Habari msomaji wa makala za Wildlife Tanzania, karibu tuendelee na uchambuzi wa sheria hii ya wanyamapori sehemu ya nane, tutaangalia mambo muhimu yaliyotajwa kwenye vipengele vya sehemu hii.  Sehemu ya nane ya sheria hii inaelezea Migogoro baina ya binadamu na wanyamapori. Hivyo tutaangalia kwa ufupi mambo yote muhimu yaiyotajwa kwenye sehemu hii. Karibu sana.

1.Usimamizi wa wanyama hatari (Management of dangerous animals)

Hiki ni kifungu kinachoelezea hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na mamlaka husika za wanyamapori ili kuhakikisha wanyamapori hawaleti madhara au hasara kwenye maisha ya watu na maili zao, pia ni kifungu kinachoelezea wanyama wasumbufu na wanyama hatari.

2.Wanyama hatari (Dangerous animals)

Kifungu hiki cha 70 kinaelezea na kutambua uwepo wa wanyama hatari, wanyama hao wameorodheshwa kwenye Jedwali la Nne la sheria hii, mfano wa wanyama hao hatari kwa mujibu wa sheria hii ni kiboko, fisi, nyati, mamba, tembo.

3.Kifuta machozi kwa waliopoteza Maisha, kujeruhiwa, kuharibiwa mazao yao na wanyama hatari (Consolation for loss of life, crops or injury caused by dangerous animals)

Kifungu hiki kinaelezea kwa undani uwepo wa fidia au kifuta machozi kwa waliopoteza maisha, mali na mazao yao kulikosababishwa na wanyama hatari. Pia ni kifungu kinachoelezea utaratibu wa kulipwa kwa fedha hizo za kifuta machozi na Waziri. Kwa hiyo Waziri ataandaa kwa mujibu wa kanuni utaratibu wa kutoa fedha za kifuta machozi kwa wahanaga au waathirika kutokana na wanyama hatari.

  1. Kujeruhiwa kwa wanyama hatari (wounding of dangerous aniamals)

Kifungu hiki kinaelezea utaratibu unaotakiwa kufuatwa endapo mnyama hatari amejeruhiwa na kuingia kwenye eneo jingine ambalo muhusika hajaruhusiwa kuwinda au kukamata mnyama huyo. Kinaeleza nini cha kufanya, ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na kutoa taarifa kwa maofisa wanyamapori walio karibu, au mtu yeyote anayetambuliwa na mamlaka husika kwenye sekta ya wanyamapori. Kwa taarifa hiyo mnyama huyo anaweza kutafutwa na kupatikana kwa msaada wa wadau wengine kwenye sekta hii, na endapo atapatikana atauliwa mara moja.

5.Kuua mnyama katika harakati za kuokoa au kulinda maisha ya mtu (Killing animal in defence of life)

Kifungu hiki kinatoa maelekezo ya moja kwa moja endapo mtu yupo kwenye hatari ya kupoteza maisha yake kutokana na uvamizi, au kushambuliwa na wanyamapori. Sheria hii kwenye kifungu hiki imweweka wazi jambo hili, kama mnyama anataka kusababisha mdhara kwa maisha ya mtu sharti mnayama huyo auwawe. Pia endapo mnyama atauliwa kwa sababu hizo sheria inataka nyara zote ikiwemo Ngozi, meno, pembe na nyara nyingine ziwasilishwe kwa ofisa wa wanyamapori naya atazitunza, kwani nyara zote ni mali ya Serikali.

6.Masharti kufanya shuguli za kibinadamu karibu na maeneo ya hifadhi ya wanyamapori (Restriction on human activities etc. in wildlife protected area border line)

Sheria ya wanyamapori kwenye kifungu hiki cha 74, imeweka wazi kabisa kwamba shughuli zozote za kibinadamu kama vile kilimo, ujenzi, makazi na shughuli nyingine ambazo zitapelekea kuathiri maisha ya wanyamapori na makazi yao hazitaruhusiwa kufanyika ndani ya eneo la mita mia tano (500m) kutoka katika mpaka wa hifadhi ya wanyamapori. Hii ni sehemu muhimu sana ya kuzingatia kwa wawekezaji na watu wanaoendesha shughuli zao karibu na maeneo ya hifadhi ya wanyamapori.

  1. 7. Kuua au kujeruhi wanyama kwa ajali au bahati mbaya ili kujihami na kujilinda (Accidental killing or wounding in self-defence)

Sheria hii inaeleza kwenye kifugu hiki endapo mtu ameua mnyama kwa bahati mbaya au katika harakati za kujihami. Sheria imeweka wazi kabisa ikiwa muhusika aliyemuua mnyama huyo alifanya kila linalowezekana ndani ya uwezo wake ili asimuue mnyama huyo bila kufanikiwa na pia jambo hilo lilikuwa juu ya uwezo wake ndio maana akaamua kumuua mnyama huyo. Kifungu hiki kinaelezea kabisa mambo ya kufanya endapo hali kama hii inatokea.

  1. Kuua mnyama kwa faida au manufaa ya umma. (killing of animal for public interest)

Kifungu cha 76 ndio kifungu cha mwisho kwenye sehemu hii ya nane (Part VIII), kinaelezea mamlaka ya Mkurugenzi wa wanyamapori kutoa ruhusa ya kuua, kukamata wanyama kwenye maeneo yote ya hifadhi za wanyama isipokuwa kwenye Hifadhi za Taifa na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Kwa hiyo licha ya kanuni na mapendekezo ya sheria hii bado kifungu hiki cha 76 kinampa Mkurugenzi mamlaka ya kutoa ruhusa kukamata au kuua wanyama kwenye maeneo husika sawa na kifungu hiki, jambo hili linatakiwa kuwa lenye maslahi makubwa na mapana kwa umma na sio kwa maslahi binafsi.

Kufikia hapa ndio tuanhitimisha mambo yote nane muhimu yaliyotajwa kwenye sehemu hii ya nane ya sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009. Naamni umejifunza mambo mengi kwenye sehemu hii ya uchambuzi wa sheria. Tuendelee kushrikiana na kujifunza kwa pamoja ili tuzitunze na kuzitumia maliasili zetu kwa maendeleo endelevu na jamii ipate uelewa na faida za moja kwa moja kutokana na uwepo wa maliasili hizi kwenye nchi yetu.

Asante sana kwa kusoma makala hii, karibu sana kwa maswali, maoni na ushauri.

Ahsante sana!

Hillary Mrosso

Wildlife Conservationist

+255 683 248 681/+255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtaalamu.net/wildlifetanzania