Habari msomaji wa makala za kila siku za wildlife Tanzania, karibu kwenye makala yetu ya leo tujifunze na tuweze kuelewa baadhi ya mambo yanayoendelea katika mazingra yetu ya kila siku, hasa kwenye maliasili zetu. Shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu, utamaduni na sayansi UNESCO huwa lina utaratibu na kanuni au vigezo ambavyo hutumia ili kuchagua na kutangaza eneo lolote la nchi wanachama kuwa eneo la urithi wa dunia. Kumbuka kuwa kwenye maeneo haya yote lazima yawe ya kitamaduni au ya kiasili.
UNESCO (the United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization), wanaamua kujihusisha na maeneo au kuendesha miradi na programu mbali mbali zenye kusaidia kuwepo na kuendelea kwa amani, usalama na heshima kwa binadamu. Hivyo wanatumia njia mbali mbali ili kufanya kazi karibu na watu na tamaduni zao. Kwa kufanya hivyo wanatambua na kujali juhudi zote na ubunifu wote au kazi ya kipaji na ya kipekee iliyofanywa na watu wa zamani au wazee wetu au wahenga. Hivyo wanatambua na kuyatangaza maeneo hayao kuwa moja ya maeneo ya urithi wa dunia. Maeneo haya yote mengi ni ya kiasili ambayo hayajaumbwa na binadamu na mengine yote ni kazi ya mikono ya binadamu.
Kwa kulijua na kutambua hilo wametoa vigezo vyao ili eneo au sehemu kuwa ni eneo la urithi wa dunia. Hivyo wamatoa vigezo kama kumi hivi;
- Ili sehemu au kitu kitangazwe kuwa ni urithi wa dunia lazima ionyeshe uwezo na ujuzi wa hali ya juu wa uumbaji au utengenezaji wa kitu hicho na faida yake kitamaduni kwa watu.
- Kigezo kingine ni kuwa eneo hilo au kitu hicho kinatakiwa kionyeshe au kieleleze mwingiliano wa maadili ya binadamu kwa muda mrefu ndani ya eneo la utamaduni duniani kama maendeleo ya ujenzi, teknologia na hata historia, Sanaa, mpango miji na mpangilio wa ardhi,
- Eneo au kitu hicho kinatakiwa kuwa cha kipekee au kimebeba upekee wa aina yake tu kwa utamaduni tunaoishi au uliopita.
- Ni jengo ambalo ni la kipekee kabisa na linawakilisha teknolojia na historia ya kuvutia ya binadamu
- Liwe ndio eneo au jengo la mfano na la kitamaduni la makazi ya yatu, mipango ardhi na ionyeshe maendeleo ya binadamu
- Kitu hicho lazima kihusianishe na mazingira halisi, utamaduni na mawazo, Imani au kazi yoyote ya Sanaa yenye thamani kwa ulimwengu.
- Lazima liwe ni eneo la kisili kweli, lenye uoto wa kiasili na pia liwe ni eneo lenye mvuto kiasili
- Pia iwakilishe hatua muhimu za maendeleo ya dunia na binadamu, na rekodi ya Maisha ya binadamu na michakato ya miamba au ardhi.
- Iwe ni sehemu nzuri na ya muhimu inayaoonyesha mabadiliko ya miamba, na ya kibaiolojia kwenye ardhi kavu, kwenye maji na kwenye jamii za mimea na wanyama
- Pia eneo hilo lazima liwe na maeneo muhimu sana kwa makazi ya wanyamapori na mimea pia ukijumuisha na wanyamapori ambao wapo hatarini kutoweka.
Vigezo hivi kumi nimeviweka pamoja vikijumuisha vigezo vya kuchagua kitu au eneo la kiasili na kigezo cha kuchagua eneo la utamaduni. Kwa hiyo namba moja hadi sita ni vigezo vya kuchagua eneo la kitamaduni na kuanzia saba hadi kumi ni vigezo vya kuchagua eneo la kiasili. Na jambo jingine ni kwamba vigezo hivi vimeandikwa kwa lugha ya kingereza hivyo nimejitahidi kutafsiri kwa uwezo wangu wote ili kuandika sentensi yenye maana sawa au karibia na hiyo ya kingereza. Hivyo kama unajua kusoma kingereza unaweza kupitia pia link hii ili kujua na kuona uhalisia wake. https://en.wikipedia.org/wiki/World_Heritage_Site
Ashasante sana kwa kusoma makala hii; mshirikishe na mwingine maarifa haya.
Hillary Mrosso
Wildlife conservationist
+255 683 258 681/ +255 742 092 569
www.mtalaam.net/wildlifetanzania