Habari msomaji wa makala za wanyamapori, karibu katika makala ya leo. Leo tunaangazia moja ya changamoto kubwa inayoikabili sekta ya uhifadhi wa wanyamapori duniani. Changamoto hiyo ni migogoro isiyoisha kati ya binadamu na wanyamapori. Kwa karne nyingi tumeshuhudia migogoro mingi ikiibuka na kusababisha vifo vya watu, uharibifu wa mali na mazao ya watu; hata hivyo, wanyamapori wengi wamepoteza maisha yao kwasababu ya migogoro hii.
Migogoro baina ya binadamu na wanyamapori ni ile hali ya mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori katika kujitafutia/ kujipatia mahitaji yao. Miingiliano hii imekuwa ikitokea pale mahitaji yao yanapopatikana sehemu moja, mfano kwenye vyanzo vya maji, sehemu za malisho na katika sehemu za shughuli mbalimbali za kiuchumi pia vyanzo vya nishati ambako huishi wanyamapori. Soma zaidi Siasa Duni Na Sehemu Zenye Migogoro Ya Vita Vimechangia Sana Kuongezeka Kwa Vitendo Vya Ujangili Wa Wanyamapori Barani Afrika.
Picha na Isacka Lemulebeli; ikionyesha uharibifu wa mazao aina ya migomba uliosababishwa na Tembo katika kijiji cha Malinzanga, Iringa Tanzania.
Migogoro hii inaongezeka kwa kasi sana na kuwa sehemu mojawapo inayotazamwa na taasisi nyingi za kiserikali na mashirika binafsi katika uimarishaji wa shughuli za uhifadhi kwenye nchi nyingi barani Afrika na duniani kwa ujumla. Makala hii imeandaliwa kutoka katika tafiti mbali mbali zilizofanyika kwa baadhi ya nchi za Afrika ambazo ni Tanzania, Kenya, Zambia, Ethiopia na Camerron pia na baadhi ya nchi za bara la Amerika na India, utafiti uliojulikana kama (National Human Wildlife Conflict Management Strategy ya mwaka 2020-2024).
Tafiti karibia zote zimeonyesha ushabihiano mkubwa wa vyanzo vikuu vya migogoro hii; Ongezeko kubwa la idadi ya watu, upanuzi mkubwa wa shughuli za kilimo, sera ya matumizi bora ya ardhi kutokujitosheleza, Mifumo ya kiikolojia haikutengwa kuweza kujumuisha maeneo tengefu pamoja na shoroba zake, ongezeko la makazi ya watu jirani na maeneo yalitotengwa kwa ajili ya uhifadhi, uwindaji haramu, kutokuwepo kwa kifuta machozi baada ya majanga ya wanyamapori, rushwa, uelewa mdogo na umaskini. Soma zaidi Migogoro Kati Ya Wanyamapori Na Binadamu, Nini Chanzo? Nani Wa Kutatua Migogoro Hii?
Picha na Thomas Mukoya; Tembo na ng’ombe katika chanzo kimoja cha maji,
Hapa chini tutaziangalia sababu saba kwa undani zaidi; –
- Ongezeko kubwa la idadi ya watu; Ongezeko kubwa la idadi ya watu duniani linaenda sambamba na mahitaji yao, ikiwemo mahitaji ya ardhi kwa ajili ya makazi na shughuli za uzalishaji mfano kilimo, vyanzo vya maji na maliasili kama vile dawa, matunda na nishati. Hivyo, kumepelekea ongezeko kubwa la idadi ya watu maeneo mengi jirani na maeneo tengefu, ambayo moja kwa moja kumekuwa na mabadiliko ya matumizi ya ardhi kwa kilimo, ufugaji na malisho ambayo mwanzo yalitumika na wanyamapori hivyo kumechangia uwepo mkubwa wa kuwanyima wanyamapori mahitaji yao ambayo katika kulazimishia kumekuwa kukitokea migogoro. Ongezeko kubwa la watu jirani na maeneo tengefu limeripotiwa mpakani mwa hifadhi ya taifa ya Serengeti na Ruaha upande wa bonde la Usangu.
- Maeneo mengi tengefu yalio chini ya mfumo mmoja wa kiikolojia hayako jirani, hivyo huunganishwa na shoroba ambazo pia ni muhimu katika malisho ya wanyamapori hasa wale wenye uhitaji wa eneo kubwa la kuchunga kama tembo na wanyama walao nyama. Na kwa bahati mbaya sana maeneo mengi ya shoroba hizi yapo jirani na makazi ya watu pia yamevamiwa na shughuli za kiuchumi, hivyo kumekuwa na migogoro mingi baina yao. Mfano, mfumo wa kiikolojia wa Manyara – Tarangire unaounganishwa na shoroba ya Kwakuchinja unaripotiwa kuwa na ongezeko kubwa la watu na shughuli zao za kiuchumi.
- Utanuzi wa shughuli za kilimo na ufugaji; Utanuzi huu mkubwa umetokana na mabadiliko makubwa ya mahitaji kijamii na kiuchumi. Na ukiangalia jamii nyingi zinazokaa pembezeno mwa maeneo tengefu zinajishughulisha na kilimo na ufugaji hivyo zimelazimika kuendana na mabadiliko hayo kwa kubadilisha mifumo ya kilimo na ufugaji ili kuweza kuendana na mahitaji yao ambayo yamepelekea ongezeko kubwa la kutokea kwa migogoro hiyo. Pamoja na yote, changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi yenye athari kubwa kwenye kilimo kumeongeza zaidi utanuzi jirani kabisa na maeneo tengefu kwa kukwepa mmomonyoko wa udongo pia kutafuta ardhi yenye rutuba.
- Utegemezi mkubwa kwenye vyanzo vya maji; Maeneo mengi nchi na nchi jirani yamekuwa na msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ikiwa watu wengi hutegemea kilimo hivyo wamejikuta wakilazimika kutumia vyanzo vikuu vya maji na hata wakati mwingine kuchepusha maji hayo. Wakati yanatokea hayo, kumepelekea wanyamapori kutopata maji ya kutosha na wakati mwingine kukosa kabisa hivyo huwalazimisha kuyatafuta na hata hutoka kabisa katika eneo tengefu ambako kumewafanya wote binadamu na wanyama kuwa hatarini zaidi kuingia kwenye migogoro. Vyanzo hii vya maji vimeripotiwa kama sababu ya migogoro hasa kipindi cha kiangazi,
- Kutokuwa na sera nzuri katika ugawaji wa mpango bora wa matumizi ya ardhi; Kipindi cha nyuma mpango wa matumizi ya ardhi haukuwepo na kwa baadhi ya maeneo ulikuwepo haujaweza kutekelezeka au pia haukuweza kuainisha gharama zitakazowezatokea. Kwa mana hiyo, kumesababisha maeneo ya kilimo, ufugaji na makazi ya watu kuwa jirani na hatarini zaidi kwa wanyama pori. Hii imechangia kwa asilimia kubwa migogoro baina ya wakulima – wafugaji, wakulima – wanyama pori na wafugaji – wanyama pori.
- Kutokuwepo kwa kifuta machozi (fidia); Kwa baadhi ya migogoro iliyotokea ikiwa imesababishwa na wanyamapori, na katika taratibu za fidia kutokupitishwa kabisa au kucheleweshwa kwa fidia hizo kwa watu husika kumesababisha migogoro kuongezeka zaidi hasa ile ya kutengenezwa na binadamu. Hii imeripotiwa kama vile wanyama kuuliwa pale wanapotokea maeneo binadamu wapo au kutiliwa sumu kwenye mawindo yao kwa lengo la kukomesha na kulipa kisasi kwa serikali. Wanyama walao nyama wengi mpaka ndege wanaotegemea mizoga wanaathirika sana na hii.
- Uvunaji wa misitu na ulishaji mifugo ulipotiliza katika maeneo jirani na yale yaliyotengwa kwa ajili ya wanyamapori na shughuli za uhifadhi; Kulingana na ongezeko kubwa la watu na mahitaji yao kumesababisha uvunaji mkubwa wa misitu kwa ajili ya mbao, kuni na vitu vingine hivyo kumepelekea kupungua zaidi kwa maeneo yatumiwayo na wanyamapori kwa mahitaji ya chakula, sehemu za viota, sehemu za kulala na sehemu za kupatia wenza. Hii imewalazimisha kuhamia mashambani mwao na ongezeko la fujo kwenye makazi yao.
Sababu tajwa hapo juu zimekuwa zinajirudia rudia kwa nchi nyingi barani Afrika hasa zile zinazoendelea kwa sababu uchumi wao mkubwa unategemea mifugo na kilimo. Ijapokuwa, zinatofautiana katika ukubwa wa maafa baada ya migogoro kutokea, wakati na sehemu inakotokea migogoro hiyo pia na wanyama wasababishi. Nyingi za tafiti hizo zinaonyesha karibia wanyamapori wote wanauwezo wa kusababisha migogoro japokuwa wakubwa ndio wamonekana ni hatari zaidi kama vile tembo, nyati, kiboko, simba, mbwa mwitu, fisi, nyani, nguruwe pori pamoja na ndege.
Makala zitakazofuata tutangalia kwa undani zaidi aina za migogoro, wanyama wasababishi mmoja baada ya mwingine, athari za migogoro na jinsi ya kuipunguza.
Kwa ushauri au maswali kuhusu makala hii, usisite kuwasiliana na mwandishi,
Leena lulandala
0755369684