Habari za siku ndugu msomaji wa makala hizi za wnyamapori. Ni matumaini yangu umzima wa afya na unaendelea na majukumu ya kulijenga Taifa letu imara kwa ufasaha na weledi zaidi. Basi kama ilivo kawaida yetu, wakati tuna shughulika na majukumu yetu ya kila siku tusisahau pia kujua machache kuhusu rasilimali zetu hapa nchini hasa kwa upande wa wanyamapori. Hizi ni rasilimali ambazo zinahitaji uangalizi na usimamizi mkubwa sana kwani tukiwa wazembe kwenye eneo dogo tu katika uhifadhi wa rasilimali hizi itabakikuwa ni majuto tu hapo baadae.

Katika makala hii ya leo tutarudi upande wa wanyama jamii ya swala. Kundi hili la jamii ya swala lina wanyama wengi na wa aina mbalimbali sana hasa ukianza kumchambua mmoja baada ya mwingine. Kama ilivo ada hapa tutajuzana mambo muhimu na yenye funzo kubwa sana kwa kila mnyama na hatimae kuhamasisha suala la uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yao kwa ujumla. Suala la uhifadhi sio la mamlaka zinazo simamia masuala ya uhifadhi wa wanyamapori peke yao, bali ni suala au wajibu wa wananchi wote kwa pamoja. Hivyo ni lazima tutoe ushirikiano katika kutekeleza uhifadhi wa wanyamapori bila kusahau na makazi ya wanyama hawa.

Na moja kwa moja leo tutamjua mnyama “KONGONI” ambae kwa lugha ya kigeni (Kingereza) mnyama huyu hujulikana kwa jina la “HARTBEEST”.

UTANGULIZI

Kongoni ni miongoni mwa wanyama jamii ya swala ambao ni wakubwa kimaumbile. Wanyama hawa wapo kwenye familia moja na wanyama kama Nyati, Nyumbu, Pofu na wengineo katika familia hii. Kuna takribani spishi nane (8) za Kongoni ambazo kati ya spishi hizi nane, spishi moja tayari imekwisha toweka duniani na tatu kati ya saba zilizo baki inasemekana wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kutoweka duniani pia. Kongoni ni wanyama ambao wanapatikana bara la Afrika tu na wameenea maeneo mbalimbali hapa barani Afrika hususani mashariki, magharibi na kusini mwa Afrika. Idadi ya wanyama hawa imekuwa ikipungua kutokana na sababu mbalimbali ambazo kwa undani tuta zizungumzia katika kipengele cha changamoto zinazo wakumba wanyama hawa. Hivyo nakusihi uwe pamoja name hadi mwisho wa makala hii.

  • SIFA NA TABIA ZA KONGONI

Wameinuka sehemu ya mabega kuliko sehemu ya nyuma, na hii ni kutokana na miguu ya mbele kuwa mirefu kuliko miguu ya nyuma.

Wana miguu mirefu, shingo fupi, uso mwembamba na mrefu huku masikio yao yakiwa yamesimama. Wanyama hawa wanapokuwa wamesimama huonekana kama wana mteremko mgongoni kuelekea upande wa nyuma na hii ni kutokana na miguu ya mbele kuwa mirefu kuliko ya nyuma.

Rangi ya miili yao huwa na rangi mchanganyiko ambazo ukiwachunguza vizuri utaona wana manyoa yenye wekungu, wuesi na hata wakati mwingine kuelekea kama rangi ya dhahabu huku mikia ikiwa mirefu na rangi ya kahawia iliyo kolea zaini kwa upande wa juu.

Kwa pamoja madume na majike wote wana pembe ambazo kwa sehemu ya chini kwenye kikonyo zimekaribiana huku pembe hizo zikiwa zimejikunja kidogo kuelekea upande wa mbele na juu huku zikiwa zimechongoka kwa upande wa ndani. Pembe zao huwa zina miduara ambapo miduara miwili hadi mitatu huweza kumtofautisha kongoni mmoja na mwingine na kwa upande wa majike miduara hii huwa ni myembamba ukilonganisha na madume.

Kongoni majike huishi kwenye kundi moja na kundi hili huwa na idadi ya kina mama 5 – 12 na watoto. Kundi hili la kina mama huwa chini ya utawala wa dume ambae huwa mwenye hasira sana hasa kipindi cha kuzaliana kinapo karibia. Madume huishi kwa pamoja hasa wale watoto wa kiume ambao hufukuzwa ndani ya kundi la kina mama.

Kongoni ni wanyama wenye uwezo wa kuona zaidi mchana kuliko usiku na huutumia muda huu kutafuta chakula na maji. Inapo fika jioni wanyama hawa hutafuta sehemu yenye usalama na kulala mahali hapo mpaka siku nyingine itakapo pambazuka.

Kongoni ni miongoni mwa wanyama jamii ya swala ambao wana uwezo wa kukimbia sana. Wanyama huwa wana uwezo wa kukimbia kilometa sabini hadi themanini kwa saa (km70 – km80/saa) hasa pale wanapokuwa wanakimbizwa na adui nakuhitaji kumkimbia zaidi adui yao.

  • UREFU, KIMO NA UZITO WA KONGONI

Urefu= Kongoni huweza kurefuka na kufikia urefu wa sentimita sm160 – 215 huku mkia ukiwa na urefu wa sentimita 30 – 70.

Kimo= kimo cha kongoni hufikia hadi sentimita 135.

Uzito= uzito kati ya dume na jike huwa ni tofauti kidogo. Dume huwa na uzito mkubwa kuliko jike ambapo huwa na kilogramu 125 – 218 huku jike wakiwa na uzito wa kilogramu 116 – 185.

  • MAZINGIRA

Wanyama hawa wanapendelea sana maeneo ya savanna iliyo wazi na sehemu zenye miti na majani mengi. Kuna wakati wanyama hawa hufika hadi maeneo yenye asili ya jangwa hasa mara tu baada ya msimu wa mvua kuisha. Miongoni mwa nchi ambazo wanyama hawa hupatikana kwa wingi ni Tanzania, Afrika kusini, Kenya, Msumbiji, Ethiopia, Botswana na baadhi ya maeneo ya pembezoni mwa Somalia.

  • CHAKULA

Kongoni ni wanyama walao majani kama walivyo swala wengine. Wanyama hawa hupendelea pia kunywa maji mara kwa mara japo unapo fika msimu wa kiangazi huwa na uwezo wa kuvumilia na kukaa bila kuywa maji kwa muda mrefu.

  • KUZALIANA

Kabla ya kuwa mtawala wa kundi la kina mama na watoto huwa kuna ugomvi mkubwa sana kati ya madume. Dume ambae atashinda katika mapambano hayo basi humiliki kundi la majike na watoto waliyopo katika kundi hilo. Mara tu baada ya kuwa mtawala wa kundi huakikisha anaweka mipaka katika eneo lake ili kuzuia madume wengine wasivamie eneo hilo. Hutumia kinyesi kuweka mipaka na wakati huo majike na watoto wote chini ya utawala wake huzungukia ndai ya eneo hilo pasi na ruhusa ya kutoka nje ya eneo hilo.

Kwnye baadhi ya maeneo wanyama hawa huanza kupandana kipindi kifupi cha msimu wa mvua, na ndio wakati huu madume huwa na hasira sana kwa ajili ya kupambana kutengeneza himaya zao. Mara baada ya kuwapanda majike, majike hawa hukaa na mimba kwa muda wa miezi minane (8) na kuzaa mtoto mmoja tu. Kabla ya kuzaa mama huondoka kwenye kundi na kutafuta sehemu yenye majani au miti mingi kwenye usalama kwa ajili ya mtoto atakae zaliwa.  Mtoto hufichwa kwa takribani wiki mbili mara tu baada ya kuzaliwa. Baada ya muda huu mtoto huwa na uwezo wa kukimbia na hata kuongozana na kundi la kina mama na watoto, na ndio wakati huu sasa mama hurudi ndani ya kundi na mwanae.

Japo mtoto hujiunga na kundi la kina mama baada ya wiki mbili, bado pia hutegemea maziwa ya mama kwa muda wa miezi minne na huwa karibu na mama kwa muda wa miaka mitatu. Watoto wa kiume mara tu wanapokuwa huondoka kwenye kundi hili la kina mamana kutengenezea kundi lao. Kipindi hiki watoto hawa wa kiume wanakuwa bado hawajawa na uwezo wa kuanzisha himaya zao hivyo hulazimika kuishi kwa kupendana sana katika makundi yao.

Tofauti na walivyo swala wengine, kongoni wanapozaa huwa hawana umoja wa kina mama ndani ya kundi na hivyo kila jike hulazimika kuwa pamoja na watoto ambao wanashabihiana kizazi yani wale ambao wanatokana na kizazi kimoja ndio hukaa pamoja kipindi hiki cha kuzaliana. Wanyama hawa huanza kuzaliana wafikishapo umri wa mwaka mmoja hadi minne.

Maisha ya Kongoni awapo porini huwa ni miaka 11- 20 japo kama anafugwa kwenye bustani maalumu za kufugia wanyama huweza kuzidi umri huo.

  • UHIFADHI

Mpaka sasa hakuna takwimu maalumu zinazo toa kipimo cha uhifadhi wa wanyama hawa. Wanyama hawa bado wameendelea kuonekana sana katika maeneo yao hususani hapa Tanzania katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ni sehemu ya urithi wa dunia na hii inasaidia kuongeza chachu ya uhifadhi wa wanyama hawa katika maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori

Shirika la umoja wa mataifa linalo shughulika na uhifadhi maumbileasili duniani (International Union for Conservation of Nature- IUCN) linawaweka wanyamahawa kwenye kundi la wanyama ambao bado hawajawa hatarini kutoweka duniani japo kati ya spishi saba ambazo zimebaki duniani, spishi tatu zimewekwa kuwa katikahatari zaidi ya kutoweka duniani. Japo kuna spishi moja ya wanyama hawa ambayo kwa sasa imekwisha toweka kabisa duniani kutokana na changamoto mbalimbali.

Kuna sensa ilifanyika mwaka 1999 na kubaini idani ya Kongoni waliyo salia bara zima la Afrika ni kongoni 362,000 tu ambapo uwepo wa kongoni hawa ulisaidiwa sana na kuwepo kwa spishi ya kongoni wekundu ambao wanapatikana sana maeneo ya kusini mwa Afrika ambao

walikadiriwa kuwa jumla ya kongono 130,000 huku kati ya idadi hii asilimia 40% wakiwa kwenye maeneo yanayo milikiwa na watu binafsi na asilimia 25% wakiwa kwenye maeneyo ya uhifadhi.

Kutokana na tafiti za IUCN, idadi ya wanyama hawa inapungua siku baada ya siku kutokana na changamoto mbalimbali hivyo jitihada madhubuti zina hitajika sana kabla hali haijawa hatari zaidi.

  • MAADUI WA KONGONI

Hapa nazungumzia maadui asilia na ambao ni lazima wawepo ili kuhakikisha kuna kuwepo na usawa wa kiikolojia katika mazingira wanayoisha wanyama hawa. Maadui wakuu wa wanyama hawa katika mazingira yao asili ni Simba, Chui, Duma, Mbwa mwitu, Mbweha na Fisi.

Adui wa nje ambae ni hatari zaidi katika ikolojia ya wanyama hawa ni BINADAMU. Kwakweli mwanadamu ni adui mkubwa sana kwa wanyama na hili pia lina hitaji utulivu na busara katika kulitatua.

  • TISHIO NA CHANGAMOTO KWA KONGONI HASA HAPA KWETU TANZANIA

Tishio kubwa kwa wanyama hawa ni ujangili uliyo kithiri kwenye maeneo ya Hifadhi za wanyamapori. Idadi ya kongoni inapungua kwa kasi kubwa sana kutokana ku kukithiri kwa ujangili hasa kutokana na ongezeko la uhitaji wa nyamapori pamoja na malighafi nyingine zitokanazo na wanyama hawa kama pembe, ngozi na kwato. Hali hii inatokana pia na kuongezeka kwa masoko ya biashara haramu ya wanyamapori kitu ambacho kina chochea sana wanyama hawa kuuwawa kwani imekuwa ni kitega uchumi kwa majangili na hatimae kusababisha upungufu mkubwa kwa wanyama hawa.

Uvamizi na upanuzi wa maeneo kwa ajili ya makazi. Hili nalo ni tatizo kubwa sana kwani watu wengi sasa wanavamia maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori na kusababisha wanyama hawa kuyakimbia makazi yao. Uvamizi huu hupelekea uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa sana na kusababisha upungufu wa mahitaji ya kiikolojia kwa kongoni kitu ambacho kina wafanya wanyama hawa kuishii kwenye hali ya wasiwasi na njaa kwa muda mrefu. Inafika hatua hadi baadhi ya kongoni wanakuwa kama wametengwa na kongoni wengine kwani tayari hapo katikati kuna kuwa na muingiliano wa makai ya binadamu na kufanya muingiliano wa wanyama hawa kuwa mgumu.

Ongezeko la wimbi la mifugo kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Kume kuwepo na tabia ya wafugaji kuingiza mifugo ndani ya hifadhi za wanyamapori hali ambayo inapelekea wanyama hawa kugombania chakula na mifugo. Hali hii imepelekea baadhi ya kongoni kuyahama makazi yao kutokana na uhaba wa chakula na kufanya wanyama hawa kuhangaika sana kutafuta maeneo tulivu mengine kama waliyo yazoea. Uingizaji wa mifugo katika hifadhi za wanyamapori unapelekea nyasi au majani kushambuliwa kwa kiasi kikubwa sana kitu ambacho kwa wana jeografia wanasema huwa ni chanzo cha utokeaji wa jangwa katika maeneo hayo.

  • NINI KIFANYIKE KUNUSURU WANYAMA HAWA HAPA NCHINI TANZANIA

Kuongeza maeneo ya hifadhi za wanyamapori na idadi kwa ujumla. Kutokana na tatizo la uvamizi wa maeneo haya ya hifadhi za wanyamapori hapa nchini, hatuna budi kutanua maeneo haya ili kuweza kuongeza maeneo ya kuishi kwa kongoni kwani imeonekana dhahiri wanyama hawa sasa wamekuwa wakiishi katika maeneo finyu sana kutokana na uvamizi wa maeneo yao. Pia kwa baadhi ya maeneo ambayo yanaweza kufanyiwa utafiti wa kiikolojia na kuona kama kuna uwezekano wa wanyama hawa kuishi basi maeneo haya yatangazwe rasmi kuwa maeneo tengefu ya hifadhi ya wanyamapori. Hili litasaidia hata kwa kongoni ambao wanaishi nje ya Hifadhi za Taifa kuwa kwenye ulinzi wa kutosha kwani si kwamba kongoni wote wanapatikana katika maeneo tengefu ya uhifadhi wa wanyamapori. Hivyo kwa kuongeza maeneo haya ita saidia hata kuongeza kasi ya kuzaliana kwa wanyama hawa na kurudi idadi ambayo itakuwa ni nzuri kama ilivyo kuwa hapo awali.

Kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori na kuishirikisha jamii katika suala zima la uhifadhi wa wanyamapori. Hapa nadhani ndio msingi mkuu wa kuimarisha suala la ulinzi na uhifadhi kwa ujumla. Jamii ni muhimu sana kushirikishwa kwani hawa ni mabalozi wazuri sana katika kufichua majangili kwani niwazi kwamba majangili wengi tuna ishinao ndani ya jamii zetu. Ongezeko la askari pia lita saidia kuongeza nguvu ya doria kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori na kupunguza kasi ya ujangili hapa nchini kwetu. Kuishirikisha jamii pia ni pamoja na kuwagawia fungu la faida ambalo linapatikana kutokana na mapato ya hifadhi hizi kwani kwakufanya hivyo jamii zitaona mchango wa hifadhi za wanyamapori na kuguswa kwa undani zaidi katika kuhifadhi wanyama hawa. Kila mwananchi akiwa balozi mzurikatika kufichua majangili walipo, basi ita saidia sana kuwapata watu hawa ambao wanatumia rasilimali zetu kwa ajili ya maendeleo yao binafsi bila kujali wenzao.

Kupambana na suala la mifugo kuingizwa ndani ya maeneo ya hifadhi za wanyamapori. Tumeona mifugo pia ni tatizo kubwa sana kwa kongoni kutokana na uwepo wa kugombania chakula na wanyama hawa. Jamii za wafugaji zinazoishi mipakani mwa hifadhi za wanyamapori zipewe elimu ya kutosha juu ya suala hili ili kupungua au kutokomeza kabisa suala la kuingiza mifugo kwenye hifadhi za wanyamapori. Nadhani hapa nchini tuna maeneo mengi sana ambayo hayajaguswa kabisa na yana chakula cha kutosha kwa ajili ya mifugo. Hivyo serikali ijitahidi kwa hali na mali inawatafutia maeneo maalumu wafugaji kutokana na kanda ili kuepuka tatizo la mifugo kwenye hifadhi za wanyamapori. Ikiwezekana hata sheria kali za uhifadhi na mazingira zichukuliwe kwa wale wafugaji ambao watakiuka maagizo au sheria hizo kwani wanapo haribu mazingira kwa ajili ya wanyamapori na kupata faida wao, husababisha hasara kwa Taifa kwa ujumla. Waziri mwenye dhamana ahakikishe anasaidia kutatua tatizo hili mapema kwani hapa nchini hili nalo limekuwa ni tatizo sugu kutokana na ukweli kwamba kila waziri anaekabidhiwa usimamizi wa maliasili ameshinwa kulitatua tatizo hili hadi kulimaliza.

Kupambana na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji pia ni tatizo kubwa sana kwa wanyama hawa kwani tumeona wanyama hawa hupendelea kunywa maji mara kwa mata sasa endapo maji yatakosekana japo wana uwezo wa kuvumilia bado litakuwa ni tatizo sana kwani mwisho wa siku wanyama hawa watakufa tu. Vyanzo vingi vya maji vimekuwa vikiharibiwa sana hapa nchini, mfano mzuri ni Mto Mkuu Ruaha, Mto huu ni muhimu sana kwa wanyamapori waishio katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni mto huu umekuwa ukikauka mara ka mara kutokana na uharibifu wa vyanzo vya mto huu. Hali hii ilipelekea wanyama kama viboko na mamba kuishi kwa tabu sana pale hifdhini.

HITIMISHO

Hakuna mtu atakaye weza kuthamini kitu chako kama wewe mwenyewe hukithamini. Kongoni ni wanyama ambao wanaliingizia Taifa fedha nyingi tu hasa kutokana na sekta ya utalii. Kuna watu wanakuja Tanzania kwa ajili yakutaka kumuona Kongoni tu kisha kurudi nchini kwao. Changamoto mbali mbali zinazo wakumba wanyama hawa na wengine pia ziwe ni fundisho kwetu sote ili kila mmoja kwa ajili ya Taifa letu tushirikiane na mamlaka husikakatika kusimamia suala la uhifadhi wa wanyamapori na mazingira yao kwa ujumla.

Kuna tafiti zinaonesha kwamba, miongoni mwa wanyama wanao cheuwa (yani wanyama wenye sehemu nne za matumbo), katika kundi hilo wakiwemo Kongoni basi Kongni ndio wanyama ambao wanaongoza kwa mazingira yao kuharibiwa kuliko wengine wote barani Afrika. Tusipokuwa makini tunaweza wakosa kabisa wanyama hawa kwani kasi ya upuguaji inaongezeka sana.

Napenda kuzipongeza mamlaka ambazo kwa dhati zinasaidia kunusuru uwepo wa wanyama hawa nakufanya Tanzania iwe ni miogoni mwa nchi pekee ambazo tunajivunia kuwa na aina nyingi za wanyama na mazingira mazuri ya kitalii kwa ajiliya kuwaona wanyama hawa. Pongezi sna kwa TANAPA, TAWA na NCAA kwa kazi kubwa sana mnayo ifanya kuhakikisha tunaendelea kuwa na wanyama hawa tena wakuwa katika maeneo salama na yenye kuvutia.

Ahsanteni

Kwa mengi zaidi kuhusu wanyamapori, maswali na ushauri juu ya makala hizi wasiliana na mwandishi wa Makala hii kupitia.

Sadick Omary

Simu= 0714116963 / 0765057969 / 0785813286

Email= swideeq.so@gmail.com

Au tembelea= www.mtaalamu.net/wildlifetantania

”I’M THE METALLIC LEGEND”