Kisiwa cha Mafia kinachopatikana Tanzania ni miongoni mwa visiwa maarufu sana duniani. Kisiwa hiki chenye ukubwa wa kilometa za mraba 435, kimekuwa maarufu sio kwasababu ya jina lake kuwa la kutisha au kuleta taswira zinazohusisha umafia, la hasha! Sifa na umaarufu wa kisiwa hiki unatokana na mandhari nzuri ya mazingira, uoto wa asili na hali nzuri ya hewa. Kisiwa hiki kina kila sifa ya kuwa maarufu duniani, watalii kutoka sehemu mbali mbali duniani hufika hapa kwa ajili ya kuogelea, kupumzika kwenye fukwe safi zenye mchanga mweupe unaovutia. Kisiwa cha Mafia sio tu sehemu ya kufurahia fukwe nzuri, bali pia unaweza kuona aina nyingi za ndege, wanyama kama vile tumbili, viboko na kasa wakitaga mayai na shughuli za uvuvi zinazofanywa na wakazi wa kisiwa hiki.
Licha ya sifa zote hizo, bado kisiwa hiki kinaendelea kuwa sehemu bora sana ya utalii kutokana na aina nyingi za samaki. Hivi karibuni, kisiwa hiki cha Mafia kimeendelea kujizoelea umaarufu mkubwa kutokana na aina za samaki wanaopatikana kisiwani hapo. Na moja ya samaki hao waliochangia umaarufu katika kisiwa hiki ni uwepo wa samaki aina ya papa. Samaki huyu aina ya papa potwe (Whale shark), jina lake la kisanyansi ni Rhincodon typus, ametokea kupendwa sana sio tu na watalii wanaofika kisiwani hapa, bali hata wenyeji wa kisiwa hiki. Sifa kubwa ya samaki huyu ni upole na rafiki wa kila mtu, hii imepelekea wenyeji wa kisiwa hiki kumpa jina la papa mwema.
Uwepo wa papa potwe katika kisiwa hiki, umefungua milango kwa watalii, wanasayansi na hata watafiti wa masuala ya uhifadhi wa Bahari kuja kutafiti sifa, tabia, ikolojia na mambo mengine mengi kuhusu samaki huyu. Watafiti wamewahi kuripoti kuwa Papa potwe kwa wastani huweza kukuwa na kufikia urefu wa mita 18 sawa na futi 59. Papa potwe wa jinsia ya kiume huwa na urefu wa mita 8 mpaka mita 9 na jinsia ya kike huanzia mita 14 mpaka mita 22, na uzito kuanzia tani 20 hadi 34. Lakini pia wana uwezo wa kuishi mpaka kufikia miaka 70 ikiwa hatakumbana na sababu nyingine zitakazo sababisha kifo chake kama uvuvi haramu au majeraha yanayosababishwa na boti zinazoenda kasi.
Shirika la Utangazaji la BBC limewahi kuandika na kuripoti makala iliyohusu Papa potwe wa kisiwa cha Mafia mnamo Mei 19, 2018 na kudai kuwa Papa potwe ni Miongoni mwa Samaki ambao wako hatarini kutoweka Duniani (Endangered species) kutoka kwenye orodha ya IUCN Redlist kutokana na sababu mbalimbali. Kutokana na Hali hii Papa potwe hawapatikani duniani kote isipokuwa katika kisiwa hiki cha Mafia, Mexico na Ufilipino. Licha ya hayo Papa potwe wa kisiwa hiki cha Mafia wamekuwa maarufa sana na hii imevutia watalii wengi duniani kutembelea kisiwa hiki kujionea maajabu ya samaki huyu. Uhifadhi wa Mazingira ya bahari ni muhimu sana katika kuweka misingi bora ya kufikia uchumi wa bluu kwa kujipatia kipato kitokanacho na uwepo wa mariasili muhimu katika Mazingira ya Bahari hususani katika kisiwa hiki cha Mafia, hii inahusisha si uhifadhi tu wa papa potwe bali aina zote za samaki, kasa na mimea mbalimbali inayopatikana baharini na kando kando ya bahari , mfano miti ya mikoko ambayo ni muhimu sana katika kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kupunguza kiasi cha hewa ya ukaa angani.
KWANINI PAPA POTWE HUPATIKANA MAFIA PEKEE KWA WINGI?
Watu wengi wamekuwa wakijiuliza maswali mengi kuhusu uwepo wa Papa Hawa katika kisiwa cha Mafia ukilinganisha na sehemu nyingine duniani. Lakini ukweli ni kwamba kisiwa cha Mafia imekuwa ni zaidi ya nyumbani kwa Samaki hawa na kuwa maarufu (Iconic species). Papa potwe hupendelea kukaa sehemu yenye uwepo wa chakula cha kutosha (planktonic foods) na Mara nyingi chakula kinapopungua huzama chini zaidi na hawaonekani vizuri kirahisi hasa kwa watalii wanaofanya utalii wa picha. Lakini kisiwa cha Mafia kimekuwa na uzalishaji mkubwa wa chakula hiki ambacho kinawavutia Samaki hawa na kuifanya sehemu hii ya Mafia kuwa makazi yao ya kudumu.
Japokuwa kisiwa cha mafia kimekuwa nyumbani kwa Papa potwe Lakini hawaonekani majira yote, Kuna muda huwezi kuwaona kirahisi mpaka uzame baharini na Kuna majira ambayo mtu hahitaji kuingia baharini ambapo huweza kuonekana hata mtu akisimama ufukweni. Majira mazuri ya kuwaona Papa potwe huanzia mwezi Oktoba mpaka Februari katika kisiwa cha mafia. Uhifadhi wa Papa potwe imekuwa hoja ya msingi jambo ambalo limepekea mashirika mbali mbali na makampuni ya utalii wa baharini na fukwe kuwekeza nguvu zaidi katika kuwahifadhi Papa potwe wa kisiwa cha Mafia, Mfano, World wildlife fund (WWF) na WATONET wamekuwa wakishirikiana kwa karibu katika kuhifadhi Mazingira ya bahari kati kisiwa cha Mafia Ili kuokoa maisha ya Papa potwe ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa uwepo wa viumbe Hawa kiuchumi na kijamii pia. Halmashauri ya Wilaya ya Mafia imekuwa ikijipatia fedha nyingi za kigeni kutokana na utalii wa Papa potwe.
SABABU ZINAZOHATARISHA MAISHA YA PAPA POTWE.
Licha umuhimu wa uwepo wa Papa potwe katika nyanja mbali mbali za kiuchumi na kijamii, viumbe Hawa wamekuwa wakikumbana na Changamoto mbalimbali ambazo zinahatarisha maisha Yao kwa ujumla. Sababu nyingi zinazohatarisha maisha ya Papa potwe zimekuwa zikisababishwa na shughuli mbalimbali za kibinadamu na sababu nyingine zimepekea uchafuzi wa Mazingira ya Bahari Kama ifuatavyo.
- Uvuvi wa kutumia neti. Aina hii ya uvuvi wa kutumia neti imekuwa ikipelekea kunasa samaki aina ya Papa potwe katika mitego ya neti ya wavuvi jambo linalopelekea kusababisha majeraha makubwa kwa viumbe hawa katika harakati za kujinasua. Katika shughuli hii ya uvuvi huleta changamoto kwa wavuvi hasa pale ambapo samaki wa kawaida hukutwa pamoja na Papa potwe katika mitego ya neti. Hii huleta mgogoro mkubwa licha ya kuwa wavuvi wengi wenye mapenzi mema na viumbe hawa wanapotega mitego yao ya neti na kukuta samaki wa kawaida wamenaswa pamoja na Papa potwe huwaachia na kuwasamehe samaki wote na kurudisha baharini Ili kuokoa maisha ya Papa potwe. Hii imetokana na kazi kubwa ya uelimishaji wa jamii juu ya umuhimu wa viumbe Hawa katika maisha yao ya kila siku.
- Uvuvi wa kutumia chupa za plastiki. Wavuvi wadogo wadogo ambao hawana uwezo wa kununua na kutumia neti rafiki (Fishing nets) mara nyingi hutumia ndoano ambazo huwa zinafungwa na kuning’inizwa katika chupa hizi za plastiki zikiwa na chambo na kuzamishwa baharini ili kunasa samaki, Baadhi ya wavuvi huziacha chupa hizi zikizama na kuelea baharini baada ya zoezi lao la kuvua samaki. Aina hii ya uvuvi huchangia kwa kiasi kikubwa uchafuzi wa Mazingira ya Bahari haswa makazi ya papa potwe hivyo kupelekea kuongezeka kwa chupa za plastiki Baharini na katika fukwe za Bahari ambapo hii imekuwa ni hatari Sana kwa afya ya Papa potwe, Kasa pamoja na Samaki wengine.
- Ajali zinazosababishwa na boti. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamepelekea kuwepo kwa boti zinazokimbia kwa kasi kubwa hivyo kuweza kudhuru na kuua papa wengi wanaopatikana kwenye mazingira ya kisiwa cha mafia. Baadhi ya boti hukimbia kwa kasi sana baharini na hali hii imesababisha ajali na kuuwa Papa potwe wengi sana baharini na wanaosalimika huachwa na majeraha makubwa ambapo mwisho wake hupelekea kifo.
Licha ya umuhimu wa bahari katika shughuli mbalimbali za usafiri na usafirishaji , vyombo hivyo ikiwa ni pamoja na boti zinachangia kwa kiasi kikubwa vifo na majeraha ya viumbe hawa wapole ambao pia ni rafiki kwa binadamu.
- Ukosefu wa elimu ya kutosha ya uhifadhi wa Papa potwe. Baadhi ya wanajamii hususani wavuvi ambao ndio walengwa wakubwa hawajapewa elimu ya kutosha juu ya namna bora ya uhifadhi wa Papa potwe. Hili ni kundi la watu muhimu sana ambalo linaweza kuchangia kuokoa au kuangamiza viumbe kutokana na ukaribu wao wa kila siku katika shughuli zao za uvuvi. Ukosefu wa Elimu ya kutosha Imesababisha kuuawa kwa Samaki hawa hasa pindi wanaponasa katika mitego ya wavuvi, japo kwa wakazi wa Wilaya ya Mafia uvuvi wa Papa potwe kwaajili ya kitoweo imekuwa sio Sana na hata Kama Ipo ni kwa kiasi kidogo. Ukosefu wa motisha ya kutosha hasa kwa wavuvi wanaoonesha ushirikiano wa kuokoa maisha ya Papa potwe umepelekea kupuuzia suala hili na kuona halina msingi.
- Mchango mdogo wa serikali kisera na kisheria. Uhifadhi wa Papa potwe unahitaji mchango mkubwa wa serikali katika kutunga sera na Sheria stahiki zenye usimamizi endelevu katika kulinda na kuhifadhi mazingira ya bahari ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazosababisha kuwepo kwa mazingira magumu ya kiutendaji hasa kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali wa masuala ya bahari. Ikiwa serikali itakosa sera na sheria bora katika uhifadhi wa Papa potwe itasababisha kuwapoteza hata wachache waliobakia.
Mwisho kabisa, nipende kutoa rai kwa serikali na wadau wengine wa Uhifadhi na Mazingira ikiwemo mashirika kama World Wildlife Fund (WWF) na makampuni ya utalii kama Whale Shark Tour Operators Network Tanzania (WATONET) kuongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha inaweka mikakati bora na rafiki ya uhifadhi wa Papa potwe. Nchi ya Tanzania imejipatia umaarufu mkubwa sana duniani kutokana na uwepo wa kisiwa hiki kilichosheheni samaki aina ya Papa potwe ambao hupatikana sehemu chache duniani. Uhifadhi katika ukanda au maeneo ya Bahari umekuwa haupewi kipaumbele Sana nchini Tanzania ukilinganisha na maliasiri zinazopatikana nchi kavu mfano, Hifadhi za Taifa (National parks), mapori tengefu (Game reserves), milima mirefu pamoja na Jumuiya za Uhifadhi (WMAs). Hivyo basi, kutokana na ongezeko la ukuaji wa soko la utalii katika maeneo ya bahari, serikali, makampuni ya utalii na mashirika ya uhifadhi yanatakiwa kuongeza nguvu zaidi katika kutenga bajeti ya kuwekeza katika uhifadhi wa mazingira ya bahari na mwambao wake ikiwa ni pamoja na kutoa elimu Rafiki kwa wavuvi na mazingira, kutoa fursa za ajira kwa wataalamu mbalimbali wa masuala ya bahari ili kuleta mchango chanya katika uhifadhi endelevu.
Makala hii imeandaliwa na kuandikwa na Mhifadhi VICTOR OBADIA WILSON ambaye ni mwandishi wa Makala ya Utalii na Uhifadhi wa maliasili nchini Tanzania kwa lugha ya Kiswahili, Karibu uendelee kumakinika nami katika makala zijazo na usisite kushauri inapobidi Ili Kazi ziwe nzuri na kuvutia zaidi.
Email: wilsonvictor712@gmail.com
Mobile: +255743880175/+255620861002
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, SUA
Idara ya Uhifadhi wa Wanyamapori.