Mara nyingi tunajisikia vizuri sana kuona watalii na magari ya kitalii yakizunguka kwenye hifadhi za wanyama na sehemu nyingine za utalii kwa ajili ya kutembeza watalii ili kuona wanyama na mimea asilia kwenye mapori ya hifadhi zetu. Kitu kikubwa ninachotaka wote tukijue na kujifunza siku zote ni kwamba uhifadhi una gharama kubwa sana. Kuna msemo mmoja wa Kiswahili unapenda kutumika sana unaosema, “ Usione vyaelea vimeundwa” kila tunachokiona na kukifurahia kwa uzuri na kwa kuvutia kuna gharama kubwa sana zilitumia na zinazotumika kwa ajili ya kuhakikisha kinaendelea kubakia kwenye hali yake nzuri nay a kuvutia.

Wanyama tunaowaona huko hifadhini wanalindwakwa gharama kubwa sana, kuna watu wanatoa maisha yao sadaka kwa ajili ya kufanya kazi za hatari kuwalinda wanyamapori dhidi ya majangili na watu wenye nia mbaya ya kuwaua. Kama wengi tunavyofahamu kuwa porini kuna hatari  nyingi sana laikini kuna watu wanajali zaidi wanyamapori wetu na wanafanya kazi ya ulinzi dhidi ya maharamia na majangili. Hii ndio sababu Tanzania ina idadi nzuri ya wanyamapori kuliko nchi nyingine. Hii ndio sababu watalii na wageni wengi wakija kutembelea Tanzania wanapenda sana maliasili zetu kwa namna zilivyotunzwa na watanzania wenyewe.

Kuna gharama kubwa sana watu wanaingia ili kusababisha wanyamapori na mimea iendelee kuwepo, licha ya kazi kubwa inayofanywa na askari na wasimamizi wa hifadhi hizi za wanyamapori na misitu, pia hata wananchi wa kawaida wanalipa gharama kubwa zaidi ya kusaidia wanyamapori waendelee kuwepo kwenye hifadhi na misitu yetu. Fikiria gharama wanayoingia wafugaji na wakulima ambao wanaishi karibu na maeneo ya hifadhi ya wanyamapori. Ni gharama kubwa sana, wanapata hasara ya kuharibiwa mazao yao, wanapata hasara ya kuliwa kwa mifugo yao na wanyama wakali kama vile simba,chui, mbwa mwitu, fisi, nk lakini bado watu hawa wanakubali yaishe na wanyamapori waendelee kuwepo kwenye mapori yao.

Gharama zote hizo, nyingine zinaenda mbali sana hata kuhatarisha uhai wa wanajamii, lakini bado kuna uvumilivu mkubwa sana kwa watanzania. Hakuna vita wala migongano na migogoro mibaya kwenye maeneo hayo. Licha ya chanagamoto zote hizo kuwapata wanajamii wanaoishi karibu na hifadhi hizi za wanyamapori na misitu, watu wameendelea kuthamini wanyamapori na mimea mingine ili viendelee kubaki na kuifanya nchi ya Tanzania kuwa na mvuto mkubwa sana kwenye masuala yote ya utalii.

Ingawa uelewa wa baadhi ya jamii sio mkubwa kwenye masula ya uhifadhi na faida zake, ingawa jamii haipati faida za moja kwa moja kutokana na uwwepo wa wanyamapori kwenye maeneo yao bado watu wamekuwa wapole na wavumilivu wanapoambiwa kuhusu uhifadhi wa wanyama.

Tunatakiwa tujue jambo hili, Tanzania inazidi kung’ara kitaifa na kimataifa kwenye sekta ya utalii na inasifika kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama adimu duniani, makundi makubwa ya tembo, nyati, nyumbu na wanyama wakubwa wanaokula nyama kama vile simba, duma, chui, mbwa mwitu na fisi. Hii ni kutokana na gharama kubwa iliyolipwa na jamii na maaskari wetu wanao walinda wanyama hawa na mazingira yao huko porini.

Tanzania ina idadi kubwa ya wanyama na mimea asilia mingi sio kwa sababu serikali na mashirika ya uhifadhi wa wanyamapori wanawalipa vizuri sana wafanyakazi wake, la hasha, hii ni kwa sababu ya utanzania na uzalendo wetu, hii ni kwasababu ya elimu kidogo tuliyopata kuhusu uhifadhi inasaidia sana watu wengi kujitambua na kuamua kufanya maamuzi ya busara ili kuhifadhi wanyamapori na mazingira yao ya asili.

Hivyo tutambue kuwa uhifadhi ni gharama kubwa na gharama hizo zinalipwa kwa kiasi kikubwa na jamii zetu zilizopo kandao ya hifadhi za wanyamapori. Lakini pia na kazi nzuri inayofanywa na serikali katika uhifadhi wa wanyamapori na mimea. Hivyo ni jambo muhimu sana kwa serikali na wadau wengine kwenye sekta hii kuhakikisha mapato na faida inayotokana na uwepo wa wanyama na faida nyingine muhimu kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu hawa muhimu.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania