Habari rafiki na msomaji wa Wildlife Tanzania, karibu kwenye makala ya leo ambayo tutangalia mambo kadhaa yaliyo muhimu kwenye kukuza utalii wetu. Hasa utalii wa ndani. Kama wengi tunavyojua Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vingi sana vya nchi kavu na vya majini, leo nitazungumzia vivutio vya majini, hususani kwenye fukwe za bahari zetu. Kuna watu wengi wamejijengea kwenye akili zao kuwa kwenda kutalii kwenye fukwe za bahari ni anasa na ni kama dhambi kufanya hivyo. Wanachukulia kuwa ni kitu kibaya ambacho wanafanya watu ambao hawana maadili na watu wanaopenda anasa. Sasa leo nataka tutoe kabisa mawazo haya na tuwe na utamaduni wa kutembelea sehemu hizi zenye mvuto.

Tanzania ni kati ya nchi kubwa barani Afrika ina ukubwa wa kilomita za mraba zaidi ya 945,000, yani ukubwa wa nchi ya Tanzania ni mara tatu ya nchi ya  Finland na nchi ya Norway, na ni mara nne ya nchi ya Japani. Ukubwa wa nchi yetu unaifanya kuwa na idadi kubwa ya maeneo yaliyohifadhiwa kwa ajili ya wanyamapori na viumbe hai wengine. Katika eneo lote hilo kuna kiasi zaidi ya kilomita 800 za fukwe safi kabisa ambazo hazijachafuliwa wala kuharibiwa na shughuli za kibinadamu, hivyo kufanya kuwa sehemu nzuri za kutalii na kutembelea kwa wageni. Kwani ni maeneo yenye mvuto na ni sehemu nzuri ya kufurahia mazingira halisi ya bahari.

Sasa haya maeneo ya fukwe au kwa kingereza wanita beach, yapo sio kwa ajili ya kuvutia wazungu kutoka Ulaya na Marekani kuja kujilaza kwenye mchanga bali ni kwa ajili ya Watanzania wenyewe kufanya utalii na kufurahia sehemu hizi. Takwimu nyingi zinaonyesha idadi ndogo sana ya watanzania kutembelea maeneo ya fukwe za bahari kwa ajili ya kufurahia na kuona mandhari nzuri ya mchanga na bahari, ni sehemu nzuri za mapumziko na unapokuwa na mapumziko kwenye sehemu kama hizi inakusaidia kukupa hamasa kwenye maisha yako na kuwaza kufanya makuu.

Kasumba kubwa iliyopo kwa watanzania wengi ni kwenye fikra na mitazamo iliyojengwa kwa muda mrefu kwenye akili zao na kuona kama hawastahili kufurahia utajiri huu ambao unapatikana kwenye maeneo yao. Watu wengi huwa wanajitoa kabisa linapokuja swala la utalii, ukimwambia mapumziko haya tuende kutembelea fukwe za bahari au beach, utashangaa atakavyo kuwa mpinzani ndani yake kabla hajakukubalia. Hii ndio imechangi kwa kiasi kukubwa utalii kwenye maeneo haya umedumaa na unashindwa kukua. Narudia kusema tena namna nzuri ya kutangaza utalii wetu ni sisi wenyewe kwenda kwenye maeneo hayo na kuona kwa macho yako, ukitoka hapo utakuwa balozi mzuri kwenye kuitangaza nchi yetu.

Nchi ya Tanzania imekaa sehemu ambayo kwa upanda wote wa mashariki imepakana na bahari ya Hindi, pia kwa upande huu wa mashariki kuna visiwa maarufu sana vya Unguja na Pemba, ambavyo vinajulikana kwa  kuwa na fukwe nzuri na za kuvutia sana, ni sehemu ambazo zinapokea watalii wengi wanaokuja kuona na kufurahia fukwe hizi safi na zenye mwonwkano mzuri. Kwa upande wa Kaskazini kuna ziwa Victoria, ambalo ni ziwa la pili kwa ukubwa duniani ambalo ni chanzo kikuu cha mto mrefu kuliko yote, mto Nile, ziwa hili pia lina fukwe zenye mandhari nzuri sana. Kusini mwa Tanzania kuna ziwa Nyasa ambalo ni moja ya kivutio kwa nchi za kusini, kwa upande wa Magharibi kuna ziwa Tanganyika lenye kina kirefu kuliko yote duniani. Ziwa hili lililo athiriwa na Bonde la Ufa, lia mandhari nzuri sana ambayo Watanzania wengi hawajaona.

Natamani kila Mtanzania kwa namna moja au nyingine aweze kuwa sehemu ya utalii wa ndani, aweze kushiriki. Watu wanaposhiriki mambo mbali mbali yanayowahusu wanakuwa na uelewa wa mambo hayo na ndio watakaotoa ushirikiano mkubwa kwenye utunzaji, uendelezaji na ulinzi dhidi ya uharibifu wa shughuli za kibinadamu. Hata ukitoa elimu itaeleweka kwa wengi kwa kuwa wataelewa na kuona hali halisi, faida na hasara za kutokuchukua hatua kwenye uhifadhi wa mazingira ya fukwe zetu.

Ahsante sana kwa kusoma makala hii, mshirikishe rafiki yako makala hii,

Hillary Mrosso

+255742092569/+255683248681

Wildlife Conservationist

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaamu.net/wildlifetanzania