Katika maisha kuna viitu vya msingi sana ambavyo mtu akivikosa maisha yake yana simama, au anakufa. Vitu hivi vya msingi kwa binadamu ni muhimu sana kwa uwepo wa binadamu katika maisha ya sasa na maisha ya baadaye. Pia kwenye maisha ya binadamu kuna vitu ambavyo sio vya msingi mtu akivikosa maisha yake bado yanaweza kuendelea na hawezi kupungukiwa na kitu chochote. Na hii dhana ipo kwa kila kiumbe hai, kwamba kuna vitu ni vya muhimu kwa viumbe hai ili viendelee kuishi hapa duniani. Kwa mfano karibia viumbe hai wote mahitaji yao ya msingi ni maji, chakula, hewa na sehemu salama kwa ajili ya kijihifadhi na kupumzika, hivi ndio vitu ambavyo ukitoa kimoja maisha hayawezi kwenda.
SOMA HAPA KUJUA ZAIDI; Mwisho wa biashara halali ya meno ya tembo
Aidha, kwa jinsi maisha yalivyo na changamoto hakuna kitu ambacho kitatokea tu mbele yako kwasababu unakihitaji, kila kitu kinahitaji juhudi, nguvu na wakati mwingine ubishi ili kuweza kufanikisha maisha yako hapa duniani. Hii ni kanuni ya asili kabisa iliyowekwa na Mungu mwenyewe kwa viumbe wote, hakuna kiumbe hai hata awe mzuri kiasi gani ataletewa chakula mdomoni kama kinda la ndege, maisha yanahitaji kujitoa na kutumia nguvu na viungo ulivyopewa na Mungu ili kupata mahitaji ya msingi kwenye maisha. Hivyo uwepo wa changamoto za maisha haupo tu kwa binadamu bali upo kwa viumbe hai wengine, wanyamapori, ndege, samaki, na hata wadudu. Hivyo ili kuweza kutatua changamoto hizi tunahitaji kuwa wazima na wenye afya nzuri, nguvu na akili sawa. Fikiria kwa changamoto za maisha haya mtu akakukata mkono au mguu, lazima atakupunguzia ufanisi wako kwenye maisha. Ninacho maanisha hapa ni kwamba kuna sehemu za miili yetu ni muhimu kwa kuyakabili maisha, na kwa wanyama wetu ni hivyo hivyo, sehemu za miili yao ni muhimi sana ili kuyakabili maisha yao na changamoto nyingine za porini.
Kwa mfano mtu anapotoa meno ya tembo, hapo hamsababishii tu ulemavu bali anaua kabisa maisha yake. Meno ya tembo ni sehemu muhimu sana kwenye mwili wake kwa ajili ya kutafuta chakula, kujilinda na mambo mengine muhimu sana. Meno ya tembo yana matumizi na ni mahitaji ya msingi sana kwa tembo na sio kwa watu wengine. Sijawahi kusikia sehemu yoyote mtu amakufa kwa kukosa meno ya tembo. Hivyo kitu ambacho sio cha msingi kwenye maisha yako, kitu hicho ni anasa na hakina umuhimu kwako.
Mwanzo kabla ya kujifunza na kujua mambo haya nilifikiri meno ya tembo yana kazi kubwa sana kwa binadamu, nilifikiri wanatengeneza dawa labda zakutibia magonjwa nk. Lakini baada ya kujifunza na kufuatilia nimegundua jambo la ajabu sana,yani matumizi ya meno ya tembo ni kutengeneza mihuri na mapambo basi! Yani nilishangaa sana. Nchini China ambako ndiko masoko na bidhaa za meno ya tembo huuzwa kwa kiwango kikubwa imekuwa ni soko kuu la meno na bidhaa zake. Wachina wanatumia mihuri iliyotengenezwa na meno ya tembo kwa sababu eti inakaa muda mrefu bila kuharibika na ni imara, wachina wanatumia zaidi mihuri kuliko kuweka saini kwenye maaandishi yao, hiyo ndio sababu wanahitaji meno ya tembo.
SOMA HAPA KUJUA ZAIDI; Tumaini Kubwa Kwa Tembo Wa Afrika
Pia kwa wachina ukiwa na bidaa au kitu kilichotengenezwa na meno ya tembo, wanalichukulia kuwa ni jambo la kifahari na utajiri. Hivyo ndio maana wenye uwezo wa kununua na kutumia vifaa vya maeno ya tembo ni watu matajiri na familia zenye uwezo. Wanatumia kutengeneza mapambo mbali mbali ya ndani kama vile visanamu, vya watu, au vifaa kama vikombe, sahani. Na pia wanatumia kutengeneza mapambo ya kuvaa kama vile mikufu, hereni, pete nk. Hayo ndio matumizi makuu ya meno ya tembo huko China. Kwa kweli ukiangalia hayo matumizi utashangaa yalivyo hayana umuhimu, ni kwa ajili ya anasa na ufahari tu. Hivyo kwa sabau kama hizi kweli waanze kuua tembo wetu ambao wana umuhimu mkubwa kwenye nchi, na mazingira yetu?
Nimeandika makala hii kuhusu matumizi kwasababu watu wengi hufikiri haya meno yanavyogombaniwa na kuuzwa kwa gharama kubwa kiasi hicho yanafanya vitu vya maana. Jambo ambalo sio kweli, hayo nilioyataja ndio matumizi makuu ya meno ya tembo huko China na sehemu nyingine. Sasa msomaji wangu hembu angalia mwenyewe upime ili ujue kwanini dunia inakataa kabisa biashara hii ya meno ya tembo. Kuacha na kuzuia biashara hii haramu ya meno ya tembo ni jambo kubwa na muhimu sana kwenye maisha yetu na maisha ya wanyamapori hawa, ni kama vile mtu aliye amua kuacha kuvuta sigara. Ni jambo lenye tija sana kwa hifadhi zetu na kwa wanyamapori wetu na mazingira yake.
Nafikiri sasa rafiki yangu umeelewa na kujua matumizi hayo ya meno ya tembo kwa hao wanao yahitaji. Sasa kwa ufahamu huo utapata nguvu ya kupaza sauti yako kuwalinda na kuwatetea wanyamapori wetu popote pale ulipo, hivi ni vita vinavyohitaji ushiriki wa kila moja wetu.
Asante kwa kusoma makala hii, nakutakia siku njema, tukutane kwenye makala ijayo hapa hapa. Karibu sana.
Hillary Mrosso
Wildlife Conservationist
+255 683 862 481/+255 742 092 569
www.mtaalamu.net/wildlifetanzania