Kheri ya mwaka mpya 2021, mpendwa msomaji wa blog yetu! Naamini umzima na unaendelea vyema na majukumu mbalimbali ya kujikwamua kimaisha. Karibu tena tujifunze maeneo yaliyopo Tanzania yenye urithi mkubwa kidunia au kiulimwengu yaliyobeba umuhimu katika historia na mali asilia.
Utangulizi:
Urithi wa ulimwengu ni kitu au sehemu fulani iliyokidhi vigezo stahiki vilivyowekwa kwa makubaliano ya wawakilishi wa mataifa mbalimbi sehemu hiyo itwe inaurithi wa dunia. Tanzania ni miongoni mwa nchi 167 duniani zenye maeneo yenye umuhimu wa urithi wa kitamaduni au Urithi wa asili kama ilivyobainishwa na shirika la umoja wa mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO) chini ya sheria zake zilizoanzishwa mwaka 1972. Maeneo yenye sifa za Urithi wa dunia, yalianzishwa kwa lengo la kuhakikisha Kuna ulinzi tosha katika tamaduni na maliasili zote zilizopo katika hatari ya kupotea na pia kuhakikisha kuna maendeleo endelevu yatokanayo na utalii wa vitu hivyo.
Kwa takwimu zilizoorodheshwa na Katharina Buchholz (Dec, 2020) pamoja na tovuti ya Starista Kuna jumla ya maeneo yenye Urithi wa dunia 1121. Ikiwa 209 ni yenye Urithi wa kiasilia na 842 yenye Urithi wa kitamaduni na yenye umuhimu kwenye historia. Tovuti ya riviera travel imetolea ufafanuzi na uchambuzi zaidi na kubainisha nchi ya China na Italy ndizo zinazoongoza kwa kuwa na maeneo mengi zaidi yanayokaliwa kuwa 55 kwa kila nchi. Na pia imetambulisha maeneo 10 mazuri zaidi kuyatembelea ikiwa ni pamoja na hifadhi ya Yellowstone iliyopo nchini Marekani, ukuta mkubwa wa China (Great wall), makaburi na majengo ya zamani ya Nubia nchini Misri na Cape Floral iliyopo Afrika kusini.
Tanzania iliipitia sheria hiyo na kuipitisha mnamo mwaka 1977 na kufanya maeneo yakemengi ya kihistotia kuwa na sifa na kuongeza idadi ya maeneo yenye urithi wa dunia. Mpaka Sasa Tanzania ina maeneo hayo Saba japokuwa mawili kati ya hayo yanapeperusha bendera ya kuwa hatarini kutoweka, kuharibika na kuhitaji ulinzi wa ziada. Maeneo hayo ni kama ifuatavyo:-
1. Eneo la hifadhi ya Ngorongoro
Eneo hili lilitambulika Kama eneo la Urithi wa dunia lenye umuhimu kitamaduni na mali asilia mnamo mwaka 1979 mkoani Arusha. Eneo hili la uhifadhi linajumuisha kreta ya Ngorongoro yenye wanyamapori wengi na baadhi yao ni wale walio hatarini kutoweka duniani. Na wanyama hao wamekuwa na mwingiliano wa moja kwa moja na binadamu jamii ya wamaasai. Pia katika eneo hili kuna kaldera kubwa zaidi duniani na maeneo mengine tofauti tofauti yenye historia ya binadamu wa kale ikiwemo ile yenye fuvu la binadamu wa kale pamoja na nyayo za watu wa kale.

2. Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Magofu haya yalitambulika kama Urithi wa dunia mnamo mwaka 1982 katika maeneo ya Kilwa Kisiwani, mkoani Mtwara. Magofu haya yalimilikiwa na bandari ya mji wa waarabu wakati huo wakiwa kama watawala wa pwani ya Afrika Mashariki katika karne ya 13. Hivyo magofu haya kubeba Urithi wa kihistoria zaidi juu ya utawala wa kiarabu katika mwambao huo wa Afrika Mashariki. Magofu ya Kilwa Kisiwani yanapeperusha bendera ya kuwa miongoni mwa maeneo ya Urithi wa dunia yaliyo katika hatari zaidi kuharibika ikisababishwa na muendelezo wa uharibifu wa binadamu na kiasilia.

3. Hifadhi ya Taifa Serengeti
Eneo hili la hifadhi ya Taifa Serengeti liliingizwa kwenye orodha ya maeneo yenye urithi wa dunia mnamo mwaka 1981 likiwa katika mikoa ya Arusha na Mara. Hifadhi hii imebeba Urithi mkubwa kwa upande wa maliasilia husunani makundi makubwa ya jamii ya wanyama wanaohama hama kila mwaka kutokea Tanzania kwenda Kenya na kurudi umbali wa takribani kilomita 1000.Hifadhi hii inamchanganyiko wa udongo wenye asili ya volkano ambao umeifanya kuwa miongoni mwa mifumo bora duniani ya kiikolojia na hivyo kuzalisha mimea mbalimbali ambayo hutumiwa na wanyama. Lakini pia hifadhi hii inahifadhi wanyama wengi pamoja na wanyama wakubwa watano ambao ni tembo, Faru, nyati, simba na chui.

4. Pori la akiba la Selous
Eneo hili linatambulika kama Urithi wa dunia tangia mwaka 1982 likiwa chini ya mikoa ya Morogoro, Mtwara, Lindi na Iringa. Kabla ya kugawanya pori hili na sehemu yake kuwa hifadhi ya taifa ya Nyerere na pori la akiba la Selous lilikuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 km ikiwa sawa na asimilia tano ya jumla ya eneo la mraba la nchi. Eneo hili linabeba umuhimu mkubwa katika Urithi wa kiasilia hasa jamii nyingi za mimea tofauti tofauti na wanyama wakubwa. Kutoka na kushamili kwa uwindaji haramu wa Tembo katika eneo hili miaka ya 2014 ilipelekea kuingizwa kwenye orodha ya maeneo ya Urithi wa dunia yaliyo katika hatari zaidi kuharibika na kupotea.

5. Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.
Eneo hili la hifadhi ya taifa ya mlima Kilimanjaro liliongezwa kwenye orodha ya maeneo yenye urithi wa dunia mnamo mwaka 1987 mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kuhifadhi na kutunza mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu zaidi Afrika wenye asili ya volkano. Mlima huu wenye umaarufu wa kuwa na barafu inayooneka nyeupe kwa mbali katika vipindi vyote vya mwaka. Pia chini/ kitako Cha mlima Kuna jamii za wanyama wakubwa tofauti tofauti ambao baadhi wapo hatarini kutoweka kama tembo.

6. Mji mkongwe wa Zanzibar.
Eneo hili lilitambulika kama eneo lenye Urithi wa dunia kwa upande wa historia mnamo mwaka 2000 likiwa visiwani Mashariki ya Tanzania bara. Eneo hili linabeba historia ya mwingiliano mkubwa wa tamaduni tofauti tofauti ambazo zimepelekea ukuaji wa mji huo kwa karne nyingi. Hata hivyo mji mkongwe bado una masalia ya watu wenye asili ya Kiarabu, Kiajemu, Kihindi na tamaduni za Pwani. Eneo la mjini mkongwe bado lina peperusha bendera ya mji mkuu wa tamaduni za kiswahili.

7. Eneo la Kondoa lenye michoro kwenye miamba
Eneo hili lilitambulika kama eneo lenye urithi wa dunia hasa likiwa na umuhimu kihistoria kwa jamii za binadamu walioishi miaka 2000 iliyopita wenye asili ya uwindaji, mnamo mwaka 2006 likiwa katika wilayani Kondoa, mkoani Dodoma. Michoro hiyo imetawanyika katika maeneo mengi yaliyokaribu na bonde la ufa, na kuwa na taarifa nyingi za kihistoria zinazohusu mabadiliko na maendeleo ya binadamu wa kipindi hicho walichotegemea zaidi uwindaji.

Hitimisho:
Ukiacha maeneo mawili ambayo ni pori la akiba la Selous na magofu ya Kilwa Kisiwani kuwa maeneo yaliyo hatarini zaidi kuharibika na kupoteza sifa ya kuwa maeneo ya urithi wa dunia. Bado Kuna changamoto zinazokabili maeneo mengi na zisipotatuliwa kwa wakati idadi ya maeneo yaliyo hatarini kutoweka yataongezeka. Changamoto hizo ni pamoja na uelewa mdogo na hafifu wa maeneo yenye urithi wa dunia kwa kundi kubwa la watu, watu wengi nchini kutokuwa na tabia ya kutembelea maeneo yaliyohifadhiwa, ujangili, ungezeko kubwa la idadi ya watu, kuchora michoro kwenye baadhi ya majengo ikiwa ni tofauti na taratibu za uhifadhi wa majengo hayo,na ulinzi mdogo katika maeneo hayo. hivyo kuharibiwa na binadamu imekuwa rahisi sana na baadhi ya watu kutupa taka taka hovyo hivyo kutokuwa na mvuto
Kupitia changamoto hizo, serikali kwa ujumla wake kuanzia ofisi ya waziri mkuu idara ya mazingira, wizara ya maliasili na utalii, taasisi zote zinazohusika katika kusimamia maeneo haya ikiwemo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori (TAWA) pamoja na wadau mbalimbali wa utalii na Uhifadhi waunde vikundi maalumu vya kusimamia maeneo yenye urithi wa dunia ikiwemo katika upande wa mawasiliano, kuelimishaji jamii, utalii, wafuatiliaji wa ukiukaji sheria pamoja na ulinzi ili kuweza kuzitatua changamoto hizo mapema na kudumisha maliasili zote za nchi yetu na zile zenye urithi wa kidunia.
Asante sana kwa kusoma Makala hii, iliyoandikwa na Leena Lulandala na kuhaririwa na Alphonce Msigwa ambaye ni mwikologia hifadhi za taifa Tanzania.
Kwa maoni, ushauri au maswali kuhusu Makala haya, usisite kuwasiliana na mwandishi kwa mawasiliano hapo chini.
Leena Lulandala.
Email: lulandalaleena@gmail.com
Simu: 255 755 369 684


Habari yako ndg Mhariri na Mwandishi wa Makala hii ya Leo kuhusu World Heritage Sites-UNESCO nchini Tanzania.
Nakushukru sana kwa makala nzuri yenye mafundisho kemukemu kuhusu Maeneo hayo adimu na ya muhimu katika Sekta ya Utalii nchini kwetu.
Nipende kukuomba kuendelea kutupatia vitu vipya kila siku vitakavyotupatia maarifa na ujuzi zaidi hasa sisi Wanazuoni wa Kozi za Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori hapa Tanzania.
Ahsante sana.
Tunashukuru sana John, karibu na endelea kufuatilia blog hii ina makala nyingi na zitaandikwa makala nyingi nzuri sana kuhusu uhifadhi na mambo mengi kwa ajili kujifunza na kuelimisha. Tunashuru sana kwa feedback
Keep it up my friend
Asante sana Tecla, karibu sana
Asante sana kwa makala nzuri, hakika nimejifunza vitu vingi.
Tunashukuru sana Vero, karibu sana tuendelee kujifunza
Your article helped me a lot, is there any more related content? Thanks!