Kwa kawida wengi hudhani kwamba wanyama wa mwituni wote ni maadui. Lakini leo ningependa nikufahamishe kuwa si wote ni maadui, wapo wanyama ambao hushirikiana kwa pamoja licha ya tofauti zao za kibaiolojia, au hata aina hapa ninazungumzia utofauti wa spishi za wanyama husika.
Inashangaza kuona wanyama wanapendana na kusaidiana katika mazingira wanayoishi. Mara nyingi ushirikiano huu ni matokeo ya changamoto wanakutana nazo mwituni, waswahili wanasema umoja ni nguvu utengano ni dhaifu na mara nyingi kauli hii hudhihirika pale ambapo baadhi ya wanyama hushirikiana kwa pamoja kutatua changamoto wanazokutana nazo.
Ushirikiano huu kwa kiingereza hujulikana kama “Mutual Relationship” ambapo pande zote mbili hunufaika kutokana na mashirikiano ambayo yatakua baina yao.
Wapo wanyama ambao hushirikiana ili kujilinda na maadui, wapo wengine ambao hushirikiana ili kujitengenezea njia rahisi ya kujipatia chakula, wengine hushirikiana ili kujilinda dhidi ya magonjwa, pia wapo wengine ambao huenda mbali zaidi na kushirikiana kwaajili ya kuweka miili yao safi au hata mashirikiano mengine hutengenezwa ili kupata sehemu nzuri za malazi, na wengine hushirikiana katika kupeana taarifa za matukio mbalimbali ambayo yanaweza yakahatarisha usalama wao kama vile majanga ya moto wa nyika, mafuriko au hata matetemeko ya ardhi.
Ningependa nikufahamishe kuwa kuna aina nyingi za ushirikiano japo leo nitazungumzia aina ya ushirikiano wenye manufaa pande zote japo kuna aina mbalimbali nyingine za mashirikiano, zinazojulikana kama vile mutualism, commensalism, na parasitism.
Katika mutualism, aina zote mbili zinanufaika kutokana na ushirikiano huo hii ndio ile aina ambayo nitaizungumzia. Katika commensalism, aina moja inanufaika na ushirikiano huo bila kusababisha madhara kwa aina nyingine. Katika parasitism, aina moja inanufaika wakati aina nyingine inapata madhara. Nina Imani umefahamu pia japo kidogo kuhusu aina nyingine za mashirikiano mbugani.
Haya turudi katika mada yetu ya “Mutualism Relationship” Ushirikiano huu unaweza kuwa wa muda mfupi au wa muda mrefu na inategemea aina za wanyama na mazingira wanamoishi. Ushirikiano kati ya wanyama mbugani ni muhimu kwa sababu inawawezesha kuishi katika mazingira yenye changamoto na kuongeza nafasi zao za kuendelea kuishi.
Mbali na ushirikiano huu kuwa kati ya wanyama na wanyama pia ushirikiano huu unaweza kuwa kati ya mimea kwa mimea au kati ya mimeana na wanyama Ushirikiano kati ya mimea unachangia katika usambazaji wa virutubisho, utambuzi wa mimea, na kuongeza nafasi za kuishi kwa mimea katika mazingira tofauti. Pia, ushirikiano kati ya mimea na wanyama unaimarisha mifumo ya ikolojia na kuchangia katika uendelevu wa makazi ya asili.
ZITAMBUE AINA TANO ZA WANYAMA/ WADUDU WANAOSHIRIKIANA MWITUNI
- MBOGO NA OXPEKER
Mbogo ni mnyama mkubwa ambaye hula nyasi wengi wamemzoea kwa jina la nyati. Mnyama huyu hushirikiana kwa karibu sana na ndege ajulikanaye kwa jina la oxpeker ndege hawa wapo aina mbili aina ya kwanza hujulikana kama red billed oxpeker na aina ya pili hujulikana kama yellow billed oxpeker. Mashirikiano yao yanakuja pale ambapo ndege huyu anapokula wadudu wadogo wadogo ambao hukaa katika mwili wa mbogo mfano kupe.
Kupe ni mdudu ambaye huweza kuleta magonjwa kwa mbogo hivyo ndege huyu anapochukua jukumu la kuwaondoa kwa kuwala humuepusha mbogo na hatari ya magojwa pia inapotokea mbogo amepatwa na jeraha ndege huyu huchukua jukumu la kusafisha kidonda cha mbogo kwa kula damu iliyogandama katika kidonda na hivyo kukiacha kidonda kikiwa safi nyakati zote na kuepusha hatari ya kidonda husika kupata mashambulizi mengine mapya kama vile kuoza. Ndege huyu aina ya oxpeker hunufaika pia kwa kupata chakula chake kupitia wadudu wanaojishikiza katika mwili wa mbogo.
Licha ya mbogo kuwa mnyama mkubwa na mkali lakini humruhusu ndege huyu aina ya oxpeker kufanya shughuli zake za kuusafisha mwili wa mbogo bila ya mbogo kuleta madhara kwa ndege huyu mdogo
2. NYEGERE NA NDEGE HONEYGUIDE
Nyegere ni mnyama ambaye hupendelea kula asali, mnyama huyu ni mwenye ngozi ngumu na hivyo hufanya vigumu kwa nyuki kumdhuru pale anapofanya mawindo katika mzinga wa nyuki.
Nyegere pia anauwezo wa kuhimili sumu hivyo ni vigumu kudhurika pale inapotokea amengatwa na nyuki. Ushirikiano kati ya nyengere na ndege anayejulikana kwa jina la honeyguide ni wa kimkakati kwakua ndege huyu huruka mwituni kutafuta mizinga ya nyuki iliyopo katika mapango ya miti au mawe na hata mizinga iliyo chini ya ardhi.
Ndege huyu aina ya honeyguide jina lake limesanifu tabia yake ya kuonyesha mizinga ya nyuki ilipo mwituni, na huonyesha mizinga hiyo kwa kutoa mlio unaoashiria uwepo wa asali katika eneo husika na hiyo mnyama nyegere anaposikia mlio huo kutoka kwa honeyguide hutambua kuwa kuna chakula yaani asali jirani na eneo analolia ndege huyo na hivyo kumfanya nyegere kufika na kuubomoa mzinga.
Nyegere anapofanikiwa kuubomoa mzinga na kula asali ndege huyu huja na kujiokotezea masega ya asali yaliyobaki baada ya nyegere kuuharibu mzinga wa nyuki. Ushirikiano huu humfanya nyegere kutambua chakula kilipo kwa urahisi kutokana na ishara anazozipata kutoka kwa ndege honeyguide. Pia ndege huyu hunufaika kwakuwa yeye hupata chakula anachokipenda ambacho ni asali bila ya kudhuriwa na nyuki.
3. NYUMBU NA PUNDAMILIA
Nyumbu ni wanyama wanaohama kutoka eneo moja kwenda jingine na hii ni katika harakatin zao za kutafuta makisho na maji. Uhamaji maarufu Zaidi wa nyumbu na unaojulikana Zaidi ni ule wa Serengeti-maasai mara wildbeest migration. Japo nikufahamishe kuwa nyumbu hupatikana katika maeneo mengine ya hifadhi pia zilizopo nchini Tanzania. Idadi ya nyumbu wanaohama ni kubwa sana na huweza kufikia hadi Zaidi ya nyumbu milioni moja na nusu. Na katika msafara huo nyumbu huambatana na mnyama pundamilia.
Nyumbu na pundamilia huandamana katika msafara huo kimkakati kwakuwa nyumbu ni hodari wa kunusa na kujua mahali malisho mabichi pamoja na maji yalipo hivyo huwarahisishia wao kutambua malisho yalipo bila kukumbana na mazingira yanye changamoto ya uhaba wa malisho au maji. Pia katika katika katika msafara huo punda milia naye hunufaika kwa kupata malisho.
Punda milia ni mnyama mwenye uono mzuri na hivyo huwa raisi kwake kumuona adui kwa urahisi kama vile simba na chui na hutoa ishara ya uwepo wa adui katika msafara na hivyo kuweza kuchukua tahadhari. Uwezo wa pundamilia katika msafara wa husaidia nyumbu kujikinga na adui pia uwepo wa nyumbu katika msafara humsaidia pundamilia kutambua uwepo wa chakula na maji kwa urahisi.
4. MAMBA NA NDEGE PLOVER
Mamba na ndege plover ni mfano maarufu wa ushirikiano wa wanyama katika mazingira ya asili. Ndege plover, ambaye pia huitwa ndege wa Mamba, hujenga viota vyao karibu na maeneo ya maji ambapo mamba huishi. Mamba ni wanyama hatari na wenye nguvu, na mara nyingi hujulikana kwa kula mawindo yao kwa ukali. Hata hivyo, ndege plover wamepata njia ya kufaidika kutokana na uwepo wa mamba.
Ndege plover hula wadudu na wanyama wengine wadogo ambao hukaa karibu na maji. Wanapojenga viota vyao kwenye mchanga wa mto au ufuo wa ziwa, ndege hawa hujikuta katika hatari ya kushambuliwa. Hata hivyo, badala ya kuwa na uhusiano wa kawaida wa mwenyeji na mgeni, mamba na ndege plover wameendeleza ushirikiano wa kipekee.
Ndege plover wana njia ya kipekee ya kuingiliana na mamba bila kuumizwa. Hivyo, ndege plover hufaidika kwa kupata ulinzi kutoka kwa mamba Kwa upande mwingine, mamba hufaidika kwa kuondolewa kwa vimelea na wadudu wengine.
Pia ndege plover huondoa vipande vidogo vodogo vya nyama winavyobaki katika kinywa cha mamba na hivyo kusafisha kinywa cha mamba baada ya mamba kupata kitoweo. Hii ni aina ya ushirikiano wa kibiolojia ambapo pande zote mbili zinafaidika.
5. SIAFU NA ALPHIDI
Aphidi ni aina ya wadudu wadogo ambao hula majani ya mimea. Wanaweza kusababisha uharibifu kwa mazao na mimea ya bustani. Hata hivyo, siafu hujilisha kwenye utomvu wenye sukari tamu unaotolewa na aphidi. Aphidi hutoa utomvu huo kama matokeo ya kula majimaji ya mimea. Siafu hula utomvu huo na kwa kufanya hivyo, siafu hunufaika kwa kupata chakula.
Kwa upande mwingine, aphidi hufaidika kutokana na uwepo wa siafu. Siafu hulinda aphidi kutokana na wadudu wengine wanaoweza kuwashambulia. Aidha, siafu hutoa ulinzi kwa aphidi kwa kuwafukuza au kushambulia wadudu wengine ambao wanaweza kuwa tishio kwao.
Kwa hiyo, siafu hupata chakula kutoka kwa aphidi na utomvu tamu wanaotoa, na aphidi hupata ulinzi kutokana na siafu. Hii ni aina nyingine ya ushirikiano wa kibiolojia ambapo pande zote mbili zinafaidika na kuishi pamoja katika mazingira ya asili.
HITIMISHO
Katika ushirikiano huu niliouzungumzia unaojulikana kama “Mutual relationship” kila mnyama anatoa mchango wake na hupata faida fulani kutoka kwa mwenzi wake. Hii inaonyesha umuhimu wa kuelewa kuwa katika mazingira ya asili, wanyama wanaweza kujenga uhusiano wenye manufaa ambao unaweza kuwasaidia kukabiliana na changamoto za mazingira, kupata chakula, na hata kujilinda.
Ushirikiano wa wanyama unatumika kama mfano mzuri wa jinsi pande mbili zinaweza kufanya kazi pamoja kwa faida ya kila mmoja. Inatufundisha umuhimu wa ushirikiano na kuishi kwa amani na wengine katika mazingira yetu.
Kwa kujifunza kutoka kwa wanyama, tunaweza kutambua kuwa ushirikiano na mshikamano vinaweza kuwa msingi wa kuishi vizuri na kufanikiwa katika jamii yetu na dunia kwa ujumla.
Leon Hermenegild
255 742 398 956