Ziwa Ngosi ni miongoni mwa vivutio vinavyopatikana nchini Tanzania. Ziwa hili ni la pili kwa ukubwa kati ya maziwa ya kreta barani Afrika baada ya ziwa lingine la kreta lililopo Ethiopia. Ziwa Ngosi linaakisi muonekano wa bara la Afrika katika upande wa Kusini, magharibi, kaskazini na mashariki pamoja na visiwa vyake vya Unguja na Pemba.
Ziwa Ngosi linapatikana kwenye milima ya Uporoto, wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya nyanda za juu kusini mwa Tanzania. Asili ya ziwa hili linatokana na mlipuko wa volcano. Hivyo ni ziwa tofauti na maziwa mengine kama Victoria , Tanganyika na Nyasa.
Ziwa ngosi lipo katika misitu ya Mporoto ambayo ilianza kuhifadhiwa tangu mwaka 1937. Msitu huu umetunzwa kwa dhamira ya dhati ya kutuhifadhi nvyanzo vya maji,mime ana Wanyama wa aina mbalimbali. Ili uweze kuliona ziwa hili kwa Pamoja na mandhari yake ya kuvutia ni lazima upande mlima wa Uporoto.
Ziwa hili lina uzuri wa kuvutia na wa kipekee utofauti na maziwa mengine. Ziwa hili ni lipo juu ya milima na katikati ya misitu. Lina urefu wa km 2.5, upana km 1.5 , kina chake ni mita 74 na lina ukubwa wa hecta 9332.
Upekee mwingine ni mwonekano wake unaofanana na ramani ya bara la Afrika. Ukiliona ziwa hili utastaajabu jinsi lilivyo dhahiri kama ramani ya Afrika pamoja na visiwa kama unguja na Pemba vinavyoonekana pia katika ziwa hili
Ujazo wa maji huwa haubadiliki kwa maana ya masika au kiangazi. Sababu inayopelekea kiwango cha maji kuto badilika ni kwamba ziwa hili halina mito inayoingiza wala kutoa maji. Inaaminika kuwa chanzo cha maji ya ziwa hili ni chini ya ardhi nay ana Ladha ya chumvi
Maajabu mengine katika ziwa hilo ni kwamba maji yake yana mwonekano wa rangi tofauti tofauti kila wakati. Kuna wakati ukifika unakuta ziwa lina rangi ya samawati , kijani au nyeusi . Hii ni kutokana na sehemu jua lilipo pamoja na uwepo wa msitu katika hifadhi hii. Kwahiyo jua linapomulika mionzi yake kwenye maji basi maji yanaakisi rangi ya uoto uliopo pembezoni mwa ziwa.
Pamoja na mandhari nzuri ya ziwa hili, pia kuna vivutio vingine kama vile ndege aina mbalimbali kama vile bata maji ambao hupenda kuogelea ziwani. Vile vile kuna Wanyama jamii ya mbega weupe na Weusi na wengineo wengi.
Imani juu ya ziwa Ngosi
Wanakijiji katika eneo hili ambao wana asili ya kabila la Wasafwa waliliita ziwa Ngosi au Ligosi kwa sababu waliona ni kubwa sana na kiimani ya kisafwa waliamini kwamba Mungu yupo huko na walikuwa wakija kufanya maombi ili mvua inyeshe.
Katika kabila lao, wao waliamini kuwa ni bwawa la ajabu kutokana na maji yake kuwa baridi juu na chini kuwa moto.
Pia maji ya ziwa hilo yaliaminika kuwa ni dawa ya ngozi, na watu walikuwa wakipaka wanapona ugonjwa wa ngozi kitu ambacho kuna ambao wanaamini hivyo mpaka leo.
Pia kuna hadithi mbalimbali za simulizi zinazohusisha ziwa hili. Ziwa Ngosi linasemekana limehama kutoka eneo la Mwakaleli mpaka katika hifadhi ya msitu Uporoto. Hii ilitokana na ziwa ngosi kuleta maafa ya vifo kwa watu wengi pamoja na mifugo katika ziwa hili na hivyo kupelekea wazee wa kimila kulihamisha ziwa hili kimila mpaka hifadhi ya mto Uporoto, lakini hizi ni simulizi za kale na haijathibitishwa kuwa ziwa hili lilihama.
Kwa sasa eneo hilo linatembelewa zaidi na wageni kutoka nje ya nchi na wanafunzi wa shule ambao wanafika hapo kwa wingi kwa ajili ya kujifunza. Hii ni fursa kwa wenyeji na watanzania kwa ujumla kutembelea ziwa Ngosi ili kuweza kufurahia na kujifunza zaidi pia kukuza utalii wa ndani na Mapato ya taifa kwa ujumla.
Asante sana kwa kusoma makala hii, naamini utapanga siku ya kuja kutembelea ziwa Ngosi ili ujionee maajabu ya ziwa hili.
Makala hii imeandikwa na Cecilia Mwashihava na kuhaririwa na Alphonce Msigwa. Kwa maswali, maoni, mapendekezo au ushauri kuhusu makala hii usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii.
Cecilia Mwashihava
+255 747 268 217
Mhifadhi wanyama pori