Hifadhi ya taifa ya Ruaha ipo katika mkoa wa Iringa, hivyo kwa asilimia kubwa ya hifadhi hii kubwa zaidi Tanzania , yenye ukubwa wa kilomitz za mraba 20,226. Hifadhi hii ina maliasili nyini sana ambazo ni kivutio kwa watu wengi wanao penda kuangali vitu ambavyo ni halisi. Kwa watu na wakazi wa maeneo ya jirani au karibu na Hifadhi, hii ni fursa nzuri sana kutembelea Hifadhi hii, mikoa kama Dodoma, Mbeya na mikoa mingine iliyokaribu na hifadhi kuu ya Ruaha.

Hifadhi ya Ruaha ipo umbali wa kilomita 100 kutoka Iringa mjini hadi kufikia kwenye geti kuu la kuingilia hifadhini, hivyo ni umbali mrefu sana kutoka mjini hadi hifadhini kwa wale wanao tumia usafiri wa magari. Pia barabara kuu ya hifadhi hii ni ya vumbi na haina lami, hivyo unapaswa kuwa na gari zuri na imara ili usipate usumbufu wakati wa safari yako. Pamoja na changamoto zote hizo bado utafurahia zaidi mazingira mazuri  kuanzia eneo unapoimaliza Kidamali hadi kufikia getini kuna mambo mazuri na uoto mzuri wa kuvutia katika barabara inayoelekea kwenye hifadhi hii.

Kwa asilimia kubwa uoto wa miti jamii ya miombo ipo katika eneo hili kwa kiasi kikubwa. Na pia kando ya barabara kuu ya kuelekea hifadhini utaona baadhi ya wanyamapori kama vile tandala wakubwa na tandala wadogo ambao wanapatikana katika hifadhi ya Ruaha pekee. Wanyamapori hawa ndio alama kuu ya hifadhi ya Ruaha. Ikumbukwe pia hifadhi hii inawanyamapori wengi sana, wengine wapo ndani ya hifadhi na wengine wapo nje ya hifadhi ya Ruaha, kwenye mapori tengefu na mapori ya vijiji. Kuonekana kwa wanyamapori kwenye maeneo ya mapori ya vijiji au karibu na maeneo ya watu ni ishara nzuri, ikimaanisha kwamba watu wa eneo hilo sio majangili,au wawindaji, hii ni sifa nzuri sana ambayo utaiona utakapotembelea hifadhi hii.

Ukiwa njiani utahadidhiwa mambo mengi ya kihistoria kuhusiana na mkoa wa Iringa, na pia kuna maeneo ukipita unaweza kupata taarifa mbali mbali za kitamaduni na za kihistoria kuhusu Chifu Mkwawa na watu wenine mashuhuri wa mkoa wa Iringa, kwa mfano ukifika Kalenga, hutakosa kusikia habari za chifu Mkwawa wa Wahehe, ushujaa wake na ujanja wake kipindi cha ukoloni.

Nyamahana/ Mlambalasi

Pia ukiwa bado njiani unaweza pia kupata habari zaidi za waasisi wa mambo mabli mbali ya kitamaduni na ya kijadi kuhusu mkoa wa Iringa. Mfano ukifika katika kijiji cha Nyamahana kama unatokea Iringa mjini, kuna sehemu inaitwa Mlambalasi, ni sehemu kame na yenye udongo wenye miamba migumu sana, hapa pana historia pana sana endapo utawapata wenyeji watakusimulia. Hapa Mlambalasi ndio penye kaburi la chifu Mkwawa. Kaburi hili lipo kilomita chache sana kutoka barabara kuu ya kuendea hifadhi ya Ruaha, hivyo kama unapenda kuona na kjua zaidi karibu sana.

Malinzanga/Mlowa

Kitu kingine cha kushangaza zaidi ni kwamba mkoa wa Iringa sio tu kwamba unakaliwa na wahehe au wabena tu, ila kuna idadi kubwa sana ya watu jamii ya kifugaji kama vile wamasai, wamang’ati, wasukuma na Wagogo. Ambao kwa asilimia kubwa jamii hizi za kifugaji huishi vijijini au sehemu ambazo kuna malisho ya mifugo yao. Hivyo ukiwa Iringa mjini unaweza usione watu hawa kwa wingi, ila utakapoanza safari ya kuja hifadhi ya Ruaha utakutana na jamii hizi, kwa wingi wakiwa ni wamasai na wamang’ati. Kwa hiyo ukifika Malinzanga au Mlowa utakutana na jamii ya wamama wa kimasai wakiuza bidhaa zao za asili walizoshona na kufuma kwa mikono yao wenyewe, wakiziuza, kwa kweli zinzvutia sana. Eneo hili ambalo wanafanyia biashara zao limeanza kutumika siku za karibuni, baada ya mradi mkubwa wa SPANEST kuwajengea kituo cha kisasa kinachoendana na utunzaji wa mazingira halisi ya eneo hili, kwa hiyo ukifika hapo unaweza kuona na kununua bidhaa mbali mbali unazozitaka kama vile hereni, bangili, mikufu ya shanga, virungu vya kijadi nk.

Pia katika eneo hili kuna wanaume au vijana wa kimasai na wa kimang’ati wanachoma nyama kitamaduni kabisa, yani nyama inachomwa na kuiva vizuri kama umechoma na oveni. Kwa wale wanaopenda kula nyama ya mbuzi, basi eneo hili la Malinzanga/ Mlowa ni sehemu nzuri ya kutulia na kula nyama za mbuzi, huku ukipata historia mbali mbali kutoka kwa wenyeji wa eneo hili. Uziri wa hapa ni kwamba kwa kuwa kuna makundi mawili huwa wanapeana zamu ya kuchoama na kuuza nyama za mbuzi ili kila mmoja apate hela ya kujikimu na matumizi mbali mbali; hivyo kunakuwa na ratiba ya wamasai na pia ipo ratiba ya wamang’ati kuchoma na kuuza nyama. Ukweli ni kwamba nyama hizi huchomwa katika hali ya usafi na pia huwa ni za moto wakati wowote utakaofika na kuhitaji. Karibu ule nyama za mbuzi hapa Mlowa ukiwa chini ya miti ya asili kabisa yenye kivuli na hali nzuri ya hewa.

Hala na Mwira

Haya ni maeneo baada ya kuondoka Mlowa na kwenda hifadhini, ni maeneo ya ajabu sana  ni maeneo yenye msitu, na vichaka vinene sana, maeneo haya yanatawaliwa na miti jamii ya miombo na acacia. Ni maeneo ambayo hayana network (mtandao wa simu) kabisa, ukiwa maeneo haya huwezi kupokea simu wala kumpigia mtu simu, ni maeneo ya ajabu sana. Na watu jamii ya wamang’ati ndio hukaa zaidi maeneo haya. Utaona mifugo kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda na mbwa wakivuka barabara kutoak upande mmoja kwenda upande mwingine. Vile vile ni maeneo ambayo yapo mbali sana na huduma muhimu kama vile afya,elimu, maji nk. Katika maeneo hayo huwezi kuona nyumba hata moja unapotoka Mlowa hadi unafika Mwira,Hala hakuna nyumba yoyote.

Never Ending

Ndio ni never ending, sehemu iliyopambwana sanamu na mabango mazuri yenye taarifa na jumbe mbali mbali kuhusiana na upekee wa hifadhi ya Ruaha, na huduma zinazopatikana ndani ya hifadhi hii. Hapa ni sehemu ya kwanza unapomaliza Mwira, ukifika hapa utaona njia panda, barabara mbili kubwa, (upande wa kulia na kushoto) upande wa kulia inaenda mpaka katika geti la hifadhi, barabara hii ni ya ajabu sana imenyooka sana na inapokatisha hakuna makazi ya watu, inakatisha katikati ya pori kubwa sana hadi unafika katiak geti kuu la hifadhi, kuanzia never ending hadi getini ni kilometa 60. Hii ni barabara inayopitia katiaka campsite ya Mabata Makali na Ranger post ya Madogolo. Barabara ya pili ambayo ipo upande wa kushoto ndio inyaopitia katika vijiji vitatu hadi unafika getini, vijiji hivyo ni Idodi, Mapogoro, na Tungamalenga.

MBOMIPA

Baada ya kufika tungamalenga inayofuata ni pori tengefu( WMA) kwa ajili ya wanyamapori. Wildlife Managemen Area (WMA). Hili ni eneo maalumu linalolinda hifadhi ya Taifa yaRuaha ili Wanyama wewe na sehemu ya kwenda kwa usalama zaidi, eneo hili ni mali ya vijiji vya Tarafa ya Pawaga na Idodi, hivyo faida zinazotokana na utalii, uwekezaji zinakwenda kuwanufaisha wanajamii wa maeneo haya muhimu. Hili ni eneo la mwisho kabisa ambalo lina idadi kubwa sana ya wanyamapori hasa simba na fisi, tembo na tandala na swala. Hivyo ni eneo kubwa sana ukilinganisha na maeneo mengine ya aina hii, japokuwa kunachangamoto zake kubwa, lakini bado lina manufaa kwa ulinzi na usalama wa wanyamapori na wanajamii kwa ujumla.

Hizi ni baadhi tu ya sehemu muhimu tu, unapoamua kuja kutembelea hifadhi ya Taifa ya Ruaha basi kabal hujafika hifadhini utakutana na vituo na sehemu hizo zenye historia nzuri nay a kuvutia kwa kila atayesikia na kutembelea sehemu hizi. Kuna sehemu nyingine nyingi sana zilizopo nje ya Hifadhi ya Ruaha ambazo zitakusisimua na kukufanya uamue kuchukua hatua ya kutembelea hifadhi hii nzuri sana. Hivyo nimeamua kukuandikia hayo machache tu yaliyopo nje ya hifadhi hii, au yaliyopo barbarani kabla ya kufika hifadhini ili ufurahiye safari yako ukiwa na gari. Ingawa itachukua muda kidogo kufika hifadhini lakini utapata mambo ambayo huwezi kuyapata unapotembelea hifadhi nyingine. Hapa ni zaidi ya Hifadhi.

Karibu sana Iringa, karibu sana Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Makala hii imeandaliwa na kuandikwa na;

Hillary Mrosso

0742092569

hillarymrosso@rocketmail.com

 

Shares:
Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *