Mchwa ni jamii ya wadudu ambao huishi kwa kujenga viota ardhini, kwenye miti, kuta za nyumba na magogo ya miti. Mchwa ni wadudu ambao hawana asili ya ukali au vurugu endapo viumbe wamevamiwa na viummbe wengine kwenye makazi yao na hawawezi kupambana na wadudu wengine wakorofi kama sisimizi. Wadudu hawa jamii ya mchwa husihi katika koo ambazo kitaalamu zinaitwa colonies. Koo za mchwa huchangia katika ukubwa wa kichuguu pia hutegemeana na idadi na aina ya mchwa. Kwa mchwa wakubwa vichuguu huwa vikubwa na kwa mchwa wadogo vichuguu huwa vidogo.Vichuguu vya mchwa mara nyingi hupatikana hasa maeneo ya kitropic , yenye udongo aina ya mfinyanzi na kichanga isipokuwa maeneo yenye Calcium nyingi. Vichuguu hivi havifanani kwa muonekano wa rangi na maumbo.
Muundo wa vichunguu una matabaka mawili ambayo ni , tabaka la udongo mgumu na tabaka na tabaka lenye matundu ya kupitishia hewa na kuwafanya mchwa kuwa imara na kupata hewa kwa urahisi.
Tafiti zinaonesha ,kuwa utengenezaji wa vichuguu kwa mchwa huanza kwa mchwa mmoja kutoa harufu (kemikali) na kuwavutia mchwa wengine kudondosha udongo sehemu moja.Uwepo wa vichuguu vya mchwa katika eneo fulani ni moja ya kiashiria cha kibaolojia kuonesha kuwa ardhi ina rutuba ya kutosha. Sambamba na hili, mchwa wanafahamika kisayansi kama mainjinia wa ikolojia (ecological engineer) kwani uwepo wao huboresha ardhi na kuifanya kuwa yenye rutuba.
Ujenzi wa vichuguu vya mchwa huanza kwa kukusanya na kusafirisha mabaki ya viumbe hai kama mimea na wanyama, pia punje ndogo za mbegu na udogo kwa kuchimba toka sehemu tofauti na kwenda kuweka sehemu moja(kwa mchwa wanaojenga vichuguu kwenye miti),ila kwa wanaojenga ardhini hutoa udongo chini ya ardhi na kuuweka sehemu ya juu.
MUUNDO WA VICHUGUU.
Muundo wa vichuguu au vijenzi hutofautiana kulingana na aina ya udongo na mabaki ya viumbe.Vichuguu ni kitovu cha rutuba katika ikolojia na hutofautiana kulingana na muda na nafasi (mahali) ambapo kichuguu hujengwa. Vijenzi vya vichuguu hupatikana maeneo karibu na kiota au kichuguu kinapojengwa. Vitu muhimu ni kama vile mabaki ya mimea( majani), wanyama pia na udongo laini wa tabaka la chini ya ardhi. Asili ya vichuguu vina udongo wa mfinyazi ambao unawezesha kutunza maji na rutuba na kuzuia mmomonyoko wa udongo. Pia mchwa hujenga vichuguu kwa kutumia mate yao ambayo husaidia kufanya udongo kushika vizuri na kuwa imara. Kichuguu huweza kudumu kwa muda wa miaka 20 na Zaidi. Baadhi ya virutubisho muhimu ambavyo hupatikana kwenye vichuguu ni kama vile Calciuma+,Magnesium,Nitrate,Phosphorus,B ,Manganese pia Potasium. Virutubisho hivyo vyote hupelekea mimea kustawi haraka hata kama liliharibiwa na wanyama wengine.
Pichani: mchoro ukionesha Muundo na namna mchwa wanavyojenga kichuguu
Hifadhi ya Tarangire na uwepo wa vichuguu
Hifadhi ya Tarangire ni miongoni mwa hifadhi zilizopo nchini Tanzania na maarufu kwa kuwa na vichuguu vingi kuliko hifadhi zote au ikiolojia zote za maeneo tengefu Tanzania. Tukiwa katika mafunzo ya vitendo katika ndaki ya uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori, tuliweza kushuhudia idadi kubwa ya vichuguu katika hifadhi ya Tarangire. Kama wataalamu wa mambo ya uhifadhi, swali tulilojiuliza ni kwamba je uwepo wa vichuguu unaweza kuathiri mtawanyiko wa wanyamapori? Na je nini kinafanya hifadhi hii kuwa na vichuguu vingi na vikubwa? Na je kuna umuhimu wa kuwa navyo katika mifumo mbalimbali ya kiikolojia?
Baadhi ya majibu ya maswali yetu ni kama ifuatavyo,
Katika vichuguu hupatikana nyasi nzuri ambazo hupenda kuliwa na Wanyama hususani kipindi cha ukame. Nyasi hizi huwa na virutubisho na kuwafanya Wanyama kama vile nyumbu, pundamilia na nyamera kupenda kuvitumia.
- Ndege na Wanyama kama vile vicheche hupenda kutumia vichuguu kama sehemu ambazo wanaweza kujipatia wadudu na ndege huweza kujenga makazi yao kwenye vichuguu
- Ustawi na mtawanyiko wa mimea,kutokana na wanyama kuchunga kwa wingi katika maeneo mengi hifadhini husababisha mimea kushindwa kustawi vizuri. Vichuguu vya mchwa huweza kurudisha hali ya mimea kuota, kukua na kutawanyika kwa jamii mbali mbali ya miti. Hii inatokana na kusafirisha maji na kuongeza unyevu katika ardhi kavu na kuongezeka kwa virutubisho katika udongo (madini kwa ajili ya ukuaji wa mimea). Mchwa wanachangia kuongeza utofauti wa maeneo katika ikolojia mfano eneo lenye vichuguu kuna ustawi mkubwa wa mimea na maeneo mengine ya kawaida ambapo mimea hukua kwa kiasi Fulani. Hivyo kupelekea kuongeza jamii za uoto na uzalishaji wa ikolojia
- Uwindaji kwa wanyama kama simba, duma na chui hutumia vichuguu ili kuweza kuona mbali kwa ajili ya kujipatia chakula .Katika kipindi hiki wanyama wala nyasi huja katika maeneo karibu na vIchuguu kuchunga na kujipatia virutubisho vingi. Pia mbwa mwitu wa Afrika na fisi huweza kuwinda katika vichuguu kwa kuwatafuta wanyama kama vile muhanga, ngiri na nguchiro.
- Makazi au maskani na ulinzi ya wanyama wengine kama muhanga na ngiri. Watu wengi wanahamu kuwa mnyama muhanga anawinda katika vichuguu, lakini mnyama huyu hutumia vichuguu pia kama makazi yake. Ngiri pia hutumia vichuguu kama makazi na kuweza kujificha na kujilinda dhidi ya adui wawindaji kama vile simba
- Kulinda mipaka kwa wanyama jamii ya swala (Topi) kwa kupanda kwenye vichuguu ikiwa ni ishara ya kulinda au kutangaza mpaka kitendo ambacho hufanywa na Topi dume na kujilinda dhidi ya mbung`o
- Husaidia katika mtawanyiko wa mbegu. Kutokana na mchwa kukusanya mabaki ya mimea, vinyesi vya wanyama na mabaki mengine ya wanyama wanapelekaea kutawanyika kwa mbegu za mimea mbali mbali hivo kusaidia kuchangia ongezeko la mitawanyiko ya mimea mbali mbali.
- Chanzo cha madini kwa wanyama wengi ambao huja kulamba udongo kando ya kichuguu. Hapa tunajifunza , tofauti na majani na nyama je nini chakula kingine cha wanyama hutumia. Tafiti zinathibitisha wanyama kulamba udongo wenye madini ikiwa wana upungufu wa madini katika miili yao, mfano pundamilia na nyumbu wanahama kwenda kutafuta sehemu zenye madini muhimu kama (Phosphorus na Calcium). hivyo hulamba kwenye vichuguu na maeneo yenye madini chumvi.
Katika ikolojia, mchwa wanaojenga vichuguu wameonekana kuwa na faida nyingi je kuna jitihada za kiuhifadhi zozote zimechukuliwa ili kuweza kulinda jamii hii ya wadudu? Je nini umejifunza kwenye hii Makala. Tunaomba maoni yako kupitia Email hapo chini.
Makala hii imeandikwa na waandishi wawili ambao ni wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro Tanzania. Pia makala hii imehaririwa na Alphonce Msigwa pamoja na Hillary Mrosso. Kwa maelezo zaidi, maswali, ushauri au maoni usisite kuwasiliana nasi. Tunakusihi uendelee kufuatilia makala zetu na kuwashirikisha wengine maarifa haya ili tujenge na kuhifadhi maliasili zetu adhimu.
WAANDISHI:
KAMANGA SHADRACK ANDREA KAMANGA
Email: bigstarshadrack@gmail.com
MARYLOVE GASPER SHOW
Email:marylovegasper478@gmail.com