Popo ni wanyama aina ya mamalia wenye damu moto, miili iliyofunikwa na nywele, wanaozaa na kunyonyesha watoto wao kwa kutumia viwele vyao.  Kibaolojia, popo wanapatikana katika oda ya kipekee ya chiroptera ikimaanisha wanyama ambao miguu yao ya mbele imekuwa mabawa. Hawa ndio wanyama pekee duniani wenye uwezo wa kupaa kwa kutumia mabawa yao. Muundo wa mifupa ya miguu ya mbele ya popo inafanana na mikono ya binadamu, ikiwa na mifupa mirefu minne mithili ya vidole iliyofunikwa na ngozi nyembamba. Mfupa mmoja umejitenga mithili ya dole gumba lenye kucha ambao hutumika kushikilia chakula, kujihami au kutambaa.

Kuna zaidi ya spishi 1400 za popo duniani, huku asilimia kubwa ya jamii hizi zikipatikana katika nchi za ukanda wa tropiki. Katika jamii hizi zipo zinazoishi kwenye mapango, misitu, au kwenye majengo, madaraja, minara nk. Popo hawa wamegawanya katika makundi mbalimbali kutokana na aina ya chakula ambacho wanakula ambapo kuna baadhi wanakula  wadudu, umajimaji wa kwenye mimea na maua (nectar), chavua (pollen), wadudu, Samaki, na wengine hufyonza damu za wanyama.  Jamii hizi zimegawanyika katika makundi makuu manne kama ifuatavyo.

Popo wala wadudu (Insects eating bats)

 Hawa ni popo wanaowinda na kula wadudu wakiwa wamegawanyika zaidi nusu oda ya Yangochiroptera, ambapo wanafanana na panya lakini wana mabawa. Jamii hii ya popo ndio wanaoongoza kwa kuwa na jamii nying zaidi duniani kuliko makundi mengine. Vile vile jamii ndogo kabisa ya popo duniani pia inapatikana miongoni mwa popo hawa, ikijulikana kama nyukibambi (bumblebee bat) na huwa na uzito wa gramu 2, na kumfanya nyukibambi kuwa spindi ndogo ya mamalia duniani.

Popo wala wadudu ndio jamii ya popo inayotumia zaidi mwangwi kwa ajili ya kubaini na kunasa wadudu warukao na kuwafanya chakula chao. Popo hawa hutoa mawimbi makali ya sauti (high frequency) ambapo yakikutana na kizuizi humrudia kama mwangwi, na kumsaidia kutambua ukubwa na umbali wa kitu kilichorudisha mwangwi. Hii humsaidia kutambua wadudu kwa urahisi kwani bila hata kutumia macho huweza kunasa wadudu warukao pale mwangwi unapomrudia ukiwa na mawimbi madogo.

Kwa kuwa ufanisi katika kuwinda kwa popo jamii hii hutegemea mwangwi , changamoto yake kubwa ni pale ambapo wanakuwa katika maeneo ambayo yana kelele au miti mingi. Hii huwafanya popo kuweza kupata mwangwi wa kitu kilicho karibu tu na si vinginevyo. Wakati mwingine wadudu wanaowawinda huwa wametulia na hawaruki, hivyo kuwapelekea popo kutumia milango mingine ya fahamu kama macho, pua na masikio kusikiliza sauti za wadudu hao.

Miongoni mwa jamii za Popo wala wadudu

Popo wanyonya damu (Vampire bats)

 Hawa ni popo wanaopatikana  bara la Amerika na wanaishi kwa kunyonya damu kutoka kwa wanyama wa aina mbalimbali . Jamii hii ya popo wana  vichwa vifupi na pua zilizo wazi zenye umbo kama majani ya miti (leaf-shaped nose). Pua zao zinaweza pia kutambua kama kiumbe chenye damu moto kipo karibu (heat sensor), ambazo husaidiana na masikio. Masikio yao huweza kusikia sauti za mnyama anayepumua akiwa amelala au ametulia, ili kuweza kwenda kuwanyonya damu. Wana meno mawili ya mbele ambayo ni makali kuliko ya mnyama yeyote yule, na huyatumia kuuma ngozi ya mnyama ili damu itoke.

Kutokana na udogo na ukali wa meno yao, mnyama mkubwa ni ngumu kusikia kama ameumwa na popo hawa. Popo hawa halamba damu kutoka kwenye jeraha mabalo wamelisababisha kwa mnyama hadi washibe. Hupendelea zaidi kuuma sehemu za mngongoni au miguuni na kufyonza damu kwa takribani nusu saa. Tafiti za kitaalamu zinaamini kuwa mate ya popo hawa husababisha ganzi (anaesthetic) kwa mnyama pindi wanapolamba damu, na kupelekea mnyama huyo kutohisi maumivu. Pia  mate hayo huzuia jeraha kuvimba. Hupendelea kufyonza damu za wanyama wengi hasa wafugwao ambao huwa wamefungiwa sehemu moja, na mara chache sana kwa popo hawa kufyonza damu ya binadamu.

Hii ndio jamii pekee ya popo ambayo wanaweza kutembea, kukimbia na kuruka kutoka ardhini. Tofauti na jamii nyingine, popo hawa wana mifupa ya nyonga na miguu ya nyuma yenye nguvu ambayo huwawezesha kuruka tokea ardhini au kutembea kwa kasi. Miili yao pia ina uzito mwepesi, wakifikia uzito wa gramu 40 tu, ambapo huweza kufyonza gramu 20 za damu za wanyama wengine kwa usiku mmoja. Popo hawa pia wanashirikiana sana kiasi kwamba hubeba damu na kwenda kuwalisha wenzao walio wazee au wagonjwa na ambao hawawezi kujipatia chakula.

Ni mara chache popo hawa kuwa na madhara ya moja kwa moja dhidi ya binadamu, na wakati mwingine watu wameonekana wakiwashika au kuwebeba bila tatizo. Madhara wanayoweza kuyaleta ni pamoja na kuwaambukiza Wanyama wengine wa kufugwa magonjwa kama kichaa cha mbwa. Utafiti unaonyesha maambukizi haya ni kwa kiwango kidogo kwani wanyama wengi kwa siku za karibuni wamekuwa wakipewa chanjo. Pia mifumo ya miili yao ina kinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa mengi yaliyopo kwenye damu za wanyama wanazofyonza. Mara nyingi popo wenye maambukizi huwa wazubaifu, hushindwa kuruka na hufanya mambo tofauti na wengine.

Popo akifyonza damu ya mnyama

Popo wavuvi (Fisherman bats or Bulldog bats)

Kuna jamii tatu za popo wenye uwezo wa kuvua samaki wadogo au uduvi kwa ajili ya kitoweo. Jamii hizo zinapatikana bara la Amerika, Mashariki mwa Asia na Kaskazini mwa Afrika. Popo hawa huwinda kwa kuruka juu karibu na uso wa maji, kisha kutoa mawimbi maalumu ya sauti ambayo humrudia kwa mfumo wa mwangwi. Wana uwezo wa kutambua aina ya kitu kilichorudisha mawimbi ya sauti kwa mfumo wa mwangwi, na iwapo samaki atakuwa anaogelea karibu na uso wa maji basi watamkamata kwa urahisi. Ukiachana na mwangwi, popo pia husikiliza mawimbi ya maji kujua kama kuna mitetemo karibu na uso wa maji, ambapo hufanya kama ubashiri kuwa samaki ndio amesababisha mitetemo hiyo, na kwenda eneo husika kwa haraka. Miguu ya popo hawa ina vidole vyenye kucha ndefu zenye nguvu ambazo huziingiza ndani ya maji na kutoa windo lake.

Popo Wavuvi

Popo wala matunda (fruits bat)

Popo hawa wanapatikana zaidi kwenye ukanda wa kitropiki barani Afrika, Asia, Australia na visiwa vya bahari ya Hindi. Aina hii ya popo wanaokula matunda wamegawanyaika pia katika makundi tofauti ambapo wapo ambao wanafanana na mbweha au mbwa wadogo wenye mabawa. Kuna spishi karibu 200 za popo hawa zikiwa zimegawanyika katika popo walao matunda, chavua ya maua (polen), asali ya maua (nectar) na chache hula majani laini ya miti. Spishi kubwa kabisa ya popo duniani inapatikana miongoni mwa popo hawa wakijulikana kama popo-mbweha wa uhindi (Indian flying fox) wakifikia uzito wa kilogramu 1.6 na mabawa yenye urefu wa mita 1.7.

Miongoni mwa spishi hizi za popo, nyingi hazina uwezo wa kutumia mwangwi bali hutumia macho na pua kufahamu chakula kilipo. Popo hawa wana macho makubwa yanayoona vyema kwenye giza au mwanga mdogo, lakini hayaoni vizuri kwenye mwanga mkali hivyo kuwafanya wafanye shughuli zao usiku zaidi. Pua zao zinaweza kunusa vyema kama zilivyo za mbwa wa nyumbani, na kuwafanya waweze kufanikiwa kujua kilipo chakula.

Popo hawa wana faida nyingi ikiwamo kuchavusha mimea mbalimbali pale wanapotafuta chakula kwenye maua na kusambaza chavua, pia wanapokula matunda husambaza mbegu zinazotoka kwenye kinyesi chao. Mbali na faida, popo hawa wanaonekana kama waharibifu miongoni mwa wakulima wa matunda. Pia, inaaminika wana uwezo mkubwa wa kubeba magonjwa yanayoweza kuathiri binadamu na wanyama jamii ya nyani/ngedere. Wanasayansi wanaamini virusi vya ebola na virusi vinavyosababisha kutokwa na damu (Marburg virus) vinaweza kubebwa na popo hawa, ambayo ni hatari  kwa binadamu. Hii haimaanishi kwamba popo wote hubeba virusi hivyo bali miili yao kuonekana na uwezo mkubwa wa kutunza magonjwa hayo. Virusi hivyo huweza kufika kwa binadamu au wanyama jamii ya ndegere endapo watadondosha vinyesi au mate kwenye matunda au mboga zinazoliwa na binadamu au kama popo watafanywa kitoweo. 

Popo matunda

Sababu za popo kuning’inia kichwa chini, miguu juu

Kwa kawaida viumbe wengi wakining’iniza kichwa chini kwa muda mfupi tu hupelekea damu kukimbilia kwenye ubongo na kusababisha kizunguzungu. Hali haipo hivyo kwa popo kwani huweza kuning’inia hata kwa miezi kadhaa bila tatizo. Popo hupenda kuning’inia sehemu ambazo zina giza au kivuli ambapo siyo rahisi maadui kuwapata. Sababu kuu za popo kuning’inia ni kama zifuatazo;

  1. Udogo wa miili yao.

Ukilinganisha na binadamu, popo wana miili midogo ambayo pia ina uzito mdogo na damu kiasi kidogo. Uzito mdogo huchangia kupunguza nguvu za uvutano (gravitational force) ambayo ndiyo inapelekea damu kurudi kichwani kwa wingi endapo kiumbe mwenye uzito mkubwa atakaponing’inia kichwa chini na miguu juu.

2. Uimara wa mifupa ya nyongaUkitoa jamii ya popo wanyonya damu, jamii nyingine zina mifupa midogo na isiyo na nguvu ya nyonga (pelvic girdle) na ya miguu ya nyuma. Mifupa hii huwasaidia viumbe warukao kama ndege kuweza kuanza kuruka kutokea ardhini kwa kukimbia ndipo wapae au kurusha mwili juu kabla ya kuanza kutumia mabawa. Popo akining’inia kutumia miguu humsaidia pindi anapotaka kuruka kwani hufanya kujiachia tu na kuendelea kupaa.

3. Muundo wa maungo yake.

Maungio ya magoti ya popo yanaelekea nyuma, na pia vidole vya miguu yake vimeundwa na misuli imara. Popo wakining’inia hawatumii nguvu yoyote na badala yake huwa ni kama wamelegeza misuli ya miguu ambayo huvifunga (lock) viungo vya miguu kukaza sehemu waliposhikilia. Hii hupelekea popo kuweza kuning’inia kwa urahisi hadi miezi kadhaa, na hata wakifa huweza kuendelea kuning’inia.

4. Kujikinga na maadui.

    Popo wengi huning’inia sehemu zenye giza ambazo siyo rahisi adui kufika. Popo pia huweka mpango wa kukimbia haraka endapo adui atagundua sehemu walipo, na hii hufanya kwa kujiachia tu. Mabawa ya popo pia huyatumia kujifunika miili yao pindi wanapolala ili kujikinga na baridi au mvua. Ni ngumu kwa popo kujifunika vyema kama atakuwa yupo ardhini.

    Kwa makala nyingine kuhusu popo usiache kufuatilia blog yetu, pia washirikishe wengine makala hii ili wajifunze mambo haya muhimu.

    Makala hii imeandaliwa na Ezra Mremi na kuhaririwa na Hillary Mrosso na Alphonce Msigwa-Afisa Uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Haifa Tanzania. Kwa maoni, ushauri, maswali na mapendekezo kuhusu makala hii unaweza kuwasiliana na mwandishi wa makala hii.

    Ezra Peter Mremi- 0786078728/0756438692

    Email: mremiezra@gmail.com

    you might also like