Habari msomaji wa makala za Wildlife Tanzania karibu tena kwenye siku ya leo tujifunze mambo mazuri sana. Jana majira ya jioni niliona tangazo ambalo lilinishangaza na kuniacha na furaha kuu ambayo ilinishinda kukaa nayo mwenyewe, ndipo nikakaa chini kuandika makala hii ili nikushirikishe msomaji wangu na Watanzania wengine waweze kufahamu na kutumia fursa hii ya kipekee sana kuwahi kutokea kwa Watanzania wote waliopo Dodoma. Hii ni fursa nzuri sana ambayo imetolewa na Shirika la Hifadhi Za Taifa TANAPA, ni ofa ambayo hupaswi kuikosa kabisa.
Kazi yote hii imefanywa na TANAPA ili kuwahamasisha Watanzania kuinua utalii wa ndani kwa kuweka ofa mbali mbali na kutoa nafasi za watu kwenda kutembelea vivutio vilivyopo katika nchi yao wenyewe kwa masharti nafuu kabisa, hivyo Mtanzania mwenzangu hili sio la kukosa kabisa. Kwa wale waliokuwa na ndoto za kutembelea hifadhi za Taifa basi ndoto zenu zimetimia kabisa. Hapa utalipia gharama kidogo sana ili kuona vivutio ulivyokuwa unavisikia na kuambiwa kwa miaka mingi bila wewe mwenyewe kuona kwa macho yako. Sasa sijui utajiteteaje hapa, maana ni bonge la ofa na utaratibu wanaoutumia ni salama kabisa kwa kuwa watakusafirisha wenyewe na kukutembeza wenyewe, huitaji kuuliza uliza kwa watu wengine ili ujue uanakotaka kwenda. Utafurahia tu.
Utaratibu wao ni mzuri kabisa kama walivyoainisha kwenye tangazo lao waliliotoa wameeleza kwa lugha rahisi kabiasa kwamba, kutakuwa na safari za kwenda kutalii Tarangire na Ruaha kutokea DODOMA wakati wa maonyesho ya Nanenane kwa gharama ya shilingi elfu 60 (60,000) kwa mtu mzima na shilingi elfu 40 (40,000) kwa watoto (miaka 5 – 16).
Gharama hizi zitahusu usafiri, kiingilio, mwongoza wageni na malazi ndani ya hifadhi.
Chakula na vinywaji utajigharamia .
Mambo muhimu ya kuzingatia
Ofa hii ni kwa watanzania tu.
Watoto chini ya miaka 5 hawaruhusiwi.
Tozo hii ni pamoja na VAT.
Ili kulipia na kujiandikisha tembelea banda la TANAPA ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika viwanja vya Nanenane Dodoma kuanzia tarehe 28/07/2017 hadi 07/08/2017.
Hilo ndilo tangazo lilivyo, hivyo wakazi wa Dodoma hii ni fursa yenu kuitumia ipasavyo kutimiza ndoto zenu za muda mrefu. Uzuri wa tangazo hili ni kwamba unatembelea hifadhi mbili hivyo ni uamuzi wako mwenyewe kuamua kwenda Ruaha au Tarangire, kwa mfano kama uliishaenda Tarangire unaweza kupanga kwenda Ruaha. Au kama ulishaenda kote basi nenda sehemu ambayo ni chaguo lako mwenyewe.
Kwa namna ya kipekee kabisa nilipongeze Shirika la Hifadhi za Taifa kwa kazi kubwa na nzuri sana wanazofanya kuinua utalii wa ndani na kutoa nafasi kubwa kwa Watanzania kutumia fursa mnazotoa ili watembelee na kujionea uzuri wa maliasili zinazopatikana kwenye hifadhi zetu. Nimefurahi sana kuona jambo hili na tangazo kama hili, kwakweli ni hatua nzuri sana ya kuwajengea Watanzania utamaduni wa kutembelea hifadhi za wanyama. Nawaunga mkono kwa asilimia 100. Tupo pamoja sana.
Mwisho, nawatakia Watanzania wenzangu kila la kheri kwenda kutembelea hifadhi za Taifa za Tarangire na Ruaha, kwa kweli mmechaguliwa hifadhi nzuri sana zenye vivutio vingi na wanyama wengi sana. Ukienda Tarangire utashangaa sana kwa hifadhi hii yenye tembo wengi na idadi kubwa sana ya ndege. Ukienda Ruaha ndio usiseme, ni hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania, njoo uuone Mto Ruaha Mkuu. Karibuni sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
0742092569/06838683
htt://www.mtalaamu.net/wildlifetanzania