“Here is your country. Cherish these natural wonders, cherish the natural resources, cherish the history and romance as a sacred heritage, for your children and your children’s children. Do not let selfish men or greedy interests skin your country of its beauty, its riches or its romance.”
― Theodore Roosevelt
Moja kati ya sifa kuu kwa kiongozi ni kuwa na maono; maono mapana na yanayoinufaisha kizazi cha sasa na kizazi kijacho. Uongozi sio nafasi uongozi ni maono, na sio tu maono lakini maono yenye tija. Nimetambua jambo hili kwa vionozi wengi waliowahi kufanya mambo makubwa kwenye nafasi zao hapa duniani. Viongozi wote waliowahi kufanya mambo makubwa bado historia na dunia inaendelea kuwataja na kuwakumbuka kwa mazuri walioyafanya kipindi cha uhai wao; nimeona jambo hili kila kitu ambacho kilifanywa na kiongozi mwenye maono kilikuwa na faida kwa watu wote, lakini pia faida kwa kizazi kijacho au kizazi cha mbele. Hembu tujifunze maneno, nukuu ya kiongozi mashuhuri na maarufu kuwahi kuishi hapa duniani.
Katika nukuu hii ambayo ilitolewa na moja kati ya aliyewahi kuwa Rais maarufu sana wa Marekani Theodore Roosevelt. Ni maneno yenye hekima na busara sana kwenye uhifadhi wa maliasili za nchi. Historia inaonyesha rais huyu alipenda sana maliasili za nchi yake na alikuwa na muda wa kuhamasisha uhifadhi wa rasilimali hizo kwa nchi yake.
Kwa maneno yake kwenye nukuu hiyo yanaonyesha jinsi alivyokuwa amedhamiria kuinua na kuhamasisha uhifadhi wa wanyamapori kwa vizazi vya sasa na vijavyo, alipenda kuona mazingira na maliasili zilizopo zinaendelea kuwanufaisha watu wote. Anataja uzuri wa urithi ambao upo kwenye nchi kama vile maajabu, mambo ya historia na mambo yote ya kiasili kuwa ni urithi ambao unatakiwa kunufaisha sio kizazi hiki pekee bali hata kwa vizazi vingi vijavyo.
Kwenye nukuu hii anatuasa kuzuia na kuwadhibiti watu wote wenye nia mbaya na wenye uroho na maslahi binafsi ya kutumia maliasili za umma kwa maslahi yao wenyewe. Haya ni mambo ambayo tukiyaacha yatatugharimu sana kama taifa, watu wachache wanatumia vibaya maliasili zetu, tena wanatumia vibaya bila kuangalia wanayaachaje mazingira ya asili.
Picha pana tunayoipata kwa Rais huyu mashuhuri ni namna anavyotutazamisha maisha ya baadaye kwa kutupa jukumu kubwa la kusimamia na kizilinda maliasili za nchi yetu kwa gharama yoyote, vitu tunavyoviona na kuvifurahia vinatakiwa viendelee kuwepo na viwafurahishe na watu wa kizazi kingine. Tunatakiwa kuwa na nidhamu kali sana ya kujizuia tamaa zetu na kuwazuia wengine wenye tamaa na wanaotaka kutumia na kuharibu rasilimali hizi adimu kwa maslahi yao binafsi.
Aidha, tuna wajibu mkubwa sana kama taifa wa kusimamia na kuhakikisha uhifadhi wa maliasili zetu unakuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo. Tunaakiwa kuacha urithi huu wa maliasili kwa watoto, wajukuu na vitukuu wetu katika hali nzuri na bora zaidi kuliko tulivyoachiwa au tulivyo kuta. Tunatakiwa kuwa na mipango mizuri ya kuboresha malisili zetu kama vile wanyamapori na misitu sio tu ili viwafikie vizazi vijavyo lakini urithi huu unatakiwa kuwafikia ukiwa katika hali bora zaidi.
Ahsante sana
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569