Maisha, malezi, na mapokeo yana sehemu kubwa sana kujenga misingi ya maisha yetu, mawazo na vitu ambavyo vinapewa vipaumbele kwenye jamii zetu kamwe haviwezi kuachwa wala kusahaulika kirahisi. Maisha yanajumuisha mambo mengi kutoka kwenye jamii yetu, mambo mengi tuliyoridhi kutoka kwa wazazi wetu, ni mambo ambayo wazazi wetu nao wameridhi kutoka kwa wazazi wao. Kila nchi hapa duniani ina utamaduni wake, ina vipaumbele vyake kwenye maeneo mbali mbali ya maisha, na kila jamii ina vitu ambavyo inavikubali na kuviheshimu sana kama sehemu muhimu ya maisha yao. Vitu hivyo kwa kuwa vina historia ndefu sana kwenye jamii, huwa vinakuwa na mguso na huchukuliwa kwa hisia na jamii husika hivyo huwa sehemu ya utamaduni au imani yao.

Nchi ya China imekuwa inahusishwa sana na biashara za meno ya tembo na pembe za faru kwa miaka mingi.  Katika kujifunza na kufuatilia sana kuhusu wanyamapori, ujangili, biashara ya meno ya tembo, na biashara nyingine za wanyamapori nimegundua kwanini nchi ya China inapenda sana pembe za faru na meno ya tembo. Licha ya dunia kulia kila siku kuhusu ujangili wa tembo na faru, jambo hili haliwashtiui kabisa wachina. Hii ni kwasababu ya imani ya ndani sana waliyonayo kuhusiana na wanyama hawa. Jambo ambalo limesababisha kuenea kwa biashara haramu za meno ya tembo na pembe za faru.

Katika kujifunza mambo haya nimegundua kuwa nchi ya China tangu enzi na enzi, wao wanaamini na wana imani tofauti kabisa linapokuja suala la wanyamapori na sehemu za miili ya wanyamapori (nyara), kama vile, ngozi, mifupa, meno, kucha, manyoya, pembe, mikia, kwato na hata sehemu za siri za wanyamapori zimekuwa na matumizi makubwa sana katika nchi ya China, hii ni kutokana na imani na mtazamo waliojengewa na walioupokea kutoka kwa wazazi wao na jamii yao. Ndio maana nimeanza na utangulizi kuhusu jinsi malezi na mfumo wa maisha wa sehemu fulani unaweza kuwa ni utamaduni ambao watu wanauabudu kiasi cha kuwa tayari kuhatarisha maisha ili kuendeleza utamaduni huo.

Katika moja ya ripoti niliyoisoma inasema kuwa michirizi na mistari ambayo ipo kwenye pembe za faru huwaunganisha watu sehemu za ndani kabisa za mioyo yao. Kwa mantiki hiyo ni kwamba faru wana sehemu kubwa sana katika mahusiano yao, na hivyo pembe za faru kuwa na maana sana kwenye maisha yao. Lakini si hivyo tu, wanaamini pia katika kipindi cha zamani cha utawala wa kifalme kuwa endapo mapovu meupe yatatokea juu ya kikombe cha mfalme kilichotengenezwa na pembe za faru basi kinywaji hicho kitakuwa na sumu au kitakuwa ni sumu. Hii ndio maana wachina wanaendeleza sana mila na desturi hizi na wana mtazamo wa kipekee sana unaoungana na imani linapokuja suala la pembe za faru.

Lakini bado watu na watafiti wa mambo haya wanajiuliza kwa kwa nini China inafanya kila linalowezekana ili kumiliki na kununua pembe za faru hata kwa gharama kubwa, huenda ni kwasababu ya maandishi yaliyopatikana kwenye moja ya kitabu kikubwa sana kinachoelezea dawa za kienyeji kinachoitwa  Bencao Gangmu (Compendium of Materia Medica) kilichoandikwa na Li Shizhen mwaka 1597. Katika kitabu hiki ambacho kinaelezea kwa kina kuhusu dawa nyingi  za kienyeji kuna sehemu katika kitabu hiki kinaelezea jinsi ambavyo pembe za faru zinavyoweza kutibu magojwa mbali mbali kama vile maumivu ya kichwa, baridi, usaha, chunusi, kuondoa sumu mwilini, mshtuko wa moyo, presha na inaaminika kuwa na matokeo mazuri kama mtu anatumia kwa ajili ya kutibu kansa na inasemakana ukitumia inaondoa kila aina ya sumu zilizo ndani ya mwili wa binadamu.

Aidha kutokana na hali hiyo, kwenye miaka ya 1950 hadi 1960 watu wengi walipenda sana kutumia dawa za kienyeji kutibu magojwa yao, hali hii ilisababisha uhitaji mkubwa sana wa pembe za faru katika nchi ya China. Na kwa mujibu wa taarifa iliyopo kwenye ripoti ya ujangili na taarifa mbali mbali zinasema, zaidi ya tani 10 za bidhaa mbali mbali za pembe za faru ziliagizwa na nchi ya China kuingia ndani ya nchi, hii ilifanyika baada ya usimamishaji wabiashara ya pembe za faru na shirika la kimataifa linalosimamia na kutoa vibali vya usafirishaji wa wanyamapori na mimea mwitu iliyo hatarini kutoweka mwaka 1977. Na ilipofika karibia miaka ya 1990, China iliondoa kabisa pembe za faru kwenye orodha ya madawa ya kifamasia. Hivyo haitambuliki na wafamasia kama ni dawa kwa ajili ya kutibu maradhi ya binadamu.

Baada ya kusaini mkataba wa kimataifa unaosimamia biashara ya speshi za wanyamapori na mimea mwitu iliyopo hatarini kutoweka CITES mwaka 1990, China iliingiza wanyamapori waliotajwa kwenye Appendex kuwa katika wanyama wanaolindwa na kuhifadhiwa na taifa hilo, wanyamapori wanaolindwa sana na taifa. Baadaye kidogo mnamo mwaka 1993 serikali ya China ilitangaza kufuta na kufunga biashara zote za pembe za faru na mifupa ya tiger (tiger ni chui mkubwa mwenye milia). Hivyo ikatangaza biashara zozote zinazohusisha kununua, kuagiza au kubeba  faru na tiger ni biashara haramu na isiyotambulika kwa mujibu wa sheria za China, na hii ilihusisha kufungia matumizi yoyote ya wanyama hawa hata kama ni kwa kusudi la kitabibu au kwasababu za kifamasia.

Hatua hii ya China kufungia biashara zozote zinazohusisha faru na tiger ziliafikiwa na uongozi wa serikali ambao unasimamia masuala ya viwanda na biashara, na kufika mbali zaidi wakatoa tamko kali sana kwa mtu yeyote atakayekamatwa na pembe za faru au mifupa ya tiger, au bidhaa za wanyamapori na hapa walijumuisha mpaka meno ya tembo hawa au nanunua au anaagiza atahukumiwa adhabu ya kifo hapo hapo.

Lakini taarifa za kitafiti kutoka China zinasema, bado China inatiliwa shaka sana linapokuja suala la pembe za faru na bishara haramu za meno ya tembo kuliko nchi nyingine duniani. Kuna ushahidi uliofanywa na timu ya watafiti na wapelelezi wanaofanya kazi kwenye shirika la Elephant Action League (EAL), kuonyesha sehemu nyingi za China zinaendesha biashara hii, majimbo kama Guangdong, Guangxi, Yunnan, na Fujian yanahusika sana na biashara hii. Pia ni ukweli usiopingika kuwa pembe za faru hazitumiki tu kama dawa za kutibu maradhi, bali hutumika kama sehemu ya kutambulika na kuheshimika na jamii, na hutumika zaidi na wale ambao wamepata utajiri hivyo kuonyesha kuwa wao sio masikini tena na wapo kwenye ngazi ya utajiri, alama kubwa wanayoangalia ni umiliki wa pembe za faru au bidhaa, kitu kilichotengenezwa na pembe za faru.

Kwa vyovyote vile, iwe ni kwa masuala ya imani, dini, kitamaduni, mapokeo, kiuchumi, na hadhi katika jamii, hakuna uhalali wowote wa msingi ambao unatakiwa kuhitaji pembe za faru wala meno ya tembo. Mambo yote ambayo huitaji pembe za faru na meno ya tembo ni mambo ya kujifurahisha na sio ya msingi. Wakati nasoma ripoti na makala mbali mbali kuhusu mwenendo wa biashara hii nchini China na sehemu nyingine sijaona sehemu yoyote kwamba watu wamepoteza maisha yao kwa kukosa pembe za faru au meno ya tembo. Badala yake watu wengi wamepoteza maisha yao kwa kufanya ujangili na biashara haramu za meno ya tembo na pembe za faru.

Ndugu zangu waafrika na watu wa Asia, ambako mnatoa na kuua wanyamapori wenu kwa ajili ya kwenda kuwafurahisha watu waliovuka na kuingia kwenye utajiri, tunaua wanyama wetu kwa ajili ya watu kutengeneza midoli na vitu ambavyo havina msaada katika maisha. Hii isiwe sababu ya sisi kuruhusu mambo haya kuendelea kwenye hifadhi za wanyamapori na kwenye mbuga, au mapori ya akiba ambayo huifadhi wanyamapori hawa muhimu. Ukiangalia tangu mwanzo wa makala hii nimejaribu kukuonyesha namna ambavyo nchi ya China ilivyo na uhusiano na wanyamapori hawa, huwezi kukuta sababu zenye mashiko za kufanya wanyamapori hawa kukuwawa kikatili kwa ajili ya maslahi ya watu wachache.

Mambo haya niliyoandika katika makala hii ni muhimu sana kuyafikiria na kufahamu ni hatua gani za kuchukua, kwa wasimamizi wote wa maliasili, viongozi wa nchi, mataifa mbali mbali na wadau wote kwenye sekta hii, ni muhimu tukawa na sauti moja tu, ya kuhakikisha wanyamapori hawa ambao wapo hatarini kutoweka wanalindwa na wote wanaojihusisha na ujangili na biashara hizi haramu wanakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Aidha juhudi zetu ni muhimu pamoja na juhudi za kimataifa, tukishikana kwa pamoja kwenye jambo hili tutatatua changamoto hii kubwa, kwa mfano mwishoni  kabisa mwa mwaka 2017, China ilitangaza kufunga baadhi ya masoko na viwanda vya meno ya tembo. Hii ni hatua nzuri na inatengeneza unafuu kwasababu hali ya tembo wetu inaweza kurejea na kufikia kwenye kiwango cha kutia moyo.

Naamini China ilifikia uamuzi huu baada ya kupata mashinikizo kutoka mataifa mengine, lakini pia kutoka kwa wadau wa sekta hii waliotapakaa duniani kote, mchango wa kila mmoja wetu ni muhimu sana kwenye uhifadhi wa wanyamapori na misitu. Hivyo tushirikiane kwenye jambo hili.

Maisha Ya Wanyamapori Yapo Mikononi Mwetu Wenyewe.

Asante sana!

Hillary Mrosso

+255 683 862 481/ +255 742 092 569

hillarymrosso@rocketmail.com

www.mtalaam.net/wildlifetanzania