Uwepo wa Wanyamapori Kwenye Mapori Ya Kijiji Chetu Unafaida Gani?

Kwa wale wanaofanya kazi kwenye sekta ya maliasili na mambo yote ya uhifadhi wa wanyamapori watakuwa wanaelewa zaidi kuhusu aina ya maswali yanayoulizwa na jamii ya wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi au karibu na maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori.

Hili ni swali linaulizwa na mzee mfugaji kwenye mojawapo ya vijiji vinavyozunguka maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori, mzee huyu alikuwa na idadi kubwa sana ya mifugo jamii ya ngombe, mbuzi, na kondoo, swali alilouliza halipaswi kujibiwa kwa wepesi wepesi bila kuingia ndani zaidi kujua nini kimemfanya kuuliza swali kama hili, mzee ambaye kwa maisha yake ya zaidi ya miaka hamsini anaishi nja idadi kubwa ya mifugo kando kando ya hifadhi, anauliza swali la namna hii.

Tusipojifunza sababu za kiundani zilizopelekea mitazamo ya namna hii kwa watu wenye mtazamo kama wa huyu mzee kamwe hatutaweza kumaliza au hata kupunguza inavyotakiwa migogoro inayosababishwa na uwepo wa wanyama hawa kwenye mapori ya vijiji vyetu.

Nitoe rai kwa wadau wa maendeleo na serikali kwa ujumla; suala la uhifadhi wa wanyamapori na rasilimali nyingine muhimu kwa nchi yetu ni la kuchukulia kwa umakini na kwa uzito. Kila pointi inayotolewa kila mawazo yanayotolewa na wananchi hawa na wadau wengine yanapaswa kuchukuliwa kwa uzito unaotakiwa.

Mahusiano tuliyonayo na jamii hii ya wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi  ni muhimu kwa mustakabadhi wa usalama na uendelevu wa maliasili zetu, mahusiano yetu yalenge kabisa kujitoa na kuwa karibu kabisa na jamii hii ili kumaliza changamoto zinazojitokeza ndani na nje ya hifadhi zetu.

Kwa uzoefu nilionao kwenye maswala ya utafiti na usimamizi wa wanyamapori nimejifunza mambo mengi sana ambayo wadau husika wa sekta ya uhifadhi na maliasili wanachukulia bila uzito unaotakiwa. Uhifadhi wa wanyamapori na usimamizi wa rasilimali asilia sio suala la kufanya kwa mara moja na kujihakikishia ushindi. Haya mambo yanahitaji kujitoa na kuthamini mawazo na mchango wa jamii zetu hizi, pia jamii hizi ni muhimu sana kama kiungo muhimu kwa uwepo wa wanyama hawa ndani na nje ya hifadhi zetu.

Makala hii imeandikwa na kuandaliwa na;

Hillary Mrosso

0742092569

hillarymrosso@rocketmail.com

Shares:
1 Comment
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *