Uzoefu kidogo nilio nao kwenye hifadhi za Kusini hasa Hifadhi ya Taifa Ya Ruaha umenifanya nishauri wanafunzi, waliimu na watalaamu wengine wanaotaka kufanya utafiti au mafunzo kwa vitendo kwenye maeneo mbali mbali yanayohusisha wanyamapori, utalii, na mambo mengine yanayohusiana na maliasili. Mara nyingi tunapozungumzia hifadhi za kusini mwa Tanzania watu wengi wanapata picha mbali mbali kwenye akili zao. Hifadhi hizi ambazo zimekuwa kama zimesahaulika na watanzania wengi zimekosa umaarufu ukilinganisha na hifadhi nyingine za kaskazini mwa Tanzania, kwa mfano ukamwambia mtu kati ya hifadhi ya Katavi na hifadhi ya Serengeti ungependa kutembelea hifadhi gani, moja kwa moja atakwabia Serengeti. Ukiangalia hapo utaona kunasababu nyingi sana mtu kuchangua Serengeti badala ya Katavi.
Wakati nikiwa chuoni mwaka wa tatu ambapo kila mwanafunzi lazima afanye utafiti wake mwenyewe ili aweze kuhitimu elimu yake ya chou kikuu, huwa tunafanya kwenye maeneo mbali mbali, mimi nilitamani sana kufanyia utafiti wangu kwenye hifadhi ya Serengeti au Kilimanjaro. Kama ilivyo kawaida sikuwa mimi pekee niliyekuwa na matamanio hayo ya kufanyia utafiti katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti bali tulikuwa wengi. Nakumbuka kabisa na sidhani kama kuna mtu alifanyia utafiti wake hifadhi ya Katavi au hifadhi ya Ruaha. Lakini wengi tuliishia kufanyia tafiti zetu hifadhi ya Mikumi, Saadani, wengine walienda Serengeti, lakini hakuna aliyekwenda Katavi. Hii inaonyesha ni jinsi gani tulivyo na ufahamu na taarifa chache sana kuhusu hifadhi hizi za kusini. Mbali na hilo si wanafunzi tu hata walimu au wahadhiri wa vyuo hupenda sana kufanyia tafiti zao kwenye hifadhi hizi za kaskazini. Sio vibaya kufanyia tafiti kwenye hifadhi hizi, la hasha bali ninachotaka tuone hapa jinsi hifadhi hizi zilivyosahaulika kwenye kila nyanja.
Utajiuliza kwanini nakushauri ufanye utafiti wako au uanzishe mradi wako wa kuhifdhi wanyamapori kwenye maeneo haya ya kusini? Nitaelezea badhi ya sababu hapa ambazo unaweza kupata kwa upana wake mambo muhimu na ya kipekee ambayo yatafanya utafiti wako kuwa wa kipekee na mzuri wenye mvuto, kuliko kila mtu kukimbilia kufanyia utafiti wake Serengeti, au Mikumi au hifadhi nyingine za Kaskazini. Hizi ni baadhi ya sababu;
Maeneo haya hayajafanyiwa tafiti nyingi sana; mara nyingi wanafunzi na wanazuoni wengi hupenda kufanyia utafiti kitu ambacho hakijafanyiwa utafiti na watu wengine, ili kumpa uwanja mpana wa kuelezea utafiti wake. Ukiangalia baadhi ya tafiti chache zilizofanyika maeneo haya ya kusini utaona nyingi zinasema hakuna utafiti wa aina hiyo au unaoendana na huo umewahi kufanyika maeneo hayo. Hata taarifa kutoka mamlaka ya hifadhi za taifa zinakiri kuwa maeneo na hifadhi nyingi za kusini hazijafanyiwa tafiti nyingi na za kutosha kama ilivyo kwa hifadhi za kaskazini, hivyo nakushauri wewe unayetaka kufanya kazi nzuri kwenye utafiti wako karibu sana hifadhi hizi za kusini utafurahia mwenyewe, kwanza utapata taarifa nzuri kabisa na kujionea wewe mwenyewe kile unachokifanyia utafiti wako hivyo utafanya kazi yako kwa wakati na kwa uhakika.
Hifadhi hizi zina maeneo mengi ambayo hayajaharibiwa na shughuli za kibinadamu; kama tunavyofahamu shughuli nyingi za kibinadamu zilivyo na madhara makubwa endapo zitafanyika kwenye maeneo yaliyopakana na hifadhi, pia maeneo haya hayana msongamano wa watu na magari ambayo yanawafanya wanyama kuwa na tabia tofauti na zile za asili. Mfano kitabia ukimwangalia tembo au simba wa Katavi na tembo au simba wa Serengeti utakuta wanatabia tofauti kidogo, hii ni kutokana na kuwepo kwa mwingiliano mkubwa wa watu na magari katika hifadhi za kaskazini. Nakubaliana kwa asilimia kubwa sana tembo au simba wa Katavi atakuwa na utulivu na ile tabia yake ya asili kuliko tembo au simba wa Serengeti. Hata kama kuna kutofautiana kwenye mazigira na maeneo kuna tabia ambazo mnyama anazionyesha au anakuwa nazo endapo atasumbuliwa au kukiwa na mwingiliano wa watu na magari katika maeneo ya wanyamapori, nadhani hapa watanielewa vizuiri wale waliosoma tasnia ya uhifadhi wa wanyamapori au wanyama kwa ujumla. Hii ndio sababu ya mimi kukushauri kuja kufanyia tafiti zako maeneo haya ya hifadhi za kusini, ili kwa kiasi kikubwa utafiti wako uwe umelenga uhalisi wa kitu kikiwa kwenye mazingira yake halisi kabisa.
Utapata uwanja mpana wa kufanyia utafiti vitu vingi; vitu vingi sana kwenye maeneo haya havijafanyiwa utafiti, kwa mfano fisi, simba, chui, Nyati, watu na tabia za wanyama na watu kuhusu uhifadhi wa wanyamapori nk. Kimsingi kuna mambo mengi sana ya kuyafanyia kazi kwenye hifadhi hizi za kusini. Unajua unapokwenda mahali ambapo hujawahi kufika utaona fursa nyingi sana kulingana na jinsi unavyotaka kuona, utaona mambo mengi yanayotakiwa kufanyika utaona vitu vingi unavyoweza kufanya ukiwa pale. Hapo ndipo utakuwa na nafasi kubwa ya kuandika makala zako vizuri ambazo zitakuwa na msaada kwa jamii na kwa taifa kwa ujumla kuhusu uhifadhi na hatua za kuchukua.
Hakuna miradi mingi ya kitafiti kwenye maeneo haya ya kusini; kuna siku nilikuwa nasoma ripoti moja kuhusu hifadhi ya taifa ya Serengeti, nilishangaa sana kuona kuna miradi mingi sana, na ya muda mrefu, miradi hiyo yenye malengo mbali mbali lakini yote ikiwa na dhima kuu ya kuhifadhi wanyamapori na mazingira yao. Kwa upande wa kusini hili ni jambo ambalo tunatakiwa tuamke na kufanya, tuwekeze na kuweka miradi ya kuhifadhi wanyamapori hawa kwenye maeneo haya. Miradi inamanufaa sana kwa jamii na watu wanaozunguka hifadhi za taifa, kwani kwa asilimia kubwa miradi hii ndio inatoa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori, na kuwaonyesha watu na jamii kwa ujumla faida zitokanazo na uwepo wa wanyamapori. Ukiangalia kwa asilimia kubwa idadi ya miradi hii inamilikiwa na wazungu, na sasa wameanza kuhamia kwenye hifadhi za kusini, wengi wanaanza kuja Ruaha, wengine wanaenda Katavi nk.
Ningependa watu wazijue na kupenda kutembelea hifadhi za kusini kama wanavyofanya kwa hifadhiza kaskazini. Pia napenda watu wafahamu kwanini nashauri sana tafiti zifanyike nyingi kwenye hifadhi hizi, ni kwasababu tafiti hizi husaidia kwa mambo mengi ya maendeleo na uhifadhi wa wanyamapori, watu wanaposoma utafiti wako kuhusu sehemu fulani au kuhusu jambo fulani wanaweza kuona fursa za kimaendeleo kutokana na utafiti wako, lakini kubwa zaidi ni kwamba utafiti husaidia njia bora na za kisasa zaidi kwenye uhifadhi na usimamizi wa wanyamapori na maliasili nyingine.
Mwisho, nawakaribisha watu wote kutembelea na kujifunza mengi kwenye hifadhi hizi za kusini. Lakini kwa namna ya pekee wanafunzi kutoka vyuo mbali mbali vya ndani nje ya nchi kuchangamkia fursa hii nzuri. Kuna watu wanapata shida wanaesma sijui pa ufanyia utafiti wangu, kama utafiti wako unahusisha maliasili, utalii, au tabia za wanyamapori au uhifadhi, nakushauri na nakukaribisha kwenye hifadhi hizi za kusini.
Hillary Mrosso
Wildlife conservationist
0742092569
hillarymrosso@rocketmail.com