Ndege maji ni moja ya kundi muhimu sana la ndege katika uhifadhi, utalii na uchumi. Ndege wa maji au kama wanavyojulikana kwa kingereza waterbirds, ni ndege ambao mara nyingi hutegemea maji katika maisha yao.
Ndege hawa hupatikana zaidi maeneo yenye maji, kama vile kwenye maeneo ya ardhi oevu, mabwawa, maziwa, mito, chemichemi, bahari, au maeneo mengine yenye vyanzovya maji. Hutegemea maji kwa ajili ya kupata chakula, makazi, kuzaliana, au kupumzika. Soma zaidi hapa kufahamu umuhimu wa maeneo oevu; Fahamu Umuhimu wa Maeneo Oevu Katika Uhifadhi, Uchumi na Utalii
Tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 10 ya spishi za ndege wote duniani wanategemea sana maji katika maisha yao. Hasa maeneo ya ardhi oevu au wetlands. Maeneo yenye maji yamekuwa na mchango mkubwa sana kwa uhifadhi wa ndege.

Ndege maji aina ya Korongo Domonundu au Open-billed Stork (African Openbill); Picha na Ester Matingisa
Mfano, Tanzania kuna ndege aina ya heroe (flamingo) ambao hupatikana katika ziwa Natroni, ndege hawa hutegemea ziwa hili lenye magadi kuzaliana. Mazingira na upekee wa ziwa Natroni umefanya kuwa sehemu muhimu sana duniani kwa uhifadhi, mazalia na makazi muhimu ya ndege hawa.
Hivyo maji ni sehemu muhimu sana ya maisha ya ndege hawa, sehemu zenye ukame au uharibifu wa mazingira yao huwezi kuwakuta ndege maji, hivyo huwa kama kiashiria cha afya ya ikolojia ya mahali fulani.
Mfano, unaweza kuona aina fulani ya ndege maji wakiwa kando kando ya mito au maziwa au maeneo oevu. Mara nyingi utawakuta hapo wakijitafutia chakula chao na pia ni sehemu inayoendana na maisha wanayoishi.
Uoto unaoota kando ya vyanzo vya maji unakuwa na aina ya kipekee ya miti, misitu na hali ya hewa ambayo inawafaa ndege maji. Hata hivyo, ndegemaji husiadia kudumisha na kuendeleza ikolojia ya uoto ulioko kando ya maeneo yenye maji.

Ndege maji aina ya Batamaji Uso-myeupe au White-faced Whistling Duck; picha na Ester Matingisa
Endapo kutatokea uharibifu wa mazingira hayo, ndege hao wanaweza kutoweka kabisa katika eneo hilo. Mfano, kama kuna ndege maji wanaishi maeneo ya bwawa au mto, ikatokea mtu akaja kuharibu yale mazingira kwa kukata miti na kuyabadilisha kabisa mazingira hayo, ndege maji wanaweza kutoweka haraka sana.
Hatahivyo, maeneo mengi oevu, mabwawa na mito yanakabiliwa na hatari kubwa sana ya kuvamiwa na kutumiwa kwa shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, viwanda, barabara au ujenzi wa mitambo mikubwa. Soma zaidi hapa; Zijue Faida Za Sensa ya Ndege wa Majini (Waterbirds)
Kwa kutambua hilo, hatuna budi kuangalia kwa makini miradi yetu ya maendeleo ambayo inafanyika au kupangwa kufanyika maeneo muhimu ya ndege maji. Kwasababu kuharibika kwa makazi yao ni jambo linaloweza kutokea haraka sana, lakini kurudisha kwa makazi yao ni jambo gumu, ambalo linachukua miaka mingi kurudi katika hali yake.
Tanzania ni nchi ya kipekee sana kwa uhifadhi wa ndege maji, uwepo wa mito mingi, mabwawa makubwa na madogo, maeneo makubwa ya ardhi oevu ambayo yana hadhi kubwa hadi kutambuliwa kama Ramsar site.

Ndege maji aina ya Korongo Domonjano na Korongo Domokijiko au Yellow-billed Stork and African Spoonbill; Picha na Ester Matingisa
Mfano wa maeneo oevu yenye hadhi ya kimataifa hapa Tanzania ni kama ifuatavyo
Malagarasi – Moyovozi, ilianzishwa mwaka 2000, ina ukubwa wa hekta 3,250,000. Ni eneo muhimu sana kwa uhifadhi wa ndege maji, mimea, ndege wanaohama, viboko, aina nyingi za samaki, na mamba, ni moja ya ardhi oevu kubwa barani Afrika.
Bonde la Kilombero, ni moja ya eneo kubwa la ardhi oevu, lina ukubwa wa hekata 796,735, ilianzishwa mwaka 2002, linatambuliwa kwa uwepo wa aina nyingi wa ndege wanaohama, idadi kubwa ya wanyama kama tembo, na mimea na samaki
Rufiji-Mafia-Kilwa, hili ni eneo muhimu sana la ardhi oevu, lina ukubwa wa hekta 596,906, lilianzishwa mwaka 2004. Eneo hili linahifadhi viumbe hai muhimu kama vile aina nyingi za mikoko, mwani, matumbawe, aina nyingi za ndge maji na aina nyingi za viumbe wa baharini.
Eneo oevu la Usangu, lina ukubwa wa hekta 413,000, lilianzishwa mwaka 2002, ni moja ya maeneo muhimu sana duniani kwa uhifadhi wa ndege maji, chanzo cha maji ya mto Ruaha Mkuu, aina nyingi za wanyama, mimea na ndege.
Bonde la ziwa Natroni, ukubwa wa hekta224,781, ilianzishwa mwaka 2001. Ni eneo muhimu sana duniani kwa uhifadhi na mazalia ya Heroe (flamingo), pia ni makazi ya viumbe hai wengine na idadi kubwa ya spishi za mimea.

Ndege maji aina ya Kwangwala Migabachuma au Black-winged Stilt; picha na Ester Matingisa
Haya ni baadhi tu ya maeneo muhimu duniani kwa uhifadhi, sio tu wa ndegemaji, bali hata viumbe hai wengine muhimu.
Tukilinda na kuyatunza maeneo ya ardhi oevu, sio tu tutalinda makazi muhimu ya ndege maji, bali ni maeneo muhimu kwa maendeleo ya utalii, uchumi, kilimo na uhifadhi.
Pia maeneo haya yana mchango mkubwa sana katika kupunguza athari za mabadiliyo ya hali ya hewa kwa kuhifadhi kiasi kikubwa cha hewa ukaa.
Hivyo, tuungane kulinda maeneo haya, tuepuke ujenzi, kilimo, uchafuzi wa meneo haya muhimu. Tuyalinde kwa nguvu zetu zote. Mshirikishe mwingine makala hii.
Asante, tukutane kwenye makala nyingine!
Hillary Mrosso|+255 683 862 481| hmconserve@gmail.com
Tunaandika makala hizi ili tuongeze uelewa wetu kuhusu wanyamapori, tunaamini tukipata uelewa tutachukua hatua kushiriki katika uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yake asilia.Kazi hii tunafanya kwa kujitolea na hakuna malipo yoyote, endapo umefurahia kazi zetu unaweza kutuunga mkono kwa kiasi chochote ili tupate mtandao, vifaa vyua kufanyia kazi kama kamera na komputa. Kwa maelezo zaidi unaweza kuwasiliana kwa mawasiliano haya; hmconserve@gmail.com |+255-683-862-481