Maendeleo kwenye biashara yoyote ile yanahitaji utafiti na uelewa wa kutosha kuhusu bidhaa na aina ya huduma ambayo unaitoa kwa mteja wako. Utafiti hapa namaaninisha ni pamoja na kutafuta njia bora na masoko mazuri ya kuuzia bidhaa yako. Hii ni kanuni ambayo ipo kila upande na kwenye kila biashara. Sekta ya utalii Tanzania inahitaji zaidi ya kufanya kazi, kwa sababu ya maeneo ambayo inayanadi kuwa vivutio kwa wageni na watu wengine ili watoe fedha zao na kuja kufanya uwekezaji au kutembelea vivutio vilivyopo nchini yana ushindani mkubwa na hivyo inahitajika zaidi ya kazi za kawaida zilizozoeleka.
Kuna kanuni ya kweli kwenye maisha ambayo inasemwa sana kwenye vitabu, na hata kwenye semina nyingi za mafanikio binafsi, mafanikio ya jamii, mafanikio ya kampuni na mafanikio ya nchi nzima, kanuni hii inasema “kama unataka kupata kile ambacho unapata kila siku endelea kufanya kile kile ambacho umezoea kufanya kila siku”. Na hapo hakuna uchawi wala muujiza, kama hatutajiongeza hakika hakuna kitakachobadilika. Mafanikio na maendeleo kwenye jambo lolote yanakuja kwa kuchukua hatua za ziada, kufanya kwa ziada, kusoma kwa ziada, kuuza kwa ziada, kutangaza kwa ziada. Hii tunaweza kuitumia kwenye sekta ya utalii hapa Tanzania, tunahitaji hatua za ziada kama tunataka kubadilisha matokeo ambayo tunayapata kila siku, hakuna kitakacho badilika kama hatutachukua hatua za ziada, wageni au watalii hawataongezeka tu, lazima hatua za ziada zichukuliwe ili tupate matokeo makubwa na mazuri.
Maeneo ambayo ninataka kuyaeleza hapa ni maeneo ambayo yanafahamika na wengi, lakini ni wachache sana wanafikiria kama kunaweza kukawa na fursa ya utalii katika maeneo haya, haya ni maeneo yanayojulkana na kwa kiasi kikubwa baadhi ya maeneo haya yapo kwenye mikoa yetu, na maeneo mengine tumeyasoma kwenye moja ya masomo ya shuleni .Kwa hiyo kwenye maeneo haya endapo kutafanyika utafiti mzuri na wa kina ni maeneo muhimu sana kwa kuwekeza kwa ajili ya utalii wa ndani na utalii wa nje. Kutokana na upekee wake maeneo haya yanaweza kuwa moja ya vivutio vikubwa sana vya watalii kutoka sehemu mbali mbali duniani.
Maeneo haya ni kama ifuatavyo,
- Hifadhi za Taifa (Tanzania National Parks)
Hapa naamini watu wengi wanafahamu maeneo haya ya hifadhi za Taifa, haya ni maeneo yanayohifadhiwa kwa umakini mkubwa, ni maeneo ambayo shughuli za kibinadamu kama kilimo au ufugaji haviruhusiwi, ni sehemu ambayo hata uwindaji wa kitalii haurususiwi, yamehifadhiwa kwa ajili ya wanyamapori na miti au uoto mwingine wa asili. Maeneo haya ni maarufu kwa utalii wa picha. Utalii wa picha ndio shughuli kubwa ya utalii inayoruhusiwa. Hivyo basi maeneo haya yana vivutio vingi sana vya wanyamapori, uoto wa asili, milima na tabia mbali mbali za nchi. Hivyo kuwa sehemu zenye mvuto wa kipekee sana. Kwa hakika sekta ya utalii Tanzania huwa inajipatia mapato mengi sana kupitia hifadhi za taifa; kwa kutambua hilo uwekezaji na ubunifu unatakiwa kuwa mkubwa kwenye maeneo kama haya ili yazidi kuleta faida kubwa na endelevu. Mfano wa hifadhi za taifa ni Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, hifadhi ya Taifa ya Katavi, Hifadhi ya Taifa ya Rubondo, Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi nk, zipo hifadhi za taifa 16 ambazo zina fursa kubwa za uwekezaji nakuvutia wageni.
- Mapori ya Akiba (Game Reserves)
Mapori ya akiba ni sehemu ninyine muhimu sana inayotoa fursa kubwa sana za uwekezaji kwenye sekta hii ya utalii. Taznzania ina jumla ya mapori ya akiba 28 ambapo pamoja na mambo mengine mapori haya yamekuwa ni sehemu muhimu ya hifadhi za wanyamapori na mimea. Maeneo haya ambayo shughuli za kitalii za uwindaji na utalii wa picha huruhusiwa yamekuwa na manufaa makubwa kwenye kukuza mapato kutokana na shughuli za utalii zinazoruhusiwa. Ingawa hakuna shughuli zozote za kibinadamu zinaruhusiwa kwenye maeneo haya, utalii wa uwindaji umekuwa ukiendeshwa kwa ruhusa, vibali na lesseni. Kutokana na wingi wa maeneo haya kuna maeneo mengine yanatoa faida kubwa na kuna mengine yanatoa faida kidogo, hii yote ni kutokana na uwekezaji uliofanywa na serikali. Lakini haya ni maeneo ambayo sekta ya utalii inaweza kuweka nguvu zaidi ili kuhakikisha yanajulikana, na watu wanayatumia kwa kufanya uwekezaji ili yalete faida kubwa. Mfano wa maeneo haya ni Pori la Akiba la Selous, Pori la Akiba la Rungwa, Pori la Akiba la Swagaswaga, Pori la Akba la Uwanda, Pori la Akiba la Biharamulo, Pori la Akiba la Lukwati, Pori la Akiba la Ibanda, nk.
- Maeneo ya hifadhi Jamii (Wildlife Management Areas, WMAs) na Mapori tengefu (Game controlled Areas)
Maeneo mengi ya aina hii hayajulikani sana kwa watu wengi lakini ni maeneo muhimu sana kuwekeza kitalii. Lengo la serikali kuatenga maeneo haya ni kwa ajili ya kuhakikisha wanyamapori wanahifadhiwa kwa usimamizi wa wanajamii lakini pia ni maeneo ambayo yanatakiwa kutoa faida na manufaa kwa jamii kutokana na uwepo wa rasilimali kama wanyama, misitu na vivutio vingine vilivypo kwenye maeneo haya. Tanzania ilitenga maeneo 38 kwa ajili ya hifadhi ya jamii, kwa kingereza maeneo haya yanaitwa, Willife management Areas na maeneo zaidi ya 44 kwa ajili ya Mapori Tengefu. Haya ni maeneo yenye fursa nyingi na pia ni maeneo yanayohitaji kufanyiwa utafiti na upembuzi yakinifu ili kubaini furs azote muhimu zenye manufaa kwa jamii na manufaa kwa uhifadhi endelevu. Maeneo haya tangu yaanzishwe hayajatofa faida inayokusudiwa, ni maeneo machache sana ambayo faida kidogo inaonekana, maeneo mengi yapo tu kama mapori. Uzuri wa maeneo haya utalii wa picha na utalii wa uwindaji unaruhusiwa, hivyo ni jukumu letu kutumia nguvu zetu kuhakikisha maeo haya yanaleta faida na wanyama na mazingira yao yanahifadhiwa. Mfano wa maeneo ya hifadhi ya jamii au WMAs ni Ikona WMA, Makao WMA, Enduimet WMA, Ipole WMA, Tunduru WMA, Ngarambe- Tapika WMA, Pawaga- Idodi WMA, Ukutu WMA, nk. Na kwa upande wa Mapori Tengefu, mfano wake ni Burunge, Gombe, Kilimawe, Kongwa, Loliondo, Ruvu Maasai, Simanjiro, Ugunda, Ziwa Manka, Ziwa Natroni, Muhuwesi, Mto wa mbu, nk
- Fukwe za Bahari na Visiwa (Coastline and Off-shore Island)
Tanzania ina zaidi ya kilomita 804 za fukwe za bahari ambazo zina mandhari nzuri na za kuvutia kwa ajili ya watalii na uwekezaji, maeneo haya ya Tanzania yapo na hayaadhiriwa na athari mbaya za uharibifu wa mazingira, hivyo ni maeneo muhimu sana kwa ajili ya uwekezaji na ni sehemu nzuri ya kuboresha ili yawe na mvuto wa kimataifa unaoendana na hadhi na kasi ya sasa ya sayansi na teknolologia. Pia kuna visiwa vya Zanzibara na Pemba ambavyo ni maarufu kwa utalii hasa utalii wa ufukweni. Haya ni maeneo yanayohitaji uwekezaji na nguvu kubwa ili yaendane na soko la kimataifa. Maeneo haya ambayo yapo kwenye bahari ya hindi ni sehemu muhimu sana endapo yatatumiwa kikamilifu.
- Maeneo ya kihistoria (Historical sites)
Hizi ni sehemu nyingine muhimu zaidi kwa uwekezaji kwenye sekta ya utalii, maeneo haya sio tu kwamba hayajulikani vizuri duniani kote lakini ni maeneo ambayo pia hayajulukani vizuri kwa watanzania wengi, hii ndio sababu watanzania wengi hawapendelei kwenda kutembelea maeneo haya. Maeneo haya ya kihistoria yapo mengi sana, ukianzia makumbusho hadi kwenye miji mikogwe ya Zanzibar na kilwa Kisiwani. Maeneo mengine yametambuliwa na kuwekwa kwenye hadhi za kuwa moja ya maeneo muhimu ya urithi wa dunia. Hivyo hiyo sio nafasi ndogo au fursa ndogo ya sisi kuiangalia kwa jicho la tatu na kuona ni namna gani tunaweza kuboresha na kuyafanya yawe na mvuto kabisa wa kuwaleta wageni kutoka nje na pia kuwavutia watanzania. Maeneo haya maarufu kama Oldupai Gorge, Bagamoyo, Kilwa, Zanzibar ni muhimu sana kwa ukuaji wa utalii kwenye nchi ya Tanzania.
- Milima (Mountains)
Kitu ambacho kinaweza kuwa cha kawaida kwako kinaweza kuwa cha ajabu kwa mwingie, au kinaweza kuwa kitu cha kushangaza na kusisimua kwa mtu mwingine na hii ndio sababu inayotusababisha kuchukulia vitu na rasilimali tulizo nazo kikawaida. Kuna watu wanapenda kuona na kupanda milima mirefu. Na hapa Tanzania tumebarikiwa kuwa na milima mirefu kuliko yote barani Afrika. Mlima Kilimanjaro unafahamika sana duniani. Watu wengi wanapenda sana kuona mlima huu na kuupanda. Hii ni sehemu yenye mvuto wa kipekee sana hapa Tanzania, na kwa kutambua hilo sekta ya utalii inatakiwa kuliwekea mikakati mipya na mizuri zaidi ili iwe ni sehemu sio tu ya kuwavutia wazungu bali hata watanzania wenyewe. Kuna milima mingine kama milima ya Usambara, mlima Meru nk ni milima ambayo inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha utalii Tanzania.
- Maziwa (Lakes)
Hapa naweza kukaa zaidi ya siku nzima kuchambua na kuelezea umuhimu wa maeneo haya kwenye nchi ya Tanzania, Tanzania kila upande imezungukwa na maji, kaskazini kuna ziwa kubwa na la pili kwa ukubwa duniani, hili ni ziwa Victoria ni ziwa ambalo linasifa nyingi ambazo ni fursa ya kupanua na kuwekeza kwenye utalii. Licha ya kuwa na manufaa kwa nchi nyingi za Afrika Mashariki ziwa hili ambalo limeunganishwa na mto mrefu kuliko yote barani Afrika mto Nile, ambao una historia ya kuvutia sehemu yoyote duniani ni sehemu muhimu sana ya kutengeneza na kuwekeza kwa utalii. Kusini kuna ziwa Nyasa, wakati upande wa Magharibi kuna ziwa Tanganyika ziwa lenye kina kirefu zaidi duniani ambalo lina historia na mandhari nzuri sana kwa utalii. Pia uwepo wa samaki na dagaa kwenye ziwa hili lililopo kwa kiasi kikubwa katika mkoa wa Kigoma ni sehemu nzuri ya kukuza utalii kwa nchi yetu. Hapo bado sijaelezea maziwa mengine madogo kwa makubwa yaliyopo hapa Tanzania, sijagusa maporomoko ya maji, sijagusa sehemu za miamba nk.
Hapa nimetaja tu maeneo saba, lakini kuna maeneo zaidi kwa ajili ya uwekezaji hasa kwenye sekta hii ya utalii. Makala hii imegusia tu yale muhimu zaidi ambayo hayo yakitumiwa vizuri hakika Tanzania itakuwa ni nchi ya kipekee zaidi na hata sura yeke itabadilika kabisa kwenye kurasa za kimataifa kuhusu utalii na fursa ambazo zinaweza kuikwamua Tanzania na kuifanya ijulikane kwa rasilimali na vivutio vyake kwenye kila pembe ya dunia. Katika uanzishwaji wa sekta ya utalii na kufungua maeneo mengi zaidi kama ilivyoelezwa kwenye sera ya utalii Tanzania, utalii unatakiwa kusaidia kupunguza umasikini kwa watanzania, na moja ya maelengo ya milenia na malengo ya miaka mitano ya nchi hii ni kuimarisha sekta kama za utalii ili ziweze kuwa na mchango mkubwa kwenye kupunguza umasikini katika nchi.
Hiyo njia nzuri ya kufanya hivyo ni kupanga mikakati ya mara kwa mara, kuwa wabunifu na kufanya tafiti nyingi kwenye sekta hii ili kuhakikisha utalii unakuwa zaidi ya ulivyo sasa. Hili ni jambo ambalo linawezekana kabisa, na endapo sekta husika watashikamana na kufanya kazi ya ziada hakuna kinachoshindikana. Kila kitu kinawezekana, kila siku tunatakiwa kupiga hatua ili kuwa bora zaidi.
Tukutane kwenye makala nyingine nzuri kabisa. Enelea kujifunza naamini utapata fursa nzuri na utafikiria na kupanga namna ya kuzitumia fursa hizi, fursa za kuwekeza kwenye sekta hii zipo wazi wa kila mtu, sio kwa wazungu pekee, bali hata kwa watanzania wazawa.
Nakutakia siku njema Rafiki yangu, kama una maswali, ushauri hata maoni usisite kuwasiliana nami kwa mawasiliano hapo chini.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania