Habari msomaji wa makala hizi za kila siku, karibu kwenye makala ya leo ambayo tunaangalia maeneo saba ya Tanzania yaliyotangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (United Nations Educational, Scientific and Cultural Organisation,UNESCO) kuwa maeneo ya urithi wa dunia .Shirika hili linajuhusisha sana na masuala ya Kielimu, Sayansi na mambo ya Utamaduni lina historia ndefu ambayo inatupeleka mpaka miaka ya 1922 ambapo ndipo lilipoanza harakati zake za kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi.
Lengo la Shirika hili ni kuendeleza amani na usalama katika jamii za watu mbali mbali duniani kupitia program mbali mbali zinazoendeshwa kama vile za kielemi, kitamaduni, na za kisayansi ya asili. Wanafanya hivyo kwa kushirikiana na wadau wengine wa kimataifa ili kuleta amani, usalama na heshima kwa nchi, jamii na tamaduni za watu wa nchi zote duniani.
Mpaka sasa UNESCO imeshatangaza maeneo 1073 katika nchi mbali mbali kuwepo kwenye urithi wa dunia ambapo nchi wanachama 195 wamesaini kuwa washiriki wa UNESCO. Katika maeneo hayo 1073 yamegawanyika kama ifuatavyo, maeneo 832 ni maeneo ya Kitamaduni (Cultural), maeneo 206 ni ya Kiasili (Natural) na maeneo 35 ni mchanganyiko wa kitamaduni na ya kiasili. Nchi ya Italia ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya maeneo ya yaliyotangazwa kuwa urithi wa daunia ikiwa na maeneo 53, na China ilkiwa ya pili na idadi kubwa ya maeneo ya urithi wa dunia ambayo ni 52, ikifuatiwa na Hispania yenye 43, Ujerumani 42, India 36, Mexico 34, Uingereza 31. Hizo ni baadhi tu ya maeneo yaliyotangazwa kuwa urithi wa dunia.
Kwa hapa Tanzania kuna maeneo yaliyotangazwa na UNESCO kuwa urithi wa Dunia maeneo hayo ni yale ya Kiasili, yaani uoto na mengine ni maeneo ya Kihistoria. Maeneo hayo yameonekana kuwa na sifa ya kipekee na mvuto kwa dunia kiasi kwamba yakatangazwa kuwa ni maeneo ya Urithi wa Dunia. Hivyo kulindwa na kutunzwa kwa uangalizi mkubwa zaidi. Maeneo hayo unaweza kuangalia kwenye linki hii, yameelezewa vizuri pia.https://en.wikipedia.org/wiki/List_of_World_Heritage_Sites_in_Tanzania
- Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
- Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro
- Eneo la hifadhi ya Ngorongoro
- Pori la Akiba la Selous
- Mji Mkongwe wa Zanzibar
- Michoro ya Mapangoni iliyopo Kondoa
- Mabaki ya Magofu ya mji Mkongwe wa Kilwa Kisiwani na Songo Mnara
Haya ni ya maeneo maalumu yaliotengwa hapa Tanzania, na pia Serikali iliamua kutunga Sharia kwa ajili ya Mambo ya Kale ili kulinda, kusimamia na kutunza maeneo haya. Hivyo UNESCO iliamua kutangaza baadhi ya maeneo ya kihistoria na kitamaduni kuwa ni Urithi wa Dunia, kutokana na historia zao za kuvutia na kusisimua kwa kila moja. Ukiangalia maeneo hayo saba utaona jinsi UNESCO walivyoweka maeneo ya kiasili ambayo mengi ni hifadhi za wanyama na mengine ni maeneo ya Kihistoria na Kitamaduni kama tulivyoona hapo juu.
Kwanini nimekushirikisha haya yote, nataka tujue jinsi ambavyo tuna vitu vyenye hadhi za kamataifa ambavyo dunia inavililia na kuvithamini ili viendelee kuwepo kwa miaka mingi na kwa vizazi vingi. Hizi ni sehemu rahisi sana kutembelea na kufika ili kujionea maajabu haya ambayo dunia inayaita ni urithi wa dunia. Unajua sio lazima uanze kutembelea hifadhi za wanyama, hapana, unaweza kenda kwenye maeneo ya kihistoria ya hapo hapo mkoani kwenu, kijijini kwenu, au hapo mjini kwenu na kujionea mambo mbali mbali yaliyofanywa na wazee wetu, au wahenga. Nenda makubusho, nenda kaangalie maeneo ya kitamaduni ya sehemu nyingine utajifunza na kufurahia.
Asante sana kwa kusoma makala hii, nitakujuza mengine mazuri siku zijazo endelea kuwa mfuatiliaji wa mtandao huu wa wildlife Tanzania, jifunze na umshirikishe na mwingine. Pamoja tutunze na kuenzi maliasili zetu.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 248 681/+255 742 092 569
www.mtaalam.net/wildlifetanzania