Utangulizi.
Tanzania imebarikiwa kuwa na mazingira tofauti tofauti ambayo kwa ujumla wake imewezesha nchi yetu kuwa na zaidi ya spishi 1100 za ndege. Idadi hiyo ya spishi za ndege inaifanya Tanzania kuwa nchi yenye spishi nyingi zaidi Afrika mashariki na moja kati ya nchi 5 kwa bara la Afrika. Ndege wamegawanyika katika makundi tofauti tofauti na moja wa makundi hayo ni ndege wanao hama. Kama utakuwa ukifuatilia kwa umakini muenendo wa idadi ya ndege katika mashambani, bustani zetu za nyumbani/au mazingira ambayo ni rafiki kwa ndege(makazi ya ndege ) au kwa wale waliopo katika hifadhi zetu za wanyama pori na misitu watakuwa wanaona idadi ya ndege kuna wakati inaongezeka au kupungua. Kuna miezi idadi ya ndege huwa kubwa na kuna wakati idadi hiyo hupungua. Ndege hawa huwa wanahama kutokana na sababu mbalimbali.Uhamaji tunaozungumzika katika Makala hii ni ule wa kusafiri kutoka taifa moja au bara moja kwenda lingine na kurudi,kwa ujumla tunaweza kusema ndege hawa wanahama kutoka sehemu wanazozaliana na kwenda sehemu ambazo hawazaliani.Ndege wakazi (resident) wapo pia ambao kwa majira fulani wanahama kwenda sehemu zingine.
Tanzania ni nchi ambayo hupata zaidi ya spishi 160 za ndege wanaohama na kuja kuishi katika majira ya baridi katika nchi ambazo ndege hawa wanatokea au kuzaliana. Kuanzia ndege wadogo jamii ya Shoro hadi wakubwa jamii ya Korongo. Baadhi ya ndege husafiri/kuhama usiku kwa sababu hakuna jua hivyo hali ya hewa ni nzuri kwao na pia ndege wala nyama huwinda mchana na sio usiku.Mfano wa ndege wanaohama usiku ni Shoro(Warbler), Pita(Pittas) na wengine kuhama nayakati za mchana mfano: Ndege wala nyama kama Tai na Mwewe (Eagle), Korongo (Stork) na Mbayuwayu (Swallow). Ndege ambao hupatikana pembezoni mwa bahari/maeneo ya pwani husafiri mchana na usiku.
Muda/Kipindi
Nchini Tanzania kuanza kuona ndege wanaohama kuanzia mwezi wa nane (Augosti) na ndege hawa huondoka kurudi katika nchi ambazo huzaliana kuanzia mwezi wanne (Aprili).Kuna baadhi ya ndege wahamaji huendelea kubaki nchini (kwa uchache sana).
Sababu
Ndege hawa wahamaji wapo ambao husafiri umbali mrefu sana kutoka mataifa ambayo huzaliana na kuja mataifa ambayo hawazaliani. Tafiti zinaonesha sababu ya ndege hawa kufanya zoezi hili gumu ni mabadiliko ya hali ya hewa sambamba na upatikanaji wa chakula. Mabadiliko ya hali ya hewa ya sehemu ambayo ndege hawa huzaliana tunajifunza kuwa ndege wanaotoka bara la Ulaya na Asia mara baada ya kuzaliana kuna kuwa na kipindi cha majira ya baridi kali hii hupelekea kuwa na barafu,mimea/uoto mchache,mwingi huwa umefnikwa na barafu.Ni kipindi ambacho hakuna jua na wadudu wachache sana hivyo chakula hakitoshelezi kwa ndege wote.
Kipindi hicho katika nchi za Afrika (zilizopo katika Tropiko) huwa ni majira ya joto na chakula pia kinapatikana. Hivyo ndege hawa inawalazimu kuhama ili kukabiliana na mabadiliko haya ya kimazingira.
Makundi makubwa matatu ya aina ya uhamaji wa ndege.
1. Ndege wahamaji kutoka bara la Ulaya na Asia (Palaearctic migrants)
Hawa ni ndege ambao huzaliana katika bara la Ulaya na Asia na mara baada ya msimu wa kuzaliana kuisha ndege hawa husafiri na kuja/kuhamia maeneo au bara ya kusini mwa Ulaya/Asia tunaweza kusema Afrika.Ni kundi ambalo spishi nyingi za ndege wanaohama wanapatikana. Mfano wa ndege katika kundi hili ni:
Korongo Mweupe (White Stork)
Ripoti kutoka katika Ndege wanaovishwa pete zimeonesha kuwa ndege hawa hufika Tanzania kutoka nchi zilizopo Ulaya Kati. Husafiri katika kundi kubwa na tafiti zinaonesha watoto (juveniles) hufika kabla ya wakubwa (Adults). Huwasili Tanzania mwezi Novemba na huondoka mwezi Aprili. Haijazoeleka kuwaona ndege hawa ukanda wa Pwani mwa Tanzania.
Picha:Friedemann Vetter Picha kutoka ebird
Picha ya Mbayuwayu Ulaya (Barn Swallow); Tafiti zimeonyesha kuwa Mbayuwayu Ulaya wanaofika Tanzania wanatoka katika nchi za Kazakistani, Polandi na Bulgaria. Hufika kwa wingi mwishoni mwa mwezi Agosti na kuondoka mwezi Aprili kila mwaka. Huonekana Maeneo yote Tanzania.
Picha: ya Chati Ulaya (Northern Wheatear) imepigwa na Neil Baker; Ni muhamiaji kutoka bara la Ulaya na idadi ndogo huzaliana maeneo ya Alaska ambapo ndege huyu husafari umbali mrefu sana na kufika Tanzania mwezi Octoba na kuondoka mwezi Aprili.Hupendelea maeneo yenye nyasi na hasa maeneo yaliyo tambarare husafiri mmoja moja sio katika kundi.
2. Ndege ambao hawaondoki Africa
Hili ni kundi ambalo uhusisha ndege wanao hama na kuzunguka bara la Africa tu. Ndege hawa hawatoki nje ya bara la Afrika. Jamii hii ya ndege imegawajika katika makundi madogo mawili ambayo ni wahamaji wa umbali mrefu na wahamaji wa umbali mfupi. Ni kundi ambalo sio rahisi sana kueleweka kutokana na uhaba wa taarifa wa baadhi ya spishi zinazohusika. Spishi nyingi za ndege hawa huzaliana kaskazini mwa Ikweta kwenye eneo la Sahel lenye nchi zifuatazo; Senegali,Mauritania,Mali,Niger,Nijeria,Kameruni,Burkinafaso, Chadi,Jamhuri ya Afrika ya Kati,Sudani,Sudani ya Kusini na Eritria.Na kuja kusini mwa Ikweta kipindi ambacho hawazaliani.Mifano ya ndege hawa ni Korongo Samawati,Kekeo kidari-chekundu,Carmine Bee-eater,White-throated Bee-eater,Angola Swallow,Angola Pitta, Wahlberg’s Eagle, Grasshopper Buzzard, Plain Nightjar,Pennant-winged Nightjar na spishi nyingine.
3. Ndege ambao wanahama kutoka Africa na Madagasca
Ndege wachache wapo kwenye hili kundi ambao wanahama kutoka Afrika kwenda Madagasca na kutoka Madagasca kuja Afrika. Ndege hawa huzaliana Madagaska na kuja Afrika kipindi ambacho hawazaliani. Mfano wa ndege hao ni Madagascar Squacco Heron,Madagascar Bee-eater, Caspian Tern, Broad-billed Roller na spishi nyingine.
Hitimisho
Siku ya kimataifa ya ndege wanaohama husherekewa kila Jumamosi ya wiki ya pili ya mwezi wa tano na mwezi wa kumi yaani (mwezi Mei na Oktoba), mwaka huu 2023 siku hizo ni tarehe 13 Mei na tarehe 14 Oktoba.Waangaliaji wa ndege pamoja na wapenda mazingira asili duniani kote hukutana katika makazi tofauti tofauti ya ndege na kuangalia ndege kwa pamoja. Pia hutuma taarifa za ndege waliowaona au kuwasikia kwa kutumia aplikesheni za eBird na Birdlasser na mwisho wa siku kutambua waangaliaji wa taifa/timu gani walikusanya spishi nyingi za ndege. Zoezi hili husaidia kuusanya taarifa za ndege, kukuza uelewa wa watu kwani wanapo kutana hubadilishana mawazo na kueleweshana mbinu mbalimbali za kuhifadhi ndege na mazingira kwa ujumla. Tujitokeze kushiriki siku hizi za ndege wahamaji na kutuma taarifa zetu sio lazima uende hifadhi za taifa unaweza kuangalia ndege kwenye bustani zetu za nyumbani tu.
Ndege wanaohama hukutana na changamoto nyingi sana katika safari yao hii, mfano wa changamoto hizo japo kwa uchache ni uharibifu wa mazingira maeneo ambayo ndege hawa hufikia wakati ambao hawazaliani, uharibifu wa maeneo wanayo pita na kupumzika, uwindaji haramu wa ndege, sumu, uchafuzi wa mazingira, kushikwa na nyaya za umeme na kujigonga katika majengo marefu hasa maeneo ya mjini.
Jamii inapaswa kutunza mazingira pamoja na kutokuharibu vyanzo vya maji na maeneo oevu ambayo yameonekana kupendelewa na spishi nyingi za ndege wahamaji. Kupitia elimu za uhifadhi mazingira tushirikiane kwa pamoja kulinda na kuhifadhi mazingira kwa ajili yetu yenyewe pia wa ajili ya ndege na bioanwai.
Asante kwa kusoma makala hii, washirikishe wengine pia makala hii; imehaririwa na Hillary Mrosso. Kwa maswali, maoni, mapendekezo kuhusu makala hii usisite kuwasiliana na mwandishi wa makala hii kwa mawasiliano hapo chini;
Ester Matingisa
Atlasi ya Ndege wa Tanzania-Iringa
0762351997.