Mamba ni wanyama wakubwa wa spishi ya reptilia, wanaopatikana zaidi maeneo mengi ya kitropiki ya bara la Afrika, Asia, Amerika na Australia. Spishi hii ya reptilia inaundwa na wanyama wanaotambaa, wenye damu baridi, wanapumua kutumua mapafu huku ngozi zao zikiwa zimefunikwa na magamba badala ya ngozi laini au nywele. Mbali zaidi, mamba wanapatikana katika oda ya Crocodilia, ikijumuisha aina 24 za mamba wanaogawanyika katika makundi au familia 3. Familia hizo ni: Alligatoridae (spishi 8 za mamba wa Marekani), Crocodylidae (spishi 14 za mamba halisi) na Gavialidae (spishi 2 za mamba wenye midomo membamba wala samaki). Wanasayansi wanaamini mamba wanatokana na jamii za Dinosaria (dinosaurs) zilizoishi na kupotea zaidi ya miaka milioni 60 iliyopita kutokana na kuongezeka joto duniani, lakini mamba waliweza kuendelea kuishi hadi hivi leo.
Mazingira Wanayoishi
Mamba hupendelea zaidi kushi kwenye maji baridi kama vile kwenye mito, mabwawa, maziwa, bahari na ardhi oevu. Mamba pia huweza kuishi kwenye mapango yenye unyevu ambapo hujisitiri dhidi ya jua kali au maadui wake. Hii haimaanishi kuwa mamba hawapendi jua, bali ni kwa sababu wana damu baridi hivyo huhitaji jua kupandisha joto la mwili, lakini jua likizidi basi hulazimika kujificha kwenye maji au mapangoni ili kuepuka kuzidiwa na joto.
Kuna jamii moja tu ya mamba ndiyo inaweza kuishi vizuri kwenye maji chumvi, nayo hupatikana kusini mashariki mwa bara la Asia pamoja na bara la Australia. Mamba hawa pia ndo wenye maumbo na uzani mkubwa zaidi kuliko mamba wengine wote duniani (kufikia tani 1). Mamba wengine hupendela maji baridi yasiyo na chumvi.
Mamba wa maji chumvi
Kuna jamii kuu tatu za mamba barani Afrika ambazo zote huishi penye maji, ardhi oevu au tope pasipo na chumvi. Jamii hizi ni mamba wa Naili (Nile crocodile), mamba kibete (dwarf crocodile) na mamba uso-mwembamba au mamba mwenye mdomo mwembamba (slender-snouted crocodiles). Mamba wa Naili ndiye maarufu na mkubwa kuliko wengine kwa Afrika, na anapatikana katika nchi tofauti 26.
Mamba wa Naili (Nile Crocodile)
Mamba uso-mwembamba (Slender-snouted crocodile)
Mamba kibete (Dwarf Crocodile) (Chanzot: The animal facts)
Mamba wa Naili (The Nile Crocodile)
Mamba hawa wanapatikana kwa wingi Zaidi barani Afrika ukilinganisha na jamii nyingine za mamba, wakipatikana maeneo mengi kusini mwa jangwa la Sahara. Ukiachana na upatikanaji wao, umaarufu wao unachangiwa pia na ukubwa wa miili yao pamoja na ukali wao.
TAARIFA MUHIMU KUHUSU MAMBA WA NAILI
Ukubwa na muonekano
Madume huwa wakubwa kuliko majike, na huwa na urefu wa wastani kati ya mita 4-5 (futi 13-16) japo huweza kufikia mita 6-7 (Zaidi ya futi 20). Majike huwa wadogo kuliko madume na kufikia urefu wa wastani wa mita 3 (futi 10). Madume hufikia uzito wa kilo 750, na majike huweza kufikia kilo 500. Rangi za mamba wakubwa wa Naili ni kijivu kilicho changanyika na rangi ya mizeituni au kahawia kwenye mgongo huku tumbo likiwa na rangi ya manjano.
Kuzaliana
Mamba huwa na uwezo wa kuanza kuzaliania wafikapo umri wa miaka saba au zaidi.Dume na jike hukutana kwenye kina kifupi cha maji na kujamiiana. Jike huchimba shimo kwenye mchanga karibu na ukingo wa maji wa sehemu atakayokuwepo kisha hutaga mayai na kuyafukia humo. Jike anaweza kutaga mayai hadi 60 kwa msimu mmoja kisha kuyaatamia kwenye shimo hilo. Jike ataendelea kulinda shimo (kiota) lenye mayai kwa muda wa miezi mitatu hadi mayai yatakapoanguliwa.
Jinsia ya watoto wa mamba huamuliwa na joto la udongo wa sehemu mayai yalipoatamiwa. Joto likiwa la wastani (kati ya 28°C na 31°C) hupelekea kuanguliwa kwa mamba majike wengi, na likiwa juu zaidi ya 33°C hupelekea kuanguliwa kwa mamba madume wengi. Watoto wakianguliwa mama yao husikia sauti yao kutoka chini ya ardhi, na huanza kuchimba na kuwatoa humo. Huwakusanya kwa kutumia mdomo wake na kuwapeleka kwenye kina kifupi cha maji ambapo maisha yao huanza humo.
Mdomo
Midomo ya mamba hawa huwa mirefu na meno kati ya 64 – 68 yakiwa na urefu wa zaidi ya inchi 4 kwa kila jino. Pia huwa na ulimi uliogandamana na taya, ambao haumsaidii katika kula kama ilivyo kwa viumbe wengine, lakini huwasaidia kuzuia maji yasiingie kwenye koromeo wakizama majini. Ndimi zao hizi huwasaidia pia kutoa jasho pindi joto linapokuwa kali, ndiyo maana mara nyingi utawaona mamba wakiwa wameachama midomo yao kwenye kingo za maji wakati wa mchana.
Mamba akiwa ameachama mdomo kwenye ukingo wa mto (Chanzo: Adobe stock)
Mamba wana uwezo wa kuuma kwa nguvu kuliko wanyama wengine wote kutokana na nguvu kubwa iliyo kwenye taya zao. Wana misuli yenye nguvu sana inayoweza kubana pamoja taya hizi, lakini misuli ya kufungua taya haina nguvu sana. Hii inamaanisha mamba ni wagumu sana kuachia kitu walichoking’ata kwa nguvu. Kitaalamu, taya la mamba linaweza kubana kwa nguvu zaidi ya 3000psi ambayo ni mara nane Zaidi ya papa mkubwa.
Chakula
Mamba wa Naili huishi kwa kula mawindo au mizoga katika maeneo wanayoishi. Hula samaki na wanyama wakubwa pundamilia, nyumbu na swala, lakini pia huweza kula ndege na jamii nyingine za reptilia. Mbali zaidi, mamba anaweza kula hata wanyama wengine waloa nyama kama chui, simba, duma na fisi. Mamba akikamata windo kubwa huweza kula nyama sawa na nusu ya uzito wa mwili wake, halafu huweza kukaa hadi miezi kadhaa bila kula tena. Akila mawindo madogo kama samaki na ndege basi humlazimu kuwinda mara kwa mara. Mfumo wa umeng’enyaji wa mamba hufanyika taratibu, na huweza kumeng’enya hadi vitu vigumu kama mifupa anayokula.
Uwindaji
Mamba ni wawindaji wa kushtukiza, na hukaa kwenye kingo za maji ya mito, mabwawa au maziwa kusubiri mawindo yao yawafuate. Hujificha kwa kuzamisha sehemu kubwa ya miili yao kwenye maji na kuacha pua na macho juu, wakisogelea mawindo yao na kuyakamata kwa haraka kisha kuyavuta ndani ya maji. Wana uwezo pia wa kuona usiku, hivyo huweza kuyashtukiza mawindo yanayopita kwenye maji au karibu na kingo za maji na kuyavuta majini. Mamba wakikamata samaki basi huwatoka nje ya maji ambapo inakuwa ngumu kwa samaki kutoroka, kisha kuwala kwa urahisi zaidi.
Mamba akijirusha toka kwenye maji ili kumkamata nyumbu (Chanzo: BBC One)
Umri wa kuishi
Mamba wana uwezo wa kuishi kipindi kirefu, na huweza kufikia hadi miaka 80-90, lakini kwa wastani wakiwa porini huishi miaka 50. Hii inaweza kuwa sababu iliyopelekea mamba kuendelea kuwepo katika uso wa dunia kwa miaka mingi, licha ya kupotea kwa dinosaria wengine wa aina yake miaka mingi iliyopita. Mamba huweza kuendana na mazingira tofauti na kukabiliana na changamoto mbalimbali.
Licha ya yote haya, mamba wengi hufa kabla ya kufikia umri wa kupevuka hadi uzee. Takwimu zinasema kwa wastani, kati ya mayai yote yanayotagwa na mamba, ni asilimia 10 tu ndiyo huweza kuanguliwa. Mengine huliwa na kenge, tumbusi, nguruwe pori, nguchiro, nyani, fisi na mamba wengine. Lakini pia katika mamba wote wanaoanguliwa, ni asilimia moja (1%) tu ya hao mamba hufikia umri wa kupevuka.Watoto wa mamba huwindwa na samaki wakubwa, tai, nguchiro, fisi na wengineo. Mamba wa umri wa kati na wazee huweza kuuliwa na Boko (hippos) pamoja na binadamu. Makala nyingine kuhusu Mamba ipo katika linki hii isome kuelewa zaidi kuhusu Mamba Yafahamu Mambo Ya Kushangaza Kuhusu Mamba (Nile Crocodile)
Uhusiano kati ya mamba na binadamu
Ifahamike kuwa mamba wa Naili ni wanyama hatari sana na ni wawindaji hodari wanapokuwa kwenye mazingira yao. Ni hatari sana kwa binadamu kumsogelea au kumchokoza mnyama huyu kwani huweza kufanya maamuzi ya haraka na yenye kuhatarisha usalama wa binadamu. Takwimu zinaonyesha kila mwaka huripotiwa visa zaidi ya 300 vya mamba wa Naili kushambulia, kudhuru au kuua binadamu. Wakiwa nchi kavu, Mamba wakubwa wa Naili huweza kukimbia kwa kasi ya hadi kilomita 24 kwa saa lakini kwa umbali mfupi. Binadamu wengi wenye wepesi wa kukimbia huweza kuwashinda ardhini. Hali ni tofauti kwenye maji kwani mamba huweza kwenda kwa haraka na kufikia kasi ya kilomita 30 kwa saa, ambayo siyo rahisi hata kwa binadamu mwenye ustadi wa kuogelea kumshinda. Pamoja na hayo, zipo baadhi ya jamii ambazo huishi na mamba hawa kwa imani za jadi kama wazee wao, na ni mara chache sana mamba huwadhuru wanajamii hao.
Watoto wakiwa wamekaa mgongoni mwa Mamba (Chanzo: The Telegraph)
Nyongo ya Mamba
Nyongo ya mamba ni maarufu sana hususani barani Afrika ambapo inajulikana kuwa sumu kali yenye uwezo wa kuua binadamu na wanyama. Miongoni mwa jamii barani Afrika ambazo hutumia nyama ya mamba kama kitoweo, watu huogopa kula nyama hiyo endapo hawataona nyongo imetolewa kwa ustadi na kufukiwa chini au kutupwa mbali. Kumekuwa na visa mbalimbali za watu kupoteza maisha kutokana na kinachodaiwa kuwa ni kula nyongo ya mamba.
Nyongo kwa kawaida hutengenezwa na ini na kuhifadhiwa kwenye kifuko kidogo karibu na ini. Nyongo huundwa na vimeng’enya vyenye asili ya asidi (acid) na chumvi kwa ajili ya kuvunja vunja mafuta (fat) yanayoingia na chakula kwenye utumbo mdogo. Kwa kawaida nyongo isingeweza kuwa na madhara kwa binadamu lakini inaaminika kiwango cha nyongo kikitumika kwa wingi basi huleta madhara.
Tafiti mbalimbali zilizofanywa na wanasayansi duniani zimeonyesha kuwa nyongo ya mamba haisababishi kifo, baada ya kuijaribu kwa viumbe jamii ya ngedere na panya, ambapo hawakudhurika. Tafiti hizi zilifanyika baada ya taharuki kubwa iliyotokea nchini Msumbiji baada ya watu 75 kufariki kutokana na kilichosemekana ni kuwekewa nyongo ya mamba kwenye pombe. Wanasayansi walipima pombe ile na kukuta ina asidi ya Bongkrek ambayo ni sumu inayozalishwa na bakteria aitwaye Burkholderia gladioli pathovar cocovenenans anayeathiri mahindi au nazi. Pombe hiyo ilitengenezwa na mahindi ambayo yaliathiriwa na bakteria huyo, na baadhi ya wanasayansi kusema ndiye chanzo cha vifo hivyo. Bado kuna utata juu ya uhalisia wa nyongo ya mamba kusababisha vifo kwani halijafanyika jaribio kwa binadamu, huku Waafrika wakiamini ni sumu kali mno, wakati wanasayansi wakipinga hilo.
Hali ya uhifadhi
Shirika la kimataifa la uhifadhi wa mazingira (IUCN) linawataja mamba wa Naili kama viumbe ambavyo bado haviko kwenye hatari ya kutoweka duniani. Hii haimaanishi kuwa hakuna viashiria vinavyopelekea kuhatarisha usalama na uwepo wao kwa siku za usoni. Hali ya mabadiliko ya tabia ya nchi yanapelekea baadhi ya maeneo kukauka au kuzidi kupungua kwa maeneo rafiki kwa mamba kuishi. Binadamu pia wamekuwa wakizidi kufanya uwindaji hasa haramu (ujangili) wa kuwauwa kwa ajili ya kitoweo, mafuta na ngozi za mamba wa Naili, na kupelekea kuzidi kupunguza idadi yao.
Shughuli nyingine za kibinadamu zinazohatarisha hali ya usalama wa mamba wa Naili ni pamoja na uchafuzi na kufungwa kwa vyanzo vya maji. Maji yakiingia sumu na kemikali kutoka mashambani, mijini, viwandani na kwenye migodi hupelekea maisha ya mamba pamoja na viumbe wengine wa majini kuwa hatarini. Sehemu nyingine mito hufungwa na maji kupelekwa kwenye mashamba kwa ajili ya umwagiliaji wa mazao ya kilimo. Hii hupelekea kuhatarisha zaidi hali ya usalama wa viumbe hawa wenye sifa ya kipekee kabisa na faida kubwa kwenye ikolojia ya Afrika.
Mamba akiificha kwenye pango baada ya mto kukauka maji (Chanzo: Alamy)
Imeandaliwa na kuandikwa na, Ezra Peter Mremi na kuhaririwa na Bartholomew Mhina. Kwa maoni, ushauri, maswali na mapendekeza kuhusu makala hii unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii.
Ezra Peter Mremi- 0786078728/0756438692
(email: mremiezra@gmail.com)