Ndugu msomaji wa makala zetu, naamini umzima na bhuheri wa afya. Ni matumaini yangu uliweza kujifunza kupitia makala iliyopita kuhusu maana na sababu za migogoro kati ya binadamu na wanyamapori. Kama hukusoma makala ya mwanzo, unaweza kuisoma hapa Migogoro Kati Ya Wanyamapori Na Binadamu, Nini Chanzo? Nani Wa Kutatua Migogoro Hii?
Makala hii ni mwendelezo wake ambao tutajifunza wanyamapori wanaohusika kwenye migogoro hii, kuanzi wadogo mpaka wale wakubwa wanaofahamika zaidi na watu wengi. Kama Makala iliyopita ilivyo, ni mkusanyiko wa taarifa za migogoro inayotokea barani Afrika, Australia na India. Pia nilitilia mkazo matukio ya migogoro inayojirudia rudia kila wakati.
Wanyamapori wakubwa wanaosababisha miogogoro kama vile tembo, simba, wamekuwa na mahitaji makubwa ya chakula na eneo la malisho. Hivyo hujikuta wakiingia kwenye maeneo ya watu kwa ajili ya kutafuta malisho na maji.
Makala hii tutaangalia mnyama mmoja mmoja kwa upana zaidi ili kuweza kujua ni maeneo gani, wakati gani na pia tutaangazia tabia gani huzionyesha kipindi wanasababisha migogoro hii.
Kuna wanyama wasiotajwa mara nyingi ila wanamchango mkubwa katika kusababisha migogoro mfano, jamii mbalimbali za ndege na nyoka.
Ndege
Jamii mbalimbali za ndege wakazi na wale wahamao walao nafaka kama jamii ya kwelea na njiwa huvamia mazao kama mpunga, alizeti, ulezi na mtama. Kupitia ripoti ya FAO (Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo) umeainisha ndege hawa huvamia wakiwa katika makundi makubwa yanayohamia mashambani hasa nyanda za juu kusini, kanda ya kati na kanda ya ziwa nchini Tanzania, Botswana na Zimbabwe.
Kwa mfano, Kwelea kundi moja hukadiriwa kuwa na zaidi ya ndege milioni mbili, ambapo ndege mmoja inakadiriwa hula 10g ya nafaka hivyo kundi moja huweza kula tani 20 kwa siku ambayo hupelekea hasara kubwa katika uzalishaji na kwa jamii. Athari nyingine kubwa ni pamoja na wakulima kulazimika kutumia muda mwingi kulinda mashamba pia hulazimika kuvuna mazao yao mapema kabla hayajakomaa vizuri. Pamaoja na hayo, hasara hizi zinazosababishwa na ndege huweza kufikia dola za Marekani zaidi ya milioni 88.6 kwa mwaka.
Nyoka
Viumbe hawa hawana matukio mengi ya migogoro kama kuvamia na kuuma watu isipokuwa wao ndio wamekuwa katika hatari kubwa ya binadamu pale wanapokuwa majumbani au mashambani mwao.
Hii imechangiwa na maumbile ya miili yao yenye kusababisha hofu na chuki kubwa kwa binadamu. Hata hivyo, mitazamo hasi na Imani za baadhi ya jamii imesababisha asilimia kubwa ya viumbe hawa kuuawa pasipo kujali faida zao.
Mfano, Katika utafiti uliofanywa na Martinez Silvestery mwaka 2014, ilionyesha kuwa zaidi ya watu 140,000 hufariki kutakana na nyoka wenye sumu. Kati ya vifo hivyo, vifo 58,000- 62,000 vimeripoptiwa kutokea katika nchi ya India. India ndio sehemu iliyoripotiwa matukio mengi ya vifo vya watu vilivyosababishwa na nyoka kuliko sehemu nyingine duniani.
Tembo
Tembo amekuwa akitajwa sana kwenye migogoro na binadamu nchini Tanzania na nchi nyingine kama vile Zambia, Kenya, Kameruni na India. Miingiliano yao imekuwa ikitokea maeneo jirani na hifadhi, ndani ya hifadhi, jirani na makazi au malisho yao pia katika mapito yao ya kawaida na kwenye shoroba.
Uvamizi huu huendana na misimu ya mvua ilivyo katika eneo husika, hivyo kwa maeneo yenye mvua msimu mmoja mazao huvamiwa yakiwa yanakaribia kukomaa na kwa maeneo ya umwagilia huvamiwa muda wote.
Tembo amekuwa akisababisha uharibifu wa mazao mashambani (mazao kama mahindi, ndizi, viazi), nyumba, maghala ya chakula na miundo mbinu ya maji. Uvamizi wake mashambani umekuwa sio rahisi kuutabiri wala athari zake, kwa sababu tukio lake moja huwa na maafa makubwa zaidi kuliko ilivyo kwa wanyamapori wengine.
Pia wakati mwingine amehusika kusababisha vifo vya watu, mfano katika kipindi cha mwaka 2017 – 2019 Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) iliripoti idadi ya watu 70 kuuliwa na tembo na 16 kupata majeraha. Matukio haya yamekuwa yakitokea pale watu wakiwa wanalinda mazao yao shambani hasa kipindi cha asubuhi sana na jioni.
Nchini Tanzania matukio haya yameripotiwa sana katika wilaya ya Bariadi, Kilombero, Itilima, Manyoni na Tunduru. Kwa upande wa maeneo yaliyohifadhiwa imekuwa ikitokea sana upande wa Magharibi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hifadhi ya jamii (WMA) ya Burunge, Randilen, Enduitmenti, Idodi – Pawaga, hifadhi ya taifa Mkomazi, Mikumi, upande wa Magharibi wa Rungwa – Kizigo Muhesi na Kilombero.
Mamba
Mamba ndiye reptilian mwenye migogoro mingi na binadamu kwa kuwajeruhi na kuwaua. Tafiti zinaonyesha kuwa mamba husababisha vifo vingi vya binadamu barani Afrika kuliko mnyama mwingine. Mfano, mwaka 2010 hadi 2020, jarida la crocBite limeripoti zaidi ya vifo 65 vilivyosababishwa na mamba nichini Tanzania.
Migongano mingine hutekea kati ya wavuvi na mamba, inaripotiwa kuwa mamba wamekuwa wakiharibu nyavu na vifaa vingine vya wavuvi wa samaki. Hali hii husababisha hasara na hatari kwa wavuvi na mamba, pamoja na hayo kuna taarifa za mifugo kama vile mbwa huvamiwa na mamba wakiwa pembezoni mwa mto.
Maeneo yenye hatari zaidi nchini kuingia kwenye migongano na mamba ni pamoja na ziwa Victoria, Tanganyika, Rukwa, Mto Rufiji, Ruvuma, Kilombero na mto Wami. Hatari hizi za kuvamiwa na mamba mara nyingi hutokea kando ya mito au maziwa ambayo yana mamba. Takwimu zinaonyesha wavuvi, vijana na watoto ndio wapo hatarini zaidi kuvamiwa na mamba.
Kiboko
Kiboko ni miongoni mwa wanyamapori ambao wanatajwa sana kwenye migogoro na watu. Uvamizi wao umekuwa ukihusisha kuharibu mazao mashambani, nyavu za uvuvi na vifaa vingine vya majini, matukio mengi ya kiboko hutokea wakati wa usiku.
Imekuwa ikitokea mara chache sana kwa mnyama huyu kusababisha vifo na majeruhi kwa binadamu. Uvamizi unaosababishwa na kiboko mara nyingi hutokea pembezoni mwa mto, ziwa au kwenye njia zake. Hivyo ni hatari watu kuifanya shughuli zao pembezoni mwa makazi ya kiboko.
Mfano, katika ripoti ya Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Migogoro ya Binadamu na Wanyamapori 2020-2024, imetaja kuwa nchini Zambia takwimu za miaka kuanzia 2002 hadi 2008 zinaonyesha asilimia 19 ya vifo vyote vinavyotokana na wanyamapori vimesababishwa na kiboko. Migogoro hii ilisababisha viboko wengi kuuwawa kwenye matukio yaliyosababisha vifo kwa watu.
Nchini Tanzania, Taasisi ya utafiti wa wanyamapori (TAWIRI)ilifanya sense ya kiboko mwaka 2001, sense hiyo ilionyesha idadi kubwa (80%) ya viboko wapo ndani ya maeneo tengefu na kwenye mto Kilombero, Rufiji, Ruaha, Katavi-Rukwa, Ugalla and Malagarasi, Serengeti na Mara.
Wanyama walao nyama (Simba, Chui, Fisi na Mbwa mwitu)
Wanyama hawa wamekuwa wakileta sana migogoro na binadamu hasa wale wafugaji wanaoishi pembezeni mwa maeneo tengefu. Wanyamapori hawa wamekuwa wakivamia maeneo mbali mbali yenye mifugo. Mifugo mingi imeripotiwa kuvamiwa ikiwa machungani na wakati mwingine wakiwa nyumbani wakati wa usiku.
Uvamizi huu umekuwa unategemeana na ukubwa wa umbo la mfugo, hivyo mara nyingi imeripotiwa fisi na duma huwinda mifugo yenye maumbo madogo ambao ni mbuzi, ndama wa ng’ombe, kondoo na mbwa wa kufugwa na vamizi hizi nyingi zimekuwa zikitokea wakati wa usiku kwenye mazizi au kwenye nyumba wanakolala.
Kwa upande wa simba, ameripotiwa akiwinda mifugo yenye maumbo makubwa kama vile ng’ombe na punda ambapo mara nyingi hutokea wakati wa malisho wakati wa mchana.
Uvamizi wa mifugo hufanyika nyakati za mchana, mfano Maasai steppe lakinikwa eneo la Idodi – Pawaga, uvamizi wa mifugo mara nyingi hutokea wakati wa usiku. Eneo la Idodi – Pawaga,limekuwa na matukio mengi ya uvamizi yanayosababishwa na simba 60%, fisi 30% na chui 10%.
Nchini Tanzania iliripotiwa idadi kubwa ya uvamivi hutokea katika tambarare za Simanjiro, Maasai steppe na Idodi – Pawaga. Na kwa kipindi cha mwaka 2012/13 – 2018/19 , ripoti ilionyesha mifugo 792 iliyouliwa na wanyamapori walao nyama, hata hivyo haizidi vifo vingi visababishwavyo na magonjwa zaidi.
Kwa upande wa Kenya, hasa upande wa hifadhi ya mashariki Tsavo wamekuwa wakivamia ng’ombe walioko kwenye ranchi na kusababisha hasara kubwa wakifwatia na duma kwa mifugo midogo. Wanyama hawa wamekuwa wakijirudia nchi mbalimbali katika kuvamia mifugo mfano nchini Zimbabwe ambako ilionekana hadi nyani nao walikuwa wakiua mifugo midogo midogo. Wanyamapori hawa hasa simba na fisi wakati mwingine husababisha vifo na majeruhi kwa binadamu, kwa chui hutokea mara chache sana na duma haijawahi kuripotiwa.
Picha hii ni kutoka katika mtandaoni imepigwa huko Kameroon na Chuo kikuu cha Leiden
Kama ilivyokuwa kwenye sababu zinazosababisha migogoro hii kujirudia katika nchi mbalimbali vivyo hivyo kwa wanyamapori wasababishao kama ilivyotajwa na kuelezwa hapo juu. Na katika kutilia mkazo ikumbukwe wanyamapori wote wanauwezo wa kusababisha athari hasi kwa binadamu, tofauti yake kubwa itakuwa ni kipimo cha athari hio kwamba ni kubwa au ndogo. Mpendwa msomaji wa Makala zetu, nikukaribishe tena kuzifatilia makala zijazo zitakazo kufundisha zaidi katika athari za wanyamapori hawa na jinsi ya kupunguza migogoro hii.
Makala hii ni muunganiko wa makala mbalimbali za lugha ya kingereza, hivyo imeandaliwa na kutafsiriwa kwa lugha Kiswahili. Mhariri wa makala hii ni Hillary Mrosso, ambaye ni mmiliki wa blogu hii. Makala hizo ni pamoja; Mpango mkakati wa taifa wa kukabiliana na migogoro ya wanyamapori na binadamu kwa kipindi cha mwaka 2020 – 2024, Yann de Mey & Matty Demont, 2013, Elisa Distefano na Philip J. Nyhus 2016.
Kwa ushauri au maswali kuhusu makala hii, usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii
Leena lulandala
0755369684