Mpendwa msomaji wa Makala  za wanyamapori. Karibu katika Makala ya mifano mitano, Makala hii itatumia mifano kutufunza masuala anuani hususani juu kutoweka kwa wanyama na  wanyama walio katika hatari ya kutoweka.

Awali ya yote tufahamu nini maana ya kiumbe/mnyama kutoweka. Kutoweka kwa viumbe/mnyama  kiikologia huitwa ‘Species Extinction’ ambayo  ni hali  kundi au makundi ya viumbe wa spishi/aina  flani kupotea katika uso wa dunia. Kiumbe/mnyama hutambulika kuwa kimetoweka  pale kiumbe wa mwisho, mathalani mnyama wa wa Spishi  husika anapokufa hivo kunakuwa hakuna tena kiumbe hicho duniani, wanasayansi wakidhibitisha hilo Shirika la Uhifadhi Duniani (IUCN) humtangaza kuimbe huyo kuwa ametoweka. Aidha, ipo aina ya extinction ambayo hufamika kwa jina la ‘’local extinction’’ ambapo kiumbe/mnyama hupotea katita eneo flani ambalo awali lilikuwa makazai yake, hivo tutasema kuwa mnyama huyo ametoweka katika eneo hilo licha ya kuwa anaweza kupatikana katika maeneo mengine. Soma zaidi SEHEMU 1: Orodha ya Spishi za Ndege Wanaopatikana Tanzania Pekee

Kadhalika, vipo viumbe ambavyo bado havijatoweka lakini vipo katika hatari ya kutoweka kutokana na changamoto ambazo zinavikabili. Miongoni mwa changamoto hizo ni: uharibifu wa mazingira, uvunaji haramu wa wanyama, uchafuzi wa mazingira, mlipuko wa magonjwa, viumbe vamizi na mabadiliko tabianchi. Changamoto hizi huweza kusababisha vifo, kuzorotesha ukuaji na kuzaliana kwa viumbe wa spishi husika na kuathiri uwezo wa spishi huyo kupata mahitaji yake muhimu kwa ajili ya kuishi. Hatari ya kutoweka kwa viumbe/wanyama hutofautiana kati ya spishi moja na nyingine huku baadhi ya spishi zikiwa katika hatari kubwa aidi ya kutoweka.

Tunapoongelea kutoweka kwa Wanyama ni hali ambayo imekwisha tokea miaka kadhaa iliyopita kwa baadhi ya spishi , ambao walikuwepo duniani kwa kipindi hicho lakini kutokana na sababu mbalimbali walitoweka kabisa duniani hivyo sasa hakuna spishi hizo tena. Mifano mitano ya spishi ambazo zimekwisha kabisa duniani ni kama ifuatayo

 1. NDEGE DODO (Jina la kisayansi: Raphus cucullatus)

Ndege huyu ni moja ya mifano maarufu zaidi ya spishi waliotoweka .Ndege huyu alikuwa ni moja ya ndege wasio na uwezo wa kupaa .Ndege huyu alipatikana katika kisiwa cha Mauritius. Dodo alikuwa ni ndege mkubwa mwenye manyonya meupe  na kijivu. Kimsingi ndege hawa waliokuwa wakiishi katika misitu , mara chache walisogea maeneo ya karibu na Pwani. Zaidi ya miaka millioni 26 iliyopita ndege hawa walifurahia walipokuwa wakizungukia maeneo ya visiwa vya Mascarene, kutokana na uwepo wa chakula tele na hakukuwa na wanyama waliokuwa wakiwawinda, ndege hawa hawakuondoka maeneo haya ya Pwani hivyo kadri miaka ilivyopita wazawa wapya wakaanza kuwa wakubwa zaidi ,wenye midomo mikubwa huku wakiwa na mabawa madogo.

Mnamo karne ya 16 binadamu walianza kuhamia katika kisiwa cha Mauritius huku wakileta na wanyama wao kama panya, mbwa na ng’ombe ambao waliharibu mazingira ya asili waliyokuwa wakiishi dodo. Pia uwindaji uliokithiri ambapo binadamu waliwawinda ndege hawa ili wapate nyama ulisababisha kwa kasi kubwa kupungua kwa idadi ya ndege hawa na mnamo karne ya 17 ndege hawa wa dodo walipotea kabisa duniani. Hii inasikitisha sana.

NDEGE DODO (Jina la kisayansi: Raphus cucullatus). Source National Geograph   

CHURA WA DHAHABU (Jina la Kisanyansi: Incilius periglenes)

Chura huyu alipatikana katika misitu ya Monteverde cloud forest pekee. Spishi hii ilikuwa  na rangi ya manjano yenye kung’aa ,hivyo ilikuwa ni rahisi kumuona katika maeneo yake. Spishi huyu alipendelea kukaa chini ya ardhi ,na alikuja juu ya ardhi mara chache mwishoni mwa msimu wa kiangazi kwa ajili ya kuzaliana.

Kupotea kwa chura huyu ni tukio la kusikitisha ambalo lilitokea mnamo karne ya 20. Walianza kupungua kwa kasi kubwa sana kuanzia mwaka1987. Spishi wa mwisho wa chura hawa alioekana mwaka 1989 ambapo wanasayansi wanasema sababu kuu inayoweza kuwa imechangia kupotea kwa spishi hawa ni mabadiliko ya tabianchi, kutokana na ongezeko la joto ambalo linasababisha ugonjwa wa Chytridiomycosis ambao unaathiri tabaka la nje la ngozi  ya chura pia uchafuzi wa mazingira uliathiri viumbe hawa. Baada ya hapo ulifanyika utafutaji wa kina wa spishi hawa lakini hawakuwahi kuonekana tena. Mwaka 2004 shirika la IUCN lilitangaza rasmi kuwa chura wa dhahabu wametoweka. Zaidi unaweza kusoma makala hii Fahamu Jinsi Shughuli Za Binadamu Zilivyoharibu Makazi Ya Chura Anayezaa Nchini Tanzania

Picha ya Vyura wa dhahabu: Chanzo:monteverdetravel.com

  1. KIFARU MWEUSI WA MAGHARIBI (Jina la kisanyasin: Diceros bicornis longipes)

Kifaru huyu ni moja ya aina nne za vifaru weusi ulimwenguni. Kifaru huyu alikuwa na uzito unaofikia pauni 1500 na 2900, urefu wa takribani futi tano na pembe mbili kubwa, huku pembe ya mbele ikiwa kubwa zaidi. Zaidi soma hapa Tumjue Faru Ni Myama wa Namna Gani

Kifaru Mweusi wa Magharibi alikuwa akipatikana Afrika Magharibi, idadi yake ilianza kupungua  kwa kasi kubwa kutokana na uwindaji haramu na uharibifu wa mazingira.Mwaka 2011 kifaru huyu alitangazwa rasmi kama spishi iliyotoweka.

Picha ya KIfaru Mweusi Magharibi: Chanzo: savetherhino.org

  1. PASSENGER PIGEON (Jina la kisanyansi: Ectopistes migratorius)

Ndege hawa waliokuwa na manyoya kijivu juu ya mgongo na kichwa chenye rangi ya bluu iliyopauka.Kutoweka kwa ndege huyu kulitokana na uwindaji wa kupita kiasi, uharibifu wa mazingira na kilimo na ufugaji wa majini. Miaka ya zamani sana ndege hawa walionekana kwa wingi na idadi yao ilifikia billioni.

Baadae watu waliwawinda ndege hawa kwa ajili ya nyama na kusababisha idadi yao kupungua, pia uharibifu wa makazi ulichangia zaidi kupotea kwa ndege hawa. Ndege aliyeitwa Martha alikuwa ndiyo ndege wa mwisho wa aina hii kufa, ambapo alikufa mwaka 1914  baada ya ndege wenzake madume wawili kutangulia Kufa mwaka 1910.

Picha ya Passenger Pigeon: Chanzo: bbcwildlife.com

  1. KOBE MKUBWA WA RODRIGUES (Jina la Kisanyansi: Cylindraspis peltastes)

Kobe hawa waliokuwa ni wanyama wa ardhini wenye magamba makubwa walikuwa wakila majani, matunda na mimea iliyopatikana katika kisiwa cha Rodrigues. Kisiwa cha Rodrigues kilifanywa kuwa kisiwa cha kibiashara na makazi ya watu. Hii ilileta usumbufu mkubwa sana kwa kobe hawa kwani binadamu walianza kuwawinda, mazingira yao ya asili yalidhurika na kuharibiwa. Hivyo kobe hawa walianza kupungua idadi yao kwa kasi na hatimaye walitoweka kabisa.

Picha ya Kobe Mkubwa Wa Rodrigues: Chanzo, mediastorehouse.com

Ingawa juhudi za uhifadhi kwa sasa zimekuwa kubwa lakini bado kuna wanyama wengi ambao wako kwenye hatari ya kutoweka. Mifano mitano ya wanyama walio katika hatari ya kutoweka ni kama ifuatayo

  1. KIFARU MWEUSI (BLACK RHINOCEROUS)

Kifaru mweusi ni mnyama mwenye mwili mkubwa mwenye rangi ya kahawia hadi nyeusi ,ana mdomo mrefu na wembamba. Kwa kawaida hupatikana katika maeneo ya savanna na misitu. Wanyama hawa katika nchi yetu wanapatikana katika hifadhi ya Serengeti, Mkomazi, Nyerere na Eneo la Hifadhi la Ngorongoro na maeneo mengine. Soma zaidi kufahamu athari kubwa kwa wanyama hawa Yafahamu Mambo Yanayochochea Uhitaji Wa Pembe Za Faru Katika Nchi Ya China

Sababu zinazokabili mnyama huyu ni uwindaji haramu na uharibifu wa makazi yao hivyo inaathiri kwa kiasi kikubwa idadi yao. Katika orodha ya IUCN spishi hii imetajwa kama critically endangered maana yake wako katika Hatari kubwa ya kutoweka. Kuna mengi hatuyajui kuhusu vifaru na tabia zake, makala hii itakupa mwanga zaidi Mambo Haya Ndio Yanayosababisha Tembo Na Faru Wasifike Miaka 20 Ijayo,

Picha ya Kifaru mweusi, Chanzo:globalgiving.com

  1. MBWA MWITU WA AFRICA (AFRICAN WILD DOG)

Ni mnyama wa familia ya Mbwa mwitu ambaye ana alama za kipekee za manyoya zenye rangi mbalimbali kama vile nyeusi, nyekundu, kahawia, nyeupe na manjano. Kila mnyama ana mfumo wake wa alama wenye umbo tofauti na wote wana maskio makubwa na ya mviringo. Sababu zinazosabisha wanyama hawa kuwa hatarini kutoweka ni uharibifu na uvamizi wa makazi yao, uwindaji haramu, magonjwa na migogoro ya binadamu vyote hivi vinachangia kwa kiasi kikubwa Mbwa hawa kupungua idadi kwa kasi kubwa. Katika orodha ya IUCN Wanyama hawa wametajwa kama wako katika hatari kubwa ya kutoweka (critically endangered). Jisomee zaidi kufahamu mengi kuhusu mbwa mwitu na tabia zake hapa Zijue Sifa Mbalimbali Za Mbwa Mwitu Wa Afrika Na Utofauti Wake Na Mbwa Wa Kufugwa

Picha ya Mbwa Mwitu wa Afrika, Chanzo: wwf.org

  1. SOKWE ( CHIMPANZEE)

Sokwe ni wanyama  jamii ya primate ambao vinasaba vyao hufanana sana na vya binadamu kwa asilima 98.7. Wana manyoya yanayofanana na kahawia hadi nyeusi, wana mikono mirefu inayofikia hadi chini ya magoti yao ya miguu. Wana mwili na viungo vyenye nguvu. Sababu zinazoathiri chimpanzee ni upungufu wa eneo la makazi kutokana na ukataji wa miti na uchomaji misitu, ujangili na magonjwa. Katika maeneo mengi duniani mnyama huyu anakabiliwa na changamoto hizi na ametajwa kuwa yuko hatarini sana kutoweka katika orodha ya IUCN. Kwa mengi unaweza kusoma makala hii zaidi Maajabu Ya Sokwe Wa Hifadhi Ya Taifa Gombe

Picha ya Sokwe, Chanzo: serengetinationalparksafaris.com

  1. KORONGO TAJI KIJIVU (GREY CROWNED CRANE)

Huyu ni ndege mkubwa mwenye kuvutia, kichwani kwake ana taji la manyoya ya kijivui nayofanana na kofia. Mwili wake kiasi kikubwa ni rangi ya kijivu na mabwawa meupe. Korongo Taji Kijivu  ana shingo na miguu mirefu, mara nyingi hupatikana sehemu yenye majimaji.

Tishio la ndege hawa ni upungufu wa eneo la makazi yao ya asili, uvamizi wa ardhi kwa ajili ya kilimo, makazi ya binadamu na ujangili. Ndege huyu ameorodheshwa kuwa katika hatari ya kupotea(endangered). Kwa mengi kuhusu ndege huyu unaweza kusoma makala hii Mfahamu Ndege Anaye Heshimika Zaidi Katika Bara La Afrika

Picha ya Korongo Taji Kijivu, Chanzo:dailnewws.com

  1. TEMBO WA SAVANA (AFRICAN SAVANNAH ELEPHANT).

Tembo ni mnyama mwenye umbo kubwa kupita wanyama wote nchi kavu. Mnyama huyu hupendelea kukaa katika maeneo ya nyika, mabwawani na kwenye fukwe za ziwa. Tishio la mnyama huyu mkubwa ni kupungua kwa eneo la makazi, ujangili, migogoro kati ya binadamu na tembo. Tembo ameorodheshwa kuwa katika hatari ya kupotea (endangered)

Picha ya Tembo wa Savana, Chanzo: thoughtco.com

Mpendwa msomaji wa makala hii ni jambo la kusikitisha sana kuona wanyama wazuri, wenye kuvutia na wenye sifa mahususi kama ndege dodo, chura wa dhahabu na wengine wakiwa hawapo tena duniani. Ni dhahiri kuwa dunia ya sasa inakosa uwepo wa viumbe muhimu sana na wenye kupendeza na kuvutia. Wanyama hawa watano nimewatumia kama mifano tu ya wanyama wengi wazuri, wenye rangi nzuri, wenye muonekano mzuri, wenye miito mizuri  ambao hawapo tena duniani.

Mifano ya pili ambayo ni ya wanyama walio katika hatari ya kupotea ni funzo, ni ukumbusho, ni kipenga kinachotukumbusha kwamba ,tusibweteke, tusiache, tusijisahau kuhamasishana , kumbushana, kufundishana njia nzuri za kuwalinda wanyama na mazingira yetu ili tusije kuwapoteza wanyama hawa muhimu, wazuri na wenye sifa kedekede duniani kote.

Katika mifano hii ni tunajifunza kwamba wanyama wote waliotoweka na walio katika hatari ya kutoweka wanakumbwa/walikumbwa na changamoto zilezile kuu ambazo ni ujangili,upungufu wa eneo la makazi na, uharibifu wa mazingira, magonjwa ,mabadiliko ya tabianchi na  shughuli mbalimbali za binadamu.

Funzo kuu ni kwamba binadamu ametokea kuwa sababu ya wanyama waliopotea au wanakabiliwa kutoweka, na inaonyesha kwamba katika kila mnyama aliyetoweka au aliyehatarini kutoweka binadamu lazima anahusika kwa namna moja au nyingine. Hivyo mimi kama mdau wa uhifadhi,mwandishi wa Makala hii, muhifadhi nitoe wito kwa watanzania wote kujitahidi kupunguza shughuli zote zinazoathiri wanyamapori na mazingira yetu shughuli hizi ni kama ujangili, ukataji miti hovyo,uvamizi wa maeneo ya hifadhi,uchafuzi wa mazingira na uchomaji misitu hii itasaidia kupunguza athari zetu kwa Wanyama wetu na kwa mazingira yetu na hata huu mchakato wa utowekaji wa Wanyama utatoweka wenyewe.

Mamlaka husika za mazingira, hifadhi, mapori ya akiba, eneo la hifadhi na serikali nzima itilie mkazo Zaidi katika sheria zinazohusu mazingira na wanyamapori wetu,na watu watakaokiuka kanuni na taratibu zilizowekwa wachukuliwe hatua kali sana ili iwe kama mfano kwa wengine wanaopanga kuharibu mazingira au kudhuru wanyamapori wetu.

TUKUMBUKE

Tusiposimama kidete kuwalinda wanyama wetu, Watoto, wajukuu ,na wajukuu wa wajukuu wetu hawatakuja kuona tembo, kifaru mweusi, korongo taji kijivu na wengine wengi kama ambavyo sisi hatujawaona dodo, chura wa dhahabu na  wanyama wengine waliotoweka.  Kwa kutowalinda vyema wanyama hawa tutakuwa hatujawatendea haki vizazi vijavyo. Hivyo tusikubali wajukuu wa wajukuu wetu kukosa uhondo wa kumuona mnyama mkubwa kuliko wote, kumuona kifaru, kumuona Mbwa mwitu na Wanyama wengine wengi wazuri na wa kuvutia.

Makala hii imehaririwa na Lucia Romward ambaye ni mwanzilishi wa taasisi ya Mwanamke katika Uhifadhi (Women in Conservation)

#Tulinde mazingira na wanyamapori kwa ajili ya wajukuu wa wajukuu wetu.

Asante

Mwandishi wa Makala

MONICA CHARLES MAHILANE

0652267935

mahialnemonica49@gmail.com