Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya wanyamapori ikiwa kama vile kitoweo, urembo, maonyesho, mavazi na dawa za kienyeji. Vile vile wanyamapori wamekuwa wanatumika katika masuala mazima ya  kiimani na tamaduni za watu mbalimbali duniani. Kila kona ya dunia ambapo wanyamapori wanapatikana, wamekuwa wanahusishwa na matumizi mbali mbali kulingana na tamaduni za watu wa eneo hilo. Mfano, nchi nyingi za Afrika, hutumia wanyamapori kama kitoweo, na mambo ya kiimani, lakini katika nchi za Ulaya, Asia na Marekani, wanyamapori wanatumika kama biashara, mavazi, urembo, chakula, na dawa.

Matumizi yaliyopitiliza ya wanyamapori ni hatari katika mifumo ya kiikolojia ambayo kwa kiasi kikubwa hutegemeana. Tishio hili kubwa ni  kwasababu idadi kubwa ya wanyamapori inaendelea kupungua na wengine kuendelea kutoweka kabisa katika uso wa dunia. Licha ya hayo, kuongezeka kwa matumizi ya wanyamapori inaenda sambamba na kushamiri kwa biashara haramu ya wanyamapori. Biashara ya wanyamapori ni janga jingine kubwa katika sekta hii kwasababu sio tu biashara haramu ya wanyamapori inasababisha kupungua kwa idadi yao bali pia inachangia kusambaa na kuenea kwa magonjwa kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa binadamu au kutoka kwa binadamu kwenda kwa wanyamapori

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu sehemu nyingi duniani, imepelekea hata mahitaji na matumizi ya wanyamapori kuwa makubwa. Mfano, utafiti wa hivi karibuni unaonyesha kuwa kati ya kaya 7978 zilizohojiwa katika nchi 24 za bara la Afrika, Marekani na Asia imebainika kuwa 39% ya kaya hizo huwinda wanyamapori angalau mara moja  kila mwaka kwa ajili ya kitoweo. Kwa namna yoyote ile matumizi haya ya wanyamapori ni makubwa kiasi cha  kuchangia kwakupungua kwa aina za wanamapori ambao wanatumiwa kama kitoweo.

Pamoja na hayo, tafiti zinaonyesha wazi madhara makubwa yanayosababishwa na uwindaji na matumizi ya wanyamapori kama kitoweo kwa wanadamu. Baadhi ya madhara hayo ni kama vile kupungua na kutoweka kwa baadhi ya spishi muhimu za wanyamapori, uharibifu wa mazingira, mabadiliko ya tabia nchi, ukame na kuenea kwa magonjwa yanayoambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu, au kutoka kwa binadamu, au mifugo kwenda kwa wanyamapori.

Magojwa kutoka kwa wanyamapori ni janga kubwa  katika nyakati hizi ambazo kuna mwingiliano mkubwa wa wanyamapori na wanadamu. Mfano, sehemu nyingi zenye rasilimali za wanyamapori kumekuwa na upanuzi mkubwa wa mashamba na maeneo ya makazi, kuingiza mifugo kwenye maeneo ya wanyamapori, mabadiliko ya matumizi ya ardhi, uwindaji wa wayamapori, kuchoma moto hovyo sehemu zenye makazi ya wanyamapori n.k

Tangu miaka ya 1940, kumekuwa na kesi nyingi za kutokea kwa magonjwa ya kuambukiza kutoka wa wanyamap kwenda kwa binadamu . Tafiti zinzonyesha hali ya hatari zaidi katika kipindi hiki kwasababu mwingiliano umekuwa mkubwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu hasa kwenye maeneo yenye rasilimali hizi. Utafiti wa hivi karibuni wa Lauren Coad na wenzake umebaini kuwa 70% ya magonjwa ya kuambukiza ya yemetoka kwa wanyamapori. Miongoni wa wanyamapori hao ni pamoja na wale wa jamii ya nyani, popo, jamii ya swala, nyati na viboko.

Matumizi ya nyamapori kama chakula, biashara au mapambo yamekuwa yakihusishwa na kusababisha milipuko ya magonjwa mabaya. Magonjwa hayo ni pamoja na Ebola, UKIMWI, mafua ya ndege, COVID-19, homa ya bonde la ufa, kichaa cha mbwa, kimeta nk. Magonjwa haya yameua watu wengi na  hivyo kuwa na umuhimu wa kuelimisha jamii juu ya magonjwa haya.

Picha na Angel Betsaida B. Luguipo; Ikionyesha mwingiliano mkubwa wa wanyamapori, mifugo na binadamu, picha hii ni mfano tu wa somo la makala hii, ili kila anayeisoma aelewe mzunguko na mwingiliano uliopo pamoja na hatari ya maambukizi.

Hata hivyo, wanyamapori kama popo, kakakuona, na wanyama jamii ya nyani, wametajwa sana kwenye tafiti nyingi kuwa wanaweza kubeba vimelea na virusi hatari ambavyo vinaweza kuleta madhara makubwa kwa afya ya binadamu. Kwenye maeneo mengi ambako wanyamapori hupatikana kunaweza kuwa na hatari zaidi kutokana na mwingiliano kuwa mkubwa. Hata hivyo, matumizi ya nyamapori katika maeneo ya mijini na vijijini ni makubwaa. Katika hali kama hii, wengi wanapata magonjwa kwasababu mara nyingi hushika nyamapori au sehemu za miili hiyo kama vile damu, nyama, manyoya, ngozi na maji maji mengine kutoka kwa mnyama bila kutumia kinga za mikono (gloves). Lakini pia watu wanaweza kupata magonjwa hayo kwa kula nyamapori ambayo hajaandaliwa vizuri kwa maana ya kupika au kuchoma.

Hata hivyo, kumekuwa na wasiwasi mwingi kuwa huenda wanyamapori wanabeba vimelea vya magonjwa hatari zaidi. Wasiwasi huu ni kwasababu wanyamapori wengi bado hawajafanyiwa tafiti za kutosha hasa kwenye eneo la magonjwa yanayoambukiza.

Nitoe rai kwa kila mtu kujua kuwa wanyamapori wanaweza kubaba magonjwa na vimelea au virusi vya magonjwa hatari, hivyo tusipendelee kuwashika au kula nyamapori ambayo haijapimwa na dakatari. Kwa wale wanaoingia porini kuwinda wanyamapori ndio wapo kwenye hatari kubwa zaidi maana uwezekano ni mkubwa wa kupata magonjwa kutoka kwa wanyamapori.

Tuwaache wanyamapori kwenye maeneo yao ya asili, tusiwaingilie wala kuharibu makazi yao ya asili, maana kwa kufanya uharibifu tutaleta majanga mabaya ambayo yatatusumbua. Tusikubali kuingia kwenye biashara haramu za wanyamapori au nyara, hii pia ni hatari.

Naamini kufikia hapa umepata elimu ya kukusaidia kuhusu wanyamapori na magonjwa ambayo wanaweza kumuambukiza binadamu na endelea kujifunza na kuwashirikisha wengine makala hii ili nao wajifunze.  Kwa pamoja tuungane kulinda na kwalinda wanyamapori wetu na mazingira yao.

Shukrani za pekee ziende kwa Alphonce Msigwa, aliyehariri makala hii. Kama una maoni, maswali, mapendekezo, usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii, kwa mawasiliano hapo chini.

Imeandikwa na Hillary Mrosso, +255 683 862 481, hmconserve@gmail.com