Habari wadau wa makala hizi za wanyamapori, jamii na wahifadhi kwa ujumla. Kwa mara nyingine tena leo nawaletea makala kuhusu wanyamapori kama ilivyo ada na kwa undani zaidi kupitia makala hizi watu hujifunza mambo mengi au machache na yenye faida kubwa sana kuhusu wanyamapori na uelekeo wa wanyama hawa kwa ujumla. Bila kusahau faida kubwa na nyingi zinazotokana na uwepo wa wanyama hawa katika maeneo yetu ya hifadhi za taifa, mapori ya akiba na maeneo mengine tengefu kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori.

Makala yetu ya leo nimepanga kukujuza kwa undani zaidi kuhusu mmoja kati ya wanyamapori jamii ya paka. Niwazi kwamba wengi wetu tunamjua paka wa nyumbani tu au paka tunao kutananao mitaani, ukweli ni kwamba jina paka lina jumuisha wanyama wengi sana na wengiwao ni wanyamapori. Katika kundi hili la wanyama jamii ya paka wapo simba, chui, simbamangu, duma na wengine wengi tu.   

Sasa makala hii leo nimeiandaa mahususi kumuelezea mnyama SIMBA kwa undani zaidi ili kila msomaji wa makala hii awe na uwezo wa kumjua samba bila kupepesa macho. Tulio wengi tunamfahamu simba kwa kumuona tu au kwa kusikia sifa zake chache kwa watu. Sasa leo tutumie muda huu kwa ufupi kumjua simba vizuri. Kupitia Makala hii tutajifunza sifa na tabia za simba, kuzaliana kwa simba, maeneo wapatikanayo simba, uhifadhi na idadi ya simba, changamoto zinazo wakumba simba hali kadhalika faida za simba katika ikologia na kiuchumi. Hivyo nakusihi ndugu nsomaji wa makala hii kuwa pamoja nami na kuisoma makala hii mwanzo mpaka mwisho kwa hakika utajifunza mambo mengi sana ambayo hapo awali hukuwahi kuyafahamu kuhusu mnyama simba.

Kundi la simba wakiwa wamepumzika katika moja ya hifdhi ya Masai mara nchini Kenya; picha hii imepigwa na Guido Amrein

UTANGULIZI
Simba ni jamii ya wanyama walao nyama na yupo kwenye kundi la wanyama jamii ya paka. Hivyo simba hufanya kazi ya kuwinda na kuwafukuza wanyama wengine walao nyama katika mazingira anayoishi ili kupunguza tabu za utafutaji wa chakula.
Simba ndiyo wanyama jamii ya paka pekee wanoishi kwa ujamaa. Katika kundi la simba huwa kuna watoto, kina mama, shangazi na wakati mwingine hata kina bibi na dume mmoja au wakati mwingine kwa mara chache sana huwepo dume zaid ya mmoja. Kitu cha kushangaza pamoja na kuwepo kwa madume lakini kundi hili la simba huongozwa na simba jike ambae ni mtawala wa kundi lile.

Kuna aina mbili za simba ambazo ni (1) Simba wa Afrika na (2) Simb wa Asia. Simba hawa wote wana sifa takribani sawa zinazofanana. Kutokana na ujasiri na nguvu walizonazo simba, simba hupewa jina la “mfalme wa mwitu”. Kwasasa simba wengi barani Afrika wanapatikana maeneo ya Afrika ya Mashariki na Afrika ya Kusini. Kati ya simba elfu ishirini (20,000) walio salia barani Afrika kutokana na takwimu, Afrika ya Magharibi wamebaki simba 1,500 tu.


SIFA NA TABIA ZA SIMBA
Ni wanyama jamii ya paka na ukiwatazama vizuri kama si ukubwa wa umbo basi huwezi kuwatofautisha na paka wafugwao majumbani. Tofauti kati yao na paka hawa wa majumbani ni ukubwa wa miili yao lakini pia mjumuiko wa rangi kwa simba ni wakufanana takribani kwa simba wote tofauti na paka wafugwao ambao huwa na rangi tofauti tofauti.

Miili yao ina rangi ya kahawia iliyo pauka ambayo kwa mbali hufanana na rangi ya kaki. Moja kati ya utambuzi mkubwa sana porini katika wanyama jamii ya paka ni rangi hii ya simba kwani wanyama wengi jamii ya paka hawana rangi kama ya simba. Pakapori ambae kwa haraka unaweza kumfananisha na simba kwa rangi ni simbamangu.

Wana miili iliyo jaa zaidi na misuli yenye nguvu huku viganja vyao vikiwa vikubwa na vyenye uwezo wa kumzuiya mnyama wamuwindae asiweze hata kusogea pale wanapo mkamata hasa kwa kutumia kucha. Simba ni miongoni mwa wanyama jamii ya paka ambao wana uwezo wa kuingiza kucha zao ndani tofauti na duma ambao hawana uwezo wa kuingiza kucha zao ndani.

Ukifanikiwa kumsogelea karibu simba au kumshika pindi ambapo anakuwa kachomwa sindano ya usingizi, mkague masikio hasa upande wa nyuma. Masikio yao yana madoa meusi upande wa nyuma, madoa haya huwa hayafutiki kabisa na simba hudumu nayo mpaka mwisho wa maisha yao. Wana mikia mirefu ambayo nchani huwa na manyoa mengi yenye rangi nyeusi. 

Dume huwa na manyoya mengi na marefu shingoni hadi maeneo ya kifuani. Hii ni moja kati ya sifa kubwa sana ambayo humtofautisha simba dume na simba jike japo wakiwa wadogo ni ngumu kuwatofautisha kwani madume wanakuwa hawana manyoa kama walivo madume wakubwa. Ukubwa wa mwili pia hutofautiana kati ya dume na jike. Madume huwa wana miili mikubwa tofauti na majike.

Huishi kwenye kundi lenye majike wengi na dume mmoja wakati mwingine (mara chache) zaidi ya mmoja na madume hawa huwa na mnasaba mmoja. Simba ndio wanyama jamii ya paka pekee wanaoishi kwenye kundi kubwa la ujamaa, kuchangia mipaka na kuwinda pamoja. Kundi hili huwa na kina mama na watoto ambao wana mnasaba mmoja hasa upande majike na watoto wa kiume. Kundi la simba huongozwa na simba jike ambae huwa na maamuzi na husikilizwa na wana familia wote.

Ili kumiliki kundi la majike madume huwa wana pigana sana na dume anaeshinda huwa na mamlaka ya kutawala himaya hiyo kasha humfukuza mbali kabisa dume mwingine. Hii ni kwasababu kila dume hutaka kizazi chake tu ndio kisalie na si kizazi cha dume mwingine. Hali hii hupelekea hata dume kuwafukuza watoto wake wa kiume pale wanapofikia umri wa kupanda majike.

Kundi la simba dume wakipigana kwa ajili ya kutaka umiliki wa himaya zao au kulinda himaya zao: picha kwa hisani ya Smithson Magazine

Ni wanyama jasiri sana na huwa tayari kupambana na maadui zao (sio waoga). Ujasiri huu wa simba unawafanya kuwa wanyama pekee ambao kwa umoja wao wanaweza hata kumuwinda twiga na kufanikiwa. Lakini pia wana uwezo wa kuwinda watoto wa tembo na kiboko kitu ambacho wanyamapori wengi jamii ya paka hawana uwezo huo.
Simba ni wanyama wenye uwezo wa kuona vizuri mchana na usiku pia na hawa kuwinda kuna wakati wanawinda mchana na usiku pia. Japo maranyingi kipindi cha jua kali simba hupendelea kupumzika chini ya miti yenye vivuli. Ni mara chache sana kuona simba wanawinda wakati wa jua au joto kali kwasababu simba huwa hawana uwezo wa kustahimili joto kati hasa wakati wa mawindo kwani hutumia nguvu kubwa sana. Wana uwezo wakuona usiku mara 8 zaidi ya binadamu.

Simba ndio mnyama wa pili kwa ukubwa katika wanyama jamii ya paka baada ya tiger. Lakini kwa barani Afrika simba ndio mnyama mkubwa kwa wanyama jamii ya paka kwasababu tiger hawapatikani barani Afrika. Simba pia ndio mnyama mkubwa katika jamii ya wanyama walao nyama barani Afrika. Ni wanyama wenye nguvu sana hasa maeneo ya kifuani na mikononi hususani simba dume ambae maranyingi majike wanapowinda mnyama mkubwa kama twiga au nyati kuna wakati hulazimika kupata msaada kutoka kwa dume mtawala wa himaya ili kumuangusha mnyama chini.

UKUBWA NA UZITO

UZITO

Uzito kato ya dume na jike hutofautiana.

Dume,175kg-250kg
Jike, 110kg-205kg

MAZINGIRA NA MAKAZI YA SIMBA
Simba hupendelea maeneo ya wazi pia wakati mwingine huishi maeneo yenye majani marefu kidogo na vichaka. Hii huwasaidia kujificha wakati wa mawindo pia.

Kundi la simba wakiwa wamepumzika chini ya kivuli cha mti katika hifadhi ya Serengeti Tanzania: Picha imepigwa na Kirsty Larmour

Kwa kawaida simba ni mnyama anaeishi aridhini maishani mwake lakini wakati mwingine hulazimika kupanda juu ya miti kutokana na mazingira anayoishi. Mfano mzuri ni simba wa hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara wanamepewa sifa pekee ya simba wapandao juu ya miti kutokana na mazingira ya hifadhi hii.


UWINDAJI NA CHAKULA
Simba ni mnyama mwenye uwezo wa kuwinda kuanzia wanyama wadogo jamii ya panya na wakubwa kama watoto wa faru, kiboko na watoto wa tembo. Lakini mara nyingi simba hupenda kuwinda wanyama saizi ya kati na wakubwa hasa walao majani kama nyati, swalapala, pofu, nyumbu, pundamilia, ngiri nk.

Simba huwaogopa sana wanyama wakubwa na hujitenga mbali nao sana, wanyama hawa ni kama tembo wakubwa, faru wakubwa, kiboko na twiga.
Shughuli yote ya uwindaji hufanywa na kina mama (simba majike) na mara tu baada ya kuuwa mnyama simba hawa kina mama, simba dume huja kujiunga nao kwa ajili ya kula tu. Kina mama humuachia simba dume nafasi ale mpaka ashibe kabisa nao ndo huanza sasa kula na watoto kwa amani. Simba dume husaidia kuwinda endapo mnyama ni mkubwa na husaidia tu kwa ajili ya kumuangusha chini. Kwa wakati mwingine simba dume hulazimika kuwinda endapo wanakuwa pekeyao kwenye kundi ambalo wamefukuzwa kwenye familia kutokana na kufikia umri wa kupanda majike.  Hivyo kukosekana kwa simba jike wa kuwawindia, hulazimika kuwinda wenyewe japo wanakuwa hawana mbinu nzuri za uwindaji kama walivyo simba majike.

Kundi la simba wakila mawindo yao (nyati) katika hifadhi ya Serengeti: Picha imepigwa na Michael Nicolas wa National Geographic

Simba hunywa maji kwa nadra sana na maji yenyewe huwa wanakunywa endapo tu watakutana nayo kwa bahati tu njiani na sio kutafuta maji kama walivyo wanyama walao majani kama nyati, tembo na wengineo. Simba anauwezo wakuishi muda mrefu bila kunywa maji kwasababu chakula anachokula kina maji ya kutosha.

KUZALIANA
Simba wanaweza kuzaa kipindi chochote cha majira ya mwaka bila kujali ni masika, kiangazi, joto au baridi. Mara nyingi kina mama huzaa wakati mmoja na kunyonyesha pamoja bila kujali ni mtoto wake au sio wake. Kila mama kwenye kundi anae nyonyesha hunyonyesha mtoto yoyote na hivo kuwa na ushirikiano katika kulea watoto. Simba hubeba mimba kwa muda wa takribani miezi mitatu na nusu (siku 110) na huzaa watoto kuanzia mmoja mpaka sita (1-6)
Watoto wa simba huzaliwa wakiwa hawaoni na mara nyingi huwa na uzito wa kilo 1-2kg.

Watoto mara nyingi hufa hasa kwa kuuliwa na madume wengine na mara nyingi ni chini ya nusu ya watoto waliozaliwa ndio hukuwa. Kina mama hulea watoto kwa muda wa miaka miwili lakini watoto wakiume huanza kufukuzwa kwenye kundi kuanzia miezi 15-20. Simba dume huwa na uwezo wakupanda majike afikishapo miaka miwili na nusu (miezi 30) wakati simba jike huwa na uwezo wakubeba mimba akiwa na miaka miwili tu (miezi 24).


Anapokuja simba dume mwingine mwenge nguvu katika kundi huwapiga madume alowakuta na kuwafukuza kisha kuuwa watoto wote atakaowakuta kwenye kundi. Na endapo atawakuta kina mama wana mimba basi hulazimisha kuwapanda wote kwa nguvu. Kitendo cha kuwapanda huaribu mimba zote na hapo hutawala kundi kisha kusubiri kuwapanda upya ili kueneza kizazi chake mwenyewe. Mara nyingi kina mama hubeba mimba kwa wakati mmoja, hali hii husaidia sana katika ushirikiano wa malezi kwa watoto kwani watoto pia huzaliwa kwa wakati mmoja au kutofautiana kwa siku chache sana.

Simba huishi miaka 15-16 anapokuwa katika mazingira asilia (yani porini), lakini kama anafugwa basi hufikisha mpaka miaka 20.


UHIFADHI
Simba wamepungua kwa kiasi kikubwa sana na hatimae kuwekwa kwennye kundi la wanyama waliyo hatarini kutoweka duniani. Miongo michache tu iliyopita kulikuwa na simba zaidi ya laki mbili (200,000) barani Afrika lakini kwasasa takwimu zinaonesha simba wamebaki elfu ishirini (20,000) bara zima la Afrika.

Simba wametoweka katika nchi 26 za bara la Afrika na hivyo kufanya nchi 27 tu ndo unaweza kuwaona simba katika bara la Afrika huku Tanzania ikiwa ni moja kati ya nchi inayo jivunia kwa kuwa na utajiri wa idadi kubwa ya simba. Japo simba wameslia nchi 27 barani Afrika na nchi moja tu barani Asia, ni nchi saba tu duniani ndo zina simba zaidi ya elfu kumi (10,000).

Kwasasa simba kaingizwa kwenye wanyama walio hatarini kutoweka duniani na shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi wa maumbile asili (International Union for Conservation of Nature-IUCN). Kwa upande wa Afrika Magharibi simba ni wanyama walio hatarini sana kutoweka maeneo hayo. Kwasababu kati ya simba 20,000 waliosalia barani Afrika ni simba 1500 tu ndo waliosalia Afrika ya Magharibi huku idadi ya simba ikiendelea kupungua siku baada ya siku kutokana na sababu mbali mbali ambazo katika vipengele vinavyo fuata.

UMUHIMU WA SIMBA

Moja kati ya wanyama ambao watalii wengi kutoka nje ya bara la Afrika wanapenda kuwaona basi simba ni mmoja wapo. Watu wengi hufarijika sana wanapo muona simba hasa katika mazingira yake asilia na hasa wanapo kuwa wanawinda hususani maeneo ya Massai mara wakati wa uhamaji wa nyumbu. Hivyo kupitia hamasa ya watalii kutaka kuwaona simba na urahisi wa upatikanaji wa simba hapa nchini kwenye hifadhi zetu za taifa na maeneo mengine ya hifadhi za wanyamapori, watalii wengi hulazimika kuja hapa nchini ili tu kuwaona simba. Hii hupelekea taifa kuingiza fedha nyingi sana za kigeni kupitia utalii hasa kwa wale wenye hamasa ya kuwaona simba.

Fedha zinazo patikana kupitia utalii hutumika kwa namna nyingi sana za kuleta maendeleo hapa nchini lakini pia kuna fedha ambazo hutumika moja kwa moja kwa maendeleo ya jamii kupitia ujirani mwema na hasa kwa jamii ambazo zinazunguka hifadhi za taifa. Jamii hizi zimekuwa zikijengewa shule, zahanati na miradi mingi ya maendeleo kutokana na fedha zinazo tokana na utalii ambao hasa huchagizwa na shughuli za uhifadhi wa wanyamapori.

Simba ni muhimu sana kwenye ikolojia kwani husaidia kupunguza idadi ya wanyama walao majani katika eneo moja. Endapo tusingekuwa na simba hasa katika maeneo ya hifadhi za taifa na maeneo mengine ya hifadhi za wanyamapori basi idadi ya wanyama walao majani ingekuwa kubwa sana kiasi kwamba maeneo yasinge tosha kutokana na wingi wa wanyama hao. Lakini kwakuwa simba wamekuwa wakiwawinda wanyama hao basi inasaidia kusawazisha ikolojia ya maeneo yetu ya hifadhi za wanyamapori na hifadhi za taifa kwa ujumla. Hivyo ni wazi kuwa uwepo wa simba ni wa umuhimu sana kwenye maeneo haya ya hifadhi za taifa na maeneo mengine ya hifadhi za wanyamapori.
CHANGAMOTO KATIKA UHIFADHI WA SIMBA HUSUSANI TANZANIA
Zipo sababu nyingi zinazo pelekea simba kupungua kwa kiasi kikubwa katika nchi nyingi barani Afrika. Zifuatazo ni miongoni mwa sababu zinazo pelekea simba kupungua kwa kasi sana hasa hapa nchini Tanzania.

Migogoro kati ya binaadamu na wanyamapori hususani kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa hifadhi za taifa na maeneo mengine ya hifadhi za wanyamapori kwasababu simba wamekuwa wakila mifugo yao. Hivyo jamii hizi huamua kuwauwa simba kwa sumu au mishale na mikuki. Hali hii imepelekea idadi kubwa sana ya simba kupungua. Lakini niwazi kwamba kama jamii za wafugaji zisingevamia maeneo ya karibu na hifadhi za taifa na maeneo mengine ya hifadhi za wanyamapori basi changamoto hii isinge kuwepo.

Usimamizi dhaifu wa vitalu vya uwindaji hasa uwindaji wa kitalii. Miaka ya nyuma usimamizi wa vitalu vya uwindaji wa wanyamapori haukuwa imara hali ambayo ilipelekea watu waliyopewa vibali vya uwindaji kukiuka masharti ya mikataba ya vitalu vyao na kuzidisha idadi ya simba waliyo takiwa kuwindwa. Wakati mwingine walikuwa wakiwinda mpaka majike kwa wingi hali ambayo ilipelekea kupungua kwa kasi ya kuzaliana kwa simba na kusababisha idadi ya simba kupungua kwa kiasi kikubwa sana hapa nchini. Jambo la kushukuru ni kusitishwa kwa uwindaji wa simba japo bado uhakika wa usitishwaji huu una kumbwa na changamoto nyingi.

Ujangili; uwindaji haramu wa wanyamapori sio changamoto kwa wanyama walao majani tu ambao hutumika kama kitoweo, bali hata kwa wanyama walao nyama kama simba. Simba wamekuwa wakiwindwa sana kutokana na malighafi zao kuwa na soko kubwa sana hasa nje ya bara la Afrika. Kucha na ngozi ya simba hutumika kutengenezea bidhaa mbali mbali zenye thamani nje ya bara la Afrika na watu hasa wa nje hunufaika sana kupitia biashara hizo. Hii inachochea sana watu kuwawinda simba kwani wanaingiza pesa kwa njia ya uwindaji haramu.

Baadhi ya wana jamii wamekuwa wakishirikina na majangili lakini pia kuwaficha wasijulikane na mamlaka husika zinazo shughulika na uhifadhi wa wanyamapori. Hali hii inapelekea ugumu katika utendaji kazi wa mamlaka husika kwani zinakosa taarifa muhimu kutoka kwa wana jamii dhidi ya vitendo vya ujangili. Majangili wanafanya uharamia kwenye rasilimali zetu kasha wanakwenda kujificha kwenye nyumba za baadhi ya wana jamii bila hata kufichuliwa. Na kuna baadhi ya wana jamii wana fahamu fika wahusika wa ujangili ni kina nani ila hawataki kuwataja. Hili ni moja kati ya tatizo kubwa sana kwenye suala zima la kutaka kutokomeza ujangili kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

Uharibifu wa mazingira na uvamizi wa maeneo ya hifadhi za taifa na maeneo mengine ya uhifadhi. Kutokana na wimbi la jamii za wafugaji kuvamia maeneo mengi ya hifadhi za wanyamapori, hali ya uharibifu wa mazingira imepelekea simba wengi kuhama baadhi ya maeneo. Mifugo imekuwa ikiharibu makazi ya simba lakini pia kumaliza chakula ambacho kilikuwa muhimu kwa mawindo ya simba ambao ni wanyama walao majani. Wanyama walao majani wanapo hama kutokana na ukosefu wa chakula uliyo sababishwa na mifugo basi hupelekea simba pia kuhama na wengine hukaa na njaa hali ambayo hupelekea vifo vya simba.

Magonjwa ya wanyama jamii ya wanyama wala nyama kama canine distemper, homa ya bonde la ufa na kimeta. Hii ni asilia na siku zote asili huchukua nafasi yake ili kuweka usawa wa mazingira. Japo wanyamapori wana uwezo wa kustahimili magonjwa kwa kiasi kikubwa ila yapo magonjwa ambayo ni hatari sana kwao. Mfano ni magonjwa niliyo yataja hapo juu yamekuwa yakiwauwa wanyama wengi walao nyama wakiwemo simba. Hairuhusiwi kumtibu mnyamapori, japo kwa wale wanyama ambao wapo hatarini kutoweka duniani na wale ambao ni alama za taifa sheria inaruhusu wanyama hawa kutibiwa.


NINI KIFANYIKE KUWANUSURU SIMBA HUSUSANI HAPA NCHINI TANZANIA

Kuzuiaa ongezeke la wafugaji kandokando na maeneo ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba; moja kati ya changamoto kubwa niliyo itaja hapo juu ni migogoro kati ya binaadamu na wanyamapori ambayo hutokana na visasi vya watu hasa jamii za wafugaji kuwauwa simba kutokana na kuvamiwa mifugo yao. Serikali inapaswa kushughulikia changamoto ya wafugaji kuvamia maeneo ya wanyamapori ili kusaidia kupunguza changamoto hii na kusaidia kutimiza adhma au malengo ya uhifadhi hapa nchini kwenye hifadhi za taifa na mapori ya akiba.

Kuongeza uwezo wa doria hasa kwa mamlaka zinazo simamia uhifadhi wa wanyamapori kama TANAPA, NCCA na TAWA ili kupambana na kutokomeza tatizo la ujangili. Niwazi kwamba mamlaka hizi zinafanya kazi kubwa sana kwenye suala la doria hivyo hazina budi kuzidisha juhudi ili kujua zaidi maficho ya majangili na kuyatokomeza kabisa. Lakini kwa jicho la tatu serikali haina budi kuzisaidia mamlaka hizi kuongeza idadi ya askari wa ulinzi kwa kuzipa vibali vya kuajiri kwani idadi ya askari doria ni ndogo sana ukilinganisha na ukubwa wa maeneo ya hifadhi za wanyamapori.

Viongozi na wana jamii wa vijiji vinavyo pakana na hifadhi za taifa au mapori ya akiba wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwafichua majangili. Hii itapelekea urahisi wa mamlaka husika kuwakamata na kuwafungulia mashtaka majangili dhidi ya uhujumu uchumi lakini pia uharibifu wa rasilimali zetu hapa nchini. Niwazi kwamba ujangili huwanufaisha wachache ambao hawana uchungu na maendeleo ya jamii au taifa kwa ujumla. Hivyo kwa kuwafichua pamoja na makazi au maficho yao itasaidia kutatua mwiba mkubwa sana uao zichoma mamlaka huzika.

Uboreshaji na kuongeza kasi kwa ujenzi wa maboma ya mifugo kwa jamii au vijiji vinavyo pakana na maeneo ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba. Moja kati ya miradi ambayo TANAPA inajitahidi sana kuitekeleza ni kujenga maboma ya mifugo kwa jamii zinazo pakana na hifadhi za taifa. Hii kwa kiasi kikubwa inasaidia kupunguza tatizo la simba kuvamia mifugo. Hivyo serikali pia inabidi kuiunga mkono mamlaka hii (TANAPA) kwenye mradi huu ili kupunguza migogoro kati ya wafugaji na wanyamapori.

Kuandaa sera sheria zitakazo saidia kupambana na uharibifu wa mazingira maeneo ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba; Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii pia kwa kushirikiana na wizara ya katiba na sheria haina budi kuandaa sheria ambazo zitakuwa na adhabu kali kwa yeyote atakaeonekana kuharibu mazingira ama kwa kuingiza mifugo ndani ya hifadhi au kwa namna yoyote ile. Lakini serikali pia inapaswa kuandaa sera mahususi za mazingira ili kupunguza wimbi la uchafuzi au uharibifu wa mazingira katika maeneo ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba.

Usimamizi mzuri wa vitalu vya uwindaji katika maeneo ambayo uwindaji wa wanyamapori unaruhusiwa. Japo kwa sasa uwindaji wa simba umepigwa marufuku ila wapo ambao kwa faida zao binafsi wanaweza kutumia mwanya wa vibali walivyopewa kuwinda wanyama wengine wakaamua kuwinda simba kwa siri. Hivyo usimamizi na ufuatiliaji wa wanyama husika tu ndio wawindwe kutokana na kibali kicho tolewa kwenye kitalu husika.

Serikali kupitia wizara ya ardhi na makazi ijitahidi kutenga maeneo ya wafugaji ili waweze kuondoka maeneo karibu na hifadhi mana inaonekana kabisa wafugaji ndio chanzo kikubwa cha kupungua kwa simba hasa hapa nchini kutokana na kuwauwa kwa kulipa kisasi. Tanzania tuna maeneo mengi sana yenye rutuba na chakula cha kutosha cha mifugo hivyo inawezekana kabisa kama serikali itaamua kuja na mikakati thabiti ya kutenga maeneo kwaajili ya wafugaji na kuepukana na tatizo la mifugo kuvamiwa na simba. Kikubwa ni kushirikisha wadau na kuandaa sera ambazo zitakuwa na faida kwa pande zote mbili (kwa wafugaji na serikali).

Kuanzisha maeneo maalumu ya kuwatunza na kuwafanya simba waweze kuzaliana na baadae kuwapeleka hifadhini; hii pia itasaidia kuongeza idadi ya simba kwa haraka zaidi. Kwa mtazamo wa kawaida inaweza kuonekana ni jambo gumu sana lakini linawezekana. Kama serikali iliweza kupambana na kusaidia mradi wa utunzaji wa mbwa mwitu wa Afrika pale Hifadhi ya Taifa ya Mkonazi basi hata mradi wa kuwatunza simba pia unawezekana. Kinacho takiwa ni utekelezaji na usimamizi imara wa sera ya utunzaji wa simba katika bustani za wanyamapori.

Elimu kuhusu uhifadhi na umuhimu wa maliasili; kwanza kwa kuanza na jamii kwa ujumla ili kila mwana jamii ajue ni nini maana ya uhifadhi na ni faida gani zinazo patikana kutokana na uhifadhi wa wanyamapori. Lakini kupitia wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kupitia wadau mbali mbali na wataalamu wa sayansi ya uhifadhi wa wanyamapori, serikali haina budi kuandaa mitala mbali mbali ya elimu kuhusu uhifadhi na umuhimu wake kuanzia ngazi ya elimu ya msingi mpaka sekondari na somo liwe ni la lazima. Kwa kufanya hivi itasaidia kuwapata watu wenye moyo wa uhifadhi kuanzia ngazi za chini na kufanya shughuli za uhifadhi kuwa rahisi hapo baadae.


HITIMISHO
Kwa mtazamo wa juu juu huwezi kuona umuhimu wa simba. Ila tazama watu wanatoka Ulaya, Marekani na Australia kuja Afrika kumuona simba na hasa pia ikiwemo Tanzania ambapo simba huonekana kwa urahisi zaidi. Lakini pia uwepo wa simba hifadhini husaidia kupunguza ongezeko kubwa la wanyama walao majani kwasababu kama wanyama hawa wataongezeka kwa idadi kubwa basi eneo litakuwa dogo na hatimae hatakuwa na usawa wa wanyama na mazingira yao. Pia nchi inaingiza kiasi kikubwa kutoka sekta ya utalii hasa watalii watokao nje kwa ajili tu yakuja kumuona simba apa nchini.

Hongera sana kwa mamlaka ya hifadhi za taifa Tanzani TANAPA kwa miradi ya maboma ya mifugo walioanzisha kwani yanasaidia angalau kupunguza matatizo ya mifugo kuvamiwa na wanyamapori kama simba, chui, fisi na mbwa mwitu. Lakini pia kwa doria ambazo zimekuwa zikiendelea kila siku ili kuhakikisha usalama wa simba na wanyamapori wengine dhidi ya ujangili.

Pongezi pia kwa mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCCA) kwa kazi kubwa sana ya uhifadhi kwani mamlaka ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro ni moja kati ya maeneo ambayo simba ni rahisi sana kuonekana na hii huchagizwa na usimamizi mzuri na utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi wa wanyamapori katika eneo hilo.

Lakini pia bila kuisahau mamlaka ya menejimenti ya wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa kazi kubwa sana wanayo fanya ya kuhakikisha simba waliyopo kwenye baadhi ya mapori ya akiba wanaendelea kuwepo katika maeneo hayo hii ni moja kati ya kazi kubwa sana inayofanywa na mamlaka hii.

Pongezi za mwisho kabisa kwa wadau wote ndani na nje ya nchi wanao pambana au kusaidia uhifadhi wa wanyamapori hasa kwa wanyama walao nyama ambao wengi wao wapo hatarini kutoweka. Mfano moja kati ya mradi muhimu sana hapa nchini ni Lion landscape (Ruaha Carnivore Project) pale hifadhi ya taifa ya Ruaha.

MWISHO

Mwisho wa makala hii ndio mwanzo wa makala nyingine.
Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori na ushauri kuhusu makala hizi wasiliana nami kupitia. Makala hii imeandikwa na Sadick Omary na kuhaririwa na Hillary Mrosso. Kwa maoni, maswali au ushauri usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano hapo chini.

Sadick Omary Hamisi

Simu:0714116963/0765057969
Email; sadickhamisi5519@gmail.com

Facebook; Envirocare and wildlife conservation/Sadikc Omary Kashushu

Instagram; wildlife_articles_tanzania

Au tembelea tovuti yetu; www.wildlifetanzania.home.blog
“I’M THE METALLIC LEGEND”