Awali ya yote, nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na afya njema, pia kwa kuiwezesha makala hii hatimaye imekufikia mikononi mpendwa msomaji wetu wa makala za wanyamapori na maliasili kiujumla ili tujifunze zaidi kuhusu mabingwa hao (big five), kwanini waitwe hivo, tabia zao na hata wanakopatikana kwa wingi barani Afrika, bila kusahau hali au ngazi ya uhifadhi wao, karibu.
Utangulizi mfupi;
Makala hii imeainisha wanyama watano ambao ndio “mabingwa katika mbuga za kiafrika” (The African big five), jina hili walipewa miaka ya nyuma na wawindaji wa kampuni za uwindaji kutokana na kuwa ni vigumu sana na hatari zaidi kuwawinda, bado jina hili linatumika kwa sasa japokuwa ni kwa makampuni ya utalii mbugani kwani ni fahari kwa mtalii kukutana nao mbugani katika mazingira yao na pia kupata fursa ya kipekee kupiga nao picha.
Ni furaha iliyoje kukutana na simba akiwa mawindoni pembeni jua linazama? haielezeki, vipi tabasamu usoni unapokutana na chui uso kwa uso macho kwa macho!! Mnyama anaeongoza kwa kasi ya kukimbia duniani, tembo je? Mnyama mkubwa nchi kavu duniani na mwenye uwezo mkubwa wa kutunza kumbukumbu na hisia kama binadamu? Au kifaru mnyama alae majani wakati wa usiku tofauti na wala majani wengine? Inakuwaje tena kukutana na nyati jamii pekee ya ng’ombe aishie mbugani na asiyehofia chochote? Ila hapa mmmmh!!!
Basi mpendwa msomaji wetu hao ndio mabingwa au nyota tano mbuga za kiafrika japokuwa wengine hawana umbo kubwa kama ulivotegemea, makala imechambua mmoja baada ya mwingine.
1.Simba
Ndiye mnyama pekee miongoni mwa walao nyama ambae hana adui mbugani zaidi ya binadamu, magonjwa na uharibifu wa mazingira, pia kwa kiikolojia anashika nafasi ya juu zaidi katka ngazi ya ulaji chakula katika mfumo wa viumbe hai (Africans’ apex predators) na pia anashika nafasi ya pili kwa umbo kubwa katika jamii za paka duniani.
Pia simba ndio paka pekee wanaoishi katika makundi makundi(pride) kuanzia simba watatu mpaka thelathini (3-30) kwa sababu wanahitajiana zaidi hata hivyo simba jike pekee ndio wanaoishi kutegemea makundi hayo mpaka kifo hii ni kutokana na kwamba wanasaidiana kutunza watoto ndani ya kundi kwa pamoja pia watotot hao hunyoya kwa simba jike yoyote anaetoa maziwa.
Rangi ya mwili; mchanganyiko wa nyekundu na kijivu inayopotea ambayo huonekana kama hudhurungi (brown).
Urefu; dume 1.15m(115cm) na jike 91cm
Uzito; dume 220kg na jike 150kg
Chakula; nyama, haswa ya wanyama wakubwa wenye kwato mfano jamii ya swala, nyati
Mazingira wanayopatikana; inategemeana, wapo wa msituni hadi jangwani
Usichokijua;
Simba jike ndiye huwinda mara nyingi hasa wakati wa usiku wakiwa kwenye kundi na mara nyingine kuiba au kunyanganya mnyama aliyetoka kuwindwa na wanyama wengine kama fisi pia ndiye mlinzi wa makazi yao.
Jamii ya paka pekee wanaoishi kwenye makundi tofauti na wengine kama chui na chui milia ambao mara nyingi wanakaa peke yao kipweke zaidi.
Jamii ya paka wengi huwinda usiku kama inavozaniwa kwa simba japo kuwa uhalisia wake simba huchangamka katika mawindo masaa yenye mwanga usio mkali sana (crespuscular animal) ambao ni mwanga wa mapema asubuhi na jioni na mara nyingine huwinda muda wowote (opportunistic hunters).
Wanyama hawa wanatumia muda mwingi sana wanalala na kupumzika, masaa yasiopungua 16 hadi 20 kwa siku
Simba waliopo barani Afrika wanapatikana asilimia 8% tu ya maeneo tengefu ya hifadhi za wanyamapori zilizopo Afrika na wengi wao wanaoishi mbugani hupatikana kusini mwa jangwa la Sahara; na 10% waliobaki duniani hupatikana hifadhi ya taifa Ruaha-Tanzania
Simba ndiye mfalme wa mbuga kutokana na sifa kuu tano za kipekee alizonazo japo leo nntataja tatu tu
- Muungurumo anaotoa simba dume, ile sauti inaweza kusikika maili tano(8km) kutoka sehemu alipo na hivyo kurahisisha mawasiliano na walio mbali na pia njia moja wapo ya kulinda himaya yake.
- Anashika nafasi ya kwanza kwa wanyama jasiri zaidi duniani, hivyo hatishiwi na kitu chochote.
- Ndevu nyingi na ndefu(mane) alizonazo simba dume zinazoanzia kidevuni hadi shingo inapoishia humfanya awe na muonekano wa kipekee miongoni mwa wanyama wa porini.
Pia simba huwasiliana kwa kugusanisha vichwa vyao na hapo hubadilishana harufu iliyobeba habari kuhusu shughuli aliyotoka kufanya simba huyo, hali zao pia ni njia mojawapo ya kuimarisha mahusiano yao.
Maeneo wanayopatikana kwa wingi:
Hifadhi ya taifa Ruaha, Serengeti, Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, ziwa Manyara-Tanzania, Luangwa ya kusini-Zambia, Etosha-Namibia, Masai mara-Kenya, Kruger-Afrika ya kusini na Okavango delta&Savuti-Botswana.
Ngazi ya uhifadhi:
Mwaka 1996-waliorodheshwa katika orodha nyekundu IUCN kama miongoni mwa wanyama waliohatarini kutoweka haraka mbugani (Vulnerable species), mnamo mwaka 2016-waliorodheshwa na CITEs Appendix II, hawatishiwi haraka zaidi kutoweka duniani japokuwa biashara haramu za wanyama pori zifungwe, ujangili uzuiliwe ili kuokoa maisha yao.
2. Chui
Chui ndie paka pekee barani Afrika wenye nguvu na uwezo mkubwa wa kupanda miti na mwenye uwezo mkubwa wa kuona usiku kuliko paka wengine hivyo humfanya kutokuonekana mara nyingi mbugani.
Rangi ya mwili; nyeupe na chungwa yenye madoa madoa meusi miguuni, mapajani na kichwani pia
Urefu; 65cm
Uzito; dume 60kg na jike 40kg
Mazingira; tofauti tofauti, misituni na kwenye milima
Chakula; nyama, saizi ya kati wanyama wenye kwato na wanyama wadogo wadogo
Usichokijua;
Chui ni wanyama wapekwe hukaa peke yao muda mwingi isipokuwa hukutana wakati wa kujamiiana na kukuza chui watoto.
Paka peke wapandao juu ya miti na kuwa na uwezo wa kupanda na windo(mnyama) lao juu ya mti hata kama ana uzito mara tatu zaidi yao pia wanauwezo mkubwa wa kuwinda wakiwa juu kwa mnyama aliye chini.
Wanapatikana maeneo yote jangwani na msituni hivyo kumewafanya kuweza kuishi mazingira mengi kwa jamii yao kwani hupatikana India, China, Asia ya kati na Afrika.
Chui hawatoi muungurumo kama samba isipokuwa hutoa sauti zenye ukali flani ambao mara nyingi hufanywa na mbwa na wakiwa na furaha sana hutoa sauti za chini zenye mwendelezo wa mtetemo miongoni mwao na hata wakati mwingine kuparua chini.
Chui ana uwezo mkubwa wa kuogelea hivyo humfanya kula samaki na mara nyingine hata kaa wa majini
Madoa yao huwapa ulinzi tosha kwani inakuwa ni vigumu chui kuonekana na mawindo yao hasa wanapokuwa juu ya miti.
Chui wanakula nyama tofauti tofauti kuanzia wadudu, panya, nyoka, mijusi ndege na jamii za wanyonyeshao.
Maeneo wanayopatikana kwa wingi: maeneo ya mfumo wa kiikolojia Serengeti Tanzania& Kenya, Sabi sands GR karibu na Kruger-Afrika ya kusini, Moremi-Botswana na Luangwa ya kusini nchini Zambia.
Ngazi ya uhifadhi:
Mwaka 2002-waliorodheshwa kama wanyama wasio hatarini kutoweka (Least Concern), mnamo mwaka 2008-namba yao ilionekana kupungua na kuorodheshwa kama baada ya miaka kadhaa mbeleni wangeingia kwenye wanyama walio hatarini kutoweka mbugani (Near Threatened) na mwaka 2016-hatarini kutoweka mbugani (Vulnerable species)
3. Tembo
Mnyama mkubwa pekee aliyebaki nchi kavu na anafahamika zaidi kwa utunzaji wake mzuri wa kumbukumbu, kama alishamshuhudia jangili kamwe hawezi msahau hata iweje. Tembo wa kiafrika anatofauti kubwa sana na wale wa India, kwani tembo wetu wana umbo kubwa zaidi kuliko wa India, masikio yao ni makubwa na manene yenye umbo kama ramani ya bara la Afrika pia wa Afrika wote wana ndovu ikiwa wa India ndovu ni kwa dume japokuwa baadhi ya majike wanazo ila ni ndogo na nyembamba.
Rangi ya mwili: kijivu na muda mwingi huwa na rangi ya udongo na tope ambalo hujimwagia kupunguza joto la mwili.
Uzito: dume 5750kg na jike 3800kg
Urefu: dume 3.50m na jike 3m
Mazingira: savanna
Chakula: magome ya miti, majani na nyasi kwa siku wanaweza kula nyasi 230kg na maji lita 150
Usichokijua:
Jua linapokuwa kali zaidi hujimwagia mchanga migongoi mwao na kichwani kuzuia ukali wa jua pia kutoa wadudu japo wanangozi nene ila wanatambua na kuhisi mdudu pale anapotembea
Katika jamii za wanyama wanyonyeshao, tembo huongozwa kwa kukaa a mimba muda mrefu usiopungua miezi 22 na kuzaa mtoto mmoja (japokuwa mara nyingine huzaa wawili ila ni mara chache sana) mwenye uzito 120kg pia waktai wa kuzaa tembo wengine hutengeneza duara kama ulinzi kwa mama na mtoto.
Mtoto wa tembo anazaliwa akiwa haoni na wakati mwingine hunyonya mkonga wake kama binadamu wanavofanya kunyonya vidole vyao.
Tembo hupendelea kuogelea na pia wana uwezo wa kuogelea kwa umbali mrefu na hutumia mikonga yao kuwaongoza kama fimbo ya dau, lakini mkonga ni mdomo wa juu ulioungana na pua kisha kurefu zaidi kama unavoonekana hutumika kunusa, kuchukulia vitu, kshika matawi ya miti na hata kujimwagia maji.
Tembo wana miguu yenye sponji chini kama godoro hivyo kuwafanya kuweza kutembea kimya ukiachana na uzito wa miili yao pia hutumika kama kifyonza milindimo ya kwenye ardhi
Ujirani mkubwa na undugu walionao unaendana na wa pimbi ambao ni wanyama wadogo wanaopatikana sana kwenye miamba na mawe makubwa.
Tembo ni binadamu wa pili mbugani, kwani hukutana kwenye kifo cha mwenzao na kumzika, mara nyingi kwa majani pia hukaa hapo kwa siku kadhaa kama ishara ya majonzi na huzuni.
Maeneo wanayopatikana kwa wingi: hifadhi nyingi za taifa-Tanzania, Chobe-Botswana, na Hwange-Zimbabwe.
Ngazi ya uhifadhi:
Mwaka 1996-waliorodheshwa wapo hatarini zaidi kutoweka mbugani(Endangered) na mnamo mwaka 2004- hatarini kutoweka mbugani baada ya idadi yao kuongezeka kidogo(Vulnerable)
4.Kifaru
Kuna aina mbili za faru wa Afrika ambao ni faru mweusi na faru mweupe japokuwa tofauti yao si kwenye rangi maana wote wanarangi ya kijivu. Faru weusi asili yao ni Afrika ya mashariki na wana mdomo wa juu ulio chongoka zaidi na kuwafanya kuchunga sana juu ya miti zaidi lakini pia faru weusi watoto wao hutembea nyuma ya mama zao wakati faru mweupe watoto hutembea mbele, ana midomo yote ilokaa sawa, uzito mkubwa kuliko faru mweusi na pia faru mweupe waliingizwa mbugani kutoka Afrika kusini.
Faru wote wana pembe mbili usoni ikiwa ya kwanza ni ndefu zaidi na zote zimezungukwa na vinyweleo hivyo sio pembe halisi kwa sababu huota juu ya misuli na sio kwenye mfupa, pia pembe zao zimeundwa na mchanganyiko wa seli kama zetu zinazopatikana kwenye nywele na kucha hivyo hakuna cha zaidi au ziada kuhusu matibabu yoyote.
Rangi ya mwili: kijivu japokwa hukolea na kuwa nyeusi hasa wakijiloanisha na matope.
Urefu:1.35-2.30m
Uzito: dume 2896kg na jike 800-1600kg
Mazingira: msitu wenye nafasi katikati ya miti(woodland)
Chakula: miti, majani ya miti, majani madogo madogo(forbs) pia nyasi
Usichojua:
Faru wote wana kwato tatu tofauti na wanyama wengine wenye kwato mbili na hivyo faru kuelekeana na farasi na pundamilia.
Hutumia muda mwingi mchana kupumzika na usiku hutumia kula hivyo kuwa wa kipekee kwa wanyama walao majani.
Makundi yao makubwa huitwa “crash” japokuwa mara nyingi hukaa peke yao. Mimba yao hudumu kwa miezi 15.5 na kuzaa mtoto mwenye uzito 35-50kg na kunyonya kwa muda wa miaka mitatu.
Faru wamegawanywa kisayansi kwenye jamii (species) nane lakini tatu tayari zimeshatoweka duniani na tano waliobaki wapo hatarini zaidi kutoweka na idadi yao ndogo hivyo wanahitaji zaidi uangalizi mkali.
Ukiachana na umbo lao kuwa kubwa wanauwezo wa kukimbia 50km kwa saa moja, hata hivyo wanategemea sana kunusa na kusikia maana macho yao yana uwezo mdogo wa kuona makadilio wanaona sawasawa na sungura waonavyo.
Faru huwasiliana kwa alama za harufu kama kurusha mikojo juu ya miti na vichakani karibu na maeneo ya kuchgunga na kunywa maji ili kurahisisha usambaaji wa taarifa na wakati mwingine hutumia kinyesi ambacho faru mwingine akiona anaweza tambua jinsia, na umri wa faru aliyeacha kinyesi hicho.
Maeneo wanayopatikana kwa wingi:
Ngorongoro, Serengeti na Mkomazi-Tanzania, nchi nyingine Namibia, Afrika ya kusini na Swaziland.
Ngazi ya uhifadhi:
Mwaka 1994-faru weupe wa kusini (Southern white rhino) waliorodheshwa kama baada ya miaka kadhaa mbeleni wangeingia kwenye wanyama walio hatarini kutoweka mbugani (Near Threatened).
Faru weusi (black rhinocerous) kipindi hicho pia waliorodheshwa kama wapo hatarini zaidi zaidi kutoweka mbugani (Critical Endangered) sababu namba yao ilipungua chini ya 5000 na kuandikwa kwenye CITEs Appendix I.
Faru weupe wa kaskazini (Northern white rhino) inaaminika wametoweka kabisa mbugani na kubaki watatu tu dume 1 na jike wawili ambao wapo chini ya uangalizi mkali nchini Kenya.
5.Nyati
Jamii ya ng’ombe pekee anayepatikana mbugani, pia wanachunga katika makundi makubwa kuanzia 100. Ni rahisi kumtofautisha na wanyama wengine kwa rangi yake nyeusi iliyokolea na pembe zake ndogo zilizojikunjia nje, nyuma na juu na kwa wale wasiopatikana msituni huwa na rangi ya wekundu uliochanganyika na hudhurungi.
Urefu: 1.4-1.7m
Uzito: dume 785kg na jike 715kg
Mazingira: msitu wenye nafasi(woodland) na maeneo yenye nyasi ndefu
Chakula: nyasi ndefu, majani na mashina ya miti
Usichokijua
Wanaishi pamoja kwenye makundi yasiyozidi 1000 na kundi hilo huundwa na majike na watoto, madume baada ya miaka 3 ya mwanzo huondoka, pia kupitia njia hizo wanaweza kupiga kura njia gani itumike kuelekea sehemu wanayokula.
Nyati ni mnyama pekee anayeongoza kuua wawindaji wengi inakadiriwa huua watu 200 kila mwaka hivyo kujizolea umaarufu na kuitwa kifo cheusi (black death/widow death)
Mnyama pekee ambaye hajawahi fugwa kutokana na hali yake isiyoeleweka wala kutabirika pia ukali alionao, mara nyingine anachanganywa na nyumu wa kimarekani.
Nyati hutumia njia ya mashambulizi pasipo kunyemelea hivyo kumnyima adui yake nafasi ya kuondoka na kupelekea vifo vya watu wengi hasa wawindaji maana pia nyati hutunza kumbukumbu na akiwaona lazima awashambulie
Nyati jike wana uhusiano mkubwa na wa karibu na inapotokea mmoja kavamiwa kundi zima humtetea mwenzao na mara nyingi wanaua samba na wanyama wengine wanaowawinda.
Anakunywa maji kiasi cha lita 40 kwa siku hivyo hupendelea kuwepo karibu na maji na huchukua simba kadhaa kumuangusha nyati mmoja.
Maeneo wanayopatikana kwa wingi:
hifadhi nyingi za taifa-Tanzania, Kruger-Afrika kusini, Hwange-Zimbabwe na Kafue-Zambia.
Ngazi ya uhifadhi:
Mwaka 2008-waliorodheshwa kama idadi yao ni kubwa hawapo hatarini kutoweka (Least Concern) japokuwa idadi yao ya kupungua inaongezeka kutokana na shughuli za kibinadamu na uharibifu wa mazingira.
Naamini umepata chochote kitu, jivunie kuwa mtanzania, nchi pekee yenye maliasili nyingi zaidi tazama wanyama wote hao wanapatikana nchini, mito na mabonde mengi ya nafaka, misitu ya ukanda wa pwani achilia mbali misitu ya mikoko, n.k. wewe kama mdau mzuri wa uhifadhi na utalii usiache kusema chochote kulinda uhifadhi wa wanyamapori hata vizazi vijavyo vikaone fahari kama tuonavyo.
Muhimu: Samahani kwa baadhi ya sehemu ambazo kidogo hazieleweki vizuri ni kutokana na umaskini wa lugha yetu ya Kiswahili kuwa na misamihati michache hivyo kwa mdau yoyote wa Baraza la Kiswahili Tanzania, naomba hili lifanyiwe kazi.
Makala hii nimetafsiriwa kutoka lugha ya kiingereza katika makala ya “Amazing facts about Africa’s Big five” iliyoandikwa na Landia Davies, mwezi Februari 11 2017 na makala nyingine “The Big five” iliyoandikwa na kampuni ya kitalii Shadows of Africa.
Imeandikwa na:
Leena Lulandala
+255 755 369 684
Mwanafunzi-UDSM.
Asanteni sanaaa,