Habari Watanzania wenzangu, hongera kwa siku nyingine ya leo, leo katika makala yetu tutakwenda kuangazia suala muhimu sana linalowasumbua watu wengi sana, na hapa kwenye makala hii nitatoa jibu zuri sana na ni njia inalotumiwa na watu wengi sana. Nikimaanisha ni njia ya wanayoumia wengi kupata fedha za kutalii na kutembelea vivutio mbali mbali msimu wa sikukuu na mapumziko mengine ya mwaka. Hivyo tutajifunza na kuona namna na sisi tunaweza kuitumi mbinu hii kwa ajili ya kufanikisha adhma yetu ya kutembelea sehemu yoyote unayotaka kutembelea.
Kwanza kabisa kwa utafiti wangu na uzoefu wangu kidogo wa kuishi na watu na kuwaelezea masuala mbali bali ya wanyamapori na vivutio vilivyopo Tanzania sijawaha kukutana na mtu ambaye hapendi kusikia au ktembelea vivutio na sehemu nzuri. Hili ni jambo la ajabu sana kuona kila mtu anatamani kuona wanyama, anatamani kutembelea maeneo yenye vivutio na hasa mbuga za wanyama, watu wengi sana wanapenda, huu ndio ukweli na uhalisia wetu. Haijalishi ni mwafrika au ni mzungu wote wana matamanio ya kuona vitu vizuri, wazee au watoto, hata kama ni tajiri au ni masikini bado wote wanatamani kuona vitu vya asili na vivutio hivyo.
Hili ndio jambo linaloniaminisha kuwa matamanio kama haya yaliyopo ndani yetu ni ya kiasili kabisa, naamini kuwa kila binadamu ameumbiwa kutamani kuona vitu vizuri kwa macho yake, kwa hiyo hii ni hali ya kiasili kabisa na ipo ndani ya kila mmoja wetu. Sema tatizo kubwa linalotusumbua ni mifumo na tamaduni zilizotulea, hazikuweka kipaumbele kwenye utambuzi wa sehemu hizi hasa huku kwetu Afrika, lakini kwasababu kitu hiki ni cha asili hakiwezi kujificha na kitaendelea kudai na kukupa shauku ya kukifanya. Mimi kama mwandishi nakushauri usikilize shauku yako kwenye eneo hili na uamue kutengeneza utaratibu wa kutembelea na kuona vivutio na mandhari mbali mbali inayopendeza ndani ya nchi yetu ya Tanzania na sehemu nyingine unazozipenda.
Jambo la kutembelea vivutio vya kitalii sio jambo linalohitaji fedha nyingi kama wengi wanavyodhani, bali ni jambo la mipango na maamuzi zaidi. Kwa mfano watu wengi wenye tabia na utamaduni wa kutembelea vivitio vya kitalii huwa wanapanga mapema kabisa, wanajua mwezi fulani tukipata likizo au tukiwa kwenye mapumziko yetu tunaweza kwenda kutembelea hifadhi fulani, hivyo wanapokubaliana na kuafikiana watatembelea hifadhi fulani, wanatafuta na kufuatilia gharama za eneo hilo, wakishajua gharama za eneo hilo, wanajipangia tena watumie siku ngapi kukaa huko siku moja, mbili au wiki. Wakishajiridhisha na taarifa hizo na eneo hilo, kazi inabaki kwao namna ya kupata fedha za kutembelea eneo hilo.
SOMA BARUA HII YA WAZI 3;Hatujakosa Muda wa kupumzika
Kwa mantiki hiyo utakuta watu wa namna hii wana nidhamu ya fedha sana, hivyo wana amua kuwa na akaunti au sehemu nyingine ambayo watakuwa wanaweka fedha wanazotenga kwa ajili ya kwenda kutalii. Hivyo kwa mahesabu yao unaweza kuangalia unahitaji kutunza fedha kiasi gani na kwa muda gani ili kufikia kiwango cha kutosha kutembelea hifadhi waliochagua kutembelea. Hii ndio njia kubwa wanayotumia watu wengi hasa wazungu ili kuja kutalii sehemu yoyote wanayotaka na nchi yoyote wanayotaka. Kwa msingi huo utaona kuwa hawakurupuki tu na kusema Kesho twende tukatalii Tanzania. Lazima kuwe na mipango, na wakati mwingine mipango ya muda mrefu ili kutimiza matamanio yao.
Kwetu watanzania sio kwamba hatuna fedha za kutalii, ni kwasababu tuna amini ili tukatalii tunahitaji kuwa na fedha nyingi ambzo hazina kazi. Mtu anakwambia mpaka apate hela ndio aanze kutalii, ukiwa na mitazamo ya namna hii ya kusema usubiri mpaka siku ambayo utapata fedha nyingi kwa mara moja ndio uende kutalii, jambo hili linaweza lisitokee, au hata kama litatokea unaweza usikumbuke kwenda kutalii hadi unashtukia fedha zimeisha na hujaenda kutembelea kvutio chochote. Ninachotaka kusisitiza hapa ni lazima tubadilike mfumo wa maisha yetu na namna tunavyofanya matumizi ya kila siku, tunataikiwa kufikiri na kupanga kufanya jambo hili, tena sio tu kufikiri bali kuwa na utaratibu wa kuandika matamanio yetu kwenye kitabu au daftari. Tena tukiwa na utaratibu wa kuandika mpaka na gharama za kutalii itatusaidia kutimiza malengo yetu tuliyojiwekea.
Pia kitu kingine cha kutusaidia ni kuwa na nidhamu kwenye mambo ya fedha hasa fedha ambazo tunazitenga kwa ajili ya kufanyia jambo fulani. Sio unaweka fedha kwa ajili ya kwenda kutalii mwisho wa mwaka halafu kabla hata ya kutimiza malengo yako unaingilia na kuiharibu tena ile fedha. Unatakiwa kuzingatia kutimiza malengo yako kwa gharama yoyote. Kipato chochote unacho pata unaweza kukitumia kufikia malengo yako, kaa chini pitia matumizi yako ya fedha na uone kama unaweza kuokoa fedha ambazo labda ulikuwa unazitumia bila kuwa na matumizi ya ulazima, unaweza kuzuia matumizi hayo kwa kupanga kuwa fedha hizo uzitumia kutembelea na kwenda sehemu tofauti na sehemu nzuri.
Nimalizie makala hii kwa kuseama, najua tumebakiza siku chache kumaliza mwaka huu, kuna waliopanga kutumia likizo na mapumziko ya mwisho wa mwaka kutembelea hifadhi za wanyama na sehemu mbali mbali za vivutio, wengine wanatamani kufanya hivyo lakini wanaona hawatakuwa na fedha au nafasi ya kufanya utalii. Nakushauri unaweza kuzingatia na kufanyia kazi tuliyojifunza kwenye makala hii na ukapata fedha, muda na sehemu nzuri ya kupumzika msimu huu wa sikukuu.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania