Kila kitu kinachoigharimu dunia kwa sasa ni matokeo ya mifumo yetu sisi binadamu tuliyoichagua kwa ajili ya kufanya maisha yaende. Kila kona ya dunia inakabiliwa na majanga mengi sana makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa yamesababishwa na shughuli za binadamu hapa duniani.
Teknolojia tunazogundua kila siku, viwanda vya kisasa tunavyoanzisha kila siku, na mtindo wa maisha tunaoishi kila siku tangu tuwepo hapa duniani umechangia madhara makubwa sana ambayo yamekuwa tishio kwa usalama wa viumbe hai hapa duniani.
Majanga kama mabadiliko ya tabia nchi, ambayo yameleta ukame, mafuriko, njaa, umasikini, magonjwa mabaya na vifo vya viumbe hai yamechangiwa sana na uwepo wa shughuli za kibinadamu hapa duniani.
Hakuna nchi iliyo salama katika majanga haya ambayo nchi mbali mbali na Jumuiya za Kimataifa zinatumia mabilioni ya dola katika kupunguza uwepo wa majanga haya.
Pamoja na uwepo wa majanga hayo mabaya yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi, bado dunia inakabiliwa na janga jingine kubwa zaidi na baya sana kwa sasa, janga hili ni uchafuzi wa mazingira kwa uwepo mifuko ya plastiki au plastiki ambazo zinazalishwa viwandani kwa ajili ya shughuli mbali mbali za matumizi ya binadamu.
Pamoja na umuhimu wa bidhaa za plastiki katika matumizi ya kila siku, bidhaa hizi zimegeuka kuwa hatari zaidi kwenye mazingira yetu na kuhatarisha sana maisha ya binadamu na wanyama. Uwepo wa mifuko ya plastiki imekuwa ni uchafuzi mkubwa sana wa mazingira yetu, mazingira ya nchi kavu na mazingira ya majini yote yameathiriwa na uwepo wa taka za plastiki.
Hakuna nchi yoyote duniani ambayo taka hizi za plastiki hazijaleta madhara kwa miasha ya viumbe hai. Wanamazingira pote duniani wanasema uwepo wa plastiki na taka za plastiki umesababisha madara makubwa sana kwenye afya za watu na wanyama.
Hii ni kwasababu malighafi iliyotumika katika kutenegeneza pastiki na mifuko ya nailoni huwa haziozi, baada ya matumizi ya mifuko au bidhaa za plstiki huwa haziozi hata kama zitachimbiwa chini ya ardhi kwa muda mrefu, hivyo watu wanapotumia bidhaa hizo au mifuko ya plastiki hutupa kama taka nyingine lakini kwa kuwa baadhi ya taka za plastiki au mifuko ya plastiki ni myepesi sana na hupeperushwa na upepo na kutua sehemu nyingine na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Licha ya kuwa taka za plastiki zinachafua mazingira, taka hizi zinaweza kuzagaa sehemu mbali mbali na kuliwa na mifugo au wanyamapori.
Zinapoliwa na wanyama huwa hazimeng’enywi katika mfumo wa uyeyushwaji wa chakula kama ilivyo vyakula vya kawaida, bali hukaa ndani ya tumbo la mnyama na kusababisha madhara mabaya kwa mnyama, madhara hayo hupelekea mnyama kufa na kuoza. Baada ya mnyama kufa na kuoza plastiki alilokula huwa haliozi hivyo hubakia ardhini na wanyama wengine wanakuja kulila tena na kifo hutokea, tena huendelea hivyo hivyo.
Halikadhalika, utupaji wa taka za plastiki au mifuko ya nailoni baharini, mtoni au ziwani kuna madhara makubwa sana kwa viumbe hai wa majini. Hii ni kutokana na ukweli kwamba viumbe hai wa majini wengi wameathiriwa na uwepo wa taka za plastiki kwenye maji.
Tafiti za watalaamu wa sayansi ya majini wanasema viumbe hai wa majini kama samaki, ndege na wengine wanaoishi majini wanaathiriwa na taka hizi kwasababu taka hizi zinapokuwa ndani ya maji zinaweza kufanana na baadhi ya samaki au wadudu wengine ambao wanaliwa na samaki wenzao.
Anatomi ya wanyama na samaki waliovuliwa baharini inaonyesha kiasi kikubwa yani zaidi ya asilimia 80% ya samaki wote waliovuliwa katika bahari ya Pacific walikuwa na vipande vya plastiki kwenye matumbo yao. Na kwa kuwa plastiki zikishamezwa na samaki au viumbe waishio baharini husababisha madhara ya afya zao na hivyo kusababisha vifo vya wanyama hao, na baada ya kufa wanyama hao huoza lakini plastiki walizokula huwa haziozi na hivyo kuelea kwenye maji na samaki wengie huja na kula tena, kwa hivyo mzunguko unaenda hivyo hivyo mpaka kwa kiumbe wa mwisho.
Msomaji wangu, umeona hali ilivyo tete kwa maisha ya viumbe hai hawa ambao tunawalinda kwa gharama kubwa? Mbaya zaidi taka hizi za plastiki zinaweza kuliwa na wanyamapori wa majini na nchi kavu ambao wapo hatarini kutoweka, hivyo kuongeza kasi ya kutokweka kwao duniani.
Pia mifuko hii au plastiki hizi zilizotapakaa zinweza kuwa mtego kwa viumbe hai wanaoruka kama ndege wadogo kwa wakubwa, hii inaweza kutokea pale ambapo ndege atanasa kwenye mfuko au plastiki na kushindwa kuruka hivyo kufa au kuuwawa na vitu vingine.
Sasa unaweza kuelewa kwanini serikali yetu ya Tanzania imeamua kufuta kabisa matumizi ya mifuko ya nailoni na plastiki. Mifuko hii ina hasara kubwa kuliko faida, ina hasara kwenye masha ya vimbe hai na maisha ya biandamu pia. Mifuko hii ya plastiki sio tu inaleta madhara kwa watu na wanyama, lakini pia inachafua sana mazingira na kusababisha milipuko ya magojwa.
Naipongeza sana serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mazingira kwa uamuzi huu dhabiti wa kufuta na kutozalisha kabisa mifuko ya plastiki au naoiloni. Ni uamuzi ambao utasaidia sana kupunguza athari zinazoletwa na plastiki kwenye afya za watu na wanyama.
Natoa rai yangu kwa watanzania wenzangu, tuunge mkono juhudi hizi nzuri zinazotetea uhai na usalama wa afya za viumbe hai. Tuwe mabalozi wazuri kwa kuwafundisha wengine madhara ya mifuko hii na pia tudhamirie kutoitumia kabisa mifuko hii hata kwa njia ya siri.
Hata hivyo, sheria ya mazingira ya Tanzania katika utekelezaji wake, na pia kwa tamko kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais mazingira, inatoa faini kwa mtu yeyote atakayekutwa anatumia mifuko ya plastiki au anazalisha mifuko hiyo.
Hili ni tamko la Waziri wa Nchi (Muungano na Mazingira) Mh. January Y. Makamba kuhusu mifuko ya plastiki;
“Ndugu Wananchi, Mwaka huu hapa nchini hatutakuwa na maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Mazingira Duniani na badala yake kila Mkoa utafanya shughuli za maadhimisho katika maeneo yake kwa kuzingatia kaulimbiu ya maadhimisho haya isemayo: “Tumia mifuko mbadala wa Plastiki; kwa ustawi wa Afya, Mazingira na Maendeleo ya Uchumi”. Kaulimbiu hii ni mwitikio wa Taifa wa Tamko la Serikali la kukataza uzalishaji, uingizaji ndani ya nchi usambazaji na matumizi ya mifuko ya plastiki na kuhimiza wananchi kutumia mifuko mbadala. Tamko hili limetokana na uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na utupaji ovyo wa mifuko ya plastiki ambayo imeleta madhara makubwa ya kimazingira, afya za viumbe hai, ikiwemo binadamu wanyama, pamoja na kuathiri uchumi wa nchi kwa ujumla. Aidha, mifuko ya plastiki imekuwa sehemu muhimu ya jamii yetu, lakini changamoto ya usimamizi na athari za taka za plastiki nchini na duniani inahatarisha mustakabali wa ustawi wa jamii, uchumi na mazingira kwa kuwa mifuko hii huchukua muda wa takriban miaka 500 kuoza”.
Pamoja na hayo, kuna madhara mengi sana yanayosababishwa na uwepo wa taka hizi za plastiki kwa afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla. Hapa kwenye makala ya leo nimejaribu kugusia tu zile athari zinazotokea kwa wanyamapori wa majini na nchi kavu.
Hadi wakati mwingine nitakaposhika kalamu yangu na kukuandalia makala nyingine kuhusu ya mifuko na bidhaa za plastiki kwenye afya ya binadamu; kwa leo niishie hapa.
Asante sana kwa kusoma makala hii, usiache kumshrikisha mwenzio makala hii ili kila mtu awe na uelewa ulioupata kuhusu madhara na athari za mifuko ya plastiki na nailoni kwenye afya za viumbe hai.
Makala hii imeandikwa na ;
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania