Ni ukweli usiopigika kuwa maeneo vijiji ambayo yapo karibu na hifadhi za wanyamapori huwa yanatembelewa na wanyama kutoka kwenye Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu, maeneo ya hifadhi za jamii kama vile WMAs na wakati mwingine kwenye maeneo ya hifadhi za Taifa. Kwa kuwa ardhi ya vijiji vinavyozunguka au vilivyo karibu na maeneo haya vinapokea na kutembelewa na wanyamapori wa aina mbali mbali, maeneo haya ya vijiji yamekuwa na mvuto wa kipekee na kwa kuwa maeneo haya hayana uangalizi wa karibu wa wanyama wanongia yamerahisisha watu mbali mbali kuwa na shauku ya kufanya uwekezaji na biashara  kwenye maeneo haya.

Kama tunavyofahamu kuwa wanyamapori hawana mipaka kusema kuwa sasa wanavuka mpaka wa hifadhi au kwamba hawatakiwi kuvuka mpaka wa hifadhi na kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya malisho, maji na kwa ajili ya kuangalia maeneo mazuri ya kuzalia. Hivyo kwenye mapori ya vijiji yanakuwa na wanyama ambao wengine hutumia mapori haya kama njia, wengine humtumia mapori haya kama sehemu za kuja kupata malisho na kuondoka, wengine ni maeneo ya kupumzika au kujificha kwa usalama, wengine ni maeneo yao ya kudumu. Hivyo basi maeneo haya ni muhimu sana kwa ajili ya uhifadhi na pia utunzaji wa maeneo muhimu kwa ajili ya wanyamapori na rasilimali nyingine.

Kutokana na hali hiyo vijiji hivi huwa vinapokea wageni ambao wengi ni wafanyabiashara wageni na wazawa, yaaani wazungu na watanzania. Huja na kuongea na uongozi wa Kijiji husika na endepo Kijiji kinakubaliana na kulitangaza jambo hilo katika mkutano mkuu ili kila mwanajamii ajue basi wanweza kuingia mikataba na kukabithi eneo kwa mwekezaji kwa ajili ya kuendesha biashara zake hapo. Kwa uzoefu na utafiti unaonyesha kabisa baadhi ya wawekezaji kwenye ardhi ya Kijiji wanatumia njia ambazo sio sahihi na ambazo sio za uwazi kwa ajili ya kuwalaghai wanavijiji na viongozi, huwa tunasikiana kupata malalamiko ya baadhi ya wanavijiji wakisema mkataba ambao wameingia na mwekezaji walikuwa hawauelewi kwa kuwa umeandikwa kwa lugha ya kingereza ilihali wao na viongozi wa vijiji hawajui kilichoandikwa humo.

Makala hii nimeandika kuonyesha jambo hili kuwa vijiji na viongozi wa vijiji wanatakiwa kuilinda ardhi yao, na pia wanataikwa kufahamu ardhi ya Kijiji chao sio yao wenyewe ni kwa ajili ya watoto wao na kizazi kijacho, hivyo hata rasilimali muhimu ambazo zipo kwenye Kijiji sio kwa ajili yao kula na kumaliza kila kitu, bali zitumike kwa maslahi ya sasa na ya baadaye, yani kuwe na mpango mzuri na wa wazi wa matumizi endelevu ya rasilimali za Kijiji. Hivyo wanavjiji na viongozi wa vijiji wasishawishiwe kuuza bila mpangilio ardhi yao ya thamani. Tunatakiwa kufahamu kuwa ardhi ni rasilimali muhimu sana sehemu yoyote ile hapa duniani, na kila siku thamani yake inapanda hivyo ni vizuri tukawa na maamuzi ya busara kwenye ardhi yetu na maliasili zetu.

Pia ningeshauri endapo jambo la kuuziana ardhi litafanyika ni vizuri mikataba yote na kila kilichoandikwa kwenye mkataba kikawa kwenye lugha ya kueleweka kwa pande zote mbili, na kama hilo halitoshi washauri na watalaamu wa mambo hayo wapo na wanaweza kutoa msaada wa kitalaamu kwenye namna ya mkataba masharti na mambo yaliyoainishwa kwenye mkataba huo. Watalaamu hawa watasaidia kuainisha faida na hasara za uwekezaji huo, pia namna mradi huo utakavyoweza kusaidia uhifadhi wa mazingira asilia na kutoa faida kwa jamii. Pia inaweza kusaidi kupunguza uwepo wa rushwa na mambo mengine ya siri ambayo sio mazuri kwa Kijiji na maliasili zake.

Kuna makala nyingi nitaendelea kuandika kwenye mambo haya hivyo endelea kufuatilia blog hii kwa mafunzo na maarifa zaidi, pia kama una maswali, maoni au maependekezo usisite kuwasiliana nami kwa mawasiliano ya namba na email hapo chini, pia unaweza kuacha ujumbe wako hapo chini kwenye comment, nitaujibu mapema. Tuendelee kujifunza na kusaidia kuinua uelewa wa jamii yetu kwenye masuala haya ya rasilimali na maliasili zake.

Ahsante sana

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 862 481/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania