Kuna masoko ya aina mbili ya meno ya tembo, kuna masoko yanayouza meno ya tembo yakiwa ghafi au vipande vya meno ya tembo yakiwa ghafi na masoko ya aina ya pili ni masoko yanayouza meno ya tembo yakiwa yameshatumika kuunda na kutengeneza vitu mbali mbali kama vile sanamu za binadamu, mihuri, bangili, cheni za shingoni na aina nyingine za mapambo na visanamu vya aina mbali mbali kulingana na utamauni wa sehemu husika.

Rafika msomaji wa makala hizi za wanyamapori, kuna mengi tunahitaji kuyafahumu kuhusiana na matumizi ya meno ya tembo, biashara na masoko ya meno ya tembo. Karibu sana katika mfululizo wa makala hizi za uchambuzi wa ripoti za wanyamapori, na leo tunaangalia ripoti inayoitwa ELEPHANT IN THE DUST, THE AFRICAN ELEPHANT CRISIS. Ripoti hii ilitoka mwaka 2013. Tufuatene pamoja katika makala hii ili tujifunze mengi kuhusiana na biashara hii ambayo kwa kiasi kikubwa hufanyika kwa njia haramu.

Hadi siku za hivi karibuni nchi nyingi za Afrika ziliruhusiwa kufanya biashara ya kuuza bidhaa za meno ya tembo ingawa ilikuwa ni haramu kufanya hivyo bila kuwa na kibali maalumu cha maandishi. Ruhusa hii ilikuwa haihusishi nchi ya Kenya ambayo ilishafunga kabisa biashara ya meno ya tembo tangu mwaka 1989 na CITES.

Utafiti na uchunguzi wa mwanzo kabisa kufanyika na kundi linalojihusisha na ufuatiliaji na upitiaji wa biashara ya meno ya tembo (Ivory Trade Review Group) katika nchi za Afrika ambazo zina masoko ya meno mnamo mwaka 1989, baada ya kufanya mapitio na kubaini katika nchi hizo mambo ya kutisha kuhusu biashara ya meno ya tembo, taarifa zilizokusanywa na kundi hili ndizo zilizopelekea CITES kusitisha biashara ya meno ya tembo mwaka 1989.

Mnamo mwaka 1990 ulifanyika tena uchunguzi na utafiti kwa nchi 15 za Afrika ambazo ndio zilikuwa kinara kwa masoko na biashara za meno ya tembo ili kubaini kama ufungaji wa masoko ya meno ya tembo ulitelata manufaa, au kujua kama sheria ya kufunga masoko ya meno ya tembo kama imetekelezwa. Kwa mwaka huo uchunguzi ulionyesha kushuka na kupungua kwa kiasi kikubwa cha baishara ya masoko ya meno ya tembo kwa nchi zote kasoro nchi ya Nigeria.

Aidha, baada ya hatua za CITES kufunga masoko ya meneo ya tembo kumekuwa na kushuka sana kwa matumizi na mahitaji ya meno ya tembo hata sehemu ambazo zilikuwa na masoko makubwa kama vile Ivori Costi (Cote Ivoire) amabako kulikuwa na masoko makubwa sana, sasa baada ya uchunguzi masoko yake yametoweka na kupungua sana ikifuatana na nchi za Misri na Zimbabwe na Gaboni. Hii inaonyesha mafanikio makubwa katika hatua za kukomesha ujangili wa wanyamapori baada ya kufunga masoko ya ndani yanayoendesha biashara ya meno ya tembo.

Ingawa kulikuwa na ishara kuwa biashara na masoko ya meno ya tembo inaweza kuinuka tena mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1990. Hata hiyo taarifa za ripoti mbali mbali zinazoelezea sana masuala haya zimetoa majumuisho ya jumla katika hali hii kama ifuatavyo;

Kwenye nchi zote ambazo zina udhaifu katika usimamizi na ufuatiliaji wa masoko ya ndni ya  meno ya tembo kama vile Angola, DRC, Misri, Msumbiji, Nigeria na Sudani masoko ya meno ya tembo yamebakia kuwa juu na yanaendelea kukua.

Pale ambapo serikali ilifanya msako  kutaifisha meno ya tembo kwa kuwakamata wafanya biashara haramu ya meno ya tembo kama ilivotokea kwa nchi za Cmarooni, Kongo na Ethiopia, uuzaji wa meno ya tembo hadharani umepungua sana.

Masoko ya meno ya tembo yamekuwa sana katika sehemu zote ambazo wachina ndio wanunuzi wakuu, kama vile Nigeria na Sudani. Hata hivyo inaonyesha pia kuwa wanadiplomasia, watu wa umoja wa mataifa, na watalii wa nje au wageni na wafanya biashara wametajwa sana kuwa wanunuzi wa meno ya tembo.

Meno ya tembo ambayo yapo katika maduka na masoko ya Afrika mengi ni madogo na mengine ni dhaifu, na wakati mwingine yanaonekana kukosa ubora. Hii ina maana kuwa meno ya tembo makubwa na yaliyo katika ubora mkubwa yalishauzwa kwenda nchi za nje kwa ajili ya kutengeneza faida kubwa.

hivyo basi, baada ya kufahamu baadhi ya taarifa za masoko ya meno ya tembo yaliyopo Afrika kuna jambo kuu tunatakiwa kujifunza siku zote kuwa kushamiri kwa ujangili sehemu nyingi za Afrika kunatokana na uwepo wa masoko mengi na ya wazi katika baadhi ya nchi za Afrika. Pia tunatakiwa kufahamu tukitaka kukomesha ujangili lazima tutafute namna ya kuipoteza hamu ya wanunuzi wa meno ya tembo sehemu yoyote duniani.

Afrika tumekuwa sehemu ambayo watu kutoka nje wanakuja hapa kwa ajenda zao za siri ili kutupora maliasili zetu mbazo ni urithi wa vizazi vingi vijavyo. Tunatakiwa kuungana na kuwa na sauti moja, kwanza tufanye kama nchi ya Kenya walivyofanya, hakuna kufanya biashara ya meno ya tembo. Na kila nchi ambayo itakiuka makubaliano italipa adhabu itakayopata.

Hata hivyo tunapaswa kuja pia kuwa uwepo wa masoko ya meno ya tembo hapa Afirka na duniani kote kunadhorotesha juhudi za uhifadhi wa wanyamapori. Hivyo kama kuna dhamira na nia ya dhati kutokomeza ujangili wa tembo na wanyamapori wengine, biashara na masoko ya meno ya tembo yanatakiwa kutokomezwa kabisa.

Uchambuzi huu umeandaliwa na;

Hillary Mrosso

+255 683 862 481/255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania

Shares:
3 Comments
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *