Kwa uzofu kidogo nilio nao wa kutembele hifadhi na vivutio mbali mbali sehemu yoyote ile, nimekutana na changamoto hii mimi mwenyewe kwa kuishia kujilaumu na kuona napoteza fursa nzuri sana zitakazo nifanya kuwa na kumbukumbu nzuri siku za baadaye kwenye maisha yangu. Hivyo changamoto hii imewakuta watu wengi hasa Watanzania wanaotembelea maeneo ya kitalii au maeneo mengine ya kuvutia, huwa wanabaki wanahangaika na hawana cha kufanya wanapokuwa katika maeneo haya ya kitalii. Hivyo basi kwa kuona changamoto zinazowapata watu wanaotembelea hifadhi na maeneo mengine ya kitalii, ndio nikaamua kukaa chini na kuandaa makala hii ambayo nitaainisha vitu vyote muhimu unavyotakiwa kuwa navyo ili safari yako inoge, au uifurahiye safari yako ya kitalii au ya kujifunza sehemu yoyote unapokwenda. Hivyo basi karibu tuangalie kwa pamoja vitu hivyo muhimu.
- Kitambulisho
Unapopanga kutembelea hifadhi za Taifa na hata maeneo mengine ya mapori ya akiba au mapori tengefu (WMA), zingatia kuchukua kitambulisho chako, ambacho kinakutambulisha uraia wako. Unaweza kuwa na kitambulisho cha taifa kama uancho, au kitambulisho cha mpiga kura au kitambulisho chochote kinachokutambulisha wewe. Ukishindwa au ukiacha kitambulisho chako huwezi kukubaliwa kuingia hifadhini. Nimeona watu wengi sana wakifunga safari mpaka hifadhini lakini wanapofika getini wanazuiliwa kuingia kwasababu hawana vitambulisho. Epuka usumbufu huu ili ufanye safari yako kuwa ya uhakika na ya furaha. Mamlaka ya hifadhi wameamua kuweka sharia na kanuni hiyo kwa usalama na mambo mengine ya kitalaamu zaidi. Kwa hiyo usiende kiholela hifadhini.
- Beba Kamera
Ili ufurahiye safari yako ni vizuri ukawa na kamera yako binafsi, hii kamera yako itakusaidia kupiga picha na kuchukua matukio mbali mbali unapotembelea hifadhi au sehemu yoyote yenye vivutio. Ndio maana huwezi kukuta mzungu anakuja kutalii hana kifaa muhimu kama kamera kwa ajili ya kuchukua picha na matukio mbali mbali, wakati wa safari yake. Lakini cha ajabu kwa watanzania wengi huwa wanapokuja hifadhini au sehemu zenye vivutio wengi wao huwa hawakumbuki kuja na kamera kwa ajili ya kupiga picha unazotakaza Wanyama na vitu vingine wanavyopenda. Wengi wanajuta na utasikia wanakwambia sijaifurahia safari yangu vizuri kwasababu sikuja na kamera. Na nipende kusisitiza hapo kuwa ni vizuri ukaja na kamera yako mwenyewe ili kuepuka kuwasumbua watu wengine walio kuja nazo. Hapa kwenye kamera unaweza kuchukua kamera yoyote inayokufaa wewe na pia zipo kamera nyingi sana za bei nafuu, hivyo jiandae ili uweze kuifurahiya safari yako, pia unapokuja na kamera yako uchukue na batri za akiba endapo chaji za betri zitaisha, na pia uwe na SD card au memory card yenye uwezo mkubwa kwa kuhifadhi picha nyingi. Kama umeshindwa kumudu kuwa na kamera yako binafsi unaweza kutumia hata simu za kisasa za smartphone, ambazo nyingi huwa na uwezo wa kupiga picha ambazo zitakuwa kumbukumbu nzuri kwako na kwa wengine pia.
- Binocular/ Hadubini
Hiki ni kifaa maalumu kwa ajili ya kuonea vitu vilivyo mbali na upeo wa macho yetu. Hivyo kama unaweza kumudu kuwa nayo ni vizuri kwa sababu itakusaidia kuangali vitu au wanyama walio mbali na upeo wa macho yako. Kwa mfano umemwona simba yupo mbali na unataka kumwangalia vizuri, lakini gari hairuhusiwa kuchepuka kwenda alipo huyo simba au barabara ya hapo haipitiki kwa gari. Hivyo unaweza kutumia kifaa hichi kuwaangalia hao simba vizuri kabisa, bila kuvunja sharia za hifadhi na kuepuka kuwasumbua wanyama. Wazungu wengi na waatii wengi wanapokuja kutembelea hifadhi zetu au hifadhi nyingine huwa na vitu hivi ambavyo huwasaidia kuona hata wanyama na mazingira yaliyo mbali na upeo wa macho yao. Pia kumbuka kwamba kifaa kama hichi sio lazima uje nacho, na usipo kuwa nacho huwezi kuchukuliwa hataua yoyote, ila nimeamua kukuandikia hapa ili ujue ni vitu gani unaweza kuwa navyo kama nyenzo ya kukufanya ufurahie safari yako na utalii wako.
- Kitabu (Guiding Book)
Hichi nacho sio lazima, ila ukiwa nacho kitakusaidia kukuongoza endapo utamwona myama au ndege au nyoka na unataka kumfahamu kwa jina basi unaweza kurejea kwenye kitabu chako ulicho nacho ili umfahamu mnyama au ndege uliyemuona. Hivyo basi kitabu hiki ni maalumu tu kwa utambuzi na uongozi napokuwa hifadhini au porini, kitabu hicho kinakuwa na aina nyingi sana ya wanyama na mimea mingi ambayo imeelezewa inakopatikana na sifa za kila kitu, hivyo kitabu hicho kitakuwa msaada sana kwako kufurahia safari yako.
- Notebook/ Diary/Daftari na Kalamu
Hivi navy sio vya lazima kuwa navyo, lakini endapo unatembelea hifadhi kwa lengo la kujifunza basi usiache kuvichukua maana vitakusaidia kuandika vitu mbali mbali ambavyo umeviona au umevisikia kutoka kwa watalamu wa hifadhi. Hivyo utaandika vitu vichache unavyopenda. Ningeshauri kila anayeingia hifadhini asiwe tu anakwenda kufurahia vivutio na mambo menine lakini aende pia wa nia ya kutaka kujifunza vitu mbali mbali ambavyo vinaweza kumsaidia kuboresha maisha yake na kushiriki katika uhifadhi na utunzaji wa mazingira na mali asili hizo.
- Snacks, soda, maji,
Unapojiandaa kwenda kutembelea hifadhi uwe na kitu laini ambacho utakuwa unakula pale utakaposikia njaa au hamu ya kula. Hii ni kwasababu mnapoingia hifadhini na kuanza kuzunguka hifadhi mnachukuwa muda mrefu na lolote linaweza kutokea kama vile gari kupata pancha, au kuharibika au kukwama kwenye mchanga, hivyo unakuta mnatumia muda mwingi sana mkiwa porini, mpaka muda wa chakula cha mchana unapita, hivyo utaanza kusikia njaa na kuona safari yako imekuwa ngumu na mbaya. Ili kuepukana na hali kama hii ambayo haitabiriki ni vema ukabeba vitu vidogo vidogo vya kula mkiwa njiani, kama vile biskuti, maji ya kunywa, au soda au vitu vingine laini. Lakini epuka unapokuwa unakula vitu kama hivi usitupe takataka ndani ya hifadhi,au makopo ya maji au soda au juice, yahifadhi ndani ya gari yenu hadi mtakapofika sehemu maalumu za kuyaweka.
- GPS
GPS ni kifaa maalumu kwa ajili ya kuonyesha mahali ulipo na uelekeo na umbali, hiki nacho sio lazima sana kuwa nacho, ila kina umuhimu wake kutegemea shughuli unayoifanya. Ni kifaa muhimu sana na ni cha gharama kidogo, kwa watafiti na watu wanoenda porini au sehemu wasizozijua hiki kifaa ni muhimu sana kwa safari zao. Kama lengo ni kutembelea hifadhi tu, sio cha lazima sana. Lakini ukiwa nacho kitakusaidia pale ambapo mmepotea njia ndani ya hifadhi, hivyo kwa tahadhari kama una kifaa hiki ni vizuri kutembea nacho unapotembelea sehemu za hifadhi. Hii itakusaidia endapo mmepata hitilafu au gari imeharibika basi unaweza kukiwasha na kurekodi GPS point za mahali ulipo na kuwatumia watu wa hifadhi kwa msaada zaidi, au kama umepotea unaweza kukifuata na kukuonyesha umbali ambao upo na sehemu ambayo unataka kufika.
Hivyo ni baadhi tu ya vitu vya msingi kuzingatia unapokwenda hifadhini, jiadae kwa vitu ambavyo huna unaweza kununua kwenye maduka mbali mbali ili uvihifadhi mpaka siku unayotaka kwenda hifadhini basi unavitumia, au sehemu yoyote ya vivutio. Jiandae kuwa na Maisha ya ndoto zako kwa kufurahia safari zako na vivutio vilivyoko Tanzania na sehemu nyingine duniani. Hivyo basi naamini umepata vitu vya kukusaidia kujipanga ili kuifanya safari yako kuya ya kipekee na ya furaha. Unaweza kuwashirikisha wengine maarifa haya ili tusiwe tena nyuma, kama watazamaji tu wasio na la kufanya.
Nakushukuru kwa kusoma makala hii iliyoandaliwa na kuandikwa na ;
Hillary Mrosso
0742092569

