Habari Rafiki yangu, naamini umekuwa na siku nzuri naya kipeke sana, leo katika makala ya wanyamapori nimetamani nikushirikishe mambo muhimu 18 ambayo yalipendekezwa na watalaamu wa ripoti tuliyoisoma, THE GLOBAL TRAFFICKING OF PANGOLINS: A comprehensive summary of seizures and trafficking routes from 2010–2015. Mambo haya ni hatua muhimu sana zinaweza kutusaidia na sisi kuchukua hatua muhimu katika uhifadhi wa kakakuona na wanyamapori wengine.
Baada ya kujifunza na kuchambua yale ya muhimu katika ripoti hii, ni vema tukajifunza na mapendekezo yaliyotolewa na wataalamu katika kukabiliana na changamoto hii ya ujangili wa wanyamapori hawa.
- Nchi zote ambazo zimehusishwa na zinajihusisha na biashara haramu ya kakakuona wanatakiwa waangalie tena kwa upya na kubadilisha pale inapobidi sheria na taratibu zao za ndani wanyamapori na makubaliano yao katika biashara za kimataifa za spishi za wanyama na mimea mwitu ambayo ipo hatarini kutoweka duniani, CITES. Lengo la kufanya mapitio ya sheria hizo ni kuhakikisha kuwa kunakuwa na utaratibu wa sheria unaotoa ulinzi na uhifadhi wa spishi zote nane za kakakuona.
- Mamlaka za serikali, mamlaka za usimamizi wa wanyamapori, na pia mamlaka za kisheria za Nchi zote ambazo zimetajwa na ripoti hii kujihusisha na biashara haramu zinatakiwa kupewa nguvu ya ziada ili kufanya kazi yao kwa ufanisi. Pia watalamu wamependekeza nguvu kubwa iwekwe kwenye nchi ambazo hazina madhara makubwa ya uhalifu na uasafirshaji wa bidhaa za kakakuona, nchi hizo ni Lao PDR, Nigeria, Myanmar, Cameroon, Guinea, Mexico, the Philippines, Pakistan, Liberia, Equatorial Guinea, Cote d’Ivoire, Ethiopia, Kenya, Singapore, Mozambique, and Togo. Kwa kufanya hivyo itasaidia sana kuhifadhi wanyamapori hawa na mazingira yake.
- Mamlaka za usimamizi, na mamlaka za kisheria za nchi zote zilizojihusisha na biashara haramu ya kakakuona zinatakiwa kutumia njia za kiintelijensia na kiupelelezi katika kuchunguza miendendo yote, njia zote na vituo vyote vya usafirishaji ili kubaini na kuweka ulinzi na usimamizi imara ili kuzuia kushamiri kwa biashara ya kakakuona na wanyamapori wengine. Pia kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote waliokiuka sheria zao na sheria za CITES.
- Uchunguzi wa kitelijensia unatakiwa kuchunguza sehemu ambako kakakuona hutoka, yani chanzo, njia ambazo hutumiwa zaidi, nchi ambazo hutumika kusambaza na pia nchi ambazo ni masoko ya kakakuona. Hii ni kwa sababu watu wanaofanya biashara hii haramu wana mbinu nyingi ili wasikamatwa na pia kila mwaka wanabuni njia nyingine mpya ya kusafirishia bidhaa zao haramu, hivyo mamlaka za uchunguzi zinzatakiwa kuelewa hilo na kujipanga.
- Ushirikiano na mamlaka nyingine ni muhmu sana katika mapambano haya, idara za wanyamapori, mamlaka za kipolisi, masharika ya usimamizi na ulinzi ya nchi mbalimbali yanatakiwa kushirikiana kwa karibu hasa kuweka ulinzi kwenye vituo vya usafirishaji, kama mipakani, viwanja vya ndege, bandarini na sehemu zote ambazo zinaweza kukisiwa kutumika kama njia za kusafirishia biashara haramu. Kwa nchi kushirikiana ni rahisi kukabiliana na tatizo hili na kulimaliza.
- Waendesha mashtaka, majaji na mahakama zinazojihusisha na kuendesha kesi za kakakuona zinatakiwa kuwa na taarifa sahihi za wakati katika kufanya maamuzi, wanatakiwa kufahamishwa mabadiliko yoyote ya sheria za usimamizi wa spishi za kakakuona na wanyamapori kwa ujumla ili waweze kutekeleza kazi zao za hukumu kwa wakati na kwa usahihi.
- Biashara haramu ya kakakuona inatakiwa kuchukuliwa kwa uzito kama uhalifu wa maliasili na pia utoaji wa adhabu kali kwa wahusika katika uhalifu wa wanyamapori hawa inatakiwa iwe kubwa ili kutoa funzo kwa wengine wenye nia ya kujihusisha na kazi hiyo haramu, Zimbabwe imekuwa mfano mzuri kwenye mampambano haya.
- Utafiti wa kiteknolojia unatakwa kuanza kutumika ili kubaini nchi ambazo kakakuona wanatoka, hii itasaidia sana katika kupata taarifa muhimu za nchi ambazo wanyama hawa huvunwa mara kwa mara, pia taarifa hizo zitasaidia sana katika kuweka ulinzi na usimamizi kwa spishi hizi za kakakuona.
- Mamlaka za usimamizi na ufuatiliaji za CITES zinatakiwa kushirikiana na kuboresha taarifa zote za kukamatwa au kushikiliwa kwa nyara za kakakuona, hii itasaidia sana kuwa na taarifa za uhakika na za kweli katika usimamizi na uhifadhi wa kakakuona.
- Utoaji wa taarifa zinazohusiana na kakakuona unatakiwa uendelee kufanyika na CITES, masharika binafsi, watafiti binafsi na watu binafsi hii itasaidia sana kuwa na taarifa za kutosha kutoka sehemu mbali mbali.
- Nguvu ya ziada inatakiwa kutumika katika kutoa elimu na uelewa kwa watumiaji wa kakakuona na wale wanaojihusisha na biashara hii, hii itasaidia kupunguza mahitaji ya kakakuona kwa nchi ambazo zinaagiza au zinawateja wa bidhaa za kakakuona.
- Mamlaka za usimamizi wa sheria na ulinzi za nchi ambazo zimepewa kipaumbele katika kupambana na biashara haramu ya kakakuona wanatakiwa kuwapa uelewa maafisa wao kuhusu kakakuona, biashara haramu zinazohusisha kakakuona na mbinu za kukabiliana na changamoto hiyo.
- Kwa kuwa inafahamika kuwa nchi za bara la Asia zina mahitaji makubwa ya kakakuona na pia inafahamika pia kuwa mahitaji yao ya kakakuona yanachochewa na nini. Kazi kubwa bado inatakiwa kufanyika kwa nchi ambazo zina uhitaji mkubwa wa kakakuona nchi kama Marekani na Uholanzi, ni nchi ambazo kuna mengi hayafahamiki sana kuhusu kichocheo cha kuhitaji kisi kikubwa cha bidhaa na viungo vya kakakuona. Hivyo katika mapendekezo haya imeshauriwa watafiti kufanya utafiti wa kina ili kubaini vichocheo vikuu vya kushamiri kwa biashara hii haramu ya kakakuona katika mataifa hayo ya Marekani na Uholanzi.
Naamini kufikia hapa utakuwa umejifunza kitu kikubwa kwenye mapendekezo haya muhimu, ni kazi yetu kuanza kufanyia kazi mapendekezo ya ripoti hii muhimu.
Ahsante sana!
Hillary Mrosso
255 683 862 481