Habari msomaji wa makala za wildlife Tanzania, karibu tena kwenye mfululizo wa makala hizi za uchambuzi wa sheria ya wanyamapori. Leo tunaendelea na sehemu ya nne ya uchambuzi wa sheria yetu ya wanyamapori ya mwaka 2009. Tutaendelea na kifungu cha 25 ambacho kinatamka wanyama wa taifa wanao ruhusiwa kuwindwa (Declaration of A National Game).

25-.(1) Waziri anaweza, baada ya kutoa taarifa kwenye gazeti la kiserikali, kutangaza mnyama au mnyama wa daraja fulani kuwa mnyama wa kuwindwa (national game). Kwa hiyo hapa tunaona mwenye mamlaka ya kutangaza wanyama wa kuwindwa kwenye nchi au taifa ni waziri mwenye dhamana hiyo.

(2) Waziri anaweza kuweka utaratibu unaoeleza jinsi ambavyo wanyama wa kuwindwa na wanyama wengine wanaweza kutumika kwa kusudi la kibiashara/ kuuzwa.

MAKATAZO KUHUSIANA NA WANYAMA WA KUWINDWA (RESTRICTION RELATING TO A NATIONAL GAME)

Kwenye kipengele hiki tutajifunza sheria inavyo weka utaratibu wake wa namna ya kuwinda wanyamapori walioruhusiwa kuwindwa na waziri. Hi ni nzuri kwa ajili ya kuweka tutaratibu mzuri wa kuwinda wanyamapori pekee walioainishwa kwenye sheria hii tu na ambao wameruhusiwa na waziri au mkurugenzi.

26-. (1) Mtu hataruhusiwa isipokuwa kulingana na ruhusa ya maandishi kutoka kwa Mkurugenzi, ambayo inaruhushu kufanya uwindaji, kuua, kukamata, kujeruhi au kusumbua mnyama wowote wa kuwindwa. Hivyo basi hata kama wanyama wa kuwindwa wametangazwa na kufahamika, utaratibu wa sheria uko wazi kwa namna ya kufanya uwindaji kwenye maeneo husika na wanyama husika walio tangazwa kuwa ni wanyama wa taifa wa kuwindwa.

(2) Mtu atakayekiuka masharti yoyote yaliyoambatanishwa kwenye kibali au ruhusa iliyotolewa ya kuwinda kwenye kifungu kidogo cha (1), anafanya kosa na atahukumiwa kuwa na hatia-

(a) kwa kesi yoyote ambayo inahusisha uwindaji, ukamataji, or uuaji wa wanyama wa taifa walioruhusiwa kuwindwa, atawajibika kutoa faini isiyopungua  mara mbili ya thamani ya mnyama aliyewindwa, kukamatwa au kuuwawa au kwenda jela kifungo kidichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka mitano; na

(b) kwa kesi nyingine yoyote, faini itakuwa sio chini ya shilingi laki tatu (300,000) lakini isizidi shilingi milioni moja (1,000,000) au kifungo cha jela kisichopungua  miezi kumi na mbili lakini kisizidi miaka mitatu.

MSIMU USIORUHUSU UWINDAJI (CLOSED SEASON)

Msimu au kipindi ambacho uwindaji hauruhusiwi, ni sehemu ya sheria hii ambayo inataka kila mtu aelewe kuwa sio wakati wote uwindaji unaruhusiwa kwenye mapori ya hifadhi za wanyamapori, lakini kuna kipindi maalumu ambacho uwindaji unasitishwa kwa ajili ya sababu za kibaiolojia na za kiikoloia kifungu cha 27 ndio kinaelezea

  1. Waziri anaweza, baada ya kutoa taarifa kwenye gazeti la serikali, kuzuia, kukataza au kurekebisha uwindaji, uuaji, au ukamataji wa mnyama yeyote au daraja la mnyama yeyote kwenye eneo kwa muda au kipindi ambacho atakielezea kama kipindi kisichoruhu uwindaji “ (closed season)”

MAKATAZO KUHUSIANA NA MSIMU USIORUHUSU UWINDAJI RSTRICTION RELATING TO CLOSED SEASON)

Kwenye kifungu hiki cha 28 kinaelezea matakwa ya sheria hii kwenye msimu usioruhusu uwindaji

  1. –(1) Taarifa ikishatolewa kwenye kifungu cha 26 kwenye eneo husika, mtu yeyote hataruhusiwa kuwinda, kuua, kukamata au kujeruhi mnyama yoyote kwenye eneo hilo kwa kipindi husika, isipokuwa kulingana na kibali cha maandishi kilichotolewa na Mkurugenzi.

(2) Mkurugenzi hataruhusiwa kutoa kibali cha maandishi kilichoelezwa kwenye kifungu kidogo cha (1) cha kifungu cha sheria hii bila ridhaa ya Waziri mwenye dhamna hiyo.

(3) Mtu yeyote atakayekiuka masharti na mapendekezo ya kifungu hiki au mapendekezo yaliyoambatanishwa  na kibali chochote kilichotolewa na kifungu kidogo cha (1) anafanya kosa na atakuwa na hatia ya;

(a) kwa kesi ya kuwa na hatia inayohusisha uwindaji, kukamata, au kuua mnyama aliyeruhusiwa kuwindwa, ata wajibika kulipa faini isiyopungua mara mbili ya thamani ya mnyama aliyewindwa, kukamatwa,kuuwawa au kwenda jela kwa kifungo kisichopungua miaka mitatu lakini kisichozidi miaka mitano;

(b) kwa kesi ya kuwa na hatia inayohusisha uwindaji, ukamataji, au uuaji wa mnyama ambaye ametajwa au kuelezwa bayana kwenye sehemu ya II ya Jedwali la Kwanza la sheria hii, atawajibika kwenda jela kwa kifungo kisichopungua miaka miwili lakini kisichozidi miaka mitano, pia mahakama inaweza kumwongezea adhabu ya kulipa faini ya kiasi kisichopungua mara mbili ya thamani ya mnyama aliyewindwa, uwawa, au kukamatwa;

(c)  Kwa kesi ya kuwa na hatia ya inayohusisha uwindaji, ukamataji au kuuwawa kwa mnyama ambaye ametajwa kwenye sehemu ya III ya Jedwali la Kwanza la sheria hii, atatakiwa kwenda jela kwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja lakini kisichozidi miaka mitatu, na pia mahakama inaweza kumwongezea adhabu ya kulipa faini mara mbili ya thamani ya mnyama aliyewindwa, uwawa, au kukamatwa; na

(d) Kwa kesi yoyote, faini itakuwa isipungue shilingi laki tatu (300,000) lakini isizidi shilingi milioni mbili (2,000,000) au kwenda jela kwa kifungo kisichopungua miezi sita na isiyozidi miezi kumi na mbili au vyote kwa pamoja.

MASHARTI YA JUMLA (GENERAL PROVISIONS)

  1. Rais anaweza, kwa faida ya wananchi au kwa faida ya umma, na baada ya kutoa taarifa kwenye Gazeti la serikali, kuboresha au kurekebisha mashinikizo au masharti yote yaliyowekwa kwenye sehemu hii kuhusiana na pori la akiba, pori tengefu,au maeneo oevu ya akiba, na wakati mapendekezo yote yatakayotolewa yatabadilishwa kulingana na mapendekezo au matakwa ya hayo mapendekezo ya Rais.
  2. Hakuna kitu katika sheria hii kitatafsiriwa kama kumpa mamlaka Mkurugezi wa wanyamapori kutoa ruhusa na vibali kufanya uwindaji, kuua, au kuakamata mnayama yoyote kwenye hifadhi yoyote ya taifa kinyume na sheria ya hifadhi za Taifa au Ngorongoro kinyume na mapendekezo ya sheria ya hifadhi ya Ngorongoro.

Kwa mantiki hiyo utaelewa sasa kwanini kwenye hifadhi za taifa uwindaji wa aina yoyote hauruhusiwi na pia hata kwenye hifadhi ya eneo la Ngorongoro shughuli zote za uwindaji haziruhusiwi kabisa kwa mujibu wa sheria hii na sheria nyingine za uhifadhi wa wanyamapori Tanzania.

Naamini kufikia hapa umepata mwanga mzuri na umeelewa jinsi ambavyo sheria hizi zinzvyofanya kazi kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Leo ndio mwisho wa uchambuzi wa sehemu hii ya nne ya sheria hii ya uhifadhi wa wanyamapori ya mwaka 2009. Makala ijayo tutaendelea na uchambuzi wa sehemu ya tano ya sheria hii. Endelea kufuatilia makala hizi kwani zina msaada mkubwa kwa watu wote ili kwa pamoja tunufaike na tushirikiane kwenye uhifadhi wa wanyamapori wetu na maliasili nyingine za nchi yetu. Karibu tuendelee kuwa pamoja kwenye hili la kuelemisha jamii kuhusu uhifadhi wa wanyamapori namaliasili nyingine, mshirikishe mwenzako au Rafiki yako makala hii.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania