Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu kwenye makala zetu za kila siku ambapo tunaichambua na kujifunza sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009. Katika makala ya jana tulielezea uanzishwaji wa mapori tengefu, na maeneo oevu, na maeneo haya ya hifadhi za wanyamapori mwenye mamlaka ya kuyatangaza ni waziri mwenye dhamana kwa kushauria na mamlaka husika na wadau wengine kwenye sekata hii. Hivyo leo tutaendelea na kuchambua kuanzia kifungu cha 19 ambacho kinahusu uwindaji kwenye mapori ya akiba, mapori tengefu na maeneo oevu. Hivyo tufuatane pamoja ili tujue sheria inaelekeza nini kwenye maeneo haya.
19- (1) Mtu hataruhusiwa, isipokuwa kwa ruhusa ya kimaandishi kutoka kwa Mkurugenzi, ambayo ilitafutwa na kupatikana kabla na kwa namna ambayo imeelezwa kwenye maandishi, kuwinda, kuchomoma mioto, kukamata, kuua, kudhuru au kujeruhi au kuudhi mnayama yoyote au kuvua kwenye pori la akiba lolote, mapori ya maeneo tengefu au maeneo oevu. Hapa ufafanuzi ni kwamba Hakuna mtu ambaye ataruhusiwa kufanya shughuli za kiwindaji, kuchoma moto, kuua , kujeruhi au kuwasumbua wanyamapori kwa namna yoyote ile bila kuwa na ruhusa ya kimaandishi ya kufanya hivyo kutoka kwa Mkurugenzi.
(2) Mtu yeyote atakayekiuka masharti ya sehemu hii au mapendekezo yaliyoambatana na mamlaka yeyote yaliyotajwa na kifungu kidogo cha (1), atakuwa amefanya kosa na atawajibika kisheria kwa
(a) Pale ambapo kesi ya kosa lake itahusishwa na uwindaji, kukamata,au kuua wanyama ambao wametajwa kwenye Jedwali sehemu ya I , kwenye sheria hii, atahukumiwa kifungo jela kwa muda usiopungua miaka mitano lakini usizidi miaka kumi, na mahakama inaweza kuongezea adhabu ya kulipa faini ya shilingi laki tano (500,000) lakini isizidi shilingi milioni mbili (2,000,000). Hii ni adhabu kwa wale watakaopatikana na hatia ya kuwinda au kufanya mambo ambayo hayatakiwi kwa mujibu wa sehemu ya kifungi cha sheria hii.
(b) Pale ambapo mtu atapatikana na kosa la kuwinda, kukamata au kuua mnyama yoyote alietajwa kwenye sehemu ya II ya Jedwali la Kwanza kwenye sheria hii, atawajibishwa kisheria kwa kufungwa jela kifungo kisichopungua miaka miwili na isiyozidi miaka mitano na mahakakma inaweza kuongeza adhabu ya kulipa faini ya shilingi laki tatu (300,000) na isizidi shilingi laki tano (500,000);
(c) Katika kesi ambayo mtu ameonekana na hatia inayohusisha uwindaji, kukamata au uuaji wa mnyama ambaye ametajwa kwenye sehemu ya III ya Jedwali la Kwanza (First Schedule) la sheria hii, atawajibishwa kisheria kwa kufungwa jela kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitatu, na mahakama inaweza kuongezea adhabu ya kulipa faini isiyopungua ya shilingi laki moja (100,000) na isiyozidi shilingi milioni moja (1,000,000) na;
(d) Kwa makosa mengine, faini ya isiyopungua shilingi laki mbili (200,000) na isiyozidi shilingi laki tano (500,000) au kufungwa jela kifungo kisichopungua mwezi mmoja lakini kisizidi miezi sita.
MAKATAZO MENGINE AMBAYO YANATUMIKA KWENYE MAPORI YA AKIBA, ARDHI OEVU NA MAPORI TENGEFU
Katika kifungu hiki cha sheria kinachoelezea amri, masharti au makatazo (restrictions) ambayo maeneo ya hifadhi ya wanyamapori na mimea mingine tutachambua kifungu hiki cha 20 ambacho ndio kinaelezea masharti yote ya namna ya kusimamia maeneo ya akiba, maeneo oevu na maeneo tengefu.
20.- (1) Mtu yeyote haruhusiwi ndani ya eneo lolote la pori la akiba, pori tengefu au eneo oevu-
(a) kuchimba, kuondosha, au kuchimba shimo lolote, kuweka wavu, kuweka mtego, kuweka waya au kutumia vifaa vingine mbavyo vina uwezo wa kuua, kukamata au kujeruhi mnyama yoyote;
(b) kubeba au kuwa na silaha yoyote ambayo ameshindwa kumridhisha Mkurugenzi kwamba silaha na zana alizonazo hajanuia kuwindia wanyama, kuua, kujeruhi au kukamata mnyama.
(c) kufanya kilimo cha mazao. Hapa sheria hairuhusu kabisa kufanya kilimo cha mazao kwenye maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya wanyamapori na mimea kama vile mapori ya akiba, mapori tengefu, na maeneo oevu.
(2) Mtu yeyote hataruhusiwa kukusanya mchanga, mawe au madini kwenye pori la akiba lolote. Sheria hapa inakataa kabisa uchimbaji wa mchanga, madini au mawe kwenye maeneo ya mapori ya akiba.
(3) Licha ya masharti ya kifungu kidogo cha (2), mtu anaweza kuchimba madini kwenye pori la akiba ikiwa shughuli hiyo itajumuisha na itakuwa inafanyika kwa kusudi la kuchimba madini ya-
(a) mafuta
(b) gesi
(c) uraniamu
Kwa kuzingatia kwamba –
(i) Makadirio ya athari za mazingira yameshafanyika kulingana na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira; (Environment Impact Assessment)
(ii) Gharama za ulinzi zimeshalipwa na mwekezaji kama itakavyoeleza mapendekezo
(iii) Ada ya umiliki wa mradi imeshalipwa kulingana na taratibu ambao umeandaliwa na Waziri; na
(iv) Serikali inatakiwa ndio imeanzisha shughuli hiyo.
(4) Mtu yeyote atakayekiuka sehemu hii anafanya kosa na atakuwa na hatia ya kulipa faini isiyopungua shilingi laki mbili (200,000) na isiyozidi shilingi milioni moja (1,000,000) au kifungo jela kwa muda wa miezi sita lakini isizidi miaka miwili au vyote kwa pamoja.
MAKATAZO YA KUCHUNGIA MIFUGO KWENYE MAPORI TENGEFU
Katika sehemu hii ya kifungu cha 21 cha sheria hii, sheria imetoa maonyo na masharti kwenye kulisha mifugo maeneo yatangazwa kuwa mapori tengefu.
- –(1) Mtu yeyote hataruhusiwa, isipokuwa kwa ruhurusa ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi ambayo ameipata kabla, kulisha mfugo wowote kwenye eneo la pori tengefu. Hivyo wafugaji wanapaswa kujua na kufahamu maeneo haya ili wajiepushe na migogoro isiyo na sababu.
(2) Mtu yeyote atakayekiuka sehemu hii atakuwa amefanya kosa na kuwa na hatia, hivyo anawajibu wa kulipa faini isiyopungua shilingi laki moja (100, 000) na isiyozidi shilingi laki tano (500,000) au kufungwa jela kifungo kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitano, au vyote kwa pamoja.
Naamini mpaka kufikia hapa tumejifunza kitu muhimu sana kwenye sheria hii, hivyo kwa haya tuliyoyapata hapa leo tuyafanyie kazi ili yatusaidie kuishi na kuwa na mahusiano mazuri kati yetu na hifadhi za wanyama na mimea. Tukitaka kujenge mahusiano mazuri na viumbe hai lazima tuwe tayari kuchukua hatua za kiakili zaidi kwani wanyama tunaowapigania hawana uwezo na akili kama tulivyo sisi binadamu. Hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunatumia vizuri uwezo wetu wa kiakili na nguvu kuwahakikishia usalama wao na mazingira yao
Mungu alipomuumba mwanadamu alimpa uwezo mkubwa wa kuwaangalia na kuwahifadhi wanyama na mimea yote. Hivyo vitu hivyo vipo chini ya mwanadamu, lakini hatari iliyopo ni pale ambapo mwanadamu hawezi kutumia uwezo wake alipewa na Mungu kwa faida ya viumbe hai wote. Pale ambapo mtu anashindwa kuishi kwa mafanikio kati yake na viumbe vingine hii ni ishara kubwa ya ubinafsi na kutokujitambua. Kujitambua ni pamoja na kuyaelewa mazingira yako na kuhakikisha yanaendelea kuwa bora na kustawi yakiwa chini yako.
Asante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania