Kuna vitu vya msingi tunatakiwa kuvielewa mapema ili kama tunapanga mipango yoyote ya maendeleo kama vile ujenzi, mashamba, au kitu kingine chochote ambacho kitachukua sehemu ya mazingira asilia tuliyo nayo. Kuna vitu tunatakiwa kujipanga na kuvifikiria kila siku ili kujipanga na kuweka utaratibu ambao hata kama idadi ya watu na makazi ya watu yataongezeka havitakuwa na athari kwenye mazingira ya viumbe hai kama vile misitu na wanyamapori. Nasema haya kwa sababu kila kukicha naona watu wanakazana kufanya mambo makubwa kwenye sekta zote za kilimo, miundombinu, na mawasiliano na biashara nk. Kila uwekezaji umekuwa unahitaji maeneo na sehemu nzuri za kuwekeza hivyo nguvu kubwa na maeneo yanayoangaliwa zaidi ni maeneo ya wazi, maeneo ya misitu na maeneo ya wanyamapori.

Siwezi kukataa maendeleo kwenye nyanja za uchumi ili kuboresha maisha ya binadamu, ili kufanya maendeleo hasa kuwekeza kwenye kiwango kikubwa cha kisasa ndio njia ya kuleta matokeo makubwa na kutoa fursa kwa jamii kunufaika kwa namna moja au nyingine. Kumekuwa na miradi na mashirika mengi kutoka sehemu nyingi duniani yanayokuja kutafuta maeneo ya kufanya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya kuinua uchumi wa watanzania na kutoa ajira. Haya yote ni mema na yanafaa sana kwani ndipo ambapo fursa za kuboresha maisha ya jamii yetu hutokea. Majaribu makubwa yanakuwa pale ambapo wawekezaji wanataka maeneo ambayo ni muhimu kwa maisha ya maelfu ya viumbe hai muhimu ambao ni kiini kwenye mfumo wa ikologia ya viumbe hai wote.

Manufaa ya kiuchumi ya miradi hii inapochanganuliwa na wataalamu wa uchumi inaonyesha ni makubwa na ya muda mfupi. Faida kubwa za muda mfupi zinakuwa na ushawishi mkubwa sana endapo jambo linachulikuliwa kisiasa. Kwa wanaofikiria manufaa ya vizazi vingi hawawezi kukubaliana na manufaa makubwa ya muda mfupi yaharibu manufaa yatakoyokuwepo kwa vizazi na vizazi hata kama manufaa hayo ni kidogo kidogo. Kwenye nchi zetu za Afrika ambako siasa ndio kila kitu tunashindwa kuona mbali kwasababu ya vitu vingi tunavyoviona sasa na kufikiri vitaendelea kuwa vingi siku zote. Siasa na uhifadhi wa misitu na wanyamapori ni vitu ambavyo vinakinzana sana, hasa linapokuja suala la kufanya maamuzi ya busara yanayohitaji busara na ukomavu wa viongozi.

Wengi kwasababu wameahidiwa na miradi hii kutatua matatizo ya muda mfupi ambayo yatakuwa na manufaa kwa jamii na kwao endapo itawaongezea muda wa kukaa madarakani, wanakubali kuingia mikataba ambayo haina tija, mikataba na makubaliano ambayo hayana manufaa ya kudumu na mazuri kwa jamii. Kuna wengine wamekwenda mbali zaidi hadi kubadili baadhi ya vipengele kwenye sheria ili wafanikishe adhma yao ya kutekeleza jambo ambalo halina manufaa kwa jamii na vizazi vijavyo, lakini pia kwa kuharibu mazingira na makazi muhimu ya wanyamapori na viumbe wengine adimu amabo endapo wapo hatarini kutoweka duniani.

Wakati naandika makala hii nimefikiri na kujifunza vitu vingi sana endapo mtu anataka kuanzisha kiwanda, biashara au mradi mkubwa ambao unahitaji eneo kubwa la ardhi kabla ya kufikiria kuongea na serikali husika ili kupata eneo la uwekezaji anatakiwa kujua angalau mambo ya msingi ili afikirie kwanza kabala ya kuchukua hatua za kutumia nguvu na ushawishi mwingi wa fedha na rushwa ili kupata eneo ambalo yeye mwenyewe anajua endapo atakubaliwa kuanzisha mradi huo sehemu hiyo mradi huo utaharibu kabisa mazingira ya mahali hapo. Hivyo basi mambo ya kuzingatia na kufikiri kwa kina endapo mwekezaji au mtu yeyote anataka kuweka mradi au kitu chochote kwenye ardhi afikiri mambo haya kwa kina;

Eneo ambalo nataka kuweka mradi wangu kuna vyanzo vya maji, chemichemi ambayo inategemewa na maelfu ya watu na viumbe hai?

Eneo ambalo nataka kuweka mradi wangu ni maeneo ya wanyamapori au ni karibu na maeneo ya wanyamapori?

Eneo ambalo nataka kuweka mradi wangu ni eneo la msitu au maeneo ya hifadhi ya misitu muhimu?

Eneo ambalo nataka kuweka mradi wangu ni njia au eneo la mapito ya wanyamapori?

Eneo ambalo nataka kuweka mradi wangu ni maeneo muhimu na adimu kwa wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka?

Eneo ambalo nataka kuweka mradi wangu ni eneo lenye uoto wa asili na miti mingi ya asili ambayo ni muhimu kwa hifadhi ya viumbe hai wadogo na wasioonekana?

Eneo ambalo nataka kuweka mradi wangi ni maeneo muhimu kwa ajili ya makazi na mazalia ya viumbe hai kama vile wanyama, ndege  na samaki?

Eneo ambalo nataka kuweka mradi wangu ni eneo oevu (wetlands)?

Eneo ambalo nataka kuweka mradi wangu ni Rafiki kwa afya za watu na jamii ya eneo hilo?

Kuna maswali mengi sana ya kujiuliza mwenyewe kabla ya kufikiria kununua au kutumia eneo hilo kama eneo la uwekezaji. Kuna masuala ya kisheria, sheria za ndani ya nchi, sheria za kimataifa na sheria nyingine za maliasili zinatakiwa kufahamimka na kufikiriwa endapo mtu anataka kuanzisha mradi wowote kwenye jamii. Mazingira salama kwa binadamu na wanyama ndio kitu muhimu cha kuangaliwa zaidi ya kufikiria kupata fedha nyingi. Endapo tutakuwa wakweli na waungwana kwetu wenyewe kuhusu namna bora ya kuanzisha na kuendelea mradi sehemu zenye mambo muhimu kwa ajili ya ikologia ya watu na wanyama hatupaswi kufikiri kwa faida za muda mfupi, bali kwa muda mrefu.

Endapo wawekezaji watakuwa na macho ya kuangalia mambo kwa namna hiyo, hata kama watashawishiwa na serikali au na watu wengine kuanzisha mradi sehemu zenye maliasili muhimu za wanyama na mimea, watasaidiana na serikali na wadau wengine kufikiri na kuangalia eneo jingine ambalo halitakuwa na madhara kwa viumbe hai na maisha ya watu. Pia wale wanaotafuta wawekezaji, mfano serikali na mashirika au watu binafsi wanatakiwa kujua jambo hili mapema ili mtu anapokuja kuwekeza kwenye maeneo hayo ajue na aelekezwe kwa ufasaha faida na madhara ya muda mfupi na ya muda mrefu endapo mradi huo utaanzishwa maeneo hayo.

Pia kama kuna kamati za ushuri kwa wawekezaji na serikali (au kama hzaipo ziundwe) kwa ajili ya kushauri namna bora ya kufanya uwekezaji bila kuathiri ardhi, misitu, wanyamapori, maeneo muhimu ya urithi na mambo ya kale.  Wanatakiwa wajue na kufanya kazi yao kwa weledi na uadilifu wa hali ya juu sana ili kusimamia ukweli na sio kuyumbishwa na upepo wa siasa za njaa ambazo zinaleta madhara kwa maliahai zetu na jamii yetu huku zikiwanufaisha wachache.

Aidha ifahamike kuwa hakuna sehemu yoyote duniani yenye migogoro kama ardhi, ardhi inagombaniwa kila kukicha, kila mtu analilia ardhi, watu wamepigana vita kwa ajili ya ardhi, watu wameuana na kuumiza na kwa ajili ya ardhi. Vita vingi vinavyotokea na kuendelea duniani chanzo kikubwa ni ardhi. Hivyo basi ardhi sio kitu cha kugawa na kutoa kama nguo, ardhi ni maisha, ardhi ni nguvu, ardhi ndio sauti ya mnyonge, kama huna ardhi huna sauti, na kama huna ardhi unahesabika kuwa maskini mkubwa. Historia inaonyesha jambo hili vizuri, kama huna ardhi ni sawa na kuwa mtumwa. Tuitunze ardhi yetu kwa kuweka sheria zinazoeleweka kwa wananchi wetu, tuwaelimishe na kuwaelimisha kila siku kuhusu umiliki wa ardhi na faida zake, hili ndio jambo tunalopaswa kuwafundisha wananchi wetu kila siku bila kuchoka. Kama hatuna ardhi hatuwezi hata kuwa na wanyamapori, misitu na maliasili nyingine kama mafuta, madini, gesi nk.

Kama huna ardhi huna uhuru.

Asante sana kwa kusoma makala hii, karibu kwa makala nyingine.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania