhi za wanyama na misitu, mimea vamizi inaondoa na kuharibu makazi na chakula cha viumbe hawa hivyo kusabisha kukimbia au kufa.

Mabadiliko ya tabia nchi, dunia ya leo tunashuhudia mabadiliko makubwa ya tabia nchi, maeneo mengi yanaendelea kuwa majangwa, mvua za mafuriko, ukame na kubadilika sana kwa hali ya hewa na majira ya misimu kama vile mvua na jua. Hizi ni baadhi tu ya changamoto kwa viumbe hawa, ambazo zinaweza pia kuwa majanga kwa viumbe wengine.

Wengi wetu tunapoangalia uhifadhi na utunzaji wa mazingira tunaangalia tu viumbe wenye majina makubwa kama tembo, simba, twiga, chui, faru, nyati nk.

Wanyama hawa maarufu na wenye majina makubwa mara nyingi wanapendelewa katika uhifadhi na kupata fedha na miradi mingi ya uhifadhi wake.

Pia kwasababu ya umaarufu wao, wamekuwa ni wanyama wanaopewa muda mwingi na vipindi vingi kwenye kwenye vyombo vya habari kuliko wanyama wengine hasa jamii ya reptilia.

Hali hii inajenga picha kwa jamii kuwa uhifadhi unawahusu wanyama wakubwa kama tembo, chui, simba, twiga nk. Pia inapunguza hamu ya jamii kupenda viumbe wengine wadogo kama mijusi, kenge, vinyonga.

Huenda hii ndio imepelekea mwelekeo na mvuto wetu kwenye uhifadhi na tafiti. Watu wanafanya tafiti kwa viumbe wanaowavutia zaidi, viumbe wanaopendwa na watu wengi, na wenye majina makubwa.

Hata watoto wetu wanaoangalia picha na video za wanyama hao wenye majina makubwa watakuwa wanajua uhifadhi ni wa wanyama wenye majina makubwa kama tembo, simba, chui, twiga, faru, nyati, nk. Maana ndio wanaoonekana mara kwa mara kwenye luninga (TV) zetu na ndio tuliowapa kipaumbele.

Hii inaweza kujenga picha kuwa endapo pori au hifadhi fulani isipokuwa na hao wanyama wakubwa na wenye majina makubwa inaweza kubadilishiwa matumizi kuwa mashamba, au ujenzi.

Tafiti za kutosha hasa kwa reptilia zinaweza kujenga uelewa mkubwa kwa jamii, na pia zitajenga ufahamu wa kuhifadhi maeneo mengi yanayotuzunguka kama vile maeneo oevu, misitu na mapori ya vijiji ambayo yana viumbe hawa.

Sio kwasababu tembo au simba hawapo kwenye huo msitu au pori ndio ubadilishiwe matumizi, inaweza kuwa ni makazi muhimu ya viumbe wengine muhimu kama reptilia.

Tupunguze kasi ya kuharibu mazingira, hasa ukataji miti, kuchoma mioto, kuchimba madini maeneo ya hifadhi, kuharibu maeneo oevu, na vyanzo vya maji ambako ndio makazi ya viumbe wengi wadogo.

Napendekeza tuongeze kasi ya kutafiti wanyama walio katika kundi la reptilia, tukazene kutoa elimu kuhusu viumbe hawa na umuhimu wake katika mazingira yetu.

Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com