Habari ndugu Watanzania wenzangu, na marafiki zangu wote wanaofuatilia mtandao huu wa wildlife Tanzania. Baada ya kupita kwa tangazo lililotoka ofisi ya Makamu wa Rais mazingira Juni 4 mwaka huu wa 2017, kwamba Watanzania wapewe ruhusa ya kutembelea hifadhi za Taifa bure kwa siku takribani 4, nimejifunza mengi sana kwa tangazo alilo litoa waziri mwenye dhamana ya mazingira na pia mwitikio wa Watanzania kwenye ruhusa hiyo ya bure ya kutembelea hifadhi za Taifa. Pamoja na changamoto zilizojitokeza, bado limekuwa ni jambo jema sana kwa serikali kuamua kufikiri hivyo, pia kwa jinsi mwitikio ulivyokuwa kwa Watanzania nadhani kuna vitu tumejifunza wote kwa pamoja. Kwa upande wangu baada ya kujifunza machache nimeamua kushika kalamu na karatasi ili niyaandike hapa ili kuboresha zaidi endapo nafasi nyingie inapotokea ya kutembelea hifadhi za taifa bure.

Kwa hatua hii iliyochukuliwa na serikali ningependa kuipongeza kwa kufanya jambo la namna hii linye tija na malengo mzuri na makubwa ya baadaye kwenye uhifadhi wa wanyamapori. Kwa kweli bila ya kumumunya maneno tangazo hilo lilikuwa ni tangazo bora sana kuwahi kutokea katika nchi yetu. Kwanza liliamsha hamasa na kiu ya watu kutembelea hifadhi za Taifa, pia tangazo hilo lilifanya watanzania wengi waliolala na kusahau kabisa kwamba kuna vivutio vingi ambavyo vinapatikana sehemu mbali mbali katika nchi yetu kutambua hata kama hawakutembelea hifadhi yoyote lakini mimi kama mtafiti bado naona ni ishara nzuri sana kwa siku za baadaye kwa kuwa sasa wataelewa kuna sehemu nzuri ya kutembelea hapa hapa Tanzania. Sisi ambao tunapenda watanzania waone fahari kwa maliasili nyingi za wanyamapori walio nao katika nchi yao wajue ni zao na ni haki yao kunufaika nazo kwa namna mbali mbali, kama kutembelea, kujifunza, kufurahia, na hata kupata fursa mbali mbali zinazoweza kupatikana katika maeneo haya ya wanyamapori.

Nisingeweza kuendelea kuandika aya nyingine kwenye makala hii bila kuwashukuru pia wahifadhi wote wa hifadhi mbali mbali hapa Tanzania kwa kuridhia na kuunga mkono juhudi za serikali kenye suala hili la watanzania kutembelea hifadhi za Taifa bure kabisa. Kipekee kabisa niwapongeze Shirika la Taifa la Hifadhi ya Wanyamapori (TANAPA), kwa maandalizi mazuri na utayari wenu kwenye hili jambo, maana litajenga imani na ufahamu mkubwa kwa watanzania, na pia endapo watanzania watatembele hifadhi za Taifa kwa wingi, wataelewa kwa undani majukumu makubwa mliyonayo ya kuhakisha uhai na usalama wa wanyamapori wetu pamoja na mazingira yao unaendelea kuwepo na kunufaisha vizazi vingi vijavyo, hivyo watakuwa tayari kutoa ushirikano pale msaada utakapohitajika.

Sambamba na hilo, kwa kuwa naiona dhamira ya serikali kwenye kuinua utalii wa ndani hasa kwa hatua iliyochukua ya kutoa ruhusa kwa watanzania kuingia hifadhini bure, naamini kabisa jambo hili likiendelea kufanyika na kuendelea kuwapa watanzania elimu na maarifa mbali mbali kuhusu umuhimu wa kutembelea hifadhi za Taifa, watatuunga mkono na watanzania ndio watakaoongoza kwa idadi kubwa ya utalii kwa kutembelea hifadhi za Taifa. Pia niwaombe watanzania wezangu kuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi za  taifa; suala la kutembelea hifadhi sio la wazungu tu, au watu kutoka nje ya nchi pekee, hapana, suala hili la kutembelea hifadhi ni la kila mtu, na kila Mtazania. Tuiondoe hiyo mitazamo ya kutegemea wazungu ndio wawe watu pekee wa kutembelea hifadhi zetu. Hata sisi tuna zipenda sana hifadhi zetu, hivyo tudhamirie kuzitembelea.

Pia pamoja na hayo yote, ningependa na pia ningeshauri, serikali na TANAPA kwa ujumla watengeneze mfumo mzuri wa watu kutembelea hifadhi za Taifa unaoendana na hali na maisha ya watanzania, tusitengeneze tu mfumo wa kuwawinda matajiri tu, bali uwepo mfumo mzuri na unaoeleweka kwa watanzania kutembelea hifadhi kwa wingi. Hatuna haja ya kusubiria watanzania wawe matajiri ndio watembelee hifadhi za Taifa, cha msingi hapa ni kuwatengenezea mfumo mzuri unaowafaa kutembelea hifadhi, mfumo ukiwa mzuri utatengeneza utamaduni wa watu kutembelea hifadhi, na baadaye sana mkisha ona mfumo umefanya kazi, na watanzania wengi wameshajenga utamaduni wa kutembelea hifadhi za Taifa, hapo hata mkipandisha bei ya kiingilio cha kuingia hifadhini bado utapata watu wengi wanao ingia na hali ya uchumi wetu itabadilika na kuwa bora kabisa, na hali za hifadhi zetu zitakuwa salama kabisa.

Kwa makampuni yanayofanya biashara kwenye maeneo yetu pia waangalie ni kwa namna gani wanaweza kuweka mifumo yao ikawa na unafuu kwa watanzania kutembelea hifadhi za taifa, makampuni yanaweza kutengeneza kila nafasi ambayo itawasaidia na wao pia kwa hela na pia kwa kuitangaza biashara zaidi, hakuna mtu anayeweza kukutangazia biashara vizuri kam mteja wako. Kwa hiyo hata makampuni ya utalii yanaweza kutumia njia hii kama njia ambayo itawanufaisha wote, na sio kulenga watu wenye pesa tu ambao huwa ni wa msimu. Tuangalie jinsi tunavyoweza kuliweka hili, naamini linawezekana kabisa.

Pia kuna changamoto kubwa sana niliyoiona wakati wa ile ruhusa ya watanzania kuingia hifadhini bure, changamoto kubwa niliyoiona ilikuwa ni ya usafiri, pamoja na kwamba watanzania waliambiwa waingie hifadhini bure, lakini sio watanzania wote wenye magari, au wenye uwezo wa kukodi magari ya kitalii, vyote hivyo vinahitaji pesa ili vifanyike, serikali na Shirika la hifadhi za Taifa wanaweza kubuni mpango wa kuwa na usafiri wa bei nafuu kwa watanzania wanaotaka kutembezwa au kutembelea hifadhi za Taifa, wanaweza pia kuwa na nyumba za kulala wageniza  bei nafuu au bei ambayo watanzania wa kawaida wanaweza kuimudu, hivyo wanaweza kuwa na idadi kubwa ya watanzania kutembelea hifadhi za Taifa. Kwa mfumo uliopo kwa sasa ni mgumu na haueleweki vizuri kwa watanzania wengi. Hivyo wengi wanakosa taarifa nzuri za jinsi ya kutembelea hifadhi husika. Taarifa nyingi za kutembelea hifadhi za taifa na maeneo mengine ya kitalii zimeandikwa kwa lugha ya kingereza ambayo sio rafiki sana kwa watanzania wengi.

Mwisho, niseme hivi tunaweza kabisa kutengeneza watalii wetu wa kitanzania, tunaweza kuwatumia hawa hawa kwa kuinua nchi yetu kiuchumi na kimaendeleo. Si kazi nyepesi kufanya mambo haya lakini yanawezekana kabisa; makampuni na mashirka mengine yaliyowekeza kwenye hifadhi za Taifa tusihangaike kutafuta masoko huko nje kwa bei kubwa, bali tengeneza hapa Tanzania masoko unayoyahitaji. Watanzania ni waelewa na ni wazalendo wakifundishwa na kupewa taarifa sahihi na nzuri watafurahiya sana huduma yako na watakupa mkono wa shirika, au msaada unapohitaji. Mambo mengine tunayoyaendekeza sawa yanatupa pesa lakini, hatuwi huru tunapangiwa na mashrti na mambo mengine yasio mema kwenye rasilimali zetu.

Ahsante sana kwa kusoma waraka huu, naamini utafanyia kazi, na pia utawashikirisha wengine maarifa haya kwa maslahi ya nchi yetu.

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

0742092569/0683862481

hillarymrosso@rocketmail.com